MKUTANO
Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), ambao unafanyika kila baada ya miaka minne unaoambatana na uchaguzi wa
viongozi wa ngazi mbali mbali, unaanza Jumatano tarehe 8, Agosti mjini Dodoma na kuendelea kwa
karibu wiki nzima.
Kwa
mujibu wa takwimu za makao makuu, zaidi ya watumishi wa Mungu 3000 wanatarajia
kukutana Dodoma na Mkutano Mkuu utafanyika
katika Chuo Kikuu cha Dodoma,
ukitanguliwa na vikao vya Halmashauri
kuu na Baraza la Waangalizi.
Akiongea na waandishi wa habari, katika
mahojiano maaalumu wiki iliyopita, Naibu
Katibu Mkuu (Shughuli) wa kanisa hilo, Mchungaji Uswege Mwakisyala, alisema kuwa,
mkutano huo mkuu utafanyika Chimwaga mjini Dodoma, na watu watakaohudhuria wanakadiriwa
kufikia 3000, ingawa sio wote watakao piga kura.
Mchungaji Mwakisyala
alieleza kuwa, siku ya Jumatatu (Agosti 6, 2012) kutakuwa na kikao cha
Halmashauri Kuu, huku kikifuatiwa na kikao cha Baraza la Waangalizi
kitakachofanyika siku ya Jumanne.
Alibainisha kwamba siku ya
Jumatano ndio mkutano mkuu utaanza kufanyika ambao utahitimishwa Ijumaa.
Hata hivyo Mchunagji
Mwakisyala akitolea ufafanuzi juu ya utaratibu wa kuwasili mkoani humo
alitanabaisha kwamba, Halmashauri Kuu watawasili siku ya Jumapili, tayari kwa
kuanza kikao Jumatatu na waangalizi watawasili Jumatatu.
Mbali na hilo aliongeza
kwamba, Wachungaji wote watakaowasili siku ya Jumanne, Agosti 7, 2012
watatakiwa kwenda moja kwa moja katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Jumapili watawasili Halmashauri
Kuu, Jumatatu Baraza la Waangalizi na Jumanne wachungaji wote, na itakuwa ni
vizuri ikiwa wataingia kwa makundi makundi, kwa kufanya hivyo magari
yatawaingiza moja kwa moja hadi chuoni,”
alisema.
Katika mkutano huo mkuu, Kwaya
mbalimbali na waimbaji binafsi watasindikiza uchaguzi huo.
Uchaguzi uliopita ulifanyika
Oktoba 2008, ambapo Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali, alichaguliwa
kuliongoza kanisa hilo, huku Makamu wake akiwa Dk. Magnus Muhiche, na nafasi ya
Katibu Mkuu ikichukuliwa na Mchungaji Ron Swai.
Katika muhula wao wa
uongozi, Askofu Mkuu, Dk. Mtokambali, na timu yake walikuja na Kauli mbiu ya
Miaka Kumi ya Mavuno iliyokuwa na lengo la kuleta watu milioni mbili kwa Yesu.
Wakati wanaingia madarakani,
kanisa hilo lililokuwa na waumini 200,000 mwaka 2008, lakini hadi sasa (Mwaka
2012) lina waumini 433,546. Wachungaji walikuwa 2600 sasa wako 4527, makanisa
yalikuwa 2134 sasa yako 4492.
Pia Seksheni zilikuwa 75, lakini
sasa ni 204 huku majimbo nayo yakibadilika kutoka 10 hadi 25.
Kimsingi uchaguzi wa TAG,
huongozwa na Roho Mtakatifu mwenye na hakuna wagombea wala kampeni, bali Bwana
mwenyewe hujitwalia viongozi.
Wasimamizi wa uchaguzi
wanatarajiwa kuwa wamisheni kutoka Marekani.
No comments:
Post a Comment