Makanisa matatu yavamiwa Kilimanjaro

Watu wasiojulikana wamevamia makanisa matatu mkoani Kilimanjaro na kuvunja milango, kuharibu mali mbalimbali zikiwemo kompyuta na samani za kanisa na kuiba fedha.

Tukio hilo limetokea katika jimbo la Kilimanjaro Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Winford Mosha, alisema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana.

Mosha aliyataja makanisa yaliyovunjwa kuwa ni usharika wa Kimbowo, Mseroe  na Mrienyi na kwamba watu hao walivunja kwa lengo la kutafuta fedha.

Mchungaji Mosha, alisema katika usharika wa Mseroe watu hao waliiba shilingi laki mbili na katika sharika nyingine waliharibu mali za kanisa na kuondoka baada ya kukosa vitu vya kuiba.

Hata hivyo, Mosha alisema tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya wizi yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi huu katika jimbo hilo ambapo makanisa mengine matatu yalivunjwa na mali zake kuharibiwa vibaya.

Aliongeza kuwa makanisa ambayo yaliyovunjwa ni Msae, Kiruweni na Ashira, hata hivyo katika matukio hayo, pia wezi hao walifanya  uharibifu wa mali mbalimbali za makanisa na kuiba fedha.

Kufuatia tukio hilo, mchungaji huyo aliwataka wakristo pamoja na wachungaji kusimama imara katika maombi ili kuimarisha ulinzi katika maeneo ya makanisa katika kipindi hiki cha sikukuu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema watu hao waliovunja makanisa hayo walikuwa na lengo la kuiba na si vinginevyo.

Maaskofu waijia juu Serikali

Wakristo wamesema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeshindwa kuwasaidia ili waishi kwa amani na utulivu katika nchi yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu, wakati akisoma tamko la Maaskofu wa madhehebu ya Kikristo Tanzania katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa lililopo eneo la Jamatini.
Katika tamko hilo alilolisoma kwa niaba ya Maaskofu wote, Kinyunyu alisema kuwa umefika wakati ambao Wakristo wamechoka na vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya waumini wa dini zingine.

“Tatizo ni kuwa Serikali inashindwa kuchukua hatua mapema, makanisa yanachomwa, migogoro inazidi, lakini hakuna hatua zozote ambazo Serikali inachukua katika kunusuru hali hiyo, tumechoka,” alisema.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu 
“ Serikali imeshindwa kuchukua hatua kwa muda mwafaka kwa kila jambo ambalo linatokea kwa Wakristo na hata inapoonyesha kuwa imechukua hatua haionyeshi sana kujali juu ya yale wanayofanyiwa Wakristo. Askofu huyo alisema kuwa matokeo yanayotokea Zanzibar mathalan, Wakristo wanaoishi huko yamewasababishia hofu hivyo wengi kuanza kuvikimbia visiwa hivyo na kukimbilia Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Askofu Kinyunyu, suala la uchomaji wa makanisa hadi sasa limeshindwa kupatiwa ufumbuzi na kila kukicha bado makanisa yanaendelea kuchomwa moto akahoji Serikali kukaa kimya maana yake nini.
Aidha, tamko hilo limeitaka Serikali kuweka utaratibu mzuri na ufafanuzi wa kina kuhusu uchinjaji wa nyama ambao umekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini. “Hapa litolewe tamko kila mtu kwa imani yake achinje mwenyewe siyo kuanza kulaumiana au kumpa haki mmoja akachinja na mwingine akaachwa. Tunaomba sana ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo ili kuondoa mgogoro baina yetu na wenzetu.”
wamekuwa wakifanyiwa, lakini akasisitiza kuwa wanatakiwa kupigana kwa maombi na ndiyo silaha kubwa ya ushindi.

Katika hatua nyingine, wakati Wakristo wakiwa na hofu ya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka watu wasiofahamika wamevamia makanisa matatu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini na kuvunja ofisi za wachungaji na wainjilisti.

Watu 40 wahofiwa kufukiwa baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Dar

Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.

Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50 ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.

Source.mwananchi

Kwaya ya Ambassadors of Christ kutua leo Dar es salaam

Kundi la muziki wa kiroho la Ambassadors of Christ ‘Kwetu Pazuri’ la Kigali, Rwanda linatarajia kutua Dar es Salaam leo kwa ajili ya Tamasha la Pasaka kesho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa kundi hilo pamoja na mambo mengine litazindua albamu yao iitwayo Kaeni Macho katika tamasha hilo litakalofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Tayari mambo yetu yanaenda vizuri na Kwetu Pazuri watawasili Jumamosi wakiwa wamepania kufanya mambo makubwa kwenye tamasha letu,” alisema Msama na kuzitaja nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo kuwa ni Kaeni Macho, Mungu Wangu, Tugireurukundo, Ewe Ndugu, Tuombeane, Umwamini Yesu, Msalaba, Twawona, Okuswala na Huruma.

Alisema kundi hilo limefurahi sana kuja hapa Tanzania na ndiyo sababu wakaipa heshima Tanzania kuzindua albamu yao wakiwa na imani mashabiki wataipenda na kwamba hivi sasa wanatamba na albamu ya Mtegemee Yesu na wamemhakikishia watang’arisha tamasha la mwaka huu.

Alibamu yao hiyo ina nyimbo nane ambazo ni JY’ Ushima Uwite, Mtegemee Yesu, Ndifuza Kugerayo, Iyana Iby’ Isi, Yesu Niwe Mungeri, Parapanda, Abasaruzi na Nenda.

Licha ya kundi hilo, wasanii wengine wa nje ya Tanzania watakaotumbuiza tamasha hilo ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.

Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone,  Bonny Mwaitege, Upendo Kilahiro, John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam kesho na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Gosple Festival in South Afrika


TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU SIKUKUU YA PASAKA

KATIKA KUELEKEA SIKUKUU YA PASAKA, INAYOTARAJIWA KUWAADHIMISHWA KUANZIA TAREHE 29 MACHI  HADI  TAREHE 1 APRILI, 2013.  JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI WOTE KUWA LIMEJIPANGA KIKAMILIFU KATIKA KUIMARISHA USALAMA WA RAIA NA MALI ZAO KWA KIPINDI CHOTE CHA SIKUKUU NA BAADA YA SIKUKUU, HIVYO WANANCHI WASHEREKEA SIKUKUU  KWA AMANI  NA UTULIVU, PASIPO VITENDO AMA VIASHIRIA VYOVYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI.

2. IKUMBUKWE KUWA, WANANCHI WENYE IMANI YA KIKRISTO NA HATA MADHEHEBU MENGINE HUTUMIA MUDA HUO KWENDA KUABUDU PAMOJA NA MUENDELEZO WA SHEREHE HIZO KWENYE MAENEO MBALIMBALI YA STAREHE. UZOEFU UNAONYESHA KUWA BAADHI YA WATU HUTUMIA KIPINDI HICHO CHA SIKUKUU KUFANYA MATUKIO YA UHALIFU KUTOKANA NA MIKUSANYIKO HIYO YA WATU KATIKA MAENEO MBALIMBALI.

3.JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI NA WAUMINI  WOTE KUWA,  ULINZI UMEIMARISHWA KWENYE MAENEO YOTE YA KUABUDIA, FUKWE ZA BAHARI, SEHEMU ZA STAREHE NA MAENEO MENGINE YOTE AMBAYO YATAKUWA NA MIKUSANYIKO MIKUBWA YA WATU.AIDHA, TUNAPENDA KUWATAHADHARISHA WALE WOTE AMBAO WATAKUWA WAKITUMIA BARABARA, KUWA MAKINI KWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI NA HASA KWA MADEREVA KUEPUKA KWENDA MWENDO KASI NA KUTUMIA VILEVI WAWAPO KAZINI.

