Askofu Mtenga amtwisha Mkuu wa wilaya ujumbe mzito

 Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Songea, Nobert  Mtega amevitaka vyombo vyenye mamlaka serikalini kuacha mchezo wa kutumia silaha kali ovyo, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchochea machafuko na kuwaumiza watu wasio na hatia, hasa watoto na wakina mama.

Kauli hiyo aliitoa siku chache zilizopita wakati wa sherehe za shirika linaloshughulikia watoto waishio katika mazingira magumu na wanawake wanaojifunza ujasiriamali  la DMI,  mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti.

Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Songea, Nobert  Mtega
Alisema mahali popote  ambapo machafuko yapo,  yalianza kidogo kidogo na waathirika wakubwa ni watoto na wakina mama kwa kuwa kundi hilo, lina uwezo mdogo wa kujitetea na kuwafanya waangamie bila sababu za msingi.

"Watoto hawana walinzi zaidi ya sisi wenyewe,na  inatakiwa kutambua kuwa taifa bila watoto bado halijakamilika. Wao ni sehemu ya msingi katika jamii yoyote ile," alisema Askofu Mtega na kuongeza:

"Nawaambieni kama tutaachilia mambo haya ya kutumia silaha ovyo, yakaendelea kwa kweli tutakuwa tunatafuta machafuko ambayo yatahatarisha maisha ya watu wasio na hatia kabisa.”

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti.
Mtega alisema kinachoumiza zaidi wanaopatwa na athari za milipuko ya silaha hizo ni watu wasio na hatia,   badala yake   watu wa kuwajibishwa wanaachwa huru, jambo alilobainisha kwamba ni dhambi mbele za Mungu.

Mtumishi huyo wa   kanisa Katoliki alisema kuwa  kutumia silaha ovyo dhidi ya binadamu tena kwa yule asiyekuwa na hatia ni jambo la kishetani ambalo halistahili hata kidogo kwa kuwa linaweza kumkaribisha shetani katika jamii husika.

Kwa upande mwingine Mkuu  wa  Wilaya  ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa shughuli hiyo alilipongeza shirika hilo kwa kazi nzuri ya kuwahudumia watoto waishio katika mazingira magumu, huku akiyaomba mashirika mengine kuiga mfano huo.

Mbali na hilo,  alichanganua kwamba jambo la msingi la kuangalia kwa makini ni eneo lililokosewa katika kumlea mtoto ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ya kudumisha amani iliyopo ili vizazi viendelee kuwa na neema ya mafanikio.

Maaskofu TAG Kanda ya Ziwa wasimikwa.

Maaskofu waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mkoani Dodoma miongoni mwao ni pamoja na viongozi wa kanda ya ziwa kutoka majimbo ya Kagera, Geita, Mwanza na Jimbo la Mara wamesimikwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk Barnabas Mtokambali kwenye ukumbi wa  Mkuyuni  jijini Mwanza hivi karibuni.

Maaskofu waliosimikwa ni pamoja na Askofu Charles Mkumbo Jimbo la Mwanza,  makamu Askofu wake Mchungaji valentine Mbuke, Makamu Askofu wa Jimbo la Mara, Mchungaji Godson Sharua na Mchungaji Elias Jacob  kuwa makamu askofu wa Jimbo la Geita.

 Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk Barnabas Mtokambal
 Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali akiongea katika sherehe hizo za usimikaji zilihudhuriwa na  Makamu Askofu Mkuu Dk. Mhiche na Katibu Mkuu wa TAG, Ron Swai, Askofu wa maimbo ya Simiyu, Geita, Mara na Moshi aliwaasa wachungaji na watumishi wengine wa Mungu kujua wameitwa kuihubiri Amani na Haki hivyo, hawapaswi kuvunja vizuizi vyote vinavyoleta kiwingu cha kupoteza amani nchini.

 Dk. Mtokambali alikumbusha kanisa la Tanzania kutambua wakati umefika wa kuivuna  nchi,  yaani mioya ya watu wote wamjue Mungu wa kweli wala si vinginevyo, kutokana na watu wengi kupoteza dira na wanatapata kutafuta msaada kwa kuamini ushirikina, uchawi na kufuata imani potofu za ushoga ambayo ni machukizo kwa Bwana.


Mtumishi wa  Mungu alikemea vitendo viovu vinavyofanywa nchini hu susan kanda ya ziwa vya kishirikina na kuamini uchawi, mauaji ya walemavu wa ngozi, na vikongwe viachwe mara moja, huku akiongeza kuwa watu hao wana haki ya kuishi.

Askofu Mkuu Dk. Mtokambali akinukuu kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume 17:16-24 alisema, watumishi wa Mungu kuwa na huruma na uchungu juu ya taifa letu jinsi linavyopotoshwa na mafundisho potofu ya kuabudu miungu na sanamu ambayo ni machukizo mbele za Bwana.

Bila Wachungaji nchi haina pa kukimbilia,KAMANDA KOVA

Huku likiendelea kulaumiwa kwa utendaji usiokidhi matumizi ya nguvu kupita kiasi, Jeshi la Polisi nchini limefungua na kueleza kuwa bila msaada wa watumishi wa Mungu juhudi zao za kukabiliana na uhalifu nchini hazitazaa matunda yoyote.

Akizungumza na chazo kimoja cha blog hii katika mahojiano maalumu  wiki  iliyopita, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,  alisema nchi inaelekea katika hali ya hatari,  hivyo  wameamua kukutana na wachungaji ili washirikiane nao katika kuirejesha  kwenye utulivu.



Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

“Tumeamua kuwashirikisha watumishi ili wamlilie Mungu wao aliye hai, awezekurejesha amani ambayo imeanza kuyumbayumba. Kweli bila hao nchi yetu hatujui itaelekea wapi, tunaimani kubwa kwamba wana kitu cha ziada juu ya nchi,” alisema Kamanda Kova.


Kamanda Kova aliweka wazi kuwa, kwa kutambua umuhimu wa watumishi wa Mungu aliye hai wiki iliyopita walilifanya kikao maalumu nao jijini hapa, ili kuwasihi wamsihi  Kristo alikumbuke taifa la Tanzania na kulirejesha katika amani.

 
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi,aliweka bayana kuwa, lengo la kikao hicho na watumishi hao wa Mungu ni kupanga mikakati ya kufanya kazi pamoja kwa kile alichodai kuwa kwa nguvu pekee za Jeshi hilo, hakuna chochote kitakachowezekana na nchi inaweza kuwa katika matatizo makubwa.


“Lengo la Jeshi la Polisi, kukutana na wachungaji lilikuwa ni nzuri tu, unajua sisi tunafanya doria ya kuzuia uhalifu kwa njia ya mwili, lakini wachungaji wanafanya doria kwa njia ya rohoni, kwa hiyo wao wana nafasi kubwa ya kuleta mafanikio makubwa nakukomesha hali iliyopo katika taifa kwa sasa, ambayo siyo nzuri,” alisema Kamanda.   
Sambamba na hilo,  alisema watumishi wa Mungu wanauwezo mkubwa wa kuwafundisha watu maadili mema, kwa kuwa kauli yao katika jamii inasikilizwa zaidi.


