TAG Isanga yawasha moto wa uamsho.

“Ndipo tukageuka, tukashika safari yetu kwenda jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia BWANA; tukawa kuizunguka milima ya Seiri siku nyingi. BWANA akanena, akaniambia, Mlivyozunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini….,” (Kumb. 2:1…), maandiko haya  na mengine ndiyo yaliyoongoza Kanisa la Tanzania Assemblies of God Isanga, Sayuni Mbeya, kuandaa semina kubwa ya kiroho iliyoleta uamsho mkubwa katika vitongoji vya miji ya mbeya na majirani..

Semina hiyo ya Neno la Mungu iliyoandaliwa na Mchungaji Kiongozi Joseph A. Chiwinga wa kanisa hilo, ilileta nguvu mpya ya kiroho na uamsho mkubwa, ambapo baadhi ya makanisa kutoka madhehebu mbalimbali kutoka Mbeya, walihudhuria na kupokea nguvu mpya na uamsho wa kufanya kazi ya Mungu kwa kasi zaidi.

Akifundisha ujumbe uliojaa nguvu za Mungu, Mchungaji na Mwinjilisti Lutengano Mwasongela, kutoka Tabora, alinukuu maandiko kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 2:1, yanayodhihirisha kuwa, wakati wa kanisa kuzungukazunguka imetosha na kwamba hakuna ajuaye uchungu wa kanisa asipokuwa Yesu pekee ambaye ndiye kiongozi na muhimili wake asiyetikisika milele yote.

Akizungumzia kuhusu Imani, Mchungaji huyo alisema kuwa, umefika wakati kwa waumini wa kweli kusimama kwenye Imani thabiti, ambapo alibainishwa kwamba, ukiwa na imani wenye uhakika na Mungu hauwezi kuogopa kitu chochote, na kwamba kile utakachokiona katika ulimwengu wa Roho ndicho kitakachokutokea.

Akinukuu maandiko yasemayo: “Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa Mkutano wote wa wana wa Israeli, katika Jangwa la Parani, huko Kadeshi wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi…..Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.” (Hes. 13:26-33). Mtumishi huyo alifafanua ujumbe huo akisema kwamba; pamoja na mambo mengi yanayoonekana kuwa magumu na yakuwakatisha tamaa wanadamu, kwa Mungu ni mepesi na yanaweza kutatuliwa mara moja.

Aidha ailiwataka watu kutoogopa mambo yote magumu kwa vile Mungu wao aliisha watangazia ushindi pale Kalvari, kilichosalia ni kuchukua hatua na kutangaza ushindi ambao tayari uliishapatikana.

Aidha alisema kuwa, mwanadamu ndiye anayeweza kumwacha Mungu, lakini Mungu hawezi kumwacha mwanadamu kamwe, kwani yeye anawapenda watu wake aliyowaumba na kuwawazia mema kila iitwapo leo. Mchungaji huyo alisema kuwa mabadiliko yoyote katika maisha ya mwanadamu yanahitaji gharama kubwa na ili mtu utoke kwenye mzunguko alionao ni lazima akubali mabadiliko hata kama yanamaumivu makali.

Aliwataka watu kutambua kwamba, Neno la Mungu ndilo lenye uwezo wa kuwajenga watu na kuwabadilisha na siyo maneno matupu, hivyo kila muumini anatakiwa kuliamini na kulitendea kazi  pasipo kulega.

 Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Joseph Chiwinga, akiongea na blog kwa njia ya simu alisema kuwa, kanisa lake limejipanga imara mwaka huu, kuendesha Semina na mikutano mingi inayokusudia kuleta uamsho na kuwavuna watu kwa Bwana Yesu, katika jiji la Mbeya, na kwamba kwa awamu ya kwanza wameanza na semina ya ndani ambayo imemalizika na sasa kuna semina ya Wanawake Watumishi wa Kristo WWK itakayofikia kilele chake leo wakati wa sikukuu yao kitaifa alimazia kwa kusema

No comments:

Post a Comment