TAG kusherehekea miaka 75 ya uhai wake Tanzania

Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) linakusudia kuadhimisha miaka 75 tangu kuanza kwake nchini, sherehe ambazo zitafanyika kitaifa mkoani Mbeya mwakani.

Hayo yalibainishwa na Askofu Mkuu wa kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, katika uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Idara ya Maandiko na Uanadunzi uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Highland Camp Morogoro, Jumatano iliyopita.
Askofu Mkuu wa kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambali

Kiongozi huyo wa kitaifa alisema kuwa Halmashauri kuu ya kanisa hilo imeamua kuwa sherehe hizo zitafanyika katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya mwaka 2014.

Alisema kuwa maadhimisho hayo yataanzia katika ngazi ya kanisa la mahali pamoja na baadaye ngazi ya Jimbo na fainali itakuwa ni ngazi ya taifa mkoani Mbeya.

Kanisa la TAG, ambalo linaongoza miongoni mwa makanisa ya TAG, kukua kwa kasi nchini linatimiza miaka 75, tangu lianze nchini huku likienea kila mahali kuanzia mijini mpaka vijijini.





“Msitarajie utukufu mnapomtumikia Mungu’

Kumtumikia Mungu si kazi ya heshima mbele ya wanadamu, bali kwa Mungu pekee, hivyo waliojitoa kikamilifu kuingia katika shamba la Bwana wasifanye huduma hiyo wakitaraji mrejeo chanya toka kwa viumbwa.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Ismaili Mwipile, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ukonga jijini Dar es Salaam, alipokuwa akihubiri katika mkutano wa injili uliokuwa kanisani hapo wiki iliyopita.

Mchungaji Mwipile aliwataka waamini wa dini ya Kikristo kutokukata tamaa pale wanapoamua kuifanya kazi ya Bwana, kwani heshima kubwa inatoka kwa Mungu ikiambatana na thawabu tele.

Aliwaasa waamini kuwa wavumilivu na wasio kata tamaa, wakijitahidi kuondokana na imani haba katika changamoto wanazokutana nazo, huku akifananisha na gereza la vifungo vya mafanikio.

"Paulo na Sila walikaa gerezani, licha ya kupata mateso, lakini walikuwa na imani na Mungu pekee waliyemwamini na ndiye aliyewaweka huru pale milango ya gereza ilipofunguka," alisema Mchungaji Mwipile.

'Waliookoka wako kwenye vita kali’

Mwinjilisti wa Kanisa la Calvary Assemblies of God,   la Matarawe, Songea mkoani Ruvuma,  John Tembo, amewataka Wakristo waliofanikiwa kupata wokovu kutambua kuwa; wapo kwenye vita kali dhidi ya shetani, hivyo wanastahili kusimama imara nyakati hizi ni za mwisho.

 Wito huo alitowa mapema wiki jana, wakati akihubiri katika kanisa hilo, kwenye ibada ya Jumapili iliyokuwa na mguso mkubwa wa nguvu za Mungu, na watu zaidi ya 30 waliitikia wito wa Injili wakayakabidhi maisha yao kwa Yesu, huku waliosetwa na ibilisi wakifunguliwa.

 Mwinjilisti Tembo, alisema kuwa nyakati hizi ni za mwisho kwa mujibu wa maandiko, hivyo ni vema watu wakasimama imara kumuomba Mungu ili awaepushe na majaribu yanayowasonga.

 Alisema, watu wa Mungu waliouona mkono wa Bwana ndio waliopo kwenye changamoto mbalimbali za kishetani, kwa kuwa shetani naye anawatafuta watu kama hao ili awaangamize.

   “Nawaambieni watu wa Mungu katika nyakati hizi za mwisho shetani anafanya kazi ya kushika fahamu za watu wenye uelewa wa Mungu ili kusiwepo na utambuzi wa mambo mema, badala yake yatendeke mabaya,” alisema Mwinjilisti huyo na kuongeza:

 “Kuna baadhi ya watumishi wa Mungu wameshikwa ufahamu na shetani, na ninyi wenyewe mnaona, wanahubiria watu  vitu ambavyo havipo kwenye maandiko na mnamwamini,  ni hatari sana kwa nyakati hizi.”
 Aidha Mtumishi huyo wa Mungu aliwageukia waumini waliookoka ambao wamenunua simu kwa bei mbaya kwa malengo ya kuangalia picha za kishetani zilizopo ndani yake, na kulaani kitendo hicho kuwa ni kinyume na matumizi ya simu.