 
 

“Lazima nchi iwe na amani kwa kutumia mbinu zozote, unafikiri ndugu mwandishi mambo yakiharibika tutakimbilia wapi, hakuna pa kukimbilia mambo yakiharibika katika taifa letu, kwa hiyo lazima tushirikiane na wachungaji kukomesha uhalifu,” alisema Kamanda Kova.

Kamanda Kova aliwataka watanzania kuacha tabia ya kuleta vurugu katika taifa,  huku wakijichukulia sheria mkononi  na kusababisha madhara makubwa katika taifa, hali inayopelekea mvurugano kutokea hata wananchi wasiokuwa na hatia kupoteza maisha.


Kadhalika anawasihi wachungaji kote nchini kuwa na uchungu na taifa hili, washirikiane na Jeshi hilo bega kwa bega kurejesha amani ya taifa ambalo ni mfano hata katika nchi mbalimbali duniani na likikifahamika kama kisiwa cha amani.


Aliongeza kuwa Jeshi la polisi lilikiri mbele ya wachungaji hao kuwa kutumia nguvu na risasi, si suluhu na haitakuwa njia ya kutatua tatizo bali ni kuongeza matatizo zaidi, hivyo likaomba ushirikiano kwa taasisi mbalimbali za kidini hapa nchini kukemea vitendo vibaya vinavyoweza kuliweka taifa pabaya.

Mchugaji Mtikila ashinda kesi iliyokuwa inamkabili.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana imemuachia huru Mchungaji na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya kutoa nyaraka za lugha ya uchochezi kuhusu Rais Jakaya Kikwete na kumiliki hati hizo isivyo halali baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi, Mfawidhi, Illivin Mgeta baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri bila kuacha shaka mahakama imemuona hana hatia.

“Bila kuacha shaka mahakama hii imepitia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri haujamgusa mshtakiwa…mashahidi wanne walitoa ushahidi upande wa mashtaka pamoja na  kuwasilisha kielelezo cha maelezo aliyotoa Mtikila Polisi wakati akihojiwa,”
 
Mchungaji na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP) Christopher Mtikila
Aliongeza kuwa “Katika kielelezo hicho hakuna mahali ambako mshtakiwa alipendekeza Rais Jakaya Kikwete ang’olewe madarakani bali Mtikila alisema kwamba wananchi wasiipigie kura CCM katika uchaguzi lakini hakuwashawishi kumng’oa Rais Kikwete madarakani.”

Alisema katika ushahidi uliotolewa na Jamhuri unadai kwamba mshtakiwa alisema Rais Kikwete anaingiza Uislamu katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba anauangamiza kabisa Ukristo hivyo Wakristo waungane kumweka Mkristo Ikulu.

Alisema ili mshtakiwa atiwe hatiani kwa uchochezi lazima kuwepo na athari zilizojitokeza kutokana na nyaraka hizo zilizodaiwa kwamba za uchochezi lakini hakuna ushahidi kama huo uliotolewa mahakamani hapo na Jamhuri.
 


“Kwa maoni yangu hakuna ushahidi wa kumtia hatiani mshtakiwa kwa mashtaka aliyoshtakiwa nayo hivyo mahakama inamwachia huru…hakuna ushahidi kwamba maneno ya Mtikila yaliamsha hisia za Wakristo na Waislamu,” alisema Hakimu Mgeta.

Baada ya mahakama kumwachia huru Mtikila akiwa bado kizimbani alisikika akisema ‘haleluyaa’ na baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa waumini wake waliitikia ‘amen’.

Alisema hukumu iliyotolewa aliitegemea na kwamba hakuwa na mashaka na hakimu aliyesikiliza kesi hiyo.

Mara baada ya kutoka ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo, Mchungaji Mtikila alijikuta katika wakati mgumu baada ya Polisi waliotanda mahakamani kutaka kumkamata na kumpeleka Polisi kwa ajili ya mahojiano kwa tuhuma za kumtishia kumuua kwa maneno, Gotam Ndunguru maeneo ya Kimara jijini.

Askari alipomwambia anatakiwa kukamatwa Mtikila alisema alikwishazungumza na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mbezi na kumfahamisha kwamba alikuwa mahakamani hivyo atakwenda leo.

Katika kesi ya msingi, Mtikila alikuwa anadaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi alitawanya kwa umma nyaraka zilizosema 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu.’

Africa Lets Worship (Aflewo ) Nairobi 2012

Tamasha la Kusifu na Kuabudu  Africa Lets Worship (AFLEWO) linalojumumisha baadhi ya Nchi za Afrika mwanzo wa weekend hii yaani siku a Ijumaa katika Jiji  la Nairobi nchini Kenya lilifanyika na kuhudhuriwa na Idadi kubwa ya watu katika kumsifu na kumtukuza Mungu.

Baadhi ya vikundi mbalimbali vya uimbaji vilikuwepo kuhudumu katika Tamasha hilo,bila kusahu Wachungaji mbalimbali kutoka nchi jirani katika kuwakilishi katika Tamasha hilo lisilo kuwa na tofauti za kidini wala kikabila bali kwa lengo la kuinua Sifa mbele za Mungu na kuomba kwa ajili ya Bara la Africa na Viongozi wake.

Miezi kadhaa iliyopita lilifanyika Dar-es-Salaam Tanzania,na baadaye kufanyika sehemu mbalimbali za Nchi na majiji mbalimbali Barani Africa ikiwa ni kwa lengo la Kuunganisha watu kwa nia ya Kusifu na Kuabudu Nchi hadi Nchi na Mwaka hadi Mwaka.

Africa Lets Worship (Aflewo ) Nairobi 2012

 Aflewo Praise and Worship Team 2012

Bass Guitar in Action Aflewo  2012

Mmoja wa Viongozi akizungumza katika Africa Lets Worship (Aflewo ) Nairobi 2012
Watu walioudhulia wakifuatilia kwa makini
Pastor Safari kutoka DPC Dar es salaam Tanzania, akitoa Neno Aflewo Nairobi 2012
Wadau wakibalikiwa na Tamasha hilo Aflewo2012

Ilikuwa full anointing watu wakideep katika maombi

Ilikuwa Fullshangwe
Mmoja wa viongozi wa  Aflewo Nairobi (kulia) aliwahikuwepo katika Tamasha la Aflewo Tanzania, akifurahi sana.

 Team mbalimbali zilikuwepo kuhudumu katika Tamasha hilo la Aflewo Nairobi 2012
Ilikuwa ni furaha sana, waliokuwepo katika Tamasha la Aflewo Tanzania UCC wanaweza kuelewa namna gani inavyokuwa!
The Voice kutoka Tanzania walikuwepo kuwakilisha
The Voice
Ilikuwa watu wengi hadi nje ya ukumbi watu wakifuatilia kwenye Big Screen
Bila kujali umbali watu walikuwa wakihudumiwa huko huko!

