Hema la Kanisa la Sulvation Ministry for all Nations lililopo Mbezi Juu, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam limevunjwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari kanisani hapo jana, Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Fredy Mwamtemi, alisema hema hilo lilivunjwa usiku wa kuamkia Jumapili Desemba 2, mwaka huu.
Alisema watu ambao wanaaminika kuwa ni vijana walifika kwenye hema hilo majira ya saa 9 usiku na kukata nguzo kuu za katikati zinazoshikilia kanisa.
Alisema tukio hilo ni la kusikitisha. “Tunalishukuru sana jeshi la Polisi wilaya ya Kinondoni kwa namna walivyoshughulikia tatizo hili, polisi wamechukua hatua za kutosha katika hili,” alisema Mchungaji Mwamtemi.
Alisema taarifa za kuvunjwa kwa kanisa hilo alipewa na dereva wa bodaboda ambaye alikwenda nyumbani kwake saa 12 asubuhi na alipofika kwenye eneo hilo alikuta hema limeanguka.
Mchungaji msaidizi wa kanisa hilo, Eliya Jumanne, alisema jioni ya Jumamosi Desemba 1, walikuja vijana wawili kanisani hapo na kuwataka wanakwaya kupunguza sauti ya muziki wa kwaya kwa kuwa walitaka kwenda kuswali.
“Sisi tulipunguza sauti lakini katika hali ya kushangaza usiku ndipo kanisa likaja kuangushwa,” alisema.
Watu kadhaa wanadaiwa kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika, lakini polisi hawajakubali wala kuthibitisha taarifa hizo.
Badala yake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo la hema la kanisa kuvunja na kueleza kwamba taarifa zaidi atazitoa leo.
No comments:
Post a Comment