Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue Ombeni, amepinga vikali madai yaliyotolewa na maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste nchini, kuwa Serikali imepuuza majina yaliyopendekezwa na makanisa hayo kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi kwa niaba ya Balozi Ombeni, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florence Turuka, alisema Serikali haikupuuzia kundi lolote lililoainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko, kuwakilisha mapendekezo ya Bunge Maalum la Katiba.
Alisema walijaribu kutafuta mapendekezo ya makanisa hayo kwenye Kanzi Data ya Msingi (Primary Data Base), lakini hawakuona chochote.
"Uchambuzi ulifanywa ili kubaini kama kulikuwa na mapendekezo kutoka Baraza kati ya mapendekezo 850 yaliyowakilishwa, lakini hakukuwa na taarifa za majina ya waliopendekezwa,"alisema Dkt. Turuka na kuongeza kuwa;
"Majina ya maaskofu watano walioshiriki katika utoaji taarifa kwa vyombo vya habari yalitumika ili kubaini kama wao pia walikuwa miongoni mwa waliopendekezwa."
Alisema utafutaji huu haukubaini kuwa Baraza lilikuwa moja ya taasisi zilizowasilisha maombi. Alisisitiza kuwa hakukuwa na jina hata moja la viongozi wa Bara walioitisha mkutano na vyombo vya habari kutoa taarifa za kulalamikia uteuzi wa wajumbe kutoka Baraza hilo kwa madai kuwa wametengwa.
Mbali na hilo, alisema kuwa juhudi za Serikali zilijielekeza kutafuta endapo kulikuwa na mapendekezo ya kundi hilo. "Hata hivyo utafutaji haukubaini majina ya viongozi hao kuwepo katika orodha hiyo,"alisisitiza Dkt. Turuka.
Kwa mujibu wa Dkt. Turuka, kulikuwa na uwezekano pia Baraza liliwasilisha mapendekezo ambayo yalifika kwa Katibu Mkuu Kiongozi nje ya muda uliopangwa kisheria wa Januari 2, mwaka huu.
Alisema uchambuzi wa mapendekezo 52 ambayo yaliwasilishwa nje ya muda haukubaini kuwepo kwa mapendekezo kutoka kwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania. Alisema juhudi za Serikali katika kufuatilia uwepo wa mapendekezo kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hazikuweza kuthibitisha kuwa Baraza lilituma mapendekezo yake kama ilivyokuwa imeagizwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa msingi huo, alisema tamko la Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste kudai kuwa wamebaguliwa halina ukweli, kwani uchunguzi waliofanya haujathibitisha kuwa Baraza lilipeleka mapendekezo.
"Ni vyema Baraza likafanyia kazi kwa nini kama kulikuwa na mapendekezo hayakufikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi (Dar es Salaam) au Katibu Mkuu Kiongozi (Zanzibar)...tunaamini kabisa kama mapendekezo hayo yangekuwa yamewasilishwa, Rais angechagua mwakilishi kutokana na mapendekezo hayo," alisema.
Alisema Baraza hilo kutokuwa na wawakilishi, lakini litawakilishwa vyema na wajumbe walioteuliwa. Hivi karibuni maaskofu watano wa Makanisa ya Kipentekoste waliitisha mkutano wa waandishi wa habari wakilalamikia mjumbe wao kutopata uwakilishi katika Bunge hilo la Katiba ambalo limeanza juzi.
source Majira
No comments:
Post a Comment