Jaji Warioba awaasa wakristo kupendana

Wakati Tume ya  Marekebisho ya Katiba ikiwa imeianza kukusanya maoni  katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza,  Mwenyekiti wa tume hiyo,Jaji Joseph  Warioba, amewakumbusha Wakristo kupendana na kusaidiana na serikali kupunguza migogoro.

Mwenyekiti wa tume Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alitoa wito huo wakati   akizungumza   kwenye  uzinduzi  wa sherehe  za miaka 50  tangu  kanisa la Anglican (ACT) lilipoanzisha  Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), mkoani Mwanza.

“ Ni  vyema  sisi waumini wa  Kikristo, tukaonyesha  utaifa kwa kutekeleza kwa vitendo amri mbili kuu  zilizotolewa na  Yesu Kristo , ikiwemo ya kututaka tuwapende jirani zetu kama nafasi zetu. Tukifanya hivyo, tutaondokana  na hii tabia  imbayo imenza kujengeka  hapa nchini; yaani  ubinafsi” alisema  Warioba  mbaye alikuwa mgeni rasmi kwenye  uzinduzi huo.

Aliwashauri  Wakristo  wawe  mfano kwa kutii  sheria za nchi  na kwamba wasichezee amani  kwani pia ni kinyume cha maandiko matakatifu ambayo  yanasisitiza  binadamu wote  kupendana





Waumini wa Dini ya Kiisilamu waandamana kote duniani.

Mapambano yametokea baina ya polisi na waanda-manaji nchini Pakistan kabla ya sala ya Ijumaa, kulalamika juu ya filamu inayokejeli Uislamu iliyotengenzwa Marekani.


Shirika moja la habari la Pakistan limesema kuwa mfanyakazi wake mmoja ameuwawa mjini Peshawar wakati polisi walipofyatua risasi kutawanya makundi ya watu wenye hasira, waliojaribu kuchoma moto jengo la sinema.

Ghasia zimeendelea hadi Magharibi, na waandamanaji hasa wakilenga ofisi za balozi wa Marekani katika miji mbali-mbali.

Ulinzi ulidhibitiwa katika nchi nyingi za kiisilamu kama Misri, Libya, Tunisia Morocco na kwingineko huku zikijiandaa kwa maandamano makubwa baada ya maombi ya Ijumaa.

Maandamano hayo yalipinga filamu iliyotengezwa nchini Marekani kumkejeli Mtume Muhammad na dini ya kiisilamu.

Nchini Pakistan, serikali ilitenga siku maalum kwa jina "special day of love" kwa miniajili ya kumsifu na kumuenzi Mtume Muhammad.

Marekani imelipia matangazo ya kibiashara nchini Pakistan, rais Obama akionekana kukashifu vikali filamu hiyo

Maandamano makubwa kupinga filamu hiyo tayari yamesababisha vifo sehemu mbali mbali duniani.

Ingawa Marekani ndiyo imeathirika zaidi kutokana na mandamano hayo, uchochezi umeoneka kuongezeka kutoka barani Ulaya baada ya jarida moja nchini Ufaransa kuchapisha picha za kumfanyia mzaha Mtume na waisilamu waliopinga vikali filamu hiyo.

Vyama vyote rasmi vya kisiasa pamoja na mashirika ya kidini wametangaza maandmano kwa ushirikiano na makundi ya kibiashara huku maandamano hayo yakitarajiwa kuwa makubwa sana.

Waziri wa mambo ya nje nchini humo, Hina Rabbani Khar, ameambia shirika la habari la AP kwamba siku hiyo maalum inanuiwa kushinikiza maandamano ya amani na kuzuia watu wenye msimamo mkali kusababisha ghasia kutokana na hasira yao dhidi ya Marekani.

Duru zinasema kuwa vituo vya mafuta, maduka na masoko yatafungwa leo na huenda usafiri ukasitishwa .

AFLEWO NAIROBI 2012

AFLEWO NAIROBI is back, bigger and better by the Grace of God after taking a break last year.

This is our 8th edition and we are ready for an improved process, bigger team and definitely a grand event!

FRIDAY 21st SEPTEMBER, 2012, all roads lead to CITAM KAREN - (NPC KAREN)

From 9pm - 6am for a night of awesome worship and prayer.

This experience is life changing and never the same, you don't want to miss it as we sing praises to our God and declaring HOPE in Africa and the rest of the World.

Africa Lets Worship.


AFLEWO NAIROBI 2012






LAUGH AGAIN CONCERT KING CHAVALA NDANI YA DPC KINONDONI.


BAADA YA KUCHEKA NA KUCHEKA NA KUCHEKA TENA KATIKA MATAMASHA KADHAA YALIYOPITA HAPA TANZANIA,

BAADA YA KUTAMBULISHA CHRISTIAN STAND UP COMEDY NA BAADA YA KUIBUA VIPAJI VINGI YA UCHESHI NA VIPAJI HALISI, SASA KWA AWAMU NYINGINE TENA GREAT POTENTIALS LTD INAKULETEA TAMASHA LINGINE KUBWA LA KIMAPINDUZI YA UCHESHI TANZANIA KATIKA MFULULIZO WAKE.

.......LINALOITWA; LAUGH AGAIN CONCERT...Revolution!!(TAMASHA LA KUCHEKA TENA)
...

NA AWAMU HII
KING CHAVALA PAMOJA NA COMEDIANS KAMA RICHARD CHIDUNDO;GERALD MREMA; SENIOR ABBY; MC PILIPILI PAMOJA NA VIPAJI VIPYA LUKUKI

WATAHUDUMU PAMOJA NA MAKUNDI MUHIMU KAMA GLORIOUS CELEBRATION, THE VOICE PAMOJA 1ST Q DANCERS; PAMOJA NA WAIMBAJI WENGINE MBALIMBALI!!!

NI PALE DPC-KINONDONI
(UKIPANDA MAGARI YA MWANANYAMALA KUPITA MANYANYA KWENDA KIVUKONI AU STESHENI UNASHUKIA KITUO CHA KANISANI)

KUTAKUWA NA KUCHEKA,KUCHEZA,KUIMBA,ZAWADI NA SUPRISE KIBAO...YAANI HII SIO YA KUIKOSA!

TAMASHA HILI NI ZAWADI KWA WASHIKA DAU WOTE WA KWELI, HIVYO......HAKUNA KIINGILIO!!!

KWA MAELEZO ZAIDI PIGA +255 713 883797
AU
www.kingchavala.blogspot.com/www.chavalapf.blogspot.com

www.gospelstandardbase.blogspot.com

Askofu Dk. Kulola ataja makanisa ya shetani nchini

  • Awatahadhirisha mabinti kuwa makini
  •  Aahidi kuwaombea akienda Israel
 Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistical Assemblies of God Tanzania (EAGT) Mwinjilisti Dk. Moses Kulola, amelionya kanisa safi la Kiristo kujitenga na wimbi kubwa la waabudu shetani wanaopenya kwa kasi makanisani wakitumia fedha nyingi kuteka na kumiliki baadhi ya makanisa.

