Afariki baada ya kuzimia miaka 42

Hatimaye siku kadhaa zilizopita Bi. Edwarda O' Bara (59) aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari uliosababisha azimie kwa kipindi cha miaka 42, amefariki dunia. Taarifa zinaonesha kuwa alipoteza fahamu akiwa mwanafunzi wa Sekondari mwaka 1970.

 Dada wa marehemu, Bi. Colleen O'Bara, aliliambia gazeti la Miami New Times, la mjini Miami, nchini Marekani kuwa, Edwarda O' Bara alipoteza fahamu mwaka 1970 akiwa na miaka 16, na tangu hapo hakuweza kufahamu lolote, hadi Alhamisi iliyopita alipofariki akiwa na umri wa miaka 59.

“Alianza kusumbuliwa na kisukari, akiwa Sekondari, baadaye alipoteza fahamu kabisa, tangu kipindi hicho akawa chini ya uangalizi wa mama na jamaa zake hadi juzi alipofariki mikononi mwangu,” alisema Bara na kuongeza:

“ Mdogo wangu alikuwa Sekondari na  huko ndiko alikoanza kuumwa  na tulipompeleka hospitali akagundulika anakisukari, baada ya hapo alimsihi sana mama asimuache peke yake kabla ya kuwa katika hiyo hali yake ya sintofahamu.”

Wakiendelea na zoezi la kupigania  afya yake kwa miaka kadhaa, hatimaye mama yake, Bi. Kaye O'Bara, naye aliaga dunia mwaka 2007 na kumwacha mgonjwa katika hali yake ya sintofahamu.

“Kweli ni huzuni kubwa, nimewataarifu watu wengi kuwa Edwarda yuko mbinguni, natumaini ataungana na mama huko mbinguni, mama alijitahidi kwa kadiri alivyoweza kufanya sawasawa na maombi ya Edwarda, hadi alipokufa mwaka 2007 na mimi kushika usukani,” alisema.

Colleen aliendelea kusema kwamba wakati wa uhai wa mama yake, alikuwa akijitahidi kumgeuza geuza kitandani ili asikae upande mmoja kwa muda mrefu, pia alikuwa akitumia mirija kumpa  chakula na dawa ya kupunguza sukari mwilini ‘Insulin’.

Ili kusaka hisia zake au kama ufahamu wake umerudi, alisema mama yake alikuwa akimsomea vitabu, akimwimbia  katika hali yake hiyo hiyo.

“Kutokana na imani yake ya Roman Katoliki alikuwa akiwaambia kuwa kwenye chumba alicholala mwanaye kuna uwepo wa Bikira Maria, kitu kilichomfanya daktari mmoja, Dyer kuandika kitabu kilichokwenda kwa jina la ‘A Promose Is A Promose’ ikielezea upendo wa mama kwa mtoto.
                       

No comments:

Post a Comment