Katibu Mkuu wa Baraza la makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Askofu David Mwasota |
Hatimaye Katibu Mkuu wa Baraza la makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Askofu David Mwasota, amevunja ukimya wa tuhuma zilizosambazwa sehemu mbali mbali zikieleza kuwa amenaswa na kundi la siri la waabudu shetani Freemasons.
Akiongea na chanzo cha habari cha blogger kwa uchungu, Askofu Mwasota alisema:
“Ndugu yangu naona haya ni mashambulizi, nimezushiwa mengi achilia mbali yaliyoandikwa na magazeti, jumbe zinasambazwa kwa watumishi wa Mungu (wachungaji) wakae mbali na mimi eti nimekuwa freemasons, lakini haya yote ni mashambulizi tu…”
Akifafanua zaidi alisema: “Nakwambia ukweli kutoka moyoni mwangu, sijui hata kiongozi mmoja wa kundi la Freemasons, wala sijui hata hekalu lao liko wapi, mimi nilikuwa nafundisha kanisani nikawaonya wapentekoste wakae mbali na watu wasiowajua kwa kuwa wengine ni waabudu shetani, na wanawajia kama watu wema ili kuwarubuni,”alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Nikatoa mfano wa waumini wangu na mimi mwenyewe, nakumbuka niliwaambia kuwa niliwahi kuhudhuria semina moja na baada ya kukamilika nilipewa nishani ambayo baadaye nilikuja kubaini kuwa ilikuwa na nembo nisisozielewa, sikusema ni ni nembo za Freemasons, nilisema nisizozielewa, nikaamua kuitupa hiyo nishani, lakini naona waandishi waliamua kunimaliza, namwachia Mungu aamue kati yetu…”
Alipoulizwa ni semina gani hiyo na kama anauhakika kuwa nembo alizoshtukia sio za kundi hilo, alijibu:
“Sikia ndugu…nilichosema kilikuwa ni mfano tu wakati nahubiri, nilimaanisha kuwa nembo hizo sikuwa na uhakika nazo, hiyo haimaanishi zilikuwa ni za kundi la Freemasons, nimekwisha kueleza sijui hata kiongozi mmoja wa kundi la Freemasons, wala sina haja nao, mimi nimeokoka naenda mbinguni waabudu shetani ni wanini?”
“Jambo la kustaajabisha zaidi ni kuwa wewe ndio Mwandishi wa kwanza kuongea nami, kuhusu jambo hili kwa mapana yake, wengine walinipigia simu nikawaambia waje ofisini sikuwaona, lakini nikashtukia habari kubwa imeandikwa, hii inaniuma sana…”
Askofu Mwasota, alisema kuwa ameshauriwa juu ya jambo la kufanya na anajiandaa kuchukua hatua kwa kuwa anaona kuwa kuna njama mbaya dhidi yake, huduma anayoiongoza na kanisa la Mungu kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa katika ibada hiyo lengo la mahubiri yake lilikuwa ni kuwaonesha wapentekoste hatari iliyopo mbele yao kwa kuwa makundi hayo ya waabudu shetani yapo na yanawawinda.
“Mimi ni Askofu na kiongozi wa baraza la Wapentekoste, ilikuwa ni wajibu wangu kuonya wenzangu, lakini mifano yangu ilipinduliwa kwa makusudi. Nadhani wakati nahubiri kulikuwa na mwandishi wa (jina linahifadhiwa) ambaye aliichukua kama alivyotaka,” alisema Askofu Mwasota.
Kwa karibu wiki nzima kumekuwa na jumbe mbali mbali zinazosambazwa kupitia simu zikieleza kuwa Askofu Mwasota amenaswa na kundi la Freemasons na kuwataka wapentekoste kukaa mbali naye.
Baadhi pia ya waumini wa makanisa ya Kipentekoste na hata wachungaji wamekuwa wakiulizana huku na kule wakitaka ukweli kuhusu habari za kiongozi huyo wa ngazi ya juu katika baraza la Wapentekoste kutajwa na kundi hilo.
Kutokana na kiu hiyo ya watu wa Mungu, Blog hii liliamua kuchunguza ukweli wa jambo hilo kuanzia kwa Askofu mhusika na vyanzo vingine vya habari ili kutoa jibu kwa wenye kuguswa na mkanganyiko huo.
Baadhi ya watu wa karibu na Askofu Mwasota, waliofanya mahojiano ya siri nachanzo kimoja cha blog wameeleza wasi wasi wao kuwa kuenea kwa kasi kwa habari hiyo na mazingira yake vinaashiria kuwa huenda kuna mbegu ya chuki inayochochea jambo hilo.
Mmoja wa watu waliohudhuria ibada siku Askofu Mwasota alipohubiri na kuwaonya watu kukimbia makundi ya wale wanaowajia ghafla kama malaika wa nuru, alisema:
“Mimi nilikuwa kwenye ibada siku Askofu Mwasota alipohubiri na kutoa mifano; nilichosikia akisema ni kuwa alihudhuria semina na mwisho akapewa nishani ambayo baadaye alibaini kuwa na nembo, ambazo hakuwa na uhakika nazo na kwa kutotaka kujichanganya akaamua kuitupa, wala hakusema kuwa amehudhuria mkutano wa Freemasons.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na mlipuko wa makundi ya vijana wanaosaka jinsi ya kujiunga na kundi la Freemasons wakidai eti ni suluhisho la maisha magumu.
Habari za kuenea kwa kasi kwa kundi la Freemasons zimekuwa zikivuta hizia za watu wengi, wengine wakidhani kuwa kujiunga nao kunaweza kuwafanya kuwa tajiri.
No comments:
Post a Comment