 Kiongozi huyo pia amewataka mabinti kutulia mbele za Bwana na kufanya ubinti wao kuwa wa utukufu wa Mungu ili siku ya mwisho Bwana ajivunie matendo yao mema waliyoyafanya ndani ya changamoto lukuki, kwa kuwa wanawindwa na waabudu shetani hao.

Askofu Mkuu wa (EAGT) Mwinjilisti Dk. Moses Kulola
Askofu Kulola alisema hayo wiki iliyopita katika mahojiano maalum na chanzo cha blog hii kilipomtembelea Chanika, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, alikokwenda kupumzika akisubiri safari ya kwenda Israel wiki ijayo.
 Askofu Kulola alisema kuwa, kanisa limevamiwa na waabudu shetani ambao wengine wamejivika majina makubwa huku wakiendesha ibada zao wenyewe na baba yao ibilisi, badala ya kufuata Bwana Yesu.

 Huku akitaja majina ya makanisa makubwa yenye idadi kubwa ya waumini, lakini yakiendeshwa na makundi ya siri kama Freemasons alisema umefika wakati wa waumini kuwa makini na kusoma Biblia kwa makini huku wakimuomba Roho Mtakatifu awanusuru.

 “Wanangu natoa wito kutoka katika ibada za mashetani, ondokeni huku wala msitazame nyuma, karibu Yesu yuaja atakuta mkimtumikia shetani kwa kukosa maarifa ya kuzipambanua roho zidanganyazo,”alisema Askofu Kulola na kutaja makanisa hayo ambayo majina yake ninayahifadhi kwa sasa.

 Alisema kuwa kuna dini zimeibuka kama uyoga na viongozi wake wakajipatia majina makubwa, huku wakiwa wanapewa kila kitu kutoka katika makundi ya siri na wala sio Wakristo wa kweli.

 Aliitaja miji iliyoboba katika ibada za mashetani kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Shinyanga,  na akawahimiza Wakristo safi waliookoka kuepuka kumeza kila fundisho kwa kuwa, hiki ni kipindi cha kutimia kwa unabii wa Bwana Yesu kuwa siku za mwisho kutakuwepo na makristo wa Uongo watakaofanya ishara na miujiza kiasi cha kudanganya hata wateule.

 “Ukiona kanisa linajenga fundisho lake katika miujiza pekee, badala ya Neno na kuwaongoza watu kwenye toba na kuishi maisha matakatifu, kimbia hilo sio la Mungu. Muujiza wa kwanza unaopaswa kutiliwa mkazo kwa nguvu kubwa ni wenye dhambi kumpokea Yesu na kuwa wafuasi wake. Mimi sipingi miujiza laa hasha! Lakini sio agizo kuu. Agizo kuu ni kuupa ulimwengu uliopotea habari njema za ufame wa Mungu na kuwafundisha kuyashika yote aliyowaamuru na ishara na miujiza itafuatana na waaminio,” alisema Askofu Kulola.


Kisha akageukia wosia kwa mabinti akisema: “ nakutuma leo ukawaambie mabinti wacha Mungu, wasimame imara kwa Kristo, najua kuna changamoto nyingi wanazokutana nazo; lakini bado wanaweza kushinda na zaidi ya kushinda ikiwa watamtegemea Bwana Yesu, ili siku ya hukumu ikiwa watakuwepo watakaosema walishinda, basi Yesu aseme mbona hawa waliweza,” alisema Askofu Kulola.

 Mtumishi huyo ambaye alieleza kwamba yeye hakufanya mambo waliyokuwa wakifanya wenzake enzi zake, aliongeza kwamba, Mungu anaweza kuwatumia ikiwa watasimama na kuwa na msimamo hata ikiwa ni kwa gharama ya kifo.
Alisema vijana wengi wako makanisani, lakini ni kama wanatumiwa na ibilisi kutaka kuwaumiza mabinti kwa maelezo ya kutaka kuwaoa, lakini mwisho wa siku huwageuka na kumwendea mwingine kwa gia hiyo hiyo, huku akichanganua kuwa  ni lazima wawe waangalifu kujua yupi anatoka kwa Bwana na yupi ni tapeli.

 “Kweli nawalilia sana mabinti zangu, namuomba Mungu awape neema ya kushinda majaribu na vishawishi wa watu wenye nia mbaya, nikienda Israeli lazima nitafanya maombi kwaajili yao,” alibainisha mtumishi huyo kwa uchungu.

 Mbali na hilo, Askofu Kulola alieleza kwamba anachukizwa na watu wanaojiita Manabii na Mitume ambao ukiangalia kwa undani utabaini kuwa wako kinyume na Mungu, ingawa machoni pa wanadamu wanaonekana ni watu wenye mapenzi mema.

 “Kumekuwepo na wimbi kubwa la watu wanaoibuka na kujiita manabii na mitume, wamekuwa wakielezea watu namna wanavyoweza kuwasaidia kutoka katika matatizo yao kana kwamba ni waganga wa kienyeji,” alisema mtumishi huyo na kuongeza:

 “Kipindi hiki kama watu hawatokuwa makini ni wazi kuwa watatapeliwa, kila kitu walicho nacho kwa kudhani kuwa wanamtolea Mungu. Ni vema ikiwa wachungaji watawafundisha waumini wao Neno la Mungu kwa ufasaha ili waweze kutofautisha mtumishi wa kweli na tapeli ‘kanjanja.’

 Kama hilo halitoshi mtumishi huyo ambaye yuko kwenye huduma kwa zaidi ya miaka 50 alisema huu ni wakati wa kila mtu kusimama kwa miguu yake mwenyewe, badala ya kutegemea mtu mwingine. Huku akichanganua kwamba Kanisa la Mungu ni lazima liombe kwa bidii ili Mungu alinusuru taifa na majanga mbalimbali ambayo yanaonekana kutaka kubisha hodi hasahasa kwa Nchi ya Tanzania,alisema mtumishi huyo.

Waziri afanyiwa maombi kwasababu ya ugumu wa Wizara.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema ni ngumu kuiongoza wizara hiyo kutokana na kunyemelewa na mafisadi wanaotaka kunufaika na rasilimali zake kwa maslahi yao binafsi.

Simbachawene alitoa kauli hiyo juzi wakati wa ibada maalum ya kumuombea iliyofanywa na Umoja wa Makanisa ya Kikiristo katika Kijiji cha Pwagu, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Akizungumza katika ibada hiyo, Simbachawene alisema kunahitajika nguvu za kupambana ili kuiongoza wizara hiyo kwa kuwa inanyemelewa na mafisadi.


