- Awatahadhirisha mabinti kuwa makini
- Aahidi kuwaombea akienda Israel
Kiongozi huyo pia amewataka mabinti kutulia mbele za Bwana na kufanya ubinti wao kuwa wa utukufu wa Mungu ili siku ya mwisho Bwana ajivunie matendo yao mema waliyoyafanya ndani ya changamoto lukuki, kwa kuwa wanawindwa na waabudu shetani hao.
Askofu Mkuu wa (EAGT) Mwinjilisti Dk. Moses Kulola |
Askofu Kulola alisema kuwa, kanisa limevamiwa na waabudu shetani ambao wengine wamejivika majina makubwa huku wakiendesha ibada zao wenyewe na baba yao ibilisi, badala ya kufuata Bwana Yesu.
Huku akitaja majina ya makanisa makubwa yenye idadi kubwa ya waumini, lakini yakiendeshwa na makundi ya siri kama Freemasons alisema umefika wakati wa waumini kuwa makini na kusoma Biblia kwa makini huku wakimuomba Roho Mtakatifu awanusuru.
“Wanangu natoa wito kutoka katika ibada za mashetani, ondokeni huku wala msitazame nyuma, karibu Yesu yuaja atakuta mkimtumikia shetani kwa kukosa maarifa ya kuzipambanua roho zidanganyazo,”alisema Askofu Kulola na kutaja makanisa hayo ambayo majina yake ninayahifadhi kwa sasa.
Alisema kuwa kuna dini zimeibuka kama uyoga na viongozi wake wakajipatia majina makubwa, huku wakiwa wanapewa kila kitu kutoka katika makundi ya siri na wala sio Wakristo wa kweli.
Aliitaja miji iliyoboba katika ibada za mashetani kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Shinyanga, na akawahimiza Wakristo safi waliookoka kuepuka kumeza kila fundisho kwa kuwa, hiki ni kipindi cha kutimia kwa unabii wa Bwana Yesu kuwa siku za mwisho kutakuwepo na makristo wa Uongo watakaofanya ishara na miujiza kiasi cha kudanganya hata wateule.
“Ukiona kanisa linajenga fundisho lake katika miujiza pekee, badala ya Neno na kuwaongoza watu kwenye toba na kuishi maisha matakatifu, kimbia hilo sio la Mungu. Muujiza wa kwanza unaopaswa kutiliwa mkazo kwa nguvu kubwa ni wenye dhambi kumpokea Yesu na kuwa wafuasi wake. Mimi sipingi miujiza laa hasha! Lakini sio agizo kuu. Agizo kuu ni kuupa ulimwengu uliopotea habari njema za ufame wa Mungu na kuwafundisha kuyashika yote aliyowaamuru na ishara na miujiza itafuatana na waaminio,” alisema Askofu Kulola.
Kisha akageukia wosia kwa mabinti akisema: “ nakutuma leo ukawaambie mabinti wacha Mungu, wasimame imara kwa Kristo, najua kuna changamoto nyingi wanazokutana nazo; lakini bado wanaweza kushinda na zaidi ya kushinda ikiwa watamtegemea Bwana Yesu, ili siku ya hukumu ikiwa watakuwepo watakaosema walishinda, basi Yesu aseme mbona hawa waliweza,” alisema Askofu Kulola.
Mtumishi huyo ambaye alieleza kwamba yeye hakufanya mambo waliyokuwa wakifanya wenzake enzi zake, aliongeza kwamba, Mungu anaweza kuwatumia ikiwa watasimama na kuwa na msimamo hata ikiwa ni kwa gharama ya kifo.
Alisema vijana wengi wako makanisani, lakini ni kama wanatumiwa na ibilisi kutaka kuwaumiza mabinti kwa maelezo ya kutaka kuwaoa, lakini mwisho wa siku huwageuka na kumwendea mwingine kwa gia hiyo hiyo, huku akichanganua kuwa ni lazima wawe waangalifu kujua yupi anatoka kwa Bwana na yupi ni tapeli.
“Kweli nawalilia sana mabinti zangu, namuomba Mungu awape neema ya kushinda majaribu na vishawishi wa watu wenye nia mbaya, nikienda Israeli lazima nitafanya maombi kwaajili yao,” alibainisha mtumishi huyo kwa uchungu.
Mbali na hilo, Askofu Kulola alieleza kwamba anachukizwa na watu wanaojiita Manabii na Mitume ambao ukiangalia kwa undani utabaini kuwa wako kinyume na Mungu, ingawa machoni pa wanadamu wanaonekana ni watu wenye mapenzi mema.
“Kumekuwepo na wimbi kubwa la watu wanaoibuka na kujiita manabii na mitume, wamekuwa wakielezea watu namna wanavyoweza kuwasaidia kutoka katika matatizo yao kana kwamba ni waganga wa kienyeji,” alisema mtumishi huyo na kuongeza:
“Kipindi hiki kama watu hawatokuwa makini ni wazi kuwa watatapeliwa, kila kitu walicho nacho kwa kudhani kuwa wanamtolea Mungu. Ni vema ikiwa wachungaji watawafundisha waumini wao Neno la Mungu kwa ufasaha ili waweze kutofautisha mtumishi wa kweli na tapeli ‘kanjanja.’
Kama hilo halitoshi mtumishi huyo ambaye yuko kwenye huduma kwa zaidi ya miaka 50 alisema huu ni wakati wa kila mtu kusimama kwa miguu yake mwenyewe, badala ya kutegemea mtu mwingine. Huku akichanganua kwamba Kanisa la Mungu ni lazima liombe kwa bidii ili Mungu alinusuru taifa na majanga mbalimbali ambayo yanaonekana kutaka kubisha hodi hasahasa kwa Nchi ya Tanzania,alisema mtumishi huyo.
No comments:
Post a Comment