Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi
baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati
ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa
wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na
jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo
zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha
vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa
kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na
Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni
ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi
wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama
lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari
takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa
na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri,
Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya
wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa
wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa
wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia
na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor
alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa
ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege,
kweli walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii
inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa
siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50
ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya
ghorofa hilo kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo
linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila
shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.
Source.mwananchi
Source.mwananchi
No comments:
Post a Comment