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, mkoani Dodoma, aliteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuunda upya Baraza la Mawaziri Mei 4, mwaka huu, alisema:

“Vita hii inatokana na uongozi mpya ulioingia katika wizara hii kubana mirija ya mafisadi ambao walikuwa wakitumia rasilimali za serikali kwa manufaa yao.”

Simbachawane alisema kutokana na kuwepo kwa vita hiyo, yeye binafsi kama Simbachawene, hawezi kushindana na mafisadi hao, bali anahitaji nguvu ya Mungu katika kupambana na watu hao.

“Vita ndani ya wizara yangu ni kubwa kwa kuwa wafanyabiashara wote wa umeme wanatuona sisi ndiyo wabaya wao kwa kubana mirija ya ulaji, sasa nahitaji zaidi maombi kutoka kwenu nyote ili kuishinda vita hiyo mimi na wenzangu,” alisema.

“Mimi naapa mbele yenu kama watumishi wa Mungu kuwa katika hili, nitamsaidia Mheshimiwa Rais kwa nafasi aliyonipa kwa kuhakikisha kuwa kilio cha wananchi juu ya wizara hiyo kinanyamaza,” alisema Simbachawene anayeshughulikia nishati.

Simbachawene alisema kwa sasa uongozi wa wizara hiyo umeanza kuona mafanikio baada ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kuanza kuongeza kukusanya maduhuli kuliko ilivyokuwa awali kabla ya kuchukuliwa hatua mbalimbali za kuhakikisha mianya yote ya kubana wizi na hujuma inazibwa.

Naibu Waziri huyo alisema kwa sasa Tanesco inakusanya zaidi ya Sh. bilioni 90 kwa mwezi ingawa lengo ni kukusanya Sh. bilioni 200 kwa mwezi.



Awali akisoma risala kwa Naibu Waziri, Mchungaji Abineri Mazuguzwa, alimtaka Simbachawene kumwogopa Mungu ndani ya moyo wake kwa kuwathamini Watanzania katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.

Mchungaji Mazuguzwa alisema Watanzania wengi wanategemea kuwa uongozi wake ndani ya wizara hiyo, utanyamazisha vilio vyao vya kila siku kutokana na wizi unaofanyika katika wizara hiyo.

Zuhura ashambulia Kanisa Asababisha mtafaruku Dar na mikoani, Wachungaji washtushwa na jumbe za hatari

Jumapili iliyopita Wachungaji wengi wa makanisa ya Tanzania Assemblies of God, TAG, jijini Dar es Salaam, na hata wale wa mikoani walishtushwa na jumbe za kutatanisha zilizokuwa zikiandikwa kuomba fedha  huku mwombaji akijifanya mchungaji/muandishi.

Mtu huyo mwenye kuvaa ngozi ya kondoo wakati uhalisia ni ‘mbwa’ mwitu, alivaa uhusika wa mchungaji na kudai mchungaji huyo anaumwa yuko Hospitalini hivyo atumiwe fedha kwa njia ya mtandao.

Miongoni mwa jumbe hizo zilizoelezwa kuwachanganya wachungaji wengi zilisomeka hivi: “Bwana Yesu asifiwe Mch. Sheyo mimi ni Mch.  Paulo Mulokozi, simu yangu ina matatizo kdg upo wapi muda huu nina shida na wewe, naomba unijibu kwa meseji nipo hospitali . Mungu akubariki.”

Baada ya ujumbe huo, ambazo baada ya uchunguzi mdogo ilibainisha zilikuwa zikitumwa kwa simu iliyokuwa na jina la Zuhura Kambangwa, na hata hivyo alituma ujumbe wa pili unaosomeka: “Samahani naomba uniazime elfu 40 nitakuona jioni saa 1 nina mgonjwa amelazwa.”

Uchunguzi wa chanzo cha habari ambacho ni gazeti la
Jibu la Maisha umebaini kuwa, Mtu huyo aliyetumia namba za simu, 0716494277, alijibiwa na Mchungaji Seiko Sheyo wa Kanisa la TAG, Sinza, kuwa hajasajili namba ya tigo hivyo ampatie namba ya Voda.

Akajibu hivi:  “Nitumie kwa namba 0758863991, line yangu wameifungia.”

Hilo lilikuwa moja ya majaribio ya mtu huyo kujipatia fedha bila jasho ambayo aliyafanya kwa wachungaji zaidi ya 30, na watumishi wengine wa gazeti hilo la Jibu la Maisha pamoja na wafanyakazi wa Makao Makuu ya TAG.

Aidha imebainika kuwa akitumia jina la Mhariri wa Gazeti la Jibu la Maisha, Bw. Singo  Mgonja, tapeli huyo aliandika ujumbe kuomba fedha kwa wachungaji kadhaa wa jiji la Dar es Salaam, na mikoani  na akafanikiwa kupata shilingi 30,000 kwa mtu anayejulikana kama Mwangomwango, mkazi wa Mbeya, ambaye bila kudadisi kasoro kadhaa katika ujumbe huo alituma fedha.

Katika jaribio lingine la kipuuzi, Mtu huyo alijaribu pia kumtapeli Mhariri wa mwingine wa Gazeti hilo
 Bw. Mgonja, akijifanya ni Joseph Ongong’a hata hivyo baada ya majibizano marefu ya jumbe za simu Mhariri alimtaka mhusika kutuma mtu achukue fedha taslimu kwa kuwa hana fedha kwenye mtandao na mwisho aliishia kuingia mitini.

Mbali na kufanikiwa kujipatia fedha kidogo zoezi hilo la udanganyifu lilisababisha usumbufu mkubwa kwa Wachungaji waliokuwa wakipokea jumbe hizo.

Kwa mujibu wa Uchunguzi wa gazeti hilo jaribio la kwanza likuwa ni kwa Mhariri wa Habari wa Jibu la Maisha, Ms. Flora Matara, ambaye alitumiwa ujumbe unaosomeka: “Bwana Yesu asifiwe dada Flora, mimi ni Kaka Samweli Thomas simu yangu ina matatizo kidogo, upo wapi muda huu nina shida na wewe, naomba nijibu kwa SMS nipo hospitali. Mungu akubariki. Ujumbe huo kutoka simu namba 0716494277, ujumbe huo ulitumwa Jumapili Septemba 9, saa mbili asubuhi.

Inaelezwa kuwa Mhariri huyo wa habari baada ya kupokea ujumbe huo akiwa karibu na kanisani, alishtuka kwa kuwa Samweli aliyetajwa ni mmoja wa maripota wa gazeti hilo, hata hivyo alipojaribu kumpigia mtumaji hakupokea na badala yake alituma ujumbe akisema atume SMS kwa kuwa yuko wodini kaka yake anaumwa kisha akaomba Sh.35,000.

Akionesha msisitizo aliandika: “Naomba utume ili punguze deni jioni nitakupa ibada njema.”

Ujumbe kama huo ulitumwa kwa kubadilisha majina ya watu na kutumwa kwa Emiliana Kalinga, Grace Luhombo, Joseph Ongong’a, Rehema Abbasi, Laston.

