Viongozi wa dini wameombwa kuelimisha wananchi juu sensa ya watu na makazi.

Viongozi wa dini mkoani Tabora wameombwa kuelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchini Agosti, 26, 2012 ili kuisaidia serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya mipango endelevu ya maendeleo ya taifa.

Mwenyekiti wa kamati ya sensa Mkoa wa Tabora, Bi. Fatma Mwassa alitoa ombi hilo kwa viongozi wa madhehebu ya dini wiki iliyopita mkoani humo ambapo aliwasihi kutumia nafasi zao wanapokuwa kwenye madhabahu kuwakumbusha waumini wao kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa.  
Alisema viongozi wa dini wana nafasi nzuri katika kuwahamasisha waumini wao, pindi wanapokuwa katika ibada zao, hivyo wamewahimiza kutumia nafasi hizo katika kutoa elimu ya sensa ambayo baadae itasaidia serikali kupata kupanga mipango yenye maendeleokwa wananchi wake.
Mwenyekiti huyo alisema, kutokana na ushawishi mkubwa walionao viongozi wa dini kwa wafuasi wao, wanamchango mkubwa katika kuwaelimisha umuhimu wa sensa.

Sambamba na hilo alibainisha kwamba, ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wakati wa zoezi la sensa utaleta mafanikio makubwa na kuiwezesha  serikali kufanya maamuzi sahihi na kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi wake.

Hata hivyo aliongezea kuwa, takwimu sahihi ya idadi ya wakazi wa Mkoa wa Tabora italiwezesha taifa kutenga fedha za kutosha kwa maendeleo mkoani humo kulingana na idadi ya wakazi wa kila Wilaya.

Alisisitiza kuwa, suala la msingi ni kuhakikisha kila mtu atakuwepo nchini tarehe Agosti 25 na 26 mwaka huu anahesabiwa mara moja.
Nao viongozi wa dini walioshiriki kwenye mazungumzo hayo, walimuahidi mkuu huyo kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa zoezi la sensa linafanikiwa ikiwa ni pamoja na kujua umuhimu wa sensa kwa kushiriki kikamilifu.

Akizungumza kwa niaba ya mwenzake, Askofu wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Tabora, Mchungaji Elias Chakupewa alisema, viongozi wa dini watatumia vizuri nafasi walizonazo ili kuhakikisha waumini wao wanapata elimu ya sensa kwa ufasaha.

Kadhalika alibainisha kuwa, viongozi wa dini ni watu muhimu katika zoezi hili la sensa kwani,wanaamini kuwa kupitia madhabahu yao waumini wengi watapata kufahamu muhimu wa sensa na kisha kuona umuhimu kwa kushiriki na hivyo kuisaidia serikali kupata takwimu kwa ajili ya kupanga maendeleo ya taifa.

Mbali na hilo, Askofu Chakupewa amewaomba waumini wa madhehebu yote kushiriki zoezi la sensa kwani,hii itasaidia serikali ya Mkoa na taifa kwa ujumla kupanga mambo mbalimbali.


No comments:

Post a Comment