4 VILEVILE, JESHI LA POLISI LINAWATAKA WANANCHI KUONDOA HOFU NA KUWAPUUZA  WATU WACHACHE AMA KIKUNDI CHA WATU WANAOTUMIA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU KUWATIA HOFU KWA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WATU MBALIMBALI KWA LENGO LA KUVURUGA AMANI NA UTULIVU KATIKA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU. KITENDO HICHO CHA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WANANCHI NI UHALIFU KAMA UHALIFU MWINGINE NA WAKIBAINIKA HATUA ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA DHIDI YAO.

5. KATIKA KUHAKIKISHA USALAMA KWENYE KUMBI ZA STAREHE, WAMILIKI WA KUMBI HIZO WAZINGATIE UHALALI NA MATUMIZI YA KUMBI ZAO KATIKA UINGIZAJI WA WATU KULINGANA NA UWEZO WA KUMBI HIZO, BADALA YA KUENDEKEZA TAMAA YA FEDHA KWA KUJAZA WATU KUPITA KIASI. VILEVILE, WAZAZI WAWE MAKINI NA WATOTO WAO NA HASA DISKO TOTO, ILI KUEPUKA AJALI NA MATUKIO MENGINE YANAYOWEZA KUSABABISHA MADHARA JUU YAO.

6. JESHI LA POLISI LINATOA TAHADHARI KWA WANANCHI WOTE KWAMBA, WATOKAPO KWENYE MAKAZI YAO WASIACHE NYUMBA WAZI AMA BILA MTU NA WATOE TAARIFA KWA MAJIRANI ZAO, NA PALE WANAPOWATILIA MASHAKA WATU WASIOWAFAHAMU WASIKAE KIMYA BALI WATOE TAARIFA KWA JESHI LA POLISI AU VIONGOZI WAO WA SERIKALI YA MTAA, SHEHIA, KIJIJI AU KITONGOJI ILI HATUA ZA HARAKA ZIWEZE KUCHUKULIWA.

7. MWISHO, NAPENDA KUWAHAKIKISHIA WANANCHI KWAMBA, JESHI LA POLISI LINATEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KUZINGATIA SHERIA ZA NCHI NA HIVYO HALITAWAJIBIKA KUMWONEA HURUMA AMA UPENDELEO MTU YEYOTE ATAKAYEENDA KINYUME NA SHERIA ZA NCHI.

NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE PASAKA NJEMA.
   
        

      IMETOLEWA NA:
      ADVERA SENSO

MSEMAJI WA JESHI LA POLISI

Askofu Kulola ampa tuzo ya heshima Alex Msama

Kanisa la EAGT hivi karibuni lilimtunuku tuzo Mkurugenzi wa makampuni ya Msama Promotions kwa kutambua mchango wake katika uchangiaji wa maendeleo ya jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhi  tuzo hiyo, juzi Askofu Philemon Phiri wa jimbo la Mikocheni akimwakilisha Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola alisema tuzo hiyo kwa Msama ni utambuzi wa anayoyafanya katika kusaidia jamii.

Askofu Phiri alitumia fursa hiyo kumpongeza Msama kwa  uandaaji wake bora wa matamasha ya Pasaka na kueleza kuwa Mungu amempa ufunuo ambao ni endelevu, naye Msama alishukuru tuzo hiyo na kueleza kwamba tamasha la Pasaka litaendelea kila leo tena kimataifa zaidi hadi duniani.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola
Katika hatua nyingine mwimbaji nguli wa muziki wa Injili wa Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi nchini Kenya, amesema atatumia tamasha la pasaka kutambulisha wimbo wake  wa Kiti Chako uliopo kwenye albamu yake mpya ya Sifa za Mungu.

Akizungumza na Pata Habari, baada ya kuwasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria tamasha la pasaka linalotarajiwa kufanyika Jumapili hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam alisema, atautambulisha wimbo huo ambao una ujumbe mzito wa neno la Mungu.

Kwa mujibu wa Solomoni Mukubwa albamu yake hiyo ni zaidi ya nyingine alizowahi kurekodi hii kwa sababu ameimba ushuhuda wa maisha yake  baada ya kupata matatizo ya kukatwa  mkono  wake.
“Nashukuru  kupata  tena  nafasi  ya kuwa mmoja wa waimbaji kwenye tamasha la mwaka huu, nimejiandaa vya kutosha mashabiki wafike kwa wingi kupata ujumbe mzito wa neno la Mungu pia nitatambulisha wimbo wangu mpya siku hiyo” alisema Mkukubwa.

Alisema albamu yake hiyo inanyimbo saba, ambazo ni Kiti chako, Shukrani ya punda, Nitaishi wakitazama, Habari njema, raha yangu, sijafika, Sifa za mungu, Nimewasamehe wote.

Kwa upande wa Faraja Ntaboba, alisema kauli mbiu ya tamasha la pasaka la mwaka huu inayosema kuwa ‘Amani na Upendo’ imempa moyo sana,  inagusa Afrika nzima kwa kuwa  kuna watu wanalia  kwa kupoteza  amani.

Aidha  mwimbaji  huyo  alitoa  wito  kwa  mashabiki  wa tamasha hilo linalotarajia kufanyika mikoa mitano, kuwa wasisherehekea tu bali waje wakijua amani inatafutwa,  aliahidi kufanya mambo makubwa siku ya Jumapili.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 Uwanja wa Samora mkoani Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Source:Fullshangwe

Pengo: Polisi nchini wanafuga uhalifu

 Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku akisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”

Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.

“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na kuongeza:

“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”

Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”


Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la amani.”

Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.

Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.

“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.

“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.

Polisi wanena

Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.

Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.

Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Mwanakwerekwe.

Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.

Source:Mwananchi

Waimbaji wa Muziki wa Injili kutoka Nchi jirani kwa ajili ya Tamasha la Pasaka waanza kuingia Nchini


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Solomon Mukubwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi yake katika tamasha la Pasaka 2013.


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba akiimba kwa hisia moja ya nyimbo zake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu Tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.

Mapato ya Tamasha la Pasaka kujenga kituo cha yatima Dar

Waratibu wa tamasha la Pasaka litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam hapo Machi 31, wamepanga kautumia sehemu ya mapato ya kiingilio kujenga kituo cha watoto yatima kama ishara ya shukrani kwa jamii.Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamatimaalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, alisema kituo hicho kitakachokuwa chini ya kampuni ya
Msama Promotions kitajengwa eneo la Pugu.Alisema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuwapa faraja watoto yatima ambao nao wana haki ya kupatiwa matunzo na mahitaji muhimu katika makuzi yao ikiwemo elimu katika kujenga taifa bora la kesho.
 
 Mwenyekiti wa Maandalizi ya Tamasha la Pasaka Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu maandalizi ya tamasha hilo lenye kauli
mbiu ya Amani na Upendo. Kulia ni Mdau wa muziki wa Injili, Mcharo Mrutu.
“Tangu kuasisiwa kwa tamasha la Pasaka mwaka 2000, tumekuwa tukirejesha sehemu ya mapato ya viingilio kwa jamii kwa njia ya misaada kwa yatima, wajane na walemavu, lakini safari hii tumeona twende zaidi ya hapo kwa kujenga kituo cha watoto,” alisema.Alisema lengo ni kujenga kituo hicho cha kisasa ambapo kama mipango itakwenda vizuri, kitakamilika kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwani wangependa ndiye akizindue kwa kutambua mchango wake kwa tamasha hilo.
 
