Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Lund, nchini Sweden, umebaini kuwa wanaume wanaokuywa angalau soda moja kwa siku wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuugua ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo.
Watafiti wamebainisha kuwa wanaume wanaokunywa soda wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupata shambulio hilo la saratani ya kibofu, ambayo ni ugonjwa wa hatari wenye maumivu makali.
“Mtu anayekunywa soda ujazo wa kawaida ambao watu wamezoea kutumia, anakuwa katika hatari kubwa ya kupata Kansa hiyo ambayo huwashambulia wanaume pekee, ‘Prostate cancer,” alisema Isabel Drake, anayekamilisha mafunzo ya shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Lund.
Utafiti huo unaokubaliwa na taasisi mbalimbali za Afya barani Ulaya ambao utachapishwa katika jarida la American Journal of Clinical Nutrition, la Desemba mwaka huu, ulihusisha wanaume 8,000 wenye umri kati ya miaka 45 na 73, waliochunguzwa kwa miaka 15.
Akiongea na Shirika la Habari la AFP, Drake, alibainisha kuwa, watu wote wenye utaratibu wa kutumia kinywaji (soda) milimita 330 kila siku wanaongeza sukari mwilini na kiwango cha sukari kinapokuwa kikubwa kinaathiri chembechembe za uhai zinazosababisha saratani.
Anasema kuwa hali inapokuwa hivyo mgonjwa huhitaji matibabu ya haraka yenye gharama kubwa na anakuwa katika mateso makali.
Utafiti huo pia unabainisha kuwa ugonjwa huo wa Kansa huonekana kwa mtu, pale tu anapoanza kuumwa na dalili kujionyesha, si kwa vipimo vya kawaida vya watu wanaocheki afya zao.
“Ili mtu ajulikane kama ana saratani ni lazima apimwe kwa kipimo kijulikanacho kama; “Prostate - Specific Antigen (PSA), na hicho hakifanyiki mara kwa mara,”alisema.
Sambamba na hilo, mtafiti huyo alibainisha kwamba, kwa wale waliozoea kula vyakula vya wanga kwa asilimia kubwa, nao wako kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa wa kansa.
“Vyakula vya wanga vinaongeza hatari ya kushambuliwa na saratani kwa asilimia 31, na hata vile vya mafuta, hasa ya wanyama huongeza hatari kwa asilimia 38,” alisema.
Mtaalamu huyo aliweka wazi kuwa, ni vyema wanaume wakawa makini kuchunguza afya zao na hata kuwaona washauri wa mambo ya lishe ili kupata ushauri utakaowasaidia kujikinga na hatari hiyo.
Wachunguzi pia walibainisha kuwa raia wa china na wajapani wanaoishi uhamishoni Marekani wanakabiliwa na magonjwa ya kansa kuliko wale wanaoishi nchini kwao kutokana na kubadilisha maisha.
No comments:
Post a Comment