Waumini wa makanisa ya Kikristo Songea, mkoani Ruvuma, wametakiwa kuliombea taifa katika kipindi hiki cha maandalizi ya sikuku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo (Krismas) ili kusherehekea siku hiyo kwa utulivu na amani.
Hayo yalisemwa Jumapili iliyopita Mchugaji wa Kanisa la Tanzania Assemblis of God (TAG), Alimosa Mwasangapole wakati akiongea na chanzo kimoja cha habari na kufuatia umuhimu wa kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha maandalizi ya sikuku ya Krismas.
Mwasangapole alisema, watu walio wengi wamekuwa wakifanya maandalizi ya kusherehekea Krismas kwa kuwaza kula, kuvaa na kufanya anasa huku wakisahau kuliombea taifa liendelee kuwa na amani.
“Starehe zote pamoja na anasa zake hufanyika wakati taifa likiwa limetulia kwa kuwepo amani, amani isipokuwepo hata maandalizi hayo ya sikukuu yatakuwa ni kazi bure; hakuna mtu atakayeweza kuthubutu kufanya kama amani haitokuwepo,”alisema.
Aidha Mwasangapole aliwataka waumini kujenga tabia ya kupendana kwa kuacha tabia ya kubagua wanye shida mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wagonjwa walioathirika na Ukimwi.
“Napenda kuona maandalizi ya sikukuu ya Krismas kwetu iwe chachu ya kufanya matendo mema, kuliombea taifa na kujenga tabia ya kupendana, kuheshimiana na kuacha kubaguana,”alisema Mchungaji Mwasangapole.
No comments:
Post a Comment