Maaskofu nchini watoa tamko zito

Maaskofu nchini, jana walitumia ibada za Krismasi kukemea maovu, huku baadhi yao wakiwatuhumu matajiri nchini kuwa ndiyo kiini cha vurugu zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa yao hivi karibuni.Wakihubiri kwa nyakati na makanisa tofauti, viongozi hao walisema uhasama huo dhidi ya Wakristo ulioanza kujengeka katika siku za hivi karibuni, unafadhiliwa na baadhi ya matajiri kwa masilahi yao binafsi.

Katika tamko lao lililotolewa na Umoja na Makanisa Tanzania, maaskofu hao wameitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mbegu za chuki zinazopandikizwa ili kuwafarakanisha Watanzania kwa misingi ya imani za dini.Tamko hilo ambalo litarejewa Desemba 30, mwaka huu, ni makubaliano ya pamoja kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moravian, Anglikana, Pentekoste, Wasabato na Kanisa Katoliki.


Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo 

 
Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini akisoma tamko hilo wakati wa ibada ya pamoja, alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya kidini, vinawachochea watu ili wawaue maaskofu na wachungaji mbalimbali wa makanisa.

Pia, alihoji kauli zinazoenezwa kuwa nchi hivi sasa inaongozwa kwa mfumo wa Kikristo ilihali asilimia 90 ya viongozi wa juu nchini ni Waislamu.“Labda niwakumbushe, viongozi wote waandamizi wa ngazi za juu nchini, asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe kwa mfumo wa Kikristo?” alihoji Askofu Shao.

Aliwataja kuwa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).“Kule Zanzibar, asilimia 100 ya viongozi wote ni Waislamu na si kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa ya kuongoza,” alisema na kuongeza:

“Hata uwakilishi kwenye Tume kama ya kuandikwa kwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu… Nchi hii haina mfumo wa Kikristo, bali ni nchi yenye mfumo wa kidemokrasia.”Aliitaka Serikali ithibitishe ukweli kuwa haiendeshwi kwa mfumo wa Kikristo badala ya kukaa kimya wakati maneno hayo ya uchochezi yanaenezwa hadharani.

“Ni wakati wa kukubali kuwa misingi ya haki, amani na upendo katika taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Kumekuwapo na dalili za wazi za uchochezi na kashfa dhidi ya Ukristo,” alidai.Maaskofu hao wamewalaumu baadhi ya viongozi wa dini kutumia vyombo vya habari vya kidini, vipeperushi, mihadhara na kanda za video kukashfu dini nyingine.

“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa linakashfiwa unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga mkono.”“Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari kubwa ya kiuhusiano siku za usoni. Tunaitaka Serikali ichukue jukumu lake la msingi la kusimamia amani.”

Askofu Pengo
Katika mahubiri yake jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo aliwaponda matajiri wanaojivunia mali, akisema siyo kigezo cha mtu kuwa na furaha maishani.

Kadinali Pengo alisema hayo katika misa ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika juzi katika Parokia mpya ya Mongolandege, Ukonga, Dar es Salaam.
Alisema ni makosa mtu kuhesabu mali kama sehemu ya mafanikio katika maisha kwani kuna wenye mali nyingi ambao hawana furaha.

“Utajiri unaambatana na shaka, hofu na wasiwasi kwa kufikiri kuwa huenda mali hii isinitoshe au itachukuliwa na watu wengine,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza:
“Tusitafute mali kiasi cha kuwafanya watu wengine waumie, wahuzunike. Kila mmoja atimize wajibu wake pale alipo, matokeo yake ndiyo yatakayoleta furaha.”

Askofu Mhongolo
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo amewataka waumini kuendelea kuienzi Krismasi kwa kujali na kuwekeza katika elimu ambayo ni msingi wa mambo yote.

Kiongozi huyo alisema kwa Wakristo, kuwa na dhana ya kujenga elimu katika maisha yao itawasaidia kujiletea heshima na kwamba watakuwa juu.

Askofu huyo alisema dhana nzuri ya kuthamini elimu hadi sasa waumini wa Kikristo nchini wamekuwa ni mfano wa kuigwa na jamii na taifa kwani kati ya jumla ya vyuo vikuu 19 vilivyoko nchini vyuo saba vinamilikiwa na Wakristo, 11 na Serikali huku kimoja kikiwa cha Kiislamu.

Askofu Mkude
Askofu Thelesphory Mkude wa Jimbo la Morogoro amewataka waumini wa dini zote kushiriki vyema katika kuendeleza na kushika neno la Mungu na kuombea nchi hasa katika kipindi hiki cha kufunga mwaka na kukaribisha Mwaka Mpya.

Katika ibada ya mkesha wa Krismasi, Askofu Mkude alisema kuwa imefikia wakati sasa wa kumshirikisha Mungu kila jambo kwani kila siku matendo maovu yanaendelea kutokea na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Askofu Sehaba
Askofu wa Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka pale inapoona kuna tishio la uvunjivu wa amani nchini kuliko kukaa kimya na kusubiri likitokea ndipo ianze taratibu za kudhibiti.
Alisema kumekuwapo na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya waumini wa dini kama uchomaji wa makanisa na kusema Serikali inapaswa kutovifumbia macho.

Askofu Mwombeki
Askofu Edson Mwombeki wa Kanisa la Free Evangelism Tanzania amewataka Watanzania wote kulinda amani na utulivu.
Akihubiri kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Manispaa ya Shinyanga, aliwaomba Watanzania wote wabadilike na kuwa na tabia njema kwani kwa sasa watu wengi wamepoteza uadilifu, amani na uzalendo.


 Source NIPASHE

No comments:

Post a Comment