Takwimu zilizotolewa katika kikao cha Baraza la Waangalizi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), kilichofanyika mjini Dodoma siku kadhaaa zimepita, zinaonesha kukua kusiko kwa kawaida katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kuwashangaza hata watu kutoka mataifa yaliyotangulia kupata muamko wa Injili kama vile Marekani.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la kila eneo kwa zaidi ya asilimia 100, katika kipindi cha miaka mitano tu yaani kuanzia mwaka 2008-2013, mfano; mwaka 2008, kanisa lilikuwa na Sehemu (section) 75, na sasa lina Sehemu 226.
Hadi kufika mwishoni mwa mwaka jana, kanisa hilo linaloongozwa na dira yake ya maendeleo ya ‘Miaka 10 ya Mavuno’ lilikuwa na watumishi wenye vyeti mbali mbali 5,026, na makanisa 5007, yaliyoenea nchi nzima na kulifanya kuwa kanisa kubwa na linalokua kwa kasi zaidi miongoni mwa yale ya Kipentekoste Tanzania.
Jambo lililolipua shangwe za wajumbe wa baraza hilo kutoka kila kona ya Tanzania, ni ukweli kuwa ukuaji wa kanisa unakwenda sambamba na ukuaji wa elimu, ujenzi na upanuzi wa Vyuo vya Biblia, vya kupanda makanisa na msisitizo wa kimaadili.
Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabs Mtokambali |
Takwimu pia zinaonesha kuwa, kanisa hilo limekuwa kiidadi likiongezeka kwa zaidi ya asilimia 200, tangu lilipozindua dira yake ya maendeleo iliyoweka lengo la kufikia kila roho inayopotea dhambini Tanzania.
Akisoma taarifa hiyo, mbele ya mamia ya wajumbe wa bbaraza hilo, Katibu Mkuu wa TAG, Rev. Ron Swai, alisema kuwa, hadi kufika Desemba mwaka jana, watenda kazi 2280, walikuwa tayari wamehitimu masomo katika vyuo vya kupanda makanisa na kuingia shambani kumtumikia Mungu.
Katika kipindi hicho, kanisa limeweza kununua magari ya thamani kwa maaskofu wake nchi nzima, wakurugenzi wa Idara, na sasa mradi wa kugawa piki piki kwa waangalizi, tayari umeanza ambapo baadhi yao walitarajiwa kukabiziwa vyombo hivyo vya kurahisisha utumishi katika kazi ya Bwana Ijumaa iliyopita mjini Dodoma.
Pamoja na vyombo vya usafiri, kanisa hilo limejikita katika Uinjilisti, likiwanunulia Wainjilisti wa kitaifa vyombo vya kisasa vya kuhubiria pamoja na vifaa maalumu vya uinjilisti kwa njia ya sinema ili kuwafikia watanzania wote. Mradi huo wa ununuzi wa piki piki za kisasa aina ya Yamaha, kutoka Japani utagharimu shilingi milioni 800,na tayari Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabs Mtokambali amepata mshirika katika kazi ya Mungu atakaye gharamia mradi huo.
Ni kwa kuguswa na matokeo chanya ya dira ya maendeleo ya Kanisa la TAG, Mtumishi wa Mungu kutoka Marekani, Dk. David M. Oliver, ambaye pia ni rais wa huduma ya Living Water LLC, yenye makao yake North Canton Ohio Marekani, aliwaambia mamia ya waangalizi hao kuwa wanapaswa kumshukuru sana Mungu kwa kuwapa viongozi wa kanisa wenye wingi wa hekima na maono makubwa ya kulifikisha mbali kanisa.
Dk. Oliver alikuwa akifundisha somo linalohusu Nguvu ya Uponyaji wa Baraka-Mwongozo wa kusikiliza, ambapo alianza kwa kufafanua maana ya Neno Baraka.
“Neno Baraka linatokana na neno la kilatini ‘benedicere’ likiwa na maana ya kusema kitu vizuri, ‘kusifu’ ‘inua’ au kutakia mema,”alifafanua Dk. Olvier katika somo lake hilo.
Huku akinukuu Maandiko Matakatifu kutoka vitabu vya Warumi 5:8 na Yohana 11:25-26, alisisitiza: “Lazima tujifunze kuishi kwa neema, rehema na Baraka za Mungu, bila kujaribu kupata utajiri kutokana na hivyo. Baraka msingi wake ni kweli na hubeba nguvu ya Mungu…..”
Dk. Oliver alifundisha kwa kina misingi ya baraka za Mungu na jinsi ya kupokea na kubariki wengine, akitoa mifano kadhaa ya maisha na utumishi wake.
No comments:
Post a Comment