Mwingine aliyejaribiwa katika utapeli huo ni Mchungaji Elingarami Munisi, ambaye alitumiwa ujumbe ukionesha unatoka kwa Mch, Mulokozi wa kuomba shilingi elfu 45,000 kwa madai kuwa anamgonjwa.

Uhalifu huo uliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Urafiki, jijini Dar es Salaam, na kufunguliwa jarida la Uchunguzi namba URP/RB/7227/2012.

Wapelezi wa jeshi hilo wanaendelea kumsaka mhalifu huyo ambaye inadhaniwa kuwa alikusudia kulishambulia kanisa tena siku ya ibada wakati watu wakiwa kanisani kumwabudu Mungu.

Uchunguzi zaidi wa Gazeti hilo umebaini kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la utapeli wa kutumia mitandao ya simu ambapo watu waovu wamekuwa wakitumia simu za mkononi kutapeli watu.

Mbali na kutumia majina ya watu mbali mbali matapeli wamekuwa wakitumia ujanja unaobadilika badilika kujipatia fedha kwa njia isiyo halali, huku wakidanganya watu kuwa watawapatia ajira na kuwaelekeza katika makampuni kadhaa.

Mbali na utapeli huo, kuna utapeli mwingine wa kutumia kadi za ATM, ambapo wenye akaunti hujikuta katika mkanganyo mkubwa baada fedha kuchukuliwa huku kumbukumbu zikionesha kuwa zilitolewa na kadi halali ya mteja.

Katika moja ya matukio mabaya mmoja wa wafanyakazi wa Idara ya Elimu ya Kanisa la TAG, Bw. Thadeus Mbutta, alitapeliwa kiasi cha shilingi 800,000 na katika tukio la kutatanisha kwenye benki moja kubwa ya kibiashara nchini (jina tunalihifadhi kwa sasa).

Uchunguzi wa gazeti hilo ulibaini kuwa wakati Bw. Mbutta akiwa mkoani Lindi kwa shughuli za kikazi, akiwa na kadi yake ya ATM, fedha zake zilichukuliwa katika mashine iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Jambo la kustaajabisha ni kuwa benki wanashikilia madai kuwa kadi iliyotumika ni ya mteja, lakini walipotakiwa kutumia picha za CCTV Camera, zilizopo kwenye mashine hizo kumtambua mhusika walidai kuwa zoezi hilo litachukua muda hadi mwezi mmoja kukamilika.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa utapeli wa kutumia teknolojia umekuwa ukitesa mabenki kadhaa nchini, japo matukio mengi hayatangazwi kutokana na hofu ya kukimbiwa na wateja.

Kipidi cha nyuma wageni kadhaa walikamatwa kwa tuhuma za kutumia mitambo maalumu kuiba fedha za wateja katika mabenki na madai hayo yamesababisha baadhi ya watu kutoa fedha zao katika mabenki na kutumia njia mbadala.


Source : Gazeti la Jibu la Maisha

Kiongozi wa Dini ya Romani apokelewa na maelfu Nchini Beirut

Maelfu ya watu walijipanga foleni siku ya Jumamosi kando kando mwa barabara za mji mkuu wa Lebanon, Beirut katika siku ya pili ya ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedict wa kumi na sita
Umati huo ulipeperusha bendera za lebanon na vatican huku msafara wa magari ya Papa ukielekea katika ikulu ya rais wa nchi hiyo.

Papa alifanya mazungumzo na Michel Suleiman wa lebanon ambaye ndiye rais pekee mkristo katika eneo hilo la mashariki ya kati.

Wakati wa ziara hiyo papa alipongeza ushirikiano na utangamano miongoni mwa wakristo na waislamu nchini lebanon huku akishutumu watu walio na misimamo mikali ya kidini.


Jengo jipya la ibada la kisasa lazinduliwa Zanzibar

Baada ya kuchomwa moto Kwa Kanisa la Elim Pentekoste, na watu wasiojulikana katika maeneo ya Kipange kisiwani Zanzibar, hatimaye jengo la kisasa lililogharimu shilingi milioni 35 limejengwa na kanisa hilo ili watu waweze kumwabudu Bwana.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni visiwani humo, kufuatia kuchomwa moto kwa kanisa hilo, na watu wasiojulikana ingawa inadhaniwa kuwa ni waislamu wenye misimamo mikali.

Akihubiri katika uzinduzi wa jengo hio, lililochukua takriban miaka miwili, Askofu Peter Konki wa kanisa hilo, alisema ni lazima kujenga madhabahu iliyoanguka, huku akibainisha kwamba hakuna ibada yoyote itakayofanyika pasipo madhabahu.

“Jambo la muhimu kabla ya yote ni kujenga madhabahu, huo ndio moyo, kama moyo wa mtu hauko sawa sawa ibada ya nje haitakuwa salama, hata kama una jengo zuri namna gani,” alisema Askofu Konki.
Alisema madhabahu ya moyoni ni chanzo cha ibada zote, hivyo basi kama madhabahu ya moyoni imeanguka ibada yote ya nje itakuwa ni dhaifu na ya kimwili.

Mbali na hilo alisema pamoja na jengo hilo zuri lililogharimu zaidi ya milioni 35, halitakuwa na maana kama madhabahu ya mioyo ya watu imebomoka.
Hata hivyo aliwataka waumini wa kanisa hilo kuendelea mbele katika kumtetea Bwana Yesu na kusimama katika imani ili Mungu aweze kuokoa na injili kuhubiriwa katika kisiwa hicho.

CASFETA kuleta ukombozi kwa vijana.

 Wadhamiria kuikabili Zanzibar kiinjili        
Moja ya mikakati ya Umoja wa wanafunzi Wakristo waliookoka “The Christian Ambassadors Student Fellowship Tanzania,” ni kuhakikisha kuwa wanamkomboa kijana wa kitanzania kutoka utumwani wa ibilisi na kuishi maisha ya kumpendeza Kristo, akiacha kutumikishwa na shetani.

 Hayo yalisemwa hivi karibuni na Rais wa CASFETA Tanzania, Kelvin Ngonyani,  katika mahojiano maalumu na Blog, katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),  City Christian Centre (CCC), lililopo Upanga jijini Dar es Salaam,  kwenye ibada maalumu ya kusifu na kuabudu.


Rais huyo aliongeza kuwa mipango mikubwa waliyo nayo ni kumhubiri Kristo katika hali yoyote, huku akibainisha kuwa, moja ya mikakati waliyonayo ni kuimarisha huduma hiyo katika Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kuwakomboa vijana na watanzania visiwani humo kuacha kumtumikia ibilisi.

“Tuna mikakati mingi sana, lakini mkubwa zaidi ni kuhubiri injili katika kila eneo la nchi hii, lengo ni kumkomboa kijana na mtanzania kuacha kutumikishwa  na shetani, pia  tutahakikisha tunaibadili Tanzania,  kwa upande wa Zanzibar tumeisha anzisha Casfeta,  lakini tunataka tuiboreshe zaidi,  tunamwamini Mungu tutafanikiwa,” alisema Rais huyo.