“Mwaka 2011, Rais Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi wa tamasha letu pale Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.“Kitendo cha Rais kuacha kazi nyingi na kuja kutuunga mkono kwenye shughuli hii ya kiroho, kwetu ni jambo kubwa sana ambalo kamwe hatutalisahau, hivyo tumeona tumpe heshima hiyo ya kuzindua kituo hicho akiwa bado madarakani,” alisisitiza.
 
 
 Msama ametoa wito kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.Kuhusu waimbaji, Msama alisema wale wa nje wataanza kuwasili wiki hii na kuongeza kuwa hadi kufikia Ijumaa, waimbaji wote  watakuwa wamefika tayari kwa tukio hilo mbalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka nchini Kenya.Baada ya kishindo cha tamasha hilokutikisa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma,

Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi kuhimishwa mkoani Mara.

Waziri Mkuu alipokutana na Papa Francis I mjini Vatican




Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akisalimiana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki  Duniani, Papa Francis 1  , Vatican City
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda na Mkewe Tunu wakisalimiana na Kiongozi  wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis 1 ,Vatican City

Askofu wa EAGT apotea, hofu yatanda

Askofu wa Kanisa la Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT) anayeishi mjini Makambako katika Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, Lomanus Lukosi (60), amepotea katika mazingira ambayo yamezua utata kutoka kwa wananchi wakiwamo waumini wa kanisa hilo.

Tukio hilo limetokea wakati ambao kuna hofu juu ya usalama wa viongozi wa dini kufuatia matukio ya kushambuliwa kwao na wengine kuuawa Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo chanzo cha habari hii kimezipata kutoka Makambako na kuthibitishwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo, askofu huyo ambaye anasimamia makanisa hayo yaliyopo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alipotea tangu Alhamisi wiki iliyopita.
Askofu Mkuu Msaafu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Moses Kulola, alipotafutwa na chanzo cha habari hii jana kuelezea tukio hilo, simu yake ilipokelewa na mtu ambaye alikataa kumpelekea huku akisema kuwa askofu huyo hawezi kuzungumzia suala hilo.

“Suala la kupotea askofu wa Makambako Askafo Mkuu hawezi kulizungumzia kwa sababu yeye yupo Dar es Salaam na tukio limetokea Makambako,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Nganyani, alipoulizwa, alithibitishwa kuwapo kwa taarifa za kupotea kwa Askofu Lukosi ambazo alisema ziliripotiwa katika kituo cha polisi Makambako.

Kamanda Ngonyani alisema kuwa Alhamisi iliyopita, askofu huyo aliondoka nyumbani kwake akiwa peke yake bila kuwasiliana na familia yake mahali alipokuwa anakwenda.

Alisema pamoja na kutokumuaga yeyote, mke wake hakuwa na wasiwasi kwa sababu alifahamu huenda alikwenda kanisani kusali.

Kamanda hiyo aliongeza kuwa mke wa askofu huyo alianza kupata wasiwasi baada ya mumewe kutorejea nyumbani siku hiyo na ndipo alipokwenda kutoa taarifa polisi.

Kamanda Ngonyani alisema baadaye uchunguzi ulipoanza kufanywa na polisi, mmoja wa waumini wa kanisa hilo alitoa taarifa kuwa amepigiwa simu na askofu huyo kuwa yupo katika maombi ya kufunga kwa ajili ya kuliombea kanisa hilo.

Alisema juzi (Jumamosi), askofu huyo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno mke wake akimweleza kuwa asiwe na wasiwasi kuna sehemu amejificha kwa ajili ya maombi.

Kamanda Ngonyani alisema kutokana na utata huo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wataalam wa simu za mkononi ili kufahamu alikojificha askofu huyo.

“Tumejaribu kumpigia simu, lakini hadi jana askofu huyo simu yake ilikuwa haipatikani, kwa hiyo tunasaidiana na wataalam wa simu kujua aliko,” alisema Kamanda Ngonyani.

Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linaamini kuwa askofu Lukosi hajapotea bali amejificha sehemu anayoijua yeye kwa ajili ya maombi na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika.

Hivi karibuni, yalitokea matukio ya kushambuliwa kwa viongozi kadhaa wa dini.

Moja ya matukio hayo ni kuuawa kwa kupigwa risasi Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Minara Miwili, visiwani Zanzibar.

Mbali na Padri Mushi, viongozi wengine wa dini waliouawa ni Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Mathayo Kachila, mkoani Geita na Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, eneo la Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Sheikh Ali Khamis Ali.

Wapo pia waliojeruhiwa akiwamo Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar, aliyejeruhiwa kwa risasi na Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Mbali na mashambulizi hayo dhidi ya viongozi wa dini, makanisa zaidi ya 25 yamekwisha kuchomwa moto katika kipindi cha mwaka mmoja nchini kote.

 Source: Nipashe

Kardinali Pengo aleta salamu kutoka kwa Papa Francis I


Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameleta ujumbe wa salamu za Papa Francis, ambaye amewataka waumini wake kuukataa ubaguzi wa kidini.

Akizungumza kwenye Ibada ya Matawi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la St Joseph Visiwani Zanzibar jana, Kardinali Pengo alisema Papa Francis amehimiza umoja miongoni mwa wafuasi wa dini zote.

Papa Francis, ambaye ni raia wa Argentina alichaguliwa kuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, Machi 13, mwaka huu akichukua nafasi ya Papa Benedict wa 16 aliyestaafu.



Pengo alisema kuwa ujumbe huo unawagusa Watanzania kwani katika siku za karibuni kumeibuka watu ambao wanadai kuwa wanapigania imani na kwamba wanafanya hivyo kwa kuua watu wengine kinyume na mapenzi ya Mungu.

Alisema vitabu vyote vya dini vinaelekeza kuwa Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake, hivyo kitendo cha mwingine kumuua mwenzake kwa kisingizio cha kutetea imani ya dini ni kufuru.

“Wakristo hatuwezi kuinua upanga kuua mtu eti kwa kisingizio kuwa tunatetea Kanisa la Mungu,” alisema Kardinali Pengo, ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa Papa mpya uliofanyika Vatican City.

Kumekuwa na matukio ya viongozi wa dini kushambuliwa katika siku za karibuni hasa Visiwani Zanzibar, akiwamo Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki ambaye aliuawa.

Katika tukio lingine Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindikali wakati Padri Ambros Mkenda pia wa Kanisa Katoliki alishambuliwa kwa risasi.

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alisema uharibifu wa mazingira umeathiri uoto wa asili na ndiyo maana hivi sasa Zanzibar visima ambavyo awali vilikuwa vinatoa majisafi ya kunywa, sasa vinatoa maji yenye chumvi

Askofu mpya wa Kanisa la Anglikan duniani atawazwa.

Justin Welby, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikan duniani
Askofu Mkuu Justin Welby ametawazwa rasmi kuwa Askofu Mkuu ,Kiongozi huyu wa umri wa miaka 57 ameapishwa rasmi kuwa mkuu wa Kanisa hilo na kiongozi wa kiroho wa jamii ya waumini millioni 77 wa kianglikana duniani.

Katika ibada yake ya kwanza alisema kuna kila sababu ya kuwa na matumaini mema kuhusu mustakbali wa imani ya kikristo katika dunia yetu

"Kuna kila sababu ya kuwa na uhakika wa kuendelea kwa imani ya kikiristo hapa duniani na nchini mwetu."

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na mrithi wa kifalme ni miongoni mwa wageni elfu mbili walioalikwa katika kanisa kuu la Canterbury.

Askofu Mkuu Welby aliwaambia : "changamoto zinazotukabili sasa za mazingira,uchumi maendeleo ya mwanaadamu na umasikini duniani ,zinaweza tu kukabiliwa na ushujaa kamambe uliokombolewa na ukristo.

