Mahali pale alipofichwa Bwana Yesu Kristo wakati akiwa bado mchanga ili asiuawe na Mfalme Herode (Misri) sasa pamegeuka dimbwi la damu za watu, huku wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu, (Islamic Brotherhood); wakiendesha kampeni ya kuufuta rasmi Ukristo, wakichoma kanisa hadi kanisa, wameweka alama za X kwenye miimo ya milango ya nyumbaza Wakristo na tayari ibada za jumapili zimefutwa.
Ugomvi wenyewe ni baina ya Jeshi la nchi hiyo, na wafuasi wa Rais wa kwanza wa kuchaguliwa kutoka chama cha udugu wa kiislamu, Mohamed Morsi, wakiwania madaraka, lakini wanaoangamizwa ni Wakristo na Ukristo katika kile kinachoonekana kuwa ni mpango mkamilifu.
Jumapili iliyopita ilikuwa ya kwanza katika kipindi cha miaka 1600 iliyopita, ambapo taifa hilo lilikuwa kimya, hapakuwa na misa iliyosikika kokote, makanisa yalishindwa kukusanyika kumuabudu Mungu wao na kila mmoja alikuwa akilia peke yake.
Shirika la Associated Press (AP) lilisema asubuhi ya Jumapili hiyo hapakuwa na yeyote aliyepewa nafasi ya kukusanyika kwa kuwa wababe wa kundi hilo walioenea kila kona ya nchi walipeana taarifa ya kusaka makanisa na nyumba za waabuduo kuzichoma, siku hiyo zaidi ya makanisa 80 yalivamiwa na kuteketezwa kwa moto.
Sanamu za Bikira Maria kwenye makanisa ya katoliki, ziling’olewa na kudhihakiwa, watu wasiokuwa na hatia kuuawa kinyama, viongozi waliokuwa wakikimbia walitoa taarifa ya kufutwa kwa ibada.
“Hatukuweza kuendesha misa kama kawaida siku ya Bwana, si jambo linalofurahisha hata kidogo ni miaka mingi sana imepita hakukuwahi kutokea jambo kama hili,” alisema Mchungaji Selwanes Lotfy, wa Virgin Mary, kusini mwa Minya, nchini humo.
Vichwa vya habari vya magazeti ya Israeli wiki kadhaa vilipambwa na taarifa za mateso hayo yanayowakumba Wakristo na kusababisha kufungwa kwa makanisa na hata biashara zao, hakuna tena amani, jambo linaloalika baa kubwa kwa waumini wa dini ya kikristo.
Lakini kuonesha kuwa kuna mpango kamili wa mauaji ya jamii fulani, watu wasiofahamika waliweka alama ya X kwenye milango ya nyumba za Wakristo.
Wakati wa mabishano ya Musa na Farao, Musa aliwahi kuagizwa na Mungu kuwaambia wana wa Israeli kuchinja kondoo na kupaka damu kwenye miimo ya milango yao ili malaika atakapopita kuua wazaliwa wa kwanza wa Misri kama adhabu kwa Farao asiwadhuru waisrael.
Shirika la AP likitolea ufafanuzi juu ya alama hiyo na tafsiri juu ya Wakristo, linaeleza kuwa, ili kuimarisha utata; kwenye nyumba za waislamu wameweka alama nyekundu ya X ikimaanisha eneo hilo halitaguswa; yaani liko salama, lakini hiyo ya X nyeusi, lazima jambo lifanyike kwa gharama ya damu.
Kwenye mitandao nako, video zenye mateso yaliyofanywa dhidi ya watu wa Mungu, imetupiwa humo ili kutia hamasa kusudio la kuutokomeza Ukristo kwenye taifa hilo lililokuwa mwanga wa Injili miaka kadhaa iliyopita, licha ya sasa kuonekana kama ni elimu ngeni.
Video hizo ni nyingi, lakini yenye kutia uchungu zaidi ni ile inayoonesha kufurika kwa furaha ya Brotherhood baada ya kuteketeza nyumba za ibada na Watawa wa Kanisa Katoliki, AP imeeleza kuwa ni uzalilishaji mkubwa unaochochea kuzimika kwa ukristo nchini Misri.
“Mtandao wa YouTube unaonesha wanaume wakisalimiana wengine kwa kutikisa mikono na tabasamu wakati nyumba za kuabudia zikiteketea nyuma yao, na sehemu nyingine wanaonekana Watawa watatu wakipigishwa kwata mitaani kama wafungwa,” lilisema shirika hilo na kuongeza:
“Sehemu nyingine inaonyesha, wanawake wakristo wawili wa shule moja wakidhalilishwa kingono walipokuwa wakijaribu kujinasua kutoka kwenye kusanyiko kubwa, tukio hilo limesababisha hofu kuu japo wapo walioshikilia imani yao hadi wanakata roho.
Kama hayo ni madogo, wakiua mamia ya watu, AP linabainisha kwamba, Udugu wa kiislamu, walimuua mwendesha Tax aliyethubutu kuweka alama ya msalaba mbele ya gari yake na kuitembeza katika mitaa ya Cairo.
Shirika hilo limeeleza kuwa, kilichojaa kwenye mioyo ya wafuasi wa kundi hilo ni uvumi kuwa, wakristo ndio wenye kubeba lawama kwa machafuko yanayoendelea kushika kasi, licha ya mataifa ya Ulaya kupiga kelele, kwa ajili ya kung’olewa madarakani kwa Mohammed Morsi, mapema mwezi Julai na Jeshi nchini humo.
Hadi sasa zaidi ya watu 1,000 wakiwemo wanajeshi wameuawa wakati wa mapambano kati ya Jeshi na watu wanaomuunga mkono Morsi wakilazimisha aliyekuwa rais aliyechaguliwa kwa demokrasia, kabla tonge lake halijatwaliwa mdomoni, kurejezwa madarakani.
Licha ya kuandamwa na wafuasi wa kundi hilo, Ijumaa iliyopita kwa uwazi bila kificho, Papa wa Coptic, Tawadros II, alitamka kuwa; Muslim Brotherhood ni chanzo cha machafuko na mauaji nchini Misri, hivyo wako upande wa serikali na Jeshi la Polisi ili kupambana na kundi hilo hatari. Hata hivyo baada ya kauli hiyo amelazimika kuwa mafichoni kukwepa mkono wa kundi hilo.
Kundi la Udugu wa kiislam ‘The Muslim Brotherhood group’ lilianzishwa mwaka 1928, lakini kwa kipindi cha miaka 80 iliyopita lilipigwa marufuku kuendesha shughuli zake nchini humo, lakini lilivikwa uwezo baada ya Mohammed Morsi kuingia madarakani kufuatia kuangushwa kwa Rais Hussein Mubarak, ingawa kuanguka kwake kulisababisha vuguvugu la mapinduzi kwenye mataifa kama Tunisia.
Morsi alilipa nguvu kundi hilo, na kulirudisha kwenye chati, akiimarisha mapinduzi ya kijeshi, hivyo kuwa mstari wa mbele kwenye utawala wake. Hilo hasa ndilo linalotia mori kutositisha mapigano dhidi ya Serikali wakitaka kiongozi huyo kurejezwa madarakani.
Hadi sasa viongozi wa kundi hilo, wanashikiliwa na Jeshi, huku polisi nao wakiomboleza baada ya askari wao zaidi ya 20 kuuawa kinyama kwa kutekwa na kupigwa risasi za kichwani.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, ilieleza kuwa, wafuasi wa kundi la Brotherhood wapatao 1004 walikamatwa mipakani wakiwa na mabomu na silaha mbalimbali katika ghasia za Ijumaa iliyopita, waliyoibatiza kuwa ni siku ya ghadhabu, “Day of Rage”.
Kulingana na mashuhuda, miongoni mwa waliouawa siku hiyo ni pamoja na mtoto wa kiongozi wa kidini wa kundi hilo la udugu wa kiislam, Mohammed Badie, aitwaye Ammar Badie. Hata hivyo siku iliyofuata, mamlaka nchini humo ilimtia mbaroni kaka wa kundi la Al-Qaida Ayman al-Zawahri, aliyejulikana kwa jina la Mohammed al-Zawahri.
Mshukiwa huyo ambaye ni kiongozi wa kundi lenye jina lingine (Jihadi Salafist) alitiwa mbaroni kwenye kituo kingine cha ukaguzi cha kuingia katika mji wa Gaza unaopakana na Nile kutoka Cairo.
Wakati hayo yakitokea Misri, aliyewahi kuwa kiongozi wa nchi hiyo kwa miaka 30, Mubarak, mwaka 2011 aliondolewa madarakani na kutiwa korokoroni kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ulaji wa rushwa na kufanya njama za mauaji, mahakama imemuona hana hatia na kutarajia kumuachia huru.
Hukumu ya Jumatatu, ilipelekea Mubarak kukaribia kurejea katika dunia yenye uhuru, Mohamed Mursi, aliyemsweka gerezani anakabiliwa na mshtaka ya kuongoza uvamizi katika gereza na kuachia huru wafungwa, wakati wa mwanzo wa vuguvugu la kimapinduzi.
Mubarak alishikiliwa kifungoni katika gereza la Tora, katika kiunga cha kusini mwa Cairo. Mwanasheria mmoja aliyetetea upande wa familia zilizoathirika na shutuma zilizoletwa mbele yake za mauaji alisema, Rais aliyepita hakutakiwa kuachiwa huru kutokana na hukumu iliyotolewa kisiasa, kwani amewaliza watu wengi.
“Kama Mubarak ataachiwa kwa kipindi hiki, kikundi cha Brotherhood kitawanyonya kwa kiasi kikubwa sana Wamisri na hiki ndicho kinachotokea Misri kutaka kurudisha utawala uliopita,” alisema mmoja wa ndugu waliouawa kipindi cha Mubarak.
Baadhi ya wanatheolojia walitoa maoni yao kuhusu kila kinachoonekana kama hatari kubwa au mateso makubwa kwa wacha Mungu wa taifa la Misri lenye historia kubwa katika ukristo, walitoa maoni yao na kusisitiza kuwa Ukristo hautetewi wala kulindwa na mwanadamu yeyote yule na pia hakuna mwanadamu anayeweza kuufuta.
Mmoja wa wahadhiri wa vyuo vikuu vya Biblia na Mwanatheolojia nguli, Rev. Ron Swai, akiongea na chanzo cha habari katika mahajiano maalumu alisema kuwa, wanaojaribu kuangamiza Ukristo Misri na hata sehemu yeyote duniani wanajisumbua kwa kuwa huwa unalindwa na Mungu mwenyewe.
“Ni kweli kuwa wanawatesa wakristo, wanaweza hata kuwaua baadhi yao, lakini hilo haliwezi kuufuta Ukristo kwa kuwa haukuanzishwa na mwanadamu na nyuma ya Ukristo kuna nguvu nyingine kutoka kwa Kristo mwenyewe. Mataifa ya Urusi na china yalitesa sana Wakristo, lakini sasa kuna maelfu ya Wakristo huko,”alisema Rev. Ron.
Akinukuu maandiko matakatifu kutoka katika Biblia kitabu cha Warumi 3:10, Rev. Ron alibainisha kuwa kile kinachoendela sasa ni upotofu mtu, na suluhisho la kweli halitapatikana kwenye siasa wala mabavu, bali kwa kufuata haki kutubu kisha kumrudia Mungu.
Mchungaji Ron, huku akinukuu maandiko kutoka katika vitabu vya 2Korinto 10:3, na Efeso 6:10-13, alisema Wakristo vita vyao sio vya nyama na mwili, bali ni vya rohoni na wanapaswa kuchukua silaha za kiroho.
Alisema kuwa historia inaonesha kuwa kanisa lilipoingia katika mateso, kisha likamkumbuka Mungu na kumlilia liliimarika kiimani zaidi ya kudhoofika.
No comments:
Post a Comment