Mchungaji wa Kanisa afumaniwa na mke wa mtu

TOFAUTI na inavyoaminika na wengi kuwa watumishi wa Mungu ni watu safi, safari hii Mchungaji Obed Ntimba wa Kanisa la Anglikana Gongo la Mboto, Dar es Salaam amejikuta akivunja agano la Muumba baada ya kunaswa gesti akiwa na mke wa mtu.
 
 Tukio hilo la aibu lilimkuta mchungaji huyo Ijumaa iliyopita saa saba na nusu za mchana katika gesti moja (jina lipo) iliyopo nyuma ya Jengo la Ubungo Plaza jijini Dar.
 
Siku moja kabla ya tukio, makachero wetu walitonywa kuhusu dhambi hiyo na mtu wa karibu na watu hao akisema kuwa anaumia kwa sababu mchungaji huyo ana mke na watoto na mwanamke huyo, Rose ni mke wa mwanajeshi kwa hiyo aliamini tendo wanalotaka kulifanya ni uovu katika jamii.
 
 Mtoa habari wetu huyo alisema tukio hilo lilipangwa kukamilika kesho yake Ijumaa katika gesti hiyo ndipo kazi ya kuwafuatilia hatua moja baada ya nyingine ilianza.
 
Ijumaa saa sita mchana, mtonyaji wetu alipiga simu  na kuweka wazi kwamba wawili hao wapo njiani kuelekea gesti, kila mmoja kwa usafiri wake.
 
 Ndipo makachero wetu  walipowatonya polisi na kuambatana nao mpaka kwenye gesti hiyo na kujipanga kwa mbinu za kisasa za kutoonwa na ‘adui’.

 Makachero hao  walifanikiwa kupata ramani ya chumba walichoingia wawili hao ambapo ‘rumu’ namba 1B ndiyo iliwasilishwa kwamba Rose na mchungaji wake wamo humo.

Saa saba na nusu mchana, Makachero wetu na polisi waliingia hadi mapokezi ya gesti hiyo kwa kificho na kutoa maelekezo kwa mhudumu. Mhudumu aliongozana nao hadi mlangoni na kugonga lakini haukufunguliwa.
 
 BAADA YA DAKIKA TANO
Wakati mlango huo ukigongwa na mhudumu bila kufunguliwa, mchungaji huyo alisikika akisema na kuuliza:
“Subirini kwanza.”
“Lakini ninyi ni akina nani?”
 
 Baada ya dakika tano kupita, mlango ulifunguliwa, mchungaji akakutana na macho ya timu nzima. Alipigwa butwaa asijue la kufanya huku akitetemeka, Rose alikuwa ndani ya khanga moja!
 
 MCHUNGAJI MSOBEMSOBE HADI POLISI
Polisi waliwabeba msobemsobe wote hadi Kituo cha Polisi cha Urafiki-Ubungo, Dar ambapo kila mmoja alianza kujieleza.
 
 MCHUNGAJI APANGULIA HUDUMA YA KIROHO
Kituoni hapo, Mchungaji Ntimba alipobanwa kuhusu sababu za kuingia gesti na mke wa mtu, alisema waliingia kwa ajili ya huduma ya kiroho kwani mwanamke huyo alikuwa anataka kufungua kanisa ndipo alipomuomba yeye amsaidie.
 
 “Mimi sikuwa na lengo baya jamani. Huyu dada alihitaji kufungua kanisa, akaniambia ili nimshauri hawezi kukaa  sehemu ya wazi kwa kuwa mume wake ni mwanajeshi anaweza kuonekana na watu wakampa taarifa.
 
 “Ndipo nikaamua kwenda naye katika nyumba ile ya kulala wageni kwani wageni wengi wanaokuja kwa ajili ya huduma, wakitokea nchi mbalimbali huwa wanalala pale na wahusika wa pale wananifahamu sana.
 
 “Baada ya kuingia gesti nilibanwa na haja ndogo, nikaenda kujisaidia. Cha kushangaza niliporudi nilimkuta huyu dada amevua nguo zote na kuanza kunishawishi lakini sikuwa na lengo hilo jamani,” alijitetea mchungaji huyo.

 Baadhi ya picha zilizopo  zinamuonesha mchungaji huyo akiwa amevaa suruali lakini amesahau kufunga zipu huku kondom zikiwa pembeni kitandani!
 
 MSIKIE MKE WA MTU SASA
Baada ya mchungaji kutoa maelezo yake, mke wa mtu naye alianza kutiririka ya kwake huku akionesha ushahidi wa meseji za simu ambazo mchungaji huyo alikuwa akimtumia akimshawishi kumpa penzi.
 
 “Huyu mchungaji nilikwenda kwake kwa lengo la kufanya kazi kanisani lakini kuanzia hapo amekuwa akinishawishi kuwa anataka nimpe penzi ili aweze kuniweka katika sehemu nzuri kanisani.
 
 “Nilikuwa nakataa, lakini akasema tukutane pale gesti tuongee zaidi. Nilikataa kukutana gesti, akaniambia pale ni ofisini, mara nyingi akiwa anaongea na waumini mambo muhimu ya huduma ya kiroho huwa anakutana nao pale.

 “Nikakubali lakini kabla hata hatujaongea chochote alianza kuvua nguo zake na kuanza kunilazimisha tufanye mapenzi huku akiwa na ‘kinga’ kabisa na mimi nikavua nguo lakini kabla hajatimiza lengo lake ndipo wakaingia watu wakiwa na askari.
 
 “Mimi nashukuru sana kwa sababu hawa ndiyo wameniokoa. Nilikuwa nikisikia habari za huyu mchungaji kuwa ana tabia ya kuwafanyia wasichana wengi vitendo hivyo na kweli leo ndiyo nimeamini,” alieleza mwanamke huyo.
 
 Katibu wa kanisa hilo (jina halikupatikana mara moja) alimuombea msamaha mchungaji kwa waandishi huku akionesha kuumizwa na kitendo hicho baada ya kuoneshwa ushahidi na kukiri kwamba una ukweli tofauti na alivyokuwa akifikiria awali kabla ya kuachiwa kwa dhamana