Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Dar akimbia Kundi la Freemason.

Aliyewahi kuwa mshindi wa kwanza wa  mashindano ya kuimba na kucheza muziki yanayojulikana kama Bongo Star Search  (BSS) mwaka 2009, Paschal Cassian, amedai kukimbia kutoka katika kundi la waabudu shetani la  Freemasons, tawi la Dar es Salaam,  akiwa katika hatua za mwisho kusaini kiapo kisichovunjika.

Huyu ni miongoni mwa wanadamu wachache wanaokiri kurubuniwa na kuingia katika makundi hayo ya waabudu shetani. Mtanzania mwingine aliyewahi kujitapa hadharani kuwa mwanachama wa kundi hilo tena mwenye hati takatifu ya kuhani Mkuu ni Andy Chande.

Kijana huyo aliyeingia jijini Dar es Salaam, akitokea mjini Mwanza ambako alikuwa muumini wa kanisa la Wasabato, alianza kuimba kwenye mashindano hayo akiwa anaimba nyimbo za injili, lakini akabadilika na kusakata rumba iliyompelekea kuwa mshindi wa shindano hilo linaloandaliwa na Kampuni ya Beanch Mark Production ya jijini  Dar es Salaam, na kurushwa na kituo cha Luninga cha ITV.

Mwimbaji wa nyimbo za Injili na aliyewahi kuwa Mshindi wa Bongo Star Search (BSS) mwaka 2009 Paschal Cassian
Akiongea katika mahojiano maalum Sinza, jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, mara baada ya kushuka jukwaani alipokuwa akiimba katika ibada maalumu ya kusifu na kuabudu iliyoandaliwa na kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Sinza alisema kuwa alikimbia kutoka katika kundi hilo akiwa bado hajasaini hati ya kiapo ambacho ni kifungo cha umilele.

Cassian kabla ya mahojiano hayo aliuambia umati wa wale waliohudhuria ibada hiyo kuwa alikimbia kutoka katika kundi hilo la waabudu shetani baada ya kuhudumu kwa miezi minne na kushiriki mipango mingi michafu.

JINSI ALIVYOINGIA FREEMASONS
Akieleza alivyojiunga alisema: “Baada ya ushindi wangu wa BSS, nilipata umaarufu mkubwa nikawa naitwa sehemu mbali mbali kuimba na kucheza. Ni wakati huo nilipopigiwa simu na watu nisiowafahamu wakanieleza jinsi ambavyo mimi ni mtu maarufu na umaarufu wangu unanipa sifa ya kujiunga na chama cha kijamii ambacho kitanifanya kuwa mtu maarufu zaidi na tajiri sana.”



Kisha aliongeza:  “Nakumbuka mtu huyo alianza mawasiliano nami tangu siku ile nilipopata ushindi, nilipomaliza tu alinipigia simu, sikuwa namfahamu lakini baada ya maongezi mengi hatimaye aliniambia kuwa yeye ni mwanachama wa chama cha kijamii chenye kuwatengeneza watu kuwa maarufu.  Nilipodadisi aliniambia kuwa kinaitwa Freemasons aliniambia kuwa nafasi iko wazi kwangu kujiunga ili kutimiza ndoto zangu. Nilijiuliza sana, lakini baadaye nikaona sina budi kujiunga, niliamini huko kuna pesa nyingi.”

“Nilikaa humo kwa muda wa miezi minne, kweli nilipata pesa na vitu vingi kwa kipindi hicho kidogo, nilipofikia hatua fulani nilitakiwa kuweka mikataba, kweli hapo nilishindwa, niliamua kikimbia, unajua siwezi kukueleza kwa undani leo, si jambo jepesi; hivi unavyoniona huwa napigiwa simu za vitisho, naomba mniombee sijawa na uhakika na maisha yangu juu ya kundi hilo.”

