Viongozi wa Dini, UVCCM watoa tamko Kali Padri kumwagiwa tindikali Z’bar

Viongozi wa Dini  na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umelaani vikali kitendo cha kumwagiwa tindikali Padri Joseph Magamba na kutaka vyombo vya ulinzi na usalama kuanzisha operesheni maalum ya kuwasaka wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu.

Aidha, kufuatia tukio hilo, viongozi wa dini wameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kumchukulia hatua za kumwajibisha Kamishna wa Polisi Zanzibar kwa kushindwa kukomesha matukio hayo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka ilieleza kuwa vitendo hivyo ni vya kinyama na ukiukwaji mkubwa wa misingi ya ubinadamu.

  Alisema tukio la kumwagiwa tindikali kiongozi huyo wa dini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui ni zaidi ya unyama na ushetani uliovuka mipaka na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya waliohusika.
“UVCCM tunalaani kitendo hicho ambacho ni cha kishenzi hakifai  na hakipendezi  kutokea machoni mwa jamii ya watu waungwana mahali popote duniani,” alieleza Shaka.

Alisema Padri Magamba ni mtumishi wa Mungu na alikuwa akitoka katika  duka la huduma ya mawasiliano ya mtandao nje ya mlango ambapo alishambuliwa na kudhuriwa  kwa kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.  “Hili ni wingu jipya la ukatili linalozidi kutanda  Visiwani Zanzibar na linalenga kutaka kuvuruga sifa za Zanzibar na jambo hili haliwezi kukubalika,” alisema.
 


 Shaka alisema  kukithiri kwa vitendo  hivyo huku wahusika wa matukio hayo kutokamatwa Zanzibar na  kutofikishwa mbele ya sheria kumesababishia kuongeza  hofu  kwa jamii  na  kwamba huenda huo ukawa ni  mpango mkakati  unaotaka kuharibu misingi ya amani na utulivu uliopo.

”Kitendo cha polisi kuchelewa kufika  kwenye  maeneo ya matukio na kutofanya fatiki za upekuzi katika maeneo  yanayolizunguka eneo la tukio, tunadhani  si sahihi kwani hutoa mwanya kwa  maharamia hawa kukimbia na kutoweka kwa urahisi na kushindwa kukamatwa,”  alisema.

Kwa upande mwingine, kufuatia tukio la Padri Mwang’amba kumwagiwa tindikali, viongozi wa dini wameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kumchukulia hatua za kumwajibisha Kamishna wa Polisi Zanzibar kwa kushindwa kukomesha matukio hayo.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein


Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za Viongozi wa dini, Mchungaji William Mwamalanga akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam muda mfupi baada ya wachungaji kutoka kumjulia hali Padri Mwang’amba aliyelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, alisema mfululizo wa matukio ya viongozi wa dini kushambuliwa ni wazi kuwa Zanzibar si mahali salama pa kuishi tena.

“Mfululizo wa kushambuliwa viongozi wa dini ni wazi kuwa Jeshi la Polisi Zanzibar limeshindwa kuwajibika na hivyo ni wakati sasa kwa SMZ kumwajibisha Kamishna wa Polisi Zanzibar,” alisema Mwamalange.

Alisema Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein badala ya kuchukua hatua za kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo kwa mamlaka aliyo nayo achukue uamuzi wa kumwajibisha Kamishna huyo ili kurejesha imani kwa wananchi.

Mwamalange alisema serikali inatakiwa kuchukua maamuzi magumu kutokana na mfululizo wa matukio ya kuchomwa makanisa, viongozi wa dini kumwagiwa tindikali na wengi kuuwawa lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na vyombo vya usalama hali ambayo inawatia mashaka wananchi ambao wanahoji kuna ajenda gani iliyojificha.

Padre  Mwang'amba, ambaye  amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi alipatwa na mkasa huo Ijumaa ya wiki iliyopita akiwa katika mgahawa wa Sun Shine Internet Café uliopo eneo la Mlandege.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Haji Hana alisema kwamba Padri Magamba (60) alikuwa akitokea katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Sun Shine saa 10.15 jioni na watu waliommwagia walimtega mlangoni kabla ya kufanya uhalifu huo na kutoweka kwenye vichochoro vya mitaa ya Mtendeni na Mchangani.

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment