Vurugu hizo zilihusisha uchomaji wa makanisa na uharibifu wa mali yakiwemo magari, baada ya waumini hao kuvamia kituo cha polisi kwa lengo kumchukua na kumdhuru mtoto mwenye umri wa miaka 14.
Mtoto huyo anadaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha Koran.
Hali ilionekana kuwa mbaya katika eneo hilo na kuwalazimu baadhi ya watu kuyakimbia makazi yao ili kuokoa maisha.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya mtoto huyo kufikishwa kituo cha polisi cha Mbagala Kizuiani kwa ajili ya kuandikisha maelezo, ambapo waumini hao walivunja vioo vya magari ya polisi, kisha zinaenea katika mitaa mbalimbali ya eneo hilo.
Makanisa matatu yakishambuliwa kwa kuvunjwa vioo na mengine kuchomwa moto nayo ni Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mbagala zakhem, kuharibu Kanisa la Anglican,kuvunja vioo katika kanisa la Wasabato, huku kanisa la Tanzania Assembly of God(TAG), Mbagala kizuiani wakilichoma moto na kuchukua vifaa vya muziki na kuviunguza hadharani. Kanisa hilo la TAG linaongozwa na Makamu Askofu wa TAG Dr. Magnus Muhiche.
Waumini hao pia walizuia barabara kwa kuchoma moto matairi ya magari katika barabara ya Kilwa na kusababisha magari kushindwa kupita.
Hamisi Salum Baba wa Kijana ambaye Quran yake ilifanyiwa vibaya.
|
"Hali ni mbaya kila sehemu ni milio ya bunduki na risasi, wananchi tumeamua kukimbia baada ya kushauriwa kuondoka haraka eneo hili, " alisema Abubakar Salum Mkazi wa Mbagala Kizuiani.
Polisi mkoani Dar es Salaam, walifanikiwa kumuokoa kutoka kwenye kifo mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14 baada ya waumini hao wenye hasira kuzingira kituo cha polisi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akizungumza katika kipindi maalum kilichorushwa na ITV jana, alisema katika tukio hilo licha ya uharibifu wa makanisa, pia limesababisha magari na mali nyingine kuharibiwa na watu hao.
Kamanda Kova alisema oktoba 10 mwaka huu huko Chamazi, watoto wawili ambao ni marafiki-majirani wakiwa wanacheza mpira, walianza kutaniana huku mmoja mwenye miaka 12 akiwa na kitabu cha Koran akitokea madrasa, alimwambia mwenzake (miaka14), kama atakapokojolea kitabu hicho anaweza kugeuka panya ama nyoka.
“Katika mabishano hayo, kijana huyo akaamua kukojolea Korani hiyo, hali iliyomfanya mtoto wa kiislamu ashitaki kwa baba yake ambaye mzazi huyo alienda kwa wazazi wa kijana (mtuhumiwa) na kuelezea tukio hilo,” alisema Kova.
Alisema kutokana na umri wa watoto hao na mazoea yao ya kutaniana, haikutarajiwa kuwa hali hiyo ingeweza kuzua vurugu kubwa kama hizo.
"Ukiangalia umri wa watoto wenyewe, mmoja ana miaka 14 na mwingine ana miaka 12...ni wadogo sana na wamezoea kutaniana kila wanapokutana," alisema na kuongeza kuwa haikutarajiwa kuwa kama watu wakubwa wangeweza kuingilia.
Alisema kutokana na wazazi wa familia zote mbili kuishi majirani, waliamua kumaliza ‘kesi’ hiyo nyumbani, lakini leo mzazi wa kiislamu aliamua kwenda na vijana wote wawili kituo cha polisi Chamazi kutoa taarifa ya tukio hilo.
Kamanda Kova alisema baada ya taarifa hizo kuandikishwa Chamazi waliamriwa waende kwa OCD kituo cha Mbagala ambako ndiko walikokutana na waumini hao waliotaka kupewa maelezo ya polisi kuhusu tukio hilo.
Baada ya watu hao kufahamishwa na OCD wa Mbagala kuhusiana na tukio hilo, ndipo waliamua kuhamasishana ili wamtoe kijana huyo ndani ya kituo cha polisi na kumdhuru kwa kumuua, lakini polisi wa kutuliza ghasia walifanikisha kumuokoa na kuwekwa katika mikono salama.
“Watu hao walivunja kioo cha gari la OCD wa kituo hicho pamoja na jingine aina ya Noah, lakini baada ya kutangaziwa hali ya hatari na FFU baadhi yao waliondoka na wengine kukaidi amri hiyo,” alisema.
Kova alisema watu hao baada ya kuona wameshindwa kumpata mtoto huyo waliendeleza vurugu katika maeneo mbalimbali ya Mbagala na kuvamia makanisa kwa kuiba vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa shughuli ya kanisa ikiwemo vya muziki na kuharibu vioo na milango ya kanisa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadiki, alilipongeza jeshi la polisi mkoani humo kwa kudhibiti na kumuokoa kijana huyo asidhuriwe na waumini hao waliokuwa na jazba.
Aliwasihi viongozi wa dini zote kurejesha amani na upendo kwa waumini wao ili matukio ya kisasi yasiweze kutokea na wapate kipindi kizuri cha kuvumiliana.
Akizungumzia tukio hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum, aliwataka viongozi wa misikiti yote mkoani humo kuwaelekeza waumini wao kutopandikiza chuki kwa dini nyingine, hali ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa.
“Wakristo wasihukumiwe kutokana na tukio hilo, kwani aliyefanya hivyo ni mtoto akiwa katika mabishano ya utani na mwenzake…hajatumwa na kanisa, ni watoto waliofanya hivyo na jazba isiwepo kabisa,” alisema Sheikh Salum.
Sheikh Salum alisema hata kipindi cha Mtume, tukio kama hilo la mtu kukojolea msikitini liliwahi kutokea na waumini kutaka kumdhuru, lakini walikatazwa kutokana na imani kutoruhusu adhabu kama hiyo.
Hivyo, aliwataka waislam wote kutulia katika kipindi hiki na kuacha jazba kutokana na kijana aliyefanya tukio hilo kushikiliwa na polisi.
Watu kadhaa wametiwa mbaroni kuhusiana na vurugu hizo huku Polisi wakiweka ulinzi mkali kila sehemu kwa kutumia magari maalum ya kumwaga maji yanayowasha.
Kamanda wa Mkoa wa kipolisi wa Temeke, David Misime, alisema idadi kamili ya watu waliokamatwa katika ghasia hizo bado haijajulikana kutokana na Jeshi hilo kuendelea kuwakamata watu waliohusika na vurugu hizo.
No comments:
Post a Comment