Maznat mdau wa Blog aadhimisha miaka 10 ya Taasisi yake na Kuzindua shule ya Urembo


 Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akiwasili kwenye Ukumbi wa VIP wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam jana jioni kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, kama Mgeni rasmi sambamba ya kuzindua Shule ya Taasisi hiyo inayofundisha masuala ya urembo.
Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam, jana, sambamba na sherehe hizo pia Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo.
Mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam, jana, sambamba na sherehe hizo pia Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo.
Sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hizo.
Mmiliki wa Saluni na Taasisi ya Maznat, Maza Sinare, akiwalisha keki baadhi ya wageni waalikwa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Taasisi ya Maznat, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam jana, sambamba na sherehe hizo pia Mgeni rasmi mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Asha, alizindua rasmi shule ya masuala ya Urembo inayosimamiwa na Taasisi hiyo.
 Msanii wa muziki wa Injili, Bahati Bukuku, akiimba jukwaani kutoa burudani wakati wa maadhimisho hayo.
The Voice

Ungana na Ask.Lazaro na Mtume Onesmo Ndegi kutembelea Israel

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Emmanuel Lazaro, akiongoza kundi la viongozi mbalimbali wa makanisa na baadhi ya waumini wanaosafiri kwenda Israeli kutembelea maeneo matakatifu yaliyopo kwenye Bibilia, ambapo pamoja na mambo mengine wataliombea kanisa na nchi kwa ujumla.

Kampuni ya Nanuri Safari LTD inayoratibu safari hiyo ya kihistoria inakukaribisha kujiunga nao ili kukupa fursa ya kipekee ya kushuhudia kwa macho maeneo hayo matakatifu kama yalivyoainishwa katika Bibilia.

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Emmanuel Lazaro

Mtume Onesmo Ndegi
Utaratibu wa Safari ni kuwa msafara huu utaondoka jijini Dar es Salaam, tarehe 14/07/2013 na kurudi tarehe 22/07/2013. Katika safari hiyo, Askofu Lazaro pamoja na mkewe, watafuatana na, Mtume Onesmo Ndegi, Maaskofu, Wachungaji na Wakristo mbalimbali.

Gharama za safari yote ni ni Dola  za Marekani 2700, ikiwa ni pamoja na gharama za malazi, chakula cha mchana na usiku, usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali nchini Israel, kibali cha kuingia maeneo ya nchi, VIZA na usafiri wa ndege.

Wanaotaka kujiunga na safari hiyo ya Baraka, ambayo imeratibiwa na NANURI SAFARI COMPANY LIMITED walipe fedha hizo kupitia:

NANURI SAFARI COMPANY LIMITED
NMB – ILALA BRANCH
ACCOUNT NO: 2036600111
DAR ES SALAAM.

Ukiwa na swali lolote, wasiliana nao kwa mawasiliano yafuatayo:
0715 – 640 777; 0782 – 640 777;  0716 – 316 109

AU
Fika katika Ofisi zao zilizopo Mwalimu House ghorofa ya 6, Ilala Boma jijini Dar es Salaam. Kumbuka nafasi ni chache wahi mapema kabla hujachelewa.

Waziri Mkuu atembelea Kanisa lilipolipuka Bomu na Kuzungumza na waumini na Viongozi wa Kanisa.


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akizungumza na Viongozi na Waumini wa Kanisa Katoliki la Olasiti Jijini Arusha  May 7,2013 alikokwenda kutoa pole kufuatia mlipuko wa bomu la kutupwa kwa mkono uliotokea kanisani hapo May 6,2013 na kusababisha vifo na majeruhi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu







 

Masikitiko ya mjane wa Mch. Kachila aliyeuwa kinyama katika mgogoro wa kuchinja

Katika mahojiano na Mwandishi wa Shirika la CBN News, mjane wa Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste aliyeuwa kinyama katika mgogoro wa kuchinja, Rev. Mathayo Kachila, Bi. Generosa Kachila, alitamka maneno yanayoashiria uchungu wa moyo wake kutokana na mkasa wenyewe na hata jinsi hatua za kisheria zilivyochukuliwa.

Kwa uchungu mama huyu alisema: "I shouted, my Jesus, my Jesus, why have you forsaken me?"  tafsiri isiyo rasmi “Nilipaza Yesu wangu Yesu wangu mbona umeniacha?” kilio hiki cha mshtuko wa kuuawa kwa mumewe aliyekuwa kiongozi wa familia, kumemuacha mjane huyu akiwa  mlezi pekee wa watoto 12.

Jambo baya zaidi ni kuwa mahojiano ya mama huyu yanaashiria uchungu zaidi kwa vile waliotekeleza  unyama huo hawajakamatwa na mwenyewe anaamini kuwa wako Mjini Mbeya na wengine  wamevuka mpaka na kuingia nchini  Burundi.

Ni wazi kuwa mjane huyo anaona jinsi juhudi zilivyofanyika kwa kuwatumia  wapelelezi wa kigeni kuwapata wauaji wa kasisi kule Zanzibar, kwa kuchorwa mchoro uliowezesha mtuhumiwa kukamatwa, na angependa kuwaona wahusika wa mkasa ule kuanzia wachochezi mpaka watekelezaji wakisimama mbele ya sheria.

Tunaamini kuwa  machozi ya mama huyu ni mashtaka mbele za Mungu ambaye Biblia inamuelezea kuwa ni baba wa yatima na Mume wa wajane.

Kwa kuwa yeye ndiye pia mhukumu Mkuu wa dunia  tuna hofu kuwa ikiwa tutazembea  kwa namna yoyote ile  kutenda haki iliyostahili, yaani kuwasaka wauaji wa mumewe kwa nguvu kubwa kama ile iliyotumika katika  matukio mengine yaliyoonekana ya muhimu.

Kwa mujibu wa utafiti wa Mwandishi wa CBN,  miongoni mwa watuhumiwa wakuu ni yule anayetajwa kwa jina moja la Abdallah ambaye inaelezwa kuwa yupo nchi jirani ya Burundi.

Tunaishauri serikali yetu kuimarisha msako wa watuhumiwa wote ili haki itendeke na wale waliopoteza mpendwa wao waione na kuitambua haki  hiyo.

Ni vyema pia serikali ikafahamu kuwa suala hili sasa lina sura ya kimataifa na ulimwengu unasubiri kusikia hatua madhubuti zinazochukuliwa katika kuilinda amani ya  nchi.Hatua hizo madhubuti zitafuata kile kilichoelezwa karibuni na mmoja wa wahubiri wa kimataifa kutoka  Ulaya kuwa mataifa ya magharibi yana kampeni maalumu ya kuionyesha dunia kuwa Tanzania si kisiwa cha amani tena.

Tunaamini kuwa haki ndiyo nguzo kuu ya amani yetu, tusipojali haki hata ya mnyonge  amani yetu itakuwa bandia au woga na wala si ile inayojengwa na nguzo ya upendo na undugu wa kweli.

Pia tunaishauri tena serikali kuliamua suala la uchinjaji ambalo ni chanzo cha  mauaji ya mchungaji huyo, liamuliwe kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi ambao ndio mkataba baina ya watawala na watawaliwa.
Wakati huu wa kusubiri serikali kuamua, pia wachungaji na viongozi wengine wa dini wajiapushe na lugha kali zinazoweza kuchochea chuki zaidi.

Wadumu katika kuomba, kushauri kwa upendo na kuelekeza kwa kuwa dunia inawatarajia kuwa waamuzi wakati mambo yanapoharibika.

Ni vyema watanzania nao wakajitambua  na kujitenga na watu wenye  nia mbaya wawe ni wa ndani au wa nje ya nchi wanaotaka kuona damu ya watu ikimwagika. Ni wazi kuwa kila mmoja wetu anajua kilichotokea katika mataifa jirani kuanzia, Rwanda, (mauaji ya kimbari 1994) Kenya ( mauaji ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007) na hata yale ya Burundi na Kongo.

Chingafirst aja na mbinu mpya uimbaji nyimbo za injili

Kutokana na kukua kwa kasi kwa muziki wa Injili nchini, na kufanya miziki ya dunia kushuka katika tasnia ya muziki, mwimbaji William Chingafirst amekuja na staili mpya ya kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.
Mwimbaji Chingafirst, akiongea na chanzo ca blog jijini Dar es Salaam, alisema amekuja kivingine katika kumtukuza Mungu, pasi na ushindani, japo nyimbo zake zimeonekana kuleta ushindani maeneo ya Kahama, Geita na Tabora.