Kwa mujibu wa utamaduni askofu alibisha mara tatu kabla ya kuingia ndani ya kanisa kuu. Alikiri kwamba watu huenda wakatofautiana kuhusu majukumu ya dola na mtu binafsi katika jamii yenye ufanisi.


Mwaandishi wa BBC wa maswala ya kidini , Robert Pigott, anasema Askofu mkuu mpya anarithi kanisa lililoshuhudia kupungukiwa na idadi ya waumini wanaohudhuria ibada katika miaka ya hivi karibuni na ambalo linajitahidi kuhubiri ujumbe wa ukristo katika jamii inayozidi kuonyesha kutotilia maanani maswala ya kidini .

Itachukuliwa kama ni jukumu lake kuliunganisha kanisa ambalo limekumbwa na migogoro kuhusu maaskofu wanawake na pengine hatari zaidi maswala ya ujinsia,Kwa mara ya kwanza katika historia ,Mwanamke Mchungaji Sheila Watson, ambae ni mkuu wa Mashemasi wa Canterbury alishiriki katika moja ya hatua mbili za kutawazwa askofu mkuu.

sourece:bbc swahili

Sipho Makhabane, Mkongwe wa muziki wa Injili A.Kusini katika Tamasha la Pasaka

 Katika kuelekea Tamasha la Pasaka Sipho Makhabane, Mkongwe wa muziki wa Injili Afrika Kusini atahudumu katika tamasha hilo katika na ametunga wimbo maalum kwa Watanzania katika tamasha la Pasaka

Historia ya muziki Duniani, inaonesha kuwa muziki wa makanisani, ambao unajulikana kama muziki wa Injili ndio chimbuko la aina zote za muziki ulimwenguni,Hakuna ubishi kuwa kila mwanamuziki mwenye kuujua muziki, ukimuuliza chanzo cha yeye kujihusisha na muziki ni lazima atakueleza kuwa alianzia kwenye kwaya.
Hata hivyo pamoja na ukongwe wa muziki huo, bado unaonekana kutopewa nafasi sana kwenye vituo vya redio na Televisheni, labda kutokana na kuegemea dini fulani.

Pamoja na hilo, lakini pia haujaweza kuwanufaisha wanamuziki wa muziki huo hapa nchini tofauti na wanavyofaidika wanamuziki wa mataifa mengine kama ilivyo nchini Afrika Kusini.Sipho Makhabane ambaye anajihusisha na muziki huo nchini Afrika Kusini  ni mmoja wa wanamuziki wa Injili wenye mafanikio makubwa.Makhabane ambaye pia ametajwa kuja nchini kushiriki tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Machi 31, mwaka huu, anamiliki kampuni kubwa ya Big Fish, ambapo kazi yake kubwa ni kukuza na kuibua vipaji vipya vya wanamuziki wa Injili.

Jina la mwanamuziki huyo ni kubwa barani Afrika, ambapo umaarufu wake umepatikana kutokana na uwezo wake wa kutunga nyimbo zenye ujumbe wa hali ya juu wa kumsifu na kumtukuza Mungu.Kutokana na uwezo wake huo mashabiki wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakimfananisha na wanamuziki mahiri kama Joyous Celebration ama Sfiso Ncwane.

Makhabane mwenye umri wa miaka 45 ni mmoja wa magwiji wa uimbaji nchini Afrika Kusini, ameshiriki katika shughuli mbalimbali za kiroho na kijamii.Kutokana na kutingwa na shughuli zake mwaka 2010 alitangaza kuachana na kazi ya kuimba, hata hivyo mwaka 2012 aliushangaza ulimwengu kwa kuachia albamu yake mpya iliyokubalika na watu wengi.
Historia ya maisha yake inaonesha kuwa ni mtu aliyekulia katika muziki huo.Kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa ukiikabili familia yake, Makhabane alilazimika kuacha shule akiwa darasa la tano na akiamua kufanya kazi katika shamba la miwa la Kaaruls huko Mpumalanga kama ilivyokuwa kwa mwimbaji mwingine nguli Rebecca Malope.
Makhabane alifanya hivyo walau aweze kupata fedha ya kuwasaidia wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walikuwa wakimtegemea yeye.

 Alipotimiza  miaka 17, alihamia kwenye kazi za ujenzi kwenye hifadhi ya Taifa ya Afrika Kusini ya Kruger.
akiwa huko alifanya kazi ya kuwasaidia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba kambini hapo na alipotimiza miaka 21 alikuwa tayari na ujuzi wa kutosha katika kazi ya ujenzi na akapata kazi katika eneo la Pienaar.
Mwaka 1986, Makhabane alipata ofa nzuri katika kampuni ya Telkom kama fundi, lakini katika kuhangaika kwake alijikuta akiishia kwenye muziki wa Injili.

Hata hivyo hakuwa akijua kuwa nyota ya mafanikio yake ilikuwa kwenye huduma hiyo ya uimbaji na badala yake alikuwa akifanya muziki wa kujifurahisha zaidi na si wa biashara.
Mwaka 1990, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Makhabane alifunga ndoa na binti aliyekuwa na umri wa miaka 18.

Baada ya hapo ndipo alianza kazi ya kununua na kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi ya Afrika Kusini.
Kutokana na kuona muziki umeanza kuingia kwa kasi kwenye maisha yake, Makhabane aliamua kuachana na kazi ya ufundi mitambo ya simu na kujikita kwenye muziki.

Katika kuhakikisha anaingiza kipato mwanamuziki huyo aliamua kusambaza kazi zake mwenyewe, lakini kikwazo kwake kikawa ni namna ya kuwavutia wasambazaji waliokuwa tayari kununua kazi kutoka kwake.
Kazi yake iliyomfanya kukubalika ilianza kusikika kwenye redio ya Swazi ambayo inajulikana zaidi kwa jina la Ligwalagwala FM, ambapo kibao kilichomtambulisha ni kile cha Ngitinikela Kuwe.Hatimaye mwaka 1996, Makhabane aliamua rasmi kuifanya kazi hiyo ya muziki wa Injili na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kampuni ya simu.

 Mwaka huo huo aliachia album yake iitwayo “Yek’intokozo” wimbo ambao mpaka leo unakumbukwa na mashabiki wake kwani ndio ulimtambulisha vema, ingawa tayari alishatoa album nyingine mbili miaka ya 1993 hadi 1999 za ‘THUM’UMLOLO” na “JESU ULIQHAWE”.
Mwaka 1998, kupitia kampuni ya CCP Records aliachia album yake ya nne iitwayo “Uyigugu” iliyofanya vema kabla ya mwaka uliofuata kuachia nyingine iitwayo “Makadunyiswe,”.
Mwaka 2001, alifyatua album ya Calvary ambayo iliuza kufikia kiwango cha juu na mwaka uliofuata  (2002), aliachia albamu  nyingine ya ‘Akukhalwa’ ambayo ilitikisa kama album ya “Yek’intokozo,” akiuza zaidi ya nakala 70,000.
Mwaka 2003, Makhabane aliachia album ya ‘Moya wami’ ambayo pia iliuza zaidi ya nakala 70,000.
Kutokana na umahiri wake, Makhabane ameweza kushirikishwa katika album na waimbaji wakongwe wa nchini kwake kama Jabu Hlongwane, Marehemu Vuyo Mokoena, Lundi, Hlengiwe Mhlaba na wengine wengi.
 
Pia akiwa nyuma ya mafanikio ya waimbaji lukuki kama Hlengiwe Mhlaba, Ncandweni Christ Ambassadors, Shongwe na Khuphuka Saved Group.

Nje ya uimbaji, Makhabane ni mtayarishaji wa kazi za muziki wa injili akiwa daraja la waimbaji wengine kutokana na kuwika vilivyo kupitia kazi zao zilizoandaliwa na gwiji huyo.Makhabane ametunga wimbo maalum kwa ajili ya mashabiki wake wa Tanzania.Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam siku chache zimepita na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa amezungumza na msanii huyo na amemueleza kuwa amewaandalia zawadi Watanzania kwa ajili ya tamasha hilo.

“Sipho amefurahi sana kumualika kwenye tamasha letu, amenihakikishia licha ya nyimbo zake za kawaida, lakini pia atakuwa na wimbo maalum kwa Watanzania, amesema anawapenda Watanzania na ameandaa wimbo mzuri ambao ana uhakika mashabiki wataupenda.
“Mashabiki watakaokuja kwenye tamasha Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 31 watapata fursa ya kumsikiliza msanii huyo pamoja na wimbo wake mpya ambao jina hakunambia lakini amesema ni zawadi nzuri kwa Watanzania,” alisema Msama na kuzitaja baadhi ya nyimbo za msanii huyo kuwa ni Moya Wami, Indonga, Akukhalwa, Over&Over, Nguy’zolo, Yizwa Nkosiseju, Hlalanami Nkosi Jesu, Yek’intokozo, Injabulo, Hlalanami Jesu, Makadunyiswe, Vuka Mphemlo, Mphefumlo na Moya Wami.

Kuhusiana na maandalizi mengine ya tamasha hilo alisema yanaenda vizuri na kwamba mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwamba ni matumaini yake mashabiki watajitokeza kwa wingi.
Licha ya Sipho Makhabane, wasanii wengine wa nje ya Tanzania ambao tayari wamethibitisha kushiriki tamasha hilo ni , Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya na kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda inayotamba na albamu ya Mtegemee Yesu. Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone na John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndani ya Vatican City Roma

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  na Mkewe Tunu wakifanya mahojiano na mtangazaji wa Radio Vatican, Padri Richard Mjigwa (katikati)  kweye  moja kati ya studio  za Raido hiyo Mjini Roma walikohudhuria sherehe za  kusimikwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Diuniani, Papa Francis 1 (Picha kwa hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu na mkewe Tunu wakipata maelezo  kuhusu historia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro la Roma kutoka kwa Padri Alquine Nyirenda wa Makao Makuu ya Shirika la Watawa wa wa Benedikti, Roma walikohudhuria sherehe za kusimikwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.



Wakiongozwa na Padri  Alquine Nyirenda wa Makao Makuu ya Shirika la Watawa wa Benedikti, Roma kutoka kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro la Roma walikohudhuria  sherehe za  kumsimikwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis 1 kwenye viwanja vya Kanisa hilo
















Tamko la Pamoja la Mkutano Mkuu wa Dharura wa Jukwaa la Kikristo Tanzania

1. Utangulizi
Jumuiya ya Kikristo Tanzania – CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania – TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania – PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (Watazamaji)

Katika Mkutano wake Mkuu wa Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini, Jijini Dar es Salaam, tarehe 8 Machi, 2013; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na mauaji na mashambulizi ya viongozi wa dini; na hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya uhalifu huo unaotekelezwa na Waislamu wachache. Katika taswira hiyo, Kanisa lilitathmini juu ya wajibu, utume, na sauti yake ya kinabii kwa taifa letu kuhusiana na mambo hayo.

2. Hali halisi ilivyo hivi sasa hapa nchini kwa mtazamo wa Kanisa

Ushahidi wa kihistoria na kimazingira unaonyesha wazi kuwa kwa sasa Kanisa nchini Tanzania limo katika kipindi cha mateso ya kimfumo (systematic persecution), kama vipindi vingine 10 vya mateso katika Historia ya Kanisa hapa duniani.

Pamoja na mateso haya ya kimfumo, tunatambua wazi kuwa wanaotekeleza haya ni kikundi kidogo tu cha Waislamu wa Tanzania, kama wale wengine wa Barani Afrika (k.m. Boko Haram kule Nigeria). Waislamu walio wengi hawafurahii mambo yanayotokea. Wao pia wanaitazamia Serikali kuthibiti hawa wachache wanaochafua dini ya Kiislamu na kuwafanya Waislamu wote waonekane kuwa maadui wa Ukristo, jambo ambalo siyo kweli. Kutokana na hali hiyo, mkutano mkuu wa dharura wa Jukwaa la Wakristo umeyaangalia maeneo makuu yenye migogoro ikiwa ni pamoja na:

2.1. Mgororo wa nani anastahili kuchinja kitoweo
Hivi karibuni hapa nchini tumeshuhuduia mgogoro juu ya uchinjaji wa mifugo ambayo nyama yake inapaswa kuuzwa kwa watu wa imani mbalimbali wakiwemo Wakristo na Waislamu. Tunafahamu kwamba sheria ya nchi yetu inaweka bayana juu ya usalama wa nyama hizo kiafya, lakini sheria haielekezi kuwa dini fulani ndiyo waumini wake wanapaswa kuchinja mifugo hiyo. Kwa misingi hiyo Kanisa linatamka kuwa:-

a) Hoja ya dini moja kudai kuhodhi (exclusive right) uchinjaji wa mifugo kwa misingi ya imani yake ni kinyume cha haki ya uhuru wa kuabudu ambayo amepewa kila mtu ndani ya nchi hii kikatiba katika Ibara 19.

b) Kwa kuwa kuchinja wanyama na ndege ni Ibada kwa Waislamu, Kanisa litambue na kuheshimu jambo hilo. Lakini pamoja na kutambua haki ya Waislamu kujichinjia wanyama na ndege kama Ibada kwao, Wakristo wasilazimishwe kula nyama zilizochinjwa kwa misingi ya Ibada za Kiislamu. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania ni wa dini mbalimbali na mila za makabila mbalimbali, tunaitaka Serikali itamke wazi kuwa kila raia ana uhuru wa kufuata imani yake katika suala la uchinjaji.

c) Kuhusiana na jambo hili tunashindwa kabisa kuelewa msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali. Wakati wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia ni Muislamu, ulipotokea ugomvi wa mabucha ya nyama ya nguruwe Dar es Salaam, Rais huyu Mstaafu kwa kulinda Katiba ya nchi ambayo aliapa kuilinda, alisema mwenyewe kwa nguvu zote kuwa kila mtu ana uhuru wa kula anachotaka na mtu wa dini moja asimhukumu mtu wa dini nyingine kwa kile anachokula. Baada ya Rais Mstaafu kukemea jambo hili, hali ikawa ya amani na utulivu. Kwa nini Serikali yetu ya sasa inapata kigugumizi kuhusiana na suala zima la nani achinje?

d) Kwa mantiki hiyo hapo juu katika kipengele cha a-c, Wakristo wanaitaka Serikali iweke utaratibu wa kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu ili kila Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka. Sambamba na kuitaka Serikali kufanya hivyo, tunawakumbusha Wakristo wote Tanzania kuelewa kuwa watakuwa hawajavunja sheria yoyote ya nchi wakiamua kujichinjia kitoweo chao wenyewe. Kuhusiana na tangazo hili kwa Wakristo wote, tunaitaka mihimili ya dola (Serikali na Mahakama) kuheshimu Katiba ya Nchi yetu, na kipekee kuhusiana na jambo hili Ibara ile ya 19.

e) Kwa upande mwingine, kwa kuwa tayari zipo bidhaa za vyakula katika nchi hii ambazo zina nembo ya ‘halal’ na nyingine hazina nembo hiyo, huu ni uthibitisho kuwa vyakula hivyo vimegawanywa kwa kufuata misingi ya imani za kidini. Kwa hiyo, madai ya kugawanya machinjio na mabucha kwa kufuata misingi ya dini sio jambo jipya kwa sasa katika nchi hii.

