MUUJIZA KAMA WA PAUL NA SILA….. Mch. aliyesubiri kunyongwa huru

•    Alichagua kifo kuliko kumkana Yesu
•    Watu Milioni tatu walimlilia Mungu


“Siwezi kumkana Yesu Kristo, siwezi kuikana imani yangu, sikuwahi kuwa Muislamu, sina ninachoweza kukana..kama ni kufa nipo tayari. Mtaua mwili lakini roho yangu itakuwa kwa Baba mbinguni.”

Hayo ni baadhi ya maelezo ya kijasiri yaliyotolewa na Mchungaji Youcef Nadarkhani (32) wa Iran mbele ya jopo la makadhi waliokuwa wakimpa nafasi ya mwisho ya kumkana Bwana Yesu Kristo aachiwe huru au kuendelea na msimamo wake anyongwe.

Wakati Mchungaji huyo akiwa katika wakati mgumu wa kusubiri kifo cha taabu, huko nje ya nondo za jela watu wenye huruma zaidi ya milioni tatu walikuwa wakisugua magoti chini kumuombea rufaa katika mahakama ya haki (mbinguni) na mataifa yenye nguvu yakipaza sauti juu kushinikiza aachiwe huru.

Mchungaji Youcef Nadarkhani wa Iran
Hatimaye Septemba nane mwaka huu, majibu ya maombi hayo yakadhihirika kwenye macho na masikio ya wanadamu pale tangazo la kuachiwa huru kwa Mchungaji huyo lilipotolewa, na kweli akaachiwa huru na kupokelewa na umati wa wale waliokuwa wakiingoja siku ya Bwana ya kunyoosha mkono wake amuokoe.

Wakati wote ambao Mchungaji Nadarkhani, alikuwa akisubiri kunyongwa alikwisha kata rufaa, katika mahakama ya juu zaidi, lakini akapata pigo kubwa wakati wakili aliyekuwa akimtetea alipokamtwa na kupelekwa mahakamani na haraka haraka akahukumiwa kifungo cha miaka tisa gerezani kwa kosa la kueneza propaganda wakati wa kutetea Wakristo.

Pamoja na wakili kufungwa, tumaini la kupona likiwa limepotea kabisa, muujiza ulidhihirika wiki iliyopita baada ya Jaji wa mahakama kuingia mahakamani na kupitia rufaa hiyo kisha kutoa hukumu kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo mchungaji huyo yalikuwa kinyume cha sheria za taifa hilo.

Jaji katika hukumu yake hiyo alidai kuwa Mchungaji Nadarkhani hakustahili kutiwa hatiani kwa makosa ya kuuasi uislamu na kujiunga na Ukristo, kosa ambalo adhabu yake ni kifo, bali alistahili kushtakiwa kwa kosa la kuhubiri Injili kwa Waislamu. Kosa hili adhabu yake  ni kufungwa jela miaka mitatu.



Jaji huyo ambaye jina lake halijatajwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama, alimhukumu adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na kisha kuamuru aachiwe huru kwa kuwa tayari ameshatumikia kifungo hicho wakati akisubiri kusikilizwa kwa rufaa au amri ya kiongozi wa kidini Ayatollah Ali Khamenei ili anyongwe.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka katika mahakama hiyo, kuachiwa kwa Mchungaji huyo shujaa wa imani ni muujiza tu kwa kuwa mazingira ya kesi na hata kukosekana kwa wakili wa kumuwakilisha kwenye rufaa vilitosha kumfanya ashindwe kama sio Mungu kuingilia kati.

Mashuhuda wanasema kuwa ushindi huo wa watu wa Mungu waliosugua magoti kuomba, wakiishi kwa imani ni kama ilivyokuwa kwa  akina Daniel, Meshacki na Abednego katika nyakati za Biblia walipokuwa mikononi mwa wauaji kwa mashtaka ya kugoma kusujudia sana.
Kwa zaidi ya matoleo saba, Gazeti la Jibu la Maisha, limekuwa likifuatilia habari za Mchungaji Nadarkhani kwa kina hatua kwa hatua, hadi kuachiwa kwake.

Inaelezwa kuwa tangu kukamatwa kwake mwaka 2009 na kutupwa gerezani yamefanyika majaribio kadhaa ya kutaka amkane Yesu ili aachiwe huru, lakini alikataa na kuchagua kifo badala ya uislamu.

Msemaji wa Kituo cha Sheria na Haki cha Marekani (ACLJ), shirika ambalo lilisaidia kumtetea Mchungaji Nadarkhani, Bw.  Jordan Sekulow alisema, shitaka kubwa lililopelekwa mahakamani dhidi ya mtumishi huyo ni kukataa kukana imani yake ya kikristo.

"Leo Mchungaji ameachiwa huru na anaungana na familia yake, lakini lazima tujue kwamba tukio hilo la Mtumishi huyu ni mfano kwamba dunia inaweza kuungana kuleta uhuru wa kuabudu na haki kwa kila mmoja,” alisema Sekulow.

Kiongozi mwingine wa ACLJ aliyezungumzia kuachiwa huru kwa mchungaji huyo ni, Bw. Tiffany Barrans, aliyeliambia Fox News.com kuwa:
“Wakati tunaendelea kumsifu Mungu kwa mambo makubwa aliyoyafanya,  kumtoa Mchungaji Nadarkhani, mikononi mwa ‘wafilisti’ lazima Iran itambue wajibu wake na kuwapa watu uhuru wa kuabudu bila kutengeneza mbinu za kutishana.”

Kisha akaongeza:  “Tunashukuru Mungu kwamba kwa namna moja au nyingine muungano wa watu zaidi ya Mil. 3 duniani kote kutoa maoni yao kumtetea Mchungaji Nadarkhani, kupitia mitandao ya Twitter, Facebook na mingine, imesaidia kuachiwa huru na pia maombi ya watu wa Mungu.”

Baada ya kushtakiwa kwa kosa la kukataa kumkana Kristo na kuwekwa kizuizini kwa takriban miaka mitatu, bado aliendelea kusumbuliwa akiwa gerezani ili amkane Bwana Yesu, lakini aliendelea kukataa hadi Desemba mwaka jana ambapo alikuwa ikisubiriwa Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mwenye mamlaka kubwa katika masuala ya kiroho nchini Iran aamue moja kumwachia huru au kumnyonga.

Hata hivyo kwenye magereza ya taifa hilo la kiislam bado kuna mamia ya watu waliofungwa kwa kuonewa na wengine kwa sababu za kutetea imani yao.

No comments:

Post a Comment