Masheikh na Wanazuoni wa Kiisilamu wamruka Ponda.

Taasisi  ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiisilamu Tanzania imesema mhemko na ghadhabu zilizoonyeshwa na kikundi cha Waislamu na kutoa mwanya wa kutendeka uhalifu wa kuchomwa makanisa eneo la Mbagala, jijini Dar es Salaam siyo mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Kadhalika, Taasisi hiyo imesema kwa sasa ikipata fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania,  Sheikh Ponda Issa Ponda, itamshauri azingatie mafundisho ya Uislam katika kufanya mambo yake.
Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania,  Sheikh Ponda Issa Ponda
Tamko hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Sheikh  Khamisi Mataka, alipozungumza na waandishi wa habari.

Sheikh Mataka alisema kitendo cha kikundi cha watu kukataa kutii mamlaka za serikali zilizopo ni sawa na kupinga amri za Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Kitabu kitakatifu Qur’aan.

Tukio la kuchomwa makanisa lilitokea Oktoba 12, mwaka huu katika eneo la Mbagala baada ya kijana mmoja kukojolea Qu’raan tukufu hatua ambayo ilidaiwa kuamsha hasira.

Aidha, Taasisi hiyo imelipongeza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kwa kufanikiwa kutuliza ghasia zote kuanzia zile za kuchoma makanisa, zilizotokea Ijumaa iliyopita katika eneo la Kariakoo na Zanzibar bila ya kugharimu roho yoyote ya Mtanzania.

Sheikh Mataka aliwataka Waislamu kurejea mafunzo ya Mwenyezi Mungu yanayohimiza kumfanyia uadilifu hata adui yake (Qu’raan Surat Al-Maida (5) Aya ya 8  na kwamba kuvunja sheria za nchi kusiwe mtaji wa kudai haki.

Alisema vikundi vinavyoleta vurugu Tanzania Bara na Zanzibar havijui mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa vinataka haki ya kuhukumu.

Taasisi hiyo inatarajia kuitisha kikao cha Masheikh na viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislam ili kutafuta dawa ya kumaliza vurugu za kidini zinazoibuka mara kwa mara.

Sheikh Mataka alisema baada ya kufanyika kikao hicho, taasisi yake itawakutanisha viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislam na Kikristo ili kujadili njia bora ya kudumisha amani, utulivu na uhusiano mwema kwa wananchi wote nchini.

Aliwaonya wanasiasa kutoingilia na kuanza kushawishi vikundi vya kidini kufanya vurugu na kukataa kutii mamlaka halali zilizopo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment