Spika wa Bunge aonya hatari ya Freemason nchini.

“Maombi yanaweza kuleta katiba nzuri, amani na umoja, licha ya kuwa na tofauti za kiitikadi. Mimi uspika nilipewa na Mungu, ni msalaba, lakini namshukuru Mungu kwangu ni mwepesi, Roho Mtakatifu ananitia nguvu.”

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda, ameliomba kanisa limsihi Roho Mtakatifu aingilie kati kuikoa Tanzania, huku akiwaonya vijana kuacha kukimbilia kwenye ofisi za kundi la kishetani  la Freemason kwani halitatatua matatizo yao, bali litawaingiza mautini.

Spika Makinda alitoa rai hiyo siku chahe zimepita, mbele ya maelfu ya wanawake watumishi wa Kristo, (WWK) wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) waliokutana katika Mkutano wao Mkuu uliofanyika kwenye Ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma.


Kiongozi huyo, mmoja wa mihimili mikuu mitatu inayounda dola, aliyeongozana na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi, na viongozi wengine wa serikali alionya kuwa taifa linamhitaji sana Roho Mtakatifu ili kuvuka katika hatua iliyopo.

Alisema kuwa, vijana wengi wamekumbwa na tamaa ya kutafuta mafanikio bila ya kufanya kazi na wanahangaika kusaka ofisi za kundi la Freemason ili kupata mafanikio.
“Freemasons ni kazi ya shetani, huko hakuna kitu, ni ushetani mtupu, vijana wanapaswa kujitazama sana na kuwa makini juu ya kundi hili, lakini ikiwa watamtambua Mungu wa Kweli, basi wataweza kushinda, wanawake nyie ni jeshi kubwa, mkimlilia Bwana atawasikiliza na kuinusuru nchi,” alisema Spika huyo.

Mama huyo aliyeweka rekodi ya kuwa Spika wa kwanza Mwanamke, katika historia ya Tanzania huru, alienda mbali zaidi  na kuujongelea ulimwengu wa kitheolojia alipoitwaa Biblia takatifu akaifungua na kusoma maandiko kutoka katika kitabu cha  2Timotheo 3:1-7 . andiko hilo linasema:

 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi…….. wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu…..”

Akiisha kukariri andiko hilo, Spika Makinda alilifafanua akisema kuwa, shetani hujibadilisha kwa sura tofauti ili kupumbaza ufahamu wa watu, hivyo ni wajibu wa vijana kufahamu na kutubu maovu yao kwa kuwa Mungu ni mwingi wa rehema, atawasamehe.

Mbali na hilo, Spika Makinda aliwasihi wanawake hao, kutenga muda wao mwingi kumlilia Mungu alete amani, umoja na mshikamano katika taifa wakati huu ambao mambo mengi yanatisha.Akiamini wanajua hali isiyo ya kawaida inayoendelea nchini na duniani kwa ujumla, kama vile uasi wa ndoa za jinsia moja, Ubakaji, dawa za kulevya, kumwagiana tindikali na uchomaji wa makanisa, aliwakumbusha kuwa maombi yao yataleta tumaini jipya.

“Ninyi si wanawake watumishi tu, ni wanawake watumishi wa Kristo, Mungu husikiliza kilio cha wacha Mungu, ndani ya ukumbi huu mmefurika iombeeni nchi, matukio ni mengi na ya kutisha, watu wanabaka hadi watoto wao,” alisema.

Hakuacha kuwaomba wanawake hao kupeleka maombi yao kwa Bwana, kuhusiana na mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, ambapo Novemba 11, 2013 kutakuwa na Bunge la Katiba litakalojadili rasimu iliyokwisha tayarishwa na Tume ya Katiba chini ya jaji Joseph Warioba.

“Watu wa Mungu mwombeni Mungu kwa bidii, suala nyeti kama la Katiba linamhitaji Mungu kwa namna tofauti, mataifa mengi leo yamekuwa na machafuko kutokana na masuala ya kushindwa kuelezwa na kukubaliana kwenye katiba,” alisema na kuongeza:

“Miaka Kumi ya Mavuno!… Tanzania kwa Yesu…… salamu hii nzuri sana nimeipenda kweli,” alisema Spika Makinda, huku akiachia tabasamu lililosababisha ukumbi kulipuka kwa kelele toka kwa akina mama hao ambao wakati wote wa hotuba ya mheshimiwa huyo walikuwa katika nyuso za furaha, wakisikiliza kwa makini na wengine kuandika dondoo kwenye vitabu vyao.

Hapo mama Makinda anayetarajia kuachana na mambo ya siasa, akiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambali na mkewe, Gladmery sambamba na Mkurugenzi wa Idara ya WWK, Mchungaji Faraja Hamuli; kusalimiana  wakugurenzi wa majimbo, na wageni kutoka Marekani wakapata  wasaa wa kubadilishana mawili matatu.

Naye, Dk. Mtokambali akiongea kwenye mkutano huo, uliofurika umati wa wajumbe wa WWK kutoka kila kona ya Tanzania, wakiwa  na sare maalum zenye rangi ya  damu ya mzee, yenye kusindikizwa na ujumbe kutoka katika Biblia kitabu cha Yeremia 47:7 “Utawezaje kutulia, ikiwa BWANA amekupa agizo……” alisema anaamini katika mwanamke.

Dk. Mtokambali alimsifu Mhe. Makinda kwa kujitahidi kumudu uendeshaji wa vipindi vya bunge, licha ya wakati mwingine kutofautiana kiasi cha wabunge wengine kuchukua uamuzi wa kususia vikao hivyo.
Hata hivyo, alimuomba mheshimiwa huyo, kwa nafasi aliyonayo kuhakikisha nchi inabaki katika amani na umoja, huku akisisitiza sheria isiwe na jicho la upendeleo.

“Sheria isimwangalie mtu jinsi alivyo, awe na pesa nyingi, kwamba ni msomi, cheo. Sheria ifuate mkondo wake, izingatie haki ya aliyenacho na asiyenacho,”alimaliza kwa kusema Dk. Mtokambali.

No comments:

Post a Comment