Paroko; Wanafunzi maisha si mteremko.

Wahitimu wa kidato cha Nne katika Sekondari ya Kata ya Kigonsera, na wale wa chuo cha Katekis, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia elimu kwa kuifanyia kazi na si vinginevyo kwa kuwa maisha siyo mteremko kama baadhi ya vijana wanavyodhani.

Wito huo ulitolewa na Paroko wa Kanisa Katoliki la Litembo wilayani humo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Miito (msimamia nidhamu kwa watawa), Joseph Ngai wakati wa ibada maalum ya wahitimu wa hao iliyofanyika katika Kanisa Kigonsera.

Paroko Ngai, alisema kuwa, baadhi ya vijana wa kitanzania wameyafanya maisha kuwa rahisi rahisi kwa kushindwa kufanya kazi, na badala yake wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo viovu ambavyo ni hatari mbele ya jamii.

“Vijana wangu mliohitimu leo, mmefundishwa maadili mema ya kielimu na kiroho, hivyo naamini mtakuwa mfano bora mbele ya jamii na Taifa zima, mkipata ajira msifikirie kupata maslahi tu; bila kuwajibika,”alisema Paroko huyo.

 Akigeukia upande wa kiroho kwa wahitimu hao, Paroko Ngai aliwataka kuhakikisha elimu ya Sekondari na ya kiroho waliyoipata wanamtangaza Kristo kokote waendako, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watu wanaompinga Kristo.

 “Najua kazi ya kumtangaza kristo ni kazi ya kukatishwa tamaa na baadhi ya watu ambao hawana nia njema na utume huo, hivyo mnatakiwa kujipa moyo na kumuomba Mungu kwa kuwa hata waacha milele,”alisema mkuu huyo wa miito.   

Kwa namna nyingine Paroko huyo aliwahimiza wahitimu hao 16 kuwa na moyo wa shukrani kwa Mungu, kwa kuwa wao wamebahatika kupata elimu hiyo ambayo wengine hawakuweza kuipata.

No comments:

Post a Comment