Askofu Mkuu wa jimbo la Mashariki la Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dk Lawrence Kameta ametahadharisha kuhusu mauaji na ghasia zinazotokea nchini kwamba siyo dalili nzuri ya amani.
Askofu Kameta ametoa kauli hiyo baada ya kutokea mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi hivi karibuni ambaye anadaiwa kuuawa na polisi katika mkutano wa Chadema.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa Ibada ya kuwasimika viongozi wapya wa jimbo hilo, Dk Kameta alisema kama mambo hayo yataachwa yaendelee kuna hatari ya nchi kuingia kwenye machafuko.
Alisema hivi sasa kuna changamoto kubwa na kwamba viongozi wa dini wanapaswa kuiombea nchi kwani Serikali peke yake haiwezi kuleta amani.
“Vifo, ghasia na maandamano siyo dalili nzuri ya amani. Sisi kama viongozi wa dini tuna sehemu yetu katika kuleta amani hivyo tuchukue jukumu hilo,” alisema Dk Kameta.
Alisema pia kuna haja ya kuviombea vyama vyote vya siasa ili viwe na sera nzuri zitakazoepusha machafuko.
“Si kwamba tukifanya hivi tutakuwa tunaleta siasa makanisani kwa sababu kama vurugu zikitokea hata kanisa linaweza kuwa kuathirika,” alisema.
Pia aliwaasa viongozi wapya waliosimikwa katika jimbo hilo kuwa na hofu ya Mungu na kuwa waaminifu katika utumishi wao.
Alisema kama viongozi wakikosa uaminifu madhara yake ni makubwa kwani kanisa linaweza kuporomoka kimaadili na kukosa nguvu ya kuliwakilisha taifa.
No comments:
Post a Comment