2.2 Uchomaji wa Makanisa ulioambatana na vitisho na mauaji ya viongozi wa Kanisa

Kanisa linalaani vikali mauaji ya kidini yanayoendelea kufanywa pamoja na vitisho (systematic persecution) kwa viongozi wa Kanisa na Wakristo wote kwa ujumla. Mtiririko wa matukio mbali mbali ya nyuma yanatudhihirishia kuwa kumekuwepo na mpango wa muda mrefu wa haya yanayotokea sasa hivi. Tarehe 15 Januari 2011, kundi la Waumini wa Kiislamu walipokutana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, miongoni mwao walikuwamo mashehe, walijadili hali ya nchi ya Tanzania kuongozwa kwa mfumo wa kidini. Mkutano huo ulihitimishwa kwa kutoa tamko dhidi ya kile kilichoitwa mfumo Kristo katika nchi yetu!

Japo Serikali na vyombo vyake vya usalama wa Taifa vimekuwa vikipata taarifa za vitisho dhidi ya viongozi wa Kanisa, mauaji, kuchomwa kwa nyumba za ibada, pamoja na maneno ya uchochezi kupitia mihadhara, vipeperushi, CD na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na taasisi zinazofahamika, hata hivyo Serikali kwa kiasi kikubwa imeshindwa kuchukua hatua kwa wakati muafaka na wanasubiri hadi maovu yatendeke ndipo ati waanze kufanya uchunguzi. Kwa Serikali yetu inaonekana wazi kuwa katika hili ile methali kwamba “Kinga ni bora kuliko tiba” haina maana yoyote. Hii ni kuonyesha udhaifu mkubwa wa vyombo vya usalama wa Taifa au pia kwamba vyombo hivi vinafurahia kutoweka kwa amani nchini mwetu, jambo ambalo linalifanya Kanisa nchini Tanzania liamini kwamba matukio haya yanayoendelea kutokea ni dalili kuwa Serikali ina agenda ya siri dhidi ya Ukristo. Kutokana na hayo Jukwaa la Wakristo Tanzania linatamka kama ifuatavyo:

a) Tunatambua kwamba ni jukumu la Serikali kuwatendea raia wake kwa usawa na bila ya ubaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi wa Kanisa wanatamka kwamba Serikali imeshindwa kuheshimu Katiba juu ya hizi haki za raia wake na kupelekea waamini wa dini ya Kikristo kukosa imani na Serikali iliyoko madarakani, hasa kuhusu ulinzi na usalama wao na mali zao kama inavyoagizwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Kama Serikali inaona haiwezi kuwahakikishia wananchi usalama wa uhai wao na mali zao, na hivyo kuwafanya waishi maisha ya hofu inayotokana na vitisho, basi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, hakuna sababu ya Serikali iliyoko madarakani kung’ang’ania kuongoza nchi.

b) Kwa kuwa ulinzi wa raia ni haki ya kikatiba na kisheria, Serikali inatakiwa iwalinde raia wake. Kama Serikali imeshindwa kuwalinda raia wake, Kanisa linataka Serikali ikiri hivyo ili Kanisa liwaambie wananchi waiwajibishe Serikali na Viongozi wanaoifanya Serikali ishindwe kutimiza wajibu wake. Jukwaa la Wakristo linasema: Kama Serikali haitachukua hatua za makusudi dhidi ya mambo haya yaliyoainishwa hapo juu, Kanisa litachukua hatua ya kuwaambia waamini wake kwamba Serikali iliyoko madarakani inaibeba dini moja, na hivyo Kanisa litatafakari upya uhusiano wake na Serikali.

3. Wakristo walioko Zanzibar

Wakristo walioko Zanzibar wanatishiwa maisha yao na mali zao zinaharibiwa mara kwa mara, kiasi cha wengine kuamua kuhamia Tanzania Bara. Kigezo cha unyanyasaji huo ni suala la udini na muungano. Inaonekana ni kama vile Watanzania waliozaliwa Bara hawana haki ya kuishi Visiwani. Na kumbe wale waliozaliwa Visiwani wafikapo Barani wana haki zote. Kanisa linaitaka Serikali iwahakikishie Wakristo walioko Zanzibar usalama wao na wa mali zao maana hiyo ni haki yao ya Kikatiba.

4. Vitisho na mauaji ya Wanakanisa

Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ichukue hatua za makusudi za kuzuia vitisho na mauaji kwa Viongozi wa Kanisa na Wakristo kwa ujumla. Vinginevyo Kanisa litautangazia ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi mojawapo inayovunja haki za binadamu kwa ubaguzi wa kidini na kulitesa Kanisa kimfumo.

5. Matumizi ya Vyombo vya Habari:

Kwa kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimeruhusu vitumiwe kuwatukana Viongozi wa Kanisa, tunatoa nafasi kwa vyombo hivyo kuomba radhi; vinginevyo tutaitaka dunia ivielewe kuwa navyo ni sehemu ya chanzo cha migogoro. Pia tunachukua nafasi hii kuvitahadharisha vyombo mbalimbali vya habari kupima kwa kina ni nini kinachosemwa na viongozi wa kidini ili kuviepusha vyombo hivyo kutumika kwa nia ya uchochezi; yasije yakatukuta kama yale yaliyotokea kule Rwanda 1994.

6. Hitimisho:

Kanisa linaendelea kusisitiza kuwa silaha kuu ya Mkristo katika nyakati hizi ni maombi na kufunga. Kwa mantiki hiyo, Kanisa linawataka Wakristo wote nchini Tanzania kuungana kwa pamoja katika maombi na kufunga kwa muda wa siku saba kwa ajili ya hali hii iliyojitokeza hapa nchini. Maombi hayo na mfungo vifanyike kabla ya Pasaka, yaani kuanzia, tarehe 24/3/2013 hadi 30/3/2013.

Kwa niaba ya Maaskofu 177 walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa Dharura wa Jukwaa la Wakristo na kutoa maazimio hayo.

1. Askofu Peter Kitula – Mwenyekiti CCT…………………………………………………………….

2. Askofu Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa Rais TEC………………………………………………

3. Askofu David Batenzi Mwenyekiti PCT……………………………………………………………

Waimbaji wa Tamasha la Pasaka Dar watambulishwa.

Katika Kuelekea Tamasha la Pasaka mwaka 2013 baadhi ya waimbaji kama Upendo Nkone na Boniface Mwaitege wamesema Tamasha la mwaka huu wamejipanga vilivyo kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa watakaojitokeza siku ya tamasha hilo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Upendo Nkone mbele ya waandishi wa habari
Wakizungumza na waandishi wa habari, Nkone alisema inaonekana ana wapenzi wengi zaidi  katika nyimbo za  kumtukuza mungu ndio maana wamemchagua kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi, hivyo ana deni la kuwalipa siku hiyo.

“Nimepata furaha kwa waamini kutambua kazi yangu, ndio maana na mimni najihisi nna deni, na nawaahidi kuimba wimbo mpya siku hiyo ambao “Nimebaki na Yesu” ambao unachochea ibada kwa waamini,” alisema Nkone.

Mkurugenzi wa Msama Promotions Alex Msama
Nkone alisema uimbaji wa nyimbo za injili ni mgumu iwapo utafanya vibaya na jamii pia itakukataa ambako pia waamini wanatakliwa kuisoma biblia na kuielewa sambamba na kumuomba mungu kwa dhati ya kweli.

Naye Mwaitege alisema amefurahi kupata bahati ya kuwa mmoja wa wahudumu wa neno la Mungu siku hiyo kwa  sababu tamasha la mwaka jana hakupata bahati ya kushiriki kwa sababu alikuwa safarini nchini Kenya.

