Rufaa ya mauaji ya Yesu yaumiza vichwa ‘The Hague’


 
Rufaa ya hukumu  ya kifo aliyohukumiwa  Bwana Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita, iliyofunguliwa  mahakamani na mwanasheria mashuhuri, Bw. Dola Indidis, imezidi kusugua vichwa vya wanasheria na wanatheoloj­imeishinda mahakama kuu ya Kenya iliyohangaika nayo kwa miaka mitatu sasa imeelekeza mlalamikaji kuelekea The Hague nchini Uholanzi kuwasilisha shauri hilo kwenye Mahakama ya kimataifa ya haki (ICJ).

 Washtakiwa wanaopaswa kufika mahakamani kujitetea au wawakilishi wao ni Mtawala wa Roma, Tiberius Pontus Pilate (Pilato), Padre Annas (kiongozi wa Wayahudi, Mfalme Herode, Jamhuri ya Italia,Taifa teule la Mungu Israeli  na waalimu wa sheria za kiyahudi.

Mwanasheria huyo aliiambia korti kuwa mataifa hayo yanakesi ya kujibu kwa kuwa hadi sasa bado yanatumia sheria za utawala wa Roma na zile zilizotumika kumsulubisha Yesu msalabani  na zinaweza kutumika kuwatesa wengine
Mwanasheria mashuhuri nchini Kenya  Bw. Dola Indidis
 Mlalamikaji anasema kuwa Jaji Pilato alikiuka sheria pale aliposhuhudia mtuhumiwa akipigwa kabla ya hukumu wakati alistahili kusimamia haki ya watu wote  bila kuruhusu ukiukwaji wa haki wa aina yoyote ile.
Mateso yanayolalamikiwa ni kuwa mshtakiwa kabla ya kutiwa hatiani alichapwa na kutemewa mate, tena mbele ya jaji,  suala ambalo ni kinyume cha haki za binadamu na kwa kuwa Yesu alikuja duniani kama mwanadamu alistahili kupata haki ya kulindwa na sheria.

Mlalamikaji anasema mfumo wa maswali na adhabu aliyokuwa akiendelea kupewa tangu alipokamatwa vilikiuka kabisa sheria na haki za kiutu, hivyo anaitaka mahakama itamke kuwa Yesu hakutendewa haki.
Mwanasheria huyo alisema kuwa ameiomba mahakama ibatilishe hukumu ya Yesu na kuitamka kuwa ilikuwa batili ili wanadamu wengine wasije wakajikuta kwenye mateso kama hayo, tena analalamika kuwa Yesu hakupewa wakili wa kumtetea mahakamani.

Miongoni mwa wale waliozungumzia kesi hiyo katika muktaza wa sheria ni Wakili wa Mahakama Kuu nchini, Justin Kaleb, ambaye alisema kuwa  kesi ya mauji ya Bwana Yesu si mauaji ya halaiki ‘genoside, ni ya  mtu mmoja, inakosa sifa ya kujadiliwa na Mahakama ya  kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC). 

Kisha  mwanasheria huyo akahoji; mlalamikaji itabidi aihakikishie mahakama kuwa, kama  ni mpenzi au rafiki wa Yesu na kama amepewa mamlaka hayo na ukoo wa Yesu. Ukoo huo bado upo mpaka leo.
“Inamlazimu mlalamikaji kuidhihirishia mahakama iwapo yeye ameathirika kiasi gani na suala la kuteswa na hata kuuawa kwa Bwana Yesu Kristo,” alisema Kaleb.

Alifafanua kuwa hukumu ya Yesu ilikuwa sawa sawa kwa mujibu wa sheria za kiyahudi za wakati huo ambazo zilikuwa zikitamka wazi kuwa mtu akikashfu dini ya kiyahudi anahukumiwa adhabu ya kifo.
Kuhusu malipo ya fidia, Mwanasheria huyo alisema kuwa ikiwa mlalamikaji anataka alipwe fidia itamlazimu aandikishe orodha ya marafiki wa Yesu wanaostahili kupata  jambo ambalo ni gumu sana.
Lakani akasema kuwa,  pengine kipengele cha kutaka hukumu hiyo kuwa fundisho kwa mataifa mengine  kinaweza kufanikiwa na kuwa msaada kwa sheria za sasa.

MWANATHEOLOJIA
Mmoja wa waalimu wa theolojia, mchungaji Samwel Mwaluvanda, akiongea na chanzo cha habari, alisema rufaa inayofanywa na mkenya, Dola Indidis si jambo sahihi kwa sababu zifuatazo:

“Moja: anafanya dhambi ya Petro ya kupingana na kusudi la Mungu. Petro hakutaka Yesu asulubiwe maana aliwaza kibinadamu na kimaslahi binafsi, Yesu akijua kosa hilo alimkemea: “….Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali  ya wanadamu.” Mathayo 16:23

Pili: Lilikuwa kusudi la Yesu Mwokozi, kumtumikia Mungu na mwandamu kwa gharama ya kutoa nafsi yake, Marko 10:45. Hata Biblia ilitabiri kuwa masihi atatoa maisha yake na damu yake ili kuwakomboa wanadamu kama anavyokiri yeye mwenyewe katika Luka 24:44 - 47

Tatu: Kristo Yesu aliyatoa maisha yake mwenyewe na kwa hiari yake hakuna mwanadamu au afisa yeyote aliyemzidi Yesu na kumhukumu, kumuua, Yohana 10:18-28.

Nne: Yesu Kristo aliwatangazia msamaha wote waliomtendea mabaya, kumsulubisha na hata kumuua. Ni msamaha bila masharti yoyote Luka 23:34

Tano: Kanuni za Philosophy of Influence yaani katika kila kesi na hukumu lazima kutazama pia mitazamo ya watu kuhusu tukio. Kwa tukio la Yesu Kristo, ulimwengu umepokea na kukubali na kusherehekea tukio hilo kuwa la ukombozi kwao. Kwanini kuhukumu jambo linalokubalika?

Sita: Kuhukumiwa kifo kwa Yesu ni suala la kiroho na kiimani,  siyo suala la kisheria au kisiasa, ni mambo ya imani  na yanatambulika kwa jinsi ya imani na Roho Mtakatifu. Biblia inakataa kupeleka mambo ya imani katika mahakama za watu wa dunia wasio na Roho Mtakatifu wala wokovu, 1Wakorinthoi 6:1-12.”
Hata hivyo, mwanatheolojia huyo aliongeza kuwa, mwanasheria Indidis inaonyesha ana kiburi cha uzima, na kusisitiza kuwa amejikinai.

 “Amepoteza hofu ya Mungu, anatumia mambo Matukufu ya Mungu kujitafutia umaarufu wa kidunia kama baadhi ya viongozi wa siasa na taasisi mbalimbali 1Yohana 2:15-18,” alisema.

 Mchungaji John Masanyiwa wa Kanisa la AIC Geita, akiongea na chanzo cha habari hii kwa njia ya simu, alikuwa na haya ya kueleza: “Mgogoro uliopo baina ya Palestina na Israeli kamwe hauwezi kuisha kwa mazungumzo bali Neno lazima litimie.”

Aliongeza: “Kupoteza ukweli juu ya imani ya YESU, Tendo hilo hatuoni ajabu, watu wa jinsi hii Biblia inawataja kwamba siku za mwisho watatokea. Watafiti na wadadisi wa mambo, tutegemee mengine zaidi ya haya kuwa yanakuja.  Watu wanawaza hata sala ya Baba yetu Uliye mbinguni isiishie kutaja Baba wa mbinguni bali pia itaje mama wa mbinguni.”  

Kesi hiyo iliyofunguliwa kwa mara ya kwanza katika mahakama Kuu ya Kenya chini ya kifungu namba 65-67 cha katiba ya zamani ya Kenya, ikiwa  na walalamikaji ambao ni  marafiki wa Yesu kupitia kwa Dola Indidis  na taasisi ya kutetea haki za kiraia na Humfrey Odanga Achala.

No comments:

Post a Comment