Askofu Kulola ampa tuzo ya heshima Alex Msama

Kanisa la EAGT hivi karibuni lilimtunuku tuzo Mkurugenzi wa makampuni ya Msama Promotions kwa kutambua mchango wake katika uchangiaji wa maendeleo ya jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhi  tuzo hiyo, juzi Askofu Philemon Phiri wa jimbo la Mikocheni akimwakilisha Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola alisema tuzo hiyo kwa Msama ni utambuzi wa anayoyafanya katika kusaidia jamii.

Askofu Phiri alitumia fursa hiyo kumpongeza Msama kwa  uandaaji wake bora wa matamasha ya Pasaka na kueleza kuwa Mungu amempa ufunuo ambao ni endelevu, naye Msama alishukuru tuzo hiyo na kueleza kwamba tamasha la Pasaka litaendelea kila leo tena kimataifa zaidi hadi duniani.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Moses Kulola
Katika hatua nyingine mwimbaji nguli wa muziki wa Injili wa Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi nchini Kenya, amesema atatumia tamasha la pasaka kutambulisha wimbo wake  wa Kiti Chako uliopo kwenye albamu yake mpya ya Sifa za Mungu.

Akizungumza na Pata Habari, baada ya kuwasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria tamasha la pasaka linalotarajiwa kufanyika Jumapili hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam alisema, atautambulisha wimbo huo ambao una ujumbe mzito wa neno la Mungu.

Kwa mujibu wa Solomoni Mukubwa albamu yake hiyo ni zaidi ya nyingine alizowahi kurekodi hii kwa sababu ameimba ushuhuda wa maisha yake  baada ya kupata matatizo ya kukatwa  mkono  wake.
“Nashukuru  kupata  tena  nafasi  ya kuwa mmoja wa waimbaji kwenye tamasha la mwaka huu, nimejiandaa vya kutosha mashabiki wafike kwa wingi kupata ujumbe mzito wa neno la Mungu pia nitatambulisha wimbo wangu mpya siku hiyo” alisema Mkukubwa.

Alisema albamu yake hiyo inanyimbo saba, ambazo ni Kiti chako, Shukrani ya punda, Nitaishi wakitazama, Habari njema, raha yangu, sijafika, Sifa za mungu, Nimewasamehe wote.

Kwa upande wa Faraja Ntaboba, alisema kauli mbiu ya tamasha la pasaka la mwaka huu inayosema kuwa ‘Amani na Upendo’ imempa moyo sana,  inagusa Afrika nzima kwa kuwa  kuna watu wanalia  kwa kupoteza  amani.

Aidha  mwimbaji  huyo  alitoa  wito  kwa  mashabiki  wa tamasha hilo linalotarajia kufanyika mikoa mitano, kuwa wasisherehekea tu bali waje wakijua amani inatafutwa,  aliahidi kufanya mambo makubwa siku ya Jumapili.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 Uwanja wa Samora mkoani Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Source:Fullshangwe

No comments:

Post a Comment