“Mwaka jana nilitamani kuimba pamoja na Rebecca Malope lakini bahati haikuwa yangu, ingawa nimepata bahati ya kuimba na Sipho Mwakabane ambaye naye anatokea Afrika Kusini kama Malope na Watanzania wenzangu kama akina John Lissu, Upendo Kilahiro na Rose Muhando,” alisema Mwaitege.

Aidha Mkurugenzi wa Msama Promotions ambao ni waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama alisema siku ya Tamasha utafanyika uzinduzi wa albam ya kundi la Ambassodor of Christ ‘Kuweni Macho’ ambayo itauzwa siku hiyo.

Tamasha hilo ambalo litafanyika pia katika mikoa ya Mbeya Aprili Mosi, Iringa Aprili 3, Aprili 6 mkoani Dodoma na Mwanza Aprili 7.
Viingilio katika tamasha hilo kwa VIP ni shilingi 50,000, Viti maalum shilingi 10,000, Viti vya kawaida 5000 na watoto shilingi 2000.
Mgeni rasmi katika tamasha hilo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Boniface Mwaitege
kwa hisani ya fullshangweblog.com

Waziri Sitta amewataka Viongozi wa Dini kuwakemea Wanasiasa wanaomwaga fedha chafu kanisani.

Mh.Samuel SittaWaziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,amewataka Viongozi wa Dini kuwakemea wanasiasa wanaomwaga fedha chafu kanisani kwa lengo la kutaka kuungwa mkono na waumini.

Pia amewataka viongozi hao kuzikataa fedha hizo alizodai zinapatikana kwa rushwa na wizi wa mali ya umma.Sitta alisema hayo jana wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Bethania lililopo Tegeta jijini Dar es Salaam.

“Baba Askofu nawaomba viongozi wa kanisa msaidie sana kuondoa unafiki huu ambao sasa unaletwa kanisani,” Waziri Sitta alimweleza Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa.
Alisema,  “wapo watu wenye fedha chafu wanazileta kanisani, ninyi mnazipokea. Ni hatari sana hii, mtu anasimama madhabahuni anaanza kuwadanganya wakristo.”

Alisema wapo watu wanadanganya kwamba wao ni maskini na kwamba fedha wanazozitoa kanisani wamechangiwa na marafiki zao wakati kila mtu anafahamu kwamba ni uongo.
Aliongeza: “Wakristo tunashangilia, wakati hata ukimuita mjukuu wako na kumuuliza eti huyu ni maskini, atakueleza kuwa ni tajiri wa kukufuru,” alisema Sitta.

Alisema yeye hataacha kusema ukweli kwa sababu kuacha kufanya hivyo ni kuiua nchi hii.
“Tukiacha kuyasema haya ni kuiua nchi, sisi viongozi tukiendelea kuiibia nchi hii na vijana wanaona haya yanaendelea basi nao wataona hii ndiyo jadi nao wataiba,” alisema.

“Chonde chonde Wakristo tuzikatae fedha hizi zinazopatikana kwa rushwa kwani ni sawa na kukumbatia dhambi,” alisema Sitta bila kuwataja wanaofanya hivyo.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki alisema hakuna nchi iliyoendelea duniani kwa kukumbatia rushwa.

“Katika siasa hakuna mwanasiasa ambaye alianza siasa akiwa maskini na akatajirika kwenye siasa, ukiona hivyo huyo ujue ametuibia,” alisema Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa.

Alipoulizwa baadaye alikuwa anamlenga nani, alicheka, kasha akasema: “Ahaa, ni watu wa aina hii wako wengi, ni mtandao mkubwa.”

Kwa upande wake, Askofu Malasusa aliwaomba waumini kuwa wasilikizaji na washauri kuliko kutenda katika mtafaruku wa kidini unaondelea, ili kulinda amani iliyopo.

Harambee hiyo ilihudhuriwa na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Margareth Sitta.




Source:Mwananchi

Tamasha la Wakongwe wa Mziki wa Injili Nchini.

Siku ya Jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam lilifanyika tamasha la wakongwe wa muziki wa injili nchini,  tukio lilifanyika kwa kuhudhuriwa na waimbaji mbalimbali, viongozi na wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake bila kusahau wengine waliotoka nje ya jiji hilo.

Ambapo licha ya uimbaji pia mwandaaji wa tamasha hilo aliweza kuwatunukia vyeti waimbaji hao kwa mchango wao mkubwa katika kumwinua Kristo kupitia uimbaji wao, aidha mwandaaji huyo amesema kuna changamoto nyingi ambazo wamekutana nazo katika uandaaji wa tamasha hilo ikiwemo kutaka kushitakiwa na baraza la sanaa nchini(BASATA) kutokana na kuandaa tamasha hilo la kuwatunuku vyeti wakongwe nchini.

Kwa upande wa mke wa Waziri wa uchukuzi nchini Linna Mwakyembe amechangia katika Tamasha hilo shilingi laki tano kwa ajili ya waimbaji wakongwe pamoja na hayo pia ameeleza kuwa Bwana Yesu ni Bwana na mwokozi wa misha yake ,sambamba na kumshukuru Mungu kwa kumtendea mambo mengi katika misha yake,tazama baadhi ya picha za tukio hilo.










Source:gospelkitaa.blogspot.com

Papa Francis I akataa vitu vya kifahari

Siku chache baada ya kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewashangaza wengi mengi kwa kukataa kuvaa viatu vya kifahari na msimamo wake kuwekwa wazi kuwa hatavumilia makasisi watakaotenda uovu.

Tayari, Papa Francis ameelezwa kuwa kiongozi asiyetaka makuu, mhafidhina na mtu ambaye hataweza kubadili mengi katika kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2 duniani.

Katika siku mbili za uongozi wake, Papa Francis amelithibitisha hilo kwa kutokea hadharani akiwa amevaa viatu rahisi, vyeusi na kuachana na vyekundu vya kifahari vilivyopendelewa na mtangulizi wake, Benedict VXI.

Katika uongozi wake, siku zote Papa Benedict, alivaa viatu vyekundu vilivyotengenezwa kwa mkono, jambo ambalo Papa Francis anaonekana kuachana nalo.

Watu walio karibu naye Papa Francis, wanaeleza kuwa kabla ya kuondoka Buenos Aires, Argentina kwenda Rome, Kardinali Jorge Mario Bergoglio, kama alivyojulikana awali, alivaa viatu rahisi vya rangi nyeusi, na kuwafanya marafiki zake, wakiwamo mapadri kutaka kumnunulia viatu vingine vipya.

“Siku ile aliyoondoka mjini Buenos Aires kuelekea Rome kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi wa Papa (conclave), marafiki zake walimpa zawadi ya viatu. Yeye, siku zote amekuwa akitokea hadharani akiwa amevaa nguo rahisi, viatu vya kawaida,” walieleza mapadri hao kutoka Amerika Kusini walipozungumza na Kituo cha Redio Vatican.

Juzi Ijumaa alipokutana na makardinali 106, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, licha ya kuonyesha uso wa furaha na kuwatania aliwaonya makardinali hao kuhusu wajibu wao kama viongozi wa kanisa maeneo mbalimbali duniani akiwataka kutosahau kuwa hawarudi kwenye ujana.

Katika ukumbi wa Sala Clementina, ulioko Vatican Papa Francis pia aliwataka makardinali hao wakiwamo waliomchagua kuwategemea zaidi vijana aliosema ndio nguzo kuu muhimu ya ustawi wa Kanisa Katoliki, huku aliwashauri makardinali kusaka njia sahihi ya kueneza Ukristo pande zote za uso wa dunia katika karne ya 21.