Mbali na hilo aliweka wazi kwamba mbali na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, bado wamekuwa wakimuona Mungu akiwa upande wao na akiwafanikisha kwa kiwango kisicho cha kawaida, huku akiongeza kuwa moja ya mafanikio hayo ni kuongezeka kwa wana CASFETA kutokana na makongamano kadhaa ambayo wamekuwa wakiyafanya mashuleni ambapo  hutumia fursa hiyo kuihubiri injili na vijana wengi kumrudia Kristo.



Chanzo cha Blog kilipata fursa ya kuzungumza na Mchungaji msaidizi wa Kanisa la City Christian Centre Upanga, Deus Cheyo, aliye hudhuria ibada hiyo, ambapo alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakipotea kutokana na kukua kwa Teknolojia, hivyo kujifunza mambo yasiyofaa, na kupelekea maadili kushuka.
Katika hilo, Mtumishi huyo wa Mungu akawataka wazazi kuwapa elimu na mafunzo ya msingi wa Biblia watoto wao jinsi dunia ilivyo kwa sasa, ili kukinusuru kizazi hiki ambacho shetani anakitafuta kwa kasi ya ajabu akiangamize.

 Aliwataka  watumishi wa Mungu kuwa na ibada za vijana makanisani kwa lengo la kufundishwa Neno na jinsi ya kukabiliana na changamoto za dunia.

Mchungaji huyo ambaye pia alipata nafasi ya kutoa Neno katika ibada hiyo, aliwataka mamia ya wana CASFETA kulijua Neno la Mungu kikamilifu na kulitenda huku akiwaambia kuwa silaha kuu ya kuangusha ngome ni kujikita zaidi katika maombi na kuwa na imani dhabiti.


Mwenyekiti wa Casfeta katika Mkoa wa Dar es Salaam, Samuel Nshatsi, alisema kuwa lengo la kukutana katika ibada hiyo ni kumsifu Mungu na kumwabudu ikiwa ni pamoja na kumlilia awanusuru vijana ambao bado wanazidi kutumikishwa na shetani.

Mbali na hilo, alisema kuwa moja ya malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanatekeleza  kauli mbiu yao ya Mpango Mkakati, Mpango Shughuli na Mpango Kazi, kama dira ya vipaumbele ndani ya mwaka huu katika kumtumikia Mungu na kuhakikisha mabadiliko yanapatikana kwa viwango vya juu.

Aidha hakusita kutoa wito kwa vijana wa Tanzania, ambapo aliwataka wamkimblie Kristo na kuachana na dunia na kusemakuwa hali hivi sasa ni mbaya,  huku akibainisha kuwa shetani yuko kazini akimuwinda kijana. 

The Holy Base Guitar Concert




MUUJIZA KAMA WA PAUL NA SILA….. Mch. aliyesubiri kunyongwa huru

•    Alichagua kifo kuliko kumkana Yesu
•    Watu Milioni tatu walimlilia Mungu


“Siwezi kumkana Yesu Kristo, siwezi kuikana imani yangu, sikuwahi kuwa Muislamu, sina ninachoweza kukana..kama ni kufa nipo tayari. Mtaua mwili lakini roho yangu itakuwa kwa Baba mbinguni.”

Hayo ni baadhi ya maelezo ya kijasiri yaliyotolewa na Mchungaji Youcef Nadarkhani (32) wa Iran mbele ya jopo la makadhi waliokuwa wakimpa nafasi ya mwisho ya kumkana Bwana Yesu Kristo aachiwe huru au kuendelea na msimamo wake anyongwe.

Wakati Mchungaji huyo akiwa katika wakati mgumu wa kusubiri kifo cha taabu, huko nje ya nondo za jela watu wenye huruma zaidi ya milioni tatu walikuwa wakisugua magoti chini kumuombea rufaa katika mahakama ya haki (mbinguni) na mataifa yenye nguvu yakipaza sauti juu kushinikiza aachiwe huru.

Mchungaji Youcef Nadarkhani wa Iran
Hatimaye Septemba nane mwaka huu, majibu ya maombi hayo yakadhihirika kwenye macho na masikio ya wanadamu pale tangazo la kuachiwa huru kwa Mchungaji huyo lilipotolewa, na kweli akaachiwa huru na kupokelewa na umati wa wale waliokuwa wakiingoja siku ya Bwana ya kunyoosha mkono wake amuokoe.

Wakati wote ambao Mchungaji Nadarkhani, alikuwa akisubiri kunyongwa alikwisha kata rufaa, katika mahakama ya juu zaidi, lakini akapata pigo kubwa wakati wakili aliyekuwa akimtetea alipokamtwa na kupelekwa mahakamani na haraka haraka akahukumiwa kifungo cha miaka tisa gerezani kwa kosa la kueneza propaganda wakati wa kutetea Wakristo.

Pamoja na wakili kufungwa, tumaini la kupona likiwa limepotea kabisa, muujiza ulidhihirika wiki iliyopita baada ya Jaji wa mahakama kuingia mahakamani na kupitia rufaa hiyo kisha kutoa hukumu kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo mchungaji huyo yalikuwa kinyume cha sheria za taifa hilo.

Jaji katika hukumu yake hiyo alidai kuwa Mchungaji Nadarkhani hakustahili kutiwa hatiani kwa makosa ya kuuasi uislamu na kujiunga na Ukristo, kosa ambalo adhabu yake ni kifo, bali alistahili kushtakiwa kwa kosa la kuhubiri Injili kwa Waislamu. Kosa hili adhabu yake  ni kufungwa jela miaka mitatu.



Jaji huyo ambaye jina lake halijatajwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama, alimhukumu adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na kisha kuamuru aachiwe huru kwa kuwa tayari ameshatumikia kifungo hicho wakati akisubiri kusikilizwa kwa rufaa au amri ya kiongozi wa kidini Ayatollah Ali Khamenei ili anyongwe.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka katika mahakama hiyo, kuachiwa kwa Mchungaji huyo shujaa wa imani ni muujiza tu kwa kuwa mazingira ya kesi na hata kukosekana kwa wakili wa kumuwakilisha kwenye rufaa vilitosha kumfanya ashindwe kama sio Mungu kuingilia kati.

Mashuhuda wanasema kuwa ushindi huo wa watu wa Mungu waliosugua magoti kuomba, wakiishi kwa imani ni kama ilivyokuwa kwa  akina Daniel, Meshacki na Abednego katika nyakati za Biblia walipokuwa mikononi mwa wauaji kwa mashtaka ya kugoma kusujudia sana.
Kwa zaidi ya matoleo saba, Gazeti la Jibu la Maisha, limekuwa likifuatilia habari za Mchungaji Nadarkhani kwa kina hatua kwa hatua, hadi kuachiwa kwake.

Inaelezwa kuwa tangu kukamatwa kwake mwaka 2009 na kutupwa gerezani yamefanyika majaribio kadhaa ya kutaka amkane Yesu ili aachiwe huru, lakini alikataa na kuchagua kifo badala ya uislamu.

Msemaji wa Kituo cha Sheria na Haki cha Marekani (ACLJ), shirika ambalo lilisaidia kumtetea Mchungaji Nadarkhani, Bw.  Jordan Sekulow alisema, shitaka kubwa lililopelekwa mahakamani dhidi ya mtumishi huyo ni kukataa kukana imani yake ya kikristo.

"Leo Mchungaji ameachiwa huru na anaungana na familia yake, lakini lazima tujue kwamba tukio hilo la Mtumishi huyu ni mfano kwamba dunia inaweza kuungana kuleta uhuru wa kuabudu na haki kwa kila mmoja,” alisema Sekulow.

Kiongozi mwingine wa ACLJ aliyezungumzia kuachiwa huru kwa mchungaji huyo ni, Bw. Tiffany Barrans, aliyeliambia Fox News.com kuwa:
“Wakati tunaendelea kumsifu Mungu kwa mambo makubwa aliyoyafanya,  kumtoa Mchungaji Nadarkhani, mikononi mwa ‘wafilisti’ lazima Iran itambue wajibu wake na kuwapa watu uhuru wa kuabudu bila kutengeneza mbinu za kutishana.”

Kisha akaongeza:  “Tunashukuru Mungu kwamba kwa namna moja au nyingine muungano wa watu zaidi ya Mil. 3 duniani kote kutoa maoni yao kumtetea Mchungaji Nadarkhani, kupitia mitandao ya Twitter, Facebook na mingine, imesaidia kuachiwa huru na pia maombi ya watu wa Mungu.”

Baada ya kushtakiwa kwa kosa la kukataa kumkana Kristo na kuwekwa kizuizini kwa takriban miaka mitatu, bado aliendelea kusumbuliwa akiwa gerezani ili amkane Bwana Yesu, lakini aliendelea kukataa hadi Desemba mwaka jana ambapo alikuwa ikisubiriwa Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mwenye mamlaka kubwa katika masuala ya kiroho nchini Iran aamue moja kumwachia huru au kumnyonga.

Hata hivyo kwenye magereza ya taifa hilo la kiislam bado kuna mamia ya watu waliofungwa kwa kuonewa na wengine kwa sababu za kutetea imani yao.

‘Udini, ukabila ni hatari katika taifa’

Imeelezwa kuwa moja ya vitu hatari katika taifa lolote duniani vinavyoweza kuleta matatizo makubwa na mgawanyiko katika nchi, ni pale udini, ukabila na ubaguzi unapopewa nafasi kubwa pasipo kujua na kutambua madhara yake.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Bw. Rajabu Juma jijini Dar es Salaam katika ofisi za msajili nchini.

Msajili huyo alibainisha kuwa kumekuwa na vuguvugu la udini, hivyo kuvitaka vyama vya siasa nchini kuepuka kujiingiza katika ubaguzi wa kidini na ukabila, huku akivitaka vyama vya siasa kuendesha siasa safi na zisizo na ubaguzi wa aina yoyote kwa maslahi ya taifa.


Aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi  ya aman, ina utulivu pale wanasiasa watakapoendesha siasa zisizo na uchochezi wa aina yoyote pamoja na  kuepuka ubaguzi wa kikabila na udini huku wakimhusisha Mungu katika siasa zao, kwa lengo la kuleta maendeleo na mabadiliko katika taifa.

“Nchi yetu itazidi kuwa ya amani na utulivu kama wanasiasa watatambua wajibu wao, na si kuleta mgawanyiko katika taifa na kuendesha siasa chafu, hata vyama ambavyo vimepata usajili hivi karibuni viweze kufikia malengo yao vinatakiwa kutambua wajibu wao ili kufikia mafanikio,” alisema.

Hata hivyo hakusita kuvitaka vyama vipya vilivyosajiliwa karibuni kufuata sheria kanuni na taratibu za nchi, ikiwa ni pamoja na kutii sheria ya vyama vya siasa,  kwa lengo la kuepuka usumbufu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza endapo watashindwa kutekeleza yale yanayotakiwa kutekelezwa.

Alizungumzia mfano Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepata usajili wao kudumu hivi mara baada ya kutimiza masharti yote yanayotakiwa kutimizwa na chama chochote ili kupata usajili wa kudumu, ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kupata wanachama wa kutosha katika mikoa kumi nchini, ambapo kilipata zaidi ya watu 200, kila mkoa hivyo kuwa na sifa ya kupata usajili wa kudumu.

Saidi Miraji ni Mwenyekiti wa chama hicho kipya, ambapo mara baada ya usajili huo alipata nafasi ya kuzungumza na kusema kuwa chama chake kitakuwa tayari kufuata kanuni taratibu na sheria za nchi, huku akisisitiza kuwa hawatakuwa tayari kuendesha siasa za kuivuruga nchi bali kuleta mabadiliko katika taifa la Tanzania.
“Naamini kwamba kwa msaada wa Mungu tutayatekeleza yote ambayo tumeambiwa na msajili, chama hiki hakitakuwa na udini,ukabila wala  ubaguzi wa aina yoyote, kitakuwa na lengo moja la kuhakikisha kinaleta mabadiliko kwa taifa zima la Tanzania,” alisema Mwenyekiti huyo.

Pastor Adam Haji ndani ya VCC New Tabernacle

Mchungaji Adam Haji anahudumu Semina ya Neno la Mungu  iliyoanza Jumapili ya juzi mpaka Jumapili kwa mda wa wiki nzima ndani VCC New Tarbenacle Mbezi Beach.

Semina hiyo itakuwa inaanza saa 10:00 mpaka Saa 1:00 jioni.

Nyote mnakaribishwa,Mtabarikiwa!

 
Mchungaji Kiongozi wa VCC  Rev Dr Huruma Nkone

Pastor Adam Haji ndani ya VCC New Tabernacle
Watu walipata mda wa kumsifuu na kumtukuza  Mungu sana

Siku ya Jana Victor Aron alikuwepo kuhudumu  ndani ya VCC New Tabernacle


Watu wanajitokeza kwa wingi kuhudhulia semina hiyo.



Mchungaji Adam Haji na Mke wake


Watu walipata mda wa kuomba,kuombewa pia kufunguliwa mapepo na nguvu za giza kuwatoka.






Mchungaji Kiongozi wa VCC  Rev .Dr Huruma Nkone akimhudumia dada aliyeonekana kufungwa na nguvu za giza.

Pia Ufundishaji wa mifano ndio ulio tawala kwa sana kwa makusudi ya kueleweka zaidi.

Nguvu za Mungu zilidhihilika kupitia Mtumishi wake Adam Haji katika Semina hiyo,watu kufunguliwa nguvu za giza na mapemo kuwatoka.