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa kwa siku hizo chache alizokuwa kundini humo, aliweza kuonana na viongozi mbalimbali ambao ni wanachama; wanasiasa maarufu, waimbaji na pia watu ambao wanajiita watumishi wa Mungu wenye makanisa makubwa yanayochipua ghafla, jijini Dar es Salaam.

“Kwa sasa siwezi kuwataja kwa kuwa wanaweza kunidhuru, nawaomba wachungaji waniombee ili pale nitakapo weka wazi kila kitu niwe na ulinzi wa kutosha wa Bwana Yesu, lakini hata hivyo nitawataja siku chache zijazo, nitawaweka peupe kuna siri nyingi ambazo sikuwa nazifahamu, lakini sasa nazijua,” alisema na kuongeza:



“Kuna uchafu mwingi sana unaofanywa na hawa watu, kwa kawaida wanaonekana ni wema na wa maana; wanafanya mambo makubwa ya ajabu, sitoacha hata mmoja, wakati ukifika nitakuwa  radhi kufa, lakini niwe nimeshaweka hadharani kila kitu, ndio maana unashangaa kuona mtu anaanzisha huduma leo na kesho watu wamejaa, yote hayo nitayaweka hadharani niombeeni tu.”
Hata hivyo alisema namna nzuri ya kuweka wazi mambo hayo, ili kila mtu ajue na wakati mwingine kujifunza ameamua kuweka kwenye filamu ambayo itatoka mapema mwaka 2013.

Alisema hiyo ndiyo njia nzuri ambayo itamuwezesha kila atakayependa kuwa na muda mzuri wa kutazama. Itasaidia duniani watu wajifunze hatakama mimi nitaondoka katika mwili huu wa nyama nitakuwa nimetimiza wajibu wangu.

Mbali na hilo alisema ndani ya filamu hiyo atawashirikisha watu mbalimbali wakiwemo wachungaji, waimbaji wa nyimbo za Injili na watu wengine maarufu, huku akiongeza kwamba, inatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni sita.

“Filamu ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe, katika sinema nitaeleza kila kitu, ni filamu yenye ujumbe wa kweli na wala sio kama zingine za matukio ya kufikirika,” alisema.

Alibainisha kuwa, ingawa awali alikuwa msabato, lakini hakuwa amempa Yesu maisha yake kuwa kiongozi wake, hivyo aliishi maisha yenye mvuto na tamaa ya dhambi na kuwa rahisi kunaswa na chambo cha waabudu shetani.

Aliingia kwenye kundi hilo kutokana na kutomjua Yesu kikamilifu, huku akibainisha kuwa baada ya kutoka Freemasons aliamua kuokoka na sasa anaabudu katika kanisa la uwanja wa sifa ambapo hata hivyo Mungu amempa neema ili aweze kumwimbia na kwa sasa ameweza kuachia albamu mbili ya kwanza ikiwa na jina la Yerusalemu, huku ya pili ikibeba ujumbe wa Wasamehe bure.

Awali Cassian akiwa katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Sinza Refuge Centre, lililo chini ya Mchungaji Saiko Sheyo, katika ibada ya kusifu na kuabudu, alimsifu na kumwimbia Bwana nyimbo mbili za albamu yake ya pili.

Aliwaasa Wakristo kusimama na Kristo na kuamini kila hitaji lao watalipata kwa wakati wa Bwana badala ya kufanya kosa  kama lake la kutanguliza tamaa ya utajiri wa haraka .

Wakati mwimbaji Mwasote akiendelea kuimba,  huku kanisa zima likiwa limesimama na kila mtu akionekana kuguswa  na Roho Mtakatifu na wengine  kunena kwa lugha mpya,  watu waliokuwa na mapepo yalilipuka na kukimbia na waliokuwa wagonjwa hawakujua ni muda gani walipokea miujiza yao.

Source:Jibu la Maisha

1 comment:

  1. Anamaanisha kuacha kweli? na miezi yote aliyohudumu na kundi hilo alikuwa hajui anafanya nini?

    Hofu yangu ni asije akaingia na hiyo roho kanisani.

    ReplyDelete