Aidha, alimsifu mtangulizi wake, Papa Benedict kwa uamuzi wa kijasiri wa kustaafu, akieleza kuwa ni uamuzi wa busara, wenye kuonyesha ukomavu na kuwataka wasichoke kuiga matendo mema.

Source Mwananchi

TAG Isanga yawasha moto wa uamsho.

“Ndipo tukageuka, tukashika safari yetu kwenda jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia BWANA; tukawa kuizunguka milima ya Seiri siku nyingi. BWANA akanena, akaniambia, Mlivyozunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini….,” (Kumb. 2:1…), maandiko haya  na mengine ndiyo yaliyoongoza Kanisa la Tanzania Assemblies of God Isanga, Sayuni Mbeya, kuandaa semina kubwa ya kiroho iliyoleta uamsho mkubwa katika vitongoji vya miji ya mbeya na majirani..

Semina hiyo ya Neno la Mungu iliyoandaliwa na Mchungaji Kiongozi Joseph A. Chiwinga wa kanisa hilo, ilileta nguvu mpya ya kiroho na uamsho mkubwa, ambapo baadhi ya makanisa kutoka madhehebu mbalimbali kutoka Mbeya, walihudhuria na kupokea nguvu mpya na uamsho wa kufanya kazi ya Mungu kwa kasi zaidi.

Akifundisha ujumbe uliojaa nguvu za Mungu, Mchungaji na Mwinjilisti Lutengano Mwasongela, kutoka Tabora, alinukuu maandiko kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 2:1, yanayodhihirisha kuwa, wakati wa kanisa kuzungukazunguka imetosha na kwamba hakuna ajuaye uchungu wa kanisa asipokuwa Yesu pekee ambaye ndiye kiongozi na muhimili wake asiyetikisika milele yote.

Akizungumzia kuhusu Imani, Mchungaji huyo alisema kuwa, umefika wakati kwa waumini wa kweli kusimama kwenye Imani thabiti, ambapo alibainishwa kwamba, ukiwa na imani wenye uhakika na Mungu hauwezi kuogopa kitu chochote, na kwamba kile utakachokiona katika ulimwengu wa Roho ndicho kitakachokutokea.

Akinukuu maandiko yasemayo: “Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa Mkutano wote wa wana wa Israeli, katika Jangwa la Parani, huko Kadeshi wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi…..Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.” (Hes. 13:26-33). Mtumishi huyo alifafanua ujumbe huo akisema kwamba; pamoja na mambo mengi yanayoonekana kuwa magumu na yakuwakatisha tamaa wanadamu, kwa Mungu ni mepesi na yanaweza kutatuliwa mara moja.

Aidha ailiwataka watu kutoogopa mambo yote magumu kwa vile Mungu wao aliisha watangazia ushindi pale Kalvari, kilichosalia ni kuchukua hatua na kutangaza ushindi ambao tayari uliishapatikana.

Aidha alisema kuwa, mwanadamu ndiye anayeweza kumwacha Mungu, lakini Mungu hawezi kumwacha mwanadamu kamwe, kwani yeye anawapenda watu wake aliyowaumba na kuwawazia mema kila iitwapo leo. Mchungaji huyo alisema kuwa mabadiliko yoyote katika maisha ya mwanadamu yanahitaji gharama kubwa na ili mtu utoke kwenye mzunguko alionao ni lazima akubali mabadiliko hata kama yanamaumivu makali.

Aliwataka watu kutambua kwamba, Neno la Mungu ndilo lenye uwezo wa kuwajenga watu na kuwabadilisha na siyo maneno matupu, hivyo kila muumini anatakiwa kuliamini na kulitendea kazi  pasipo kulega.

 Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Joseph Chiwinga, akiongea na blog kwa njia ya simu alisema kuwa, kanisa lake limejipanga imara mwaka huu, kuendesha Semina na mikutano mingi inayokusudia kuleta uamsho na kuwavuna watu kwa Bwana Yesu, katika jiji la Mbeya, na kwamba kwa awamu ya kwanza wameanza na semina ya ndani ambayo imemalizika na sasa kuna semina ya Wanawake Watumishi wa Kristo WWK itakayofikia kilele chake leo wakati wa sikukuu yao kitaifa alimazia kwa kusema

Papa Francis I Kiongozi mpya wa Kanisa la Romani Duniani


Katika kile kilichokuwa kinasubiliwa kwa muda sasa kimeeleweka,ni Kardinali Jorge Bergoglio wa Argentina amechaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, akiwa ni wa kwanza kutoka barani Amerika na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000.

Baada ya kuchaguliwa na makardinali wenzake 115, Kardinali Jorge Bergoglio (76) alichagua kufahamika kwa jina la Francis I.

Maelfu ya mahujaji, watalii na waumini wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamejazana katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, Vatican kushuhudia moshi mweupe uliofuka saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kuashiria kuchaguliwa kwake, waliripuka kwa shangwe, nderemo na vifijo.
Papa Francis I kiongozi mpya wa Kanisa la Romani Duniani
Muda mfupi baada ya moshi huo kutoka, kardinali mmoja alisimama katika ‘varanda’ ya Kanisa la Mtakatifu Petro na kutangaza “Habemus Papum” (tumepata papa mpya).
Papa Francis I alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanawania nafasi hiyo na papa anayeondoka, Benedict XVI mwaka 2005, ambapo aliripotiwa kuibuka wa pili.

Kabla ya kuchaguliwa kwake, Papa Francis I ambaye kwa wadhifa wake pia anakwenda kuwa Askofu wa Roma, alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Argentine na kwa muda wote wa utumishi wa utumishi alikuwa huko huko nyumbani.

Anakuwa Papa wa 266 kuwahi kuongoza kanisa hilo lenye waumini zaidi ya bilioni 1.2 duniani.
Baada ya kutangazwa kwake, Papa Francis I alijitokeza kuzungumza  kwa mara ya kwanza kama Askofu wa Roma.

Akiwa amechaguliwa katika awamu ya tano ya upigaji kura, inaelezwa kuwa alikuwa miongoni mwa mapapa waliochaguliwa kwa haraka baada ya muda mrefu, akiwa sawa na Benedict XVI (2005) na Pius XII aliyechaguliwa mwaka 1939.
Mshindi alitakiwa kupata kuta 77 au robo tatu ya makardinali 115 walioshiriki uchaguzi huo.
Papa Francis I anachukua nafasi iliyoachwa na Papa Benedict XVI aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu, ikiwa  ni miaka 600 tangu Papa wa mwisho kujiuzulu.

Papa Francis I, ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Jesuit ambaye ametumia muda wake mwingi wa utumishi nyumbani Argentina.

Anafahamika kwa utumishi uliotukuka kwa uangalizi wa kanisa na mapadri, mambo ambayo yanatajwa kuwa sifa kubwa ya kuchaguliwa kuwa Papa.

Papa huyo amedumu katika maisha ya kufundisha na kuongoza mapadri. Amefanya kazi Amerika ya Kusini ambako kuna Wakatoliki wengi. Kardinali Bergoglio anatambulika kwa kutamadunisha Kanisa la Argentina, lililokuwa miongoni mwa makanisa ya kihafidhina huko Amerika Kusini.

Amechagua jina la Papa Francis I, chini ya uangalizi wa Mtakatifu Francis wa Assisi.
Alizaliwa Buenos Aires katika familia ya mfanyakazi wa reli. Alipata upadrisho mwaka 1969.
Aprili 15, 2005, mwanasheria wa haki za binadamu alimfungulia mashtaka ya jinai  kwa kushirikiana na maofisa wa jeshi kuwateka mapadri wawili wa Jesuit mwaka 1976, akiwa kiongozi wao aliwafukuza katika utumishi kutokana na migogoro katika jumuiya hiyo.

Source:Mwananchi