Jumapili iliyopita ilikuwa ya kipekee kwa jiji la Dar es
Salaam, wakati umati wa watu kutoka maeneo mbali mbali ya jiji la Dare s
Salaam, waliposhuhudia ishara na maajabu isivyo kawaida ikitendeka
mbele ya macho yao katika kanisa la TAG, Majumba sita, Ukonga Jijini
Dar es Salaam.
Katika Ibada hiyo ya kipekee
iliyoongozwa na Mchungaji kiongozi, Mchungaji Moses Magembe, huku
ikirushwa moja kwa moja (Live) kupitia kituo cha Radio WAPO FM, katika
jiji la Dar es Salaam, na mikoa ya jirani matukio ya uponyaji yasiyo ya
kawaida yalishuhudiwa.
Takwimu za mtandao zinaonesha
kuwa ibada hiyo pia ilikuwa ikifuatiliwa na watu zaidi ya 54 elfu,
kutoka maeneo mbalimbali ya nje ya Tanzania kupitia mtandao wa Internet,
wakiwepo kutoka Kanada na mataifa yasiyo na ruhusa ya kuhubiri Injili
kwa uhuru.
Akifundisha somo lenye kichwa; “Utendaji wa
Mungu juu ya miujiza,” huku akinukuu maandiko kutoka katika Biblia
kitabu cha Matendo ya Mitume 1:8, Mchungaji Magembe alionya wale
wanaochanganya imani halisi na vitu kama vile; mafuta yanayoitwa ya
upako, chumvi na maji ya baraka, pamoja na kubinafsisha maeneo yao kuwa
vituo maalumu vya maombezi.
“Huduma ya kuombea watu kwa
jina la Yesu inapaswa kufanywa na kila aliyempokea Bwana Yesu, haina
haja ya kubinafsishwa kwa wachache tu. Askofu ambaye kwake hakuna watu
wanaoombewa na kupona basi arudishe Biblia dukani tuchukue sisi,”
alisema kiongozi huyo.
Kisha aliongeza: “Tatizo hapa
sio waumini, bali ni baadhi ya viongozi wamekufa na kuganda kabisa, wana
majina ya Kikristo lakini hawako hai. Sasa tunamtaka BWANA atende
miujiza sio propaganda, tunataka Bwana afanye…”
Huku
akinukuu maandiko matakatifu kutoka katika Biblia vitabu vya; Waebrania
9: 14, Luka 1:31, Waebrania 13: 8 na 1Wakornto 2: 14, aliwaasa Wakristo
kuwa macho na watu wanaolitumia vibaya jina la Yesu kwa kuwanywesha
watu vitu vya ajabu ikiwa ni pamoja na mafuta na kuwapa vitambaa na maji
ya Baraka kuacha kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Neno la Mungu.
“Kinachoponya
ni kuliamini Neno la Mungu na kuishi maisha matakatifu, sio maji ya
upako wala vitambaa. Acha mara moja ……mtazame Kristo aokoaye….” alisema
Mchungaji Magembe, huku akihubiri katika mtindo wa kiinjilisti.
Mchungaji
Magembe ambaye kwa kupitia huduma ya Gospel Campaign Centre, ameendesha
harakati kubwa za umisheni huko, Msumbiji, Malawi, Zambia na sehemu
zingine duniani, alionya kuwa wale wanaosafiri hadi mataifa ya Nigeria
kusaka upako sio wa Mungu wa Wakristo.
“Mungu wa
vitambaa, chumvi, kukata viuno madhabahuni, sio Mungu wetu. Mungu wetu
Wakristo anafanyakazi na Biblia na sio vinginevyo, nitaonya na kukemea
mpaka Tanzania ipone,” alisema Mchungaji Magembe.
Miongoni
mwa shuhuda za kustaajabisha katika ibada hiyo ni Leah Eliasi ambaye
alishuhudia jinsi alivyonyweshwa mafuta na maji za upako alipokwenda
kuombewa katika Huduma moja iliyopo jijini Dar es Salaam, (jina
tunalihifadhi) lakini hakupata nafuu yoyote.
Akiwa na
Mumewe Bw. Joseph Eliasi, mbele ya maelfu ya watu waliohudhuria ibada
hiyo na wale waliokuwa wakifuatilia kupitia radioni na mitandaoni,
alisema kuwa alikuwa akiugua mwili mzima. Karibu kila kiungo kilikuwa
kikimsumbua na alikwenda hospitali mbalimbali bila msaada, mwisho
akaamua kwenda kwa waganga, lakini hali ilizidi kuwa mbaya.
Ndipo
alipoamua kwenda kuombewa katika huduma na makanisa mbalimbali lakini
akakutana na maajabu katika kanisa moja ambapo alikorogewa mafuta ya
upako, asali mbichi na maji ya Baraka na kuambiwa aogee kwa siku saba
mfululizo, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.
Alipofika
mahali pa kukata tama ndipo alipofika Majumba sita, ambapo aliombewa
kwa jina la Yesu bila maji, kitambaa wala mafuta na akapokea uponyaji
wake na sasa ni mzima kabisa.
Bi. Annamaria Kimbila,
akishuhudia jinsi Bwana alivyomuokoa, alisema kuwa mjukuu wake aitwaye
Lilian Emmanuel alipotea jijini Dar es Salaam, na kanisa likaingia
kwenye maombi na katika hali ya kustaajabisha alipatikana huko Muleba
Bukoba akiwa hai na mzima wa afya.
No comments:
Post a Comment