Saa chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasihi viongozi na waumini wa dini za Kikiristo na Kiislamu nchini kuwa wavulilivu na kujiepusha na vitendo vya kulipiza visasi, Kanisa la la Pentekoste (MMPT) lililopo Buronge katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji limechomwa moto na kutetekezwa kabisa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku majira ya saa 4:00 usiku katika eneo la Buronge mjini Kigoma.
Kashai alisema kanisa hilo lilichomwa na watu wasiojulikana na kwamba mali mbalimbali zenye thamani ya Sh. 1,337,000 ziliteketea.
Alisema sababu za kuchomwa kwa kanisa hilo hazijafahamika na kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa huku upelelezi wa tukio hili ukiendelea ili kuwabaini wahalifu hao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Emmanuel Simon, alisema: “Nilipata taarifa kuwa kanisa langu limeteketea kwa moto, nilikwenda Polisi Central kutoa taarifa ndipo tulikwenda eneo la tukio tukakuta kanisa lote limeteketea kwa moto.”
Alisema katika kanisa kulikuwa na mabechi 14, mlango mmoja, virago vitatu, masanduku ya sadaka na ubao wa kufundishia, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 1,337,000.
Mchungaji Simon alisema hajui watu waliochoma kanisa hilo na kuiomba serikali iangalie matukio ya uchomaji wa makanisa yanayoendelea nchi nzima.
Pia, alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria kwenye makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa makanisa.
Alisema kanisa ni taasisi ya jamii, hivyo anaomba serikali ichangie gharama ya ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa hilo wapate sehemu ya kuabudia.
No comments:
Post a Comment