Akiongelea kuhusu albamu yake yenye nyimbo 11, alisema ameimba na kucheza kwa mitindo tofauti tofauti ikiwemo;  kwaito yenye asili ya Afrika Kusini, Rumba na Sebene toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, sambamba na Dansi asili yake Tanzania na nyimbo za kuabudu zenye mchanganyiko wa lugha ya kiingereza, kiswahili na kifaransa.

Alisema lengo lake ni kumwimbia Bwana kama ilivyo kule mbinguni ambapo malaika, wazee 24 na watakatifu wanavyomsifu Mungu kwa ukuu wake.

Aidha, aliongeza kuwa, yuko tayari kuimba kwenye kanisa lolote linalomhubiri Kristo aliye hai, linaloamini habari ya wokovu na tayari alishafanya katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam, akitamba na wimbo wa Sina Deni Aka Mie japo wimbo uliyobeba albamu yake ni Namshangilia Mwokozi.

Mwimbaji huyo anabainisha kuwa, uimbaji ni ibada tosha mbele za Mungu, huku akiongeza kuwa, Neno linahubiriwa kwa sababu watu wamemuacha Mungu, lakini kinachoendelea mbinguni katika ulimwengu wa roho ni sifa na kuabuudu.

Miongoni mwa nyimbo ndani ya albamu hiyo ni; Niko huru (mwanawane), This is the day you have made for me, Namshangilia Mwokozi, Ibelieve in You, Sina Deni Aka Mie, Tanzania Tunaweza kuuponya ulimwengu kwa jina la Yesu, Heri Wenye Moyo Safi, Twende kwa Bwana, Tutaimba Milele, Mtakatifu na Kila Jambo.
Alisema nyimbo hizo zimesanifiwa kiroho katika studio ya Hosana na maproduza tofauti tofauti.

Bomu larushwa kanisani Arusha, mmoja afariki wengine kujeruhiwa!

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 59 kujeruhiwa akiwamo Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla jana asubuhi baada ya mtu asiyejulikana kurusha bomu wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.

Miongoni mwa majeruhi, imeelezwa kuwa wanne ni mahututi.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amelielezea kuwa tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na kumlenga Balozi wa Papa nchini na kwamba mtu mmoja anashikiliwa akihusishwa nalo.

Wataalamu wa mabomu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanachunguza aina ya bomu lililotupwa lakini uchunguzi wa awali unaonyesha lilikuwa limetengenezwa kienyeji.

Watu walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa bomu hilo lilirushwa yapata saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi akijiandaa kufungua jengo la kanisa baada ya ujenzi wake kukamilika.

Shambulio hilo lilitokea wakati balozi huyo akiwa amesimama na mwenyeji wake, Askofu Mkuu, Josephat Lebulu, mapadri na watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya kukata utepe wa uzinduzi.

Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono wa kulia... “Alifanya jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini alishindwa kutokana na wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”

Padri Moses Mwaniki aliyemshikia Balozi Padilla maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa hilo, alisema kilichosaidia bomu hilo kutomfikia mwakilishi huyo wa Papa ni kutua mgongoni mwa mmoja wa waumini na kuanguka chini kabla ya kulipuka na kujeruhi watu.

“Ingawa hatuwezi kusema kwa uhakika, tunaamini mlengwa mkuu alikuwa mgeni wetu, Balozi Askofu Mkuu Padilla. Tunatakiwa kuliombea sana Taifa liondokane na matukio mabaya kama haya,” alisema Padri Mwaniki.

Baada ya tukio hilo, Balozi Padilla, Askofu Lebulu na viongozi wa kanisa hilo waliondolewa na kuhifadhiwa katika moja ya vyumba vya kanisa hilo kabla ya kutolewa kwenye eneo hilo yapata saa 5.30 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwapo kanisani hapo.
Mapaka sasa mtu mmoja ashikiliwa na  Jeshi la Polisi kwa wa uchunguuzi wa tukio hilo

Baada ya bomu kuulipuka na jereuhