Kanisa lavamiwa Jijini Dar

Vitendo vya kuvamiwa kwa makanisa nchini, vimekosa mwarobaini hivyo kuvutia maadui wa ukristo kuendelea kuharibu nyumba za ibada bila hofu. Tukio la hivi karibuni, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Mbezi Kati, kuvamiwa usiku tena wakati ambao vijana walikuwa wakiendela na mkesha ni ushahidi kuwa hali inazidi kuwa mbaya badala ya suluhisho kupatikana.
   
 Mchungaji Samson Swai wa kanisa hilo, akizungumza na chazo cha habari alisema kuwa, Ijumaa flani majira ya saa saba usiku, alipigiwa simu na vijana waliokuwa katika mkesha kanisani hapo na kumjulisha kuwa palikuwa na mtu aliyefahamika (jina tunalihifadhi kwa sasa) ameliharibu kanisa kwa kubomoa milango yote.
  
Aliongeza kuwa mara baada ya taarifa hiyo alipiga simu kituo cha Polisi Kawe, na kuwajulisha kuhusu tukio na walipofika eneo la tukio,mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa maeneo hayo alikwisha kimbilia nyumbani kwake.

  Alisema, uharibifu uliofanywa na mtu huyo majira hayo ya usiku mnene bila sababu ya msingi ni kuing'oa milango vibaya.Kwa mujibu wa Mchungaji Swai, Polisi walionyeshwa nyumba anamoishi mtuhumiwa huyo na walipofika nyumbani kwake kwa lengo la kujua sababu ya kufanya uharifu huo, hakuwafungulia mlango licha ya kumgongea  kwa muda mrefu lakini  jitihada hizo ziligonga mwamba, hivyo Polisi kuahidi kumfuatilia.
 Mchungaji Swai aliweka wazi kuwa, ikiwa Serikali haitaiangalia kati suala la uvamizi wa makanisa na kulishughulikia kwa jicho pevu; huenda vikatokea vita vya kidini, wakristo watakapochoka na matukio hayo kila kona.

 Mtumishi huyo alisema baada ya kushindwa kumpata mtu huyo, Polisi waliondoka eneo hilo, na kesho yake mtu huyo aliendelea kujigamba kuwa, Jeshi la Polisi limeshindwa kumtia hatiani ili aeleze nani anamtuma kufanya uhalifu katika nyumba ya Bwana.

Mtu huyo anayehisiwa kuwa, pengine alikuwa na silaha ya moto, anadaiwa kuendelea kutamba mitaani kuwa hakuna wa kumfanyajambo lolote na ataendelea na mashambulizi yake.

Pengine Serikali isipokuwa makini na kung'oa mizizi hii, hali ya vurugu inaweza kuchukua nafasi mpya na kusababisha kutoweka kwa amani na kuifanya Tanzania yenye sifa ya kuwa 'kisiwa cha amani' kupoteza sifa hiyo ya kipekee na kuingia kwenye sintofahamu.

Chanzo chetu kilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, ambaye alisema kuwa, taarifa ya kuvamiwa kwa kanisa haijafika mezani kwake na kuahidi kulifuatilia, na kubainisha kibarua hicho amemwachia OCD kulifuatilia kwa karibu ili apate taarifa.

No comments:

Post a Comment