Waziri afanyiwa maombi kwasababu ya ugumu wa Wizara.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema ni ngumu kuiongoza wizara hiyo kutokana na kunyemelewa na mafisadi wanaotaka kunufaika na rasilimali zake kwa maslahi yao binafsi.

Simbachawene alitoa kauli hiyo juzi wakati wa ibada maalum ya kumuombea iliyofanywa na Umoja wa Makanisa ya Kikiristo katika Kijiji cha Pwagu, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Akizungumza katika ibada hiyo, Simbachawene alisema kunahitajika nguvu za kupambana ili kuiongoza wizara hiyo kwa kuwa inanyemelewa na mafisadi.


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene
Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, mkoani Dodoma, aliteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuunda upya Baraza la Mawaziri Mei 4, mwaka huu, alisema:

“Vita hii inatokana na uongozi mpya ulioingia katika wizara hii kubana mirija ya mafisadi ambao walikuwa wakitumia rasilimali za serikali kwa manufaa yao.”

Simbachawane alisema kutokana na kuwepo kwa vita hiyo, yeye binafsi kama Simbachawene, hawezi kushindana na mafisadi hao, bali anahitaji nguvu ya Mungu katika kupambana na watu hao.

“Vita ndani ya wizara yangu ni kubwa kwa kuwa wafanyabiashara wote wa umeme wanatuona sisi ndiyo wabaya wao kwa kubana mirija ya ulaji, sasa nahitaji zaidi maombi kutoka kwenu nyote ili kuishinda vita hiyo mimi na wenzangu,” alisema.

“Mimi naapa mbele yenu kama watumishi wa Mungu kuwa katika hili, nitamsaidia Mheshimiwa Rais kwa nafasi aliyonipa kwa kuhakikisha kuwa kilio cha wananchi juu ya wizara hiyo kinanyamaza,” alisema Simbachawene anayeshughulikia nishati.

Simbachawene alisema kwa sasa uongozi wa wizara hiyo umeanza kuona mafanikio baada ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kuanza kuongeza kukusanya maduhuli kuliko ilivyokuwa awali kabla ya kuchukuliwa hatua mbalimbali za kuhakikisha mianya yote ya kubana wizi na hujuma inazibwa.

Naibu Waziri huyo alisema kwa sasa Tanesco inakusanya zaidi ya Sh. bilioni 90 kwa mwezi ingawa lengo ni kukusanya Sh. bilioni 200 kwa mwezi.



Awali akisoma risala kwa Naibu Waziri, Mchungaji Abineri Mazuguzwa, alimtaka Simbachawene kumwogopa Mungu ndani ya moyo wake kwa kuwathamini Watanzania katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.

Mchungaji Mazuguzwa alisema Watanzania wengi wanategemea kuwa uongozi wake ndani ya wizara hiyo, utanyamazisha vilio vyao vya kila siku kutokana na wizi unaofanyika katika wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment