Askofu bandia ajipenyeza mkutano wa makadinali

Askofu bandia amefanikiwa kujipenyeza na kuingia kwenye mkutano wa makadinali unaoendelea mjini Vatican, kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya.

Askofu huyo bandia, Ralph Napierski ambaye ni mzawa wa Ujerumani alifanikiwa kujipenyeza na kusalimiana kisha kupiga picha za kumbukumbu na baadhi ya makadinali waliopo kwenye mkutano huo bila kugundulika.

Uzamiaji wake ambao ulileta mashaka kuhusu uimara wa usalama eneo hilo wanapokutana makadinali 103, ambao wamekusajika kwenye Makao Makuu ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya, huku wengine 12 wakiwa hawajawasili.

Katika mkutano huo, Kadinali wa juu kutoka Uingereza, Cormac Murphy O'Connor pia anahudhuria.

Mtu aliyejifanya Kardinali wa Kanisa Katoliki, Ralph Napierski (kushoto) akisalimiana na Kardinali Sergio Sebiastiana. Napierski alikamatwa akijaribu kuingia kwenye mkutano wa makardinali unaoendelea Vatican 
Napierski alionekana akisalimiana na Kadinali Sergio Sebiastiana nje ya ukumbi wa Papa Paul VI akiwa hajatambua kuwa siyo miongoni mwa wenzake, huku akiwa amezungukwa na makasisi wengine wa kanisa hilo ambao pia hawakuweza kutambua.

Walinzi wa kundi la Swiss Guars linaloshughulika na ulinzi wa Makao Makuu ya Kanisa Katoliki  Vatican, walimbaini kuwa siyo miongoni mwa wahusika kutokana na vazi lake alilofunga kiunoni, ambalo siyo sahihi bali ulikuwa ni mtandio uliokunjwa vizuri.

Pamoja na vazi hilo la rangi ya zambarau kutokuwa sahihi, pia kofia aliyokuwa ameivaa haikuwa miongoni mwa zile zinazotambulika kuvaliwa na viongozi wa kanisa hilo.

Tofauti nyingine iliyobainika ni ufupi wa kanzu yake na rozari aliyovaa haikuwa halisi, kwa kuwa ilikuwa ni fupi kuliko wanazotumia viongozi wa kanisa hilo.

Kabla ya kubainika, Napierski alijitambulisha kwa waandishi wa habari kwamba jina lake ni Basilius ni miongoni mwa wawakilishi wa Kanisa la Orthodox kutoka Italia.

Awali, kulikuwa na taarifa kwamba aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kanisa Katoliki limefanya “Kosa kubwa” kwa kuwaruhusu makasisi wanaotuhumiwa kwa makosa ya ngono kubadilishwa kutoka maeneo yao ya awali na kupelekwa kwingine, kuficha kashfa zao badala ya kuzishughulikia.

Mtuhumiw ahuyo ambaye baada ya kubainika aliondolewa eneo hilo, anaongoza tovuti ambayo aliitumia kujitambulisha kwamba yeye ni kasisi kupitia Shirika la Kikatoliki la Corpus Dei, huku akiwa amevaa mavazi ya kikasisi na kujidhihirisha kama “Mtumwa na Nabii kama Mtakatifu Paul”.

Msemaji wa Kanisa Katoliki mjini Vatican, Federico Lombardi alisema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu hajapata taarifa yoyote na muda wote alikuwa  akishughulika katika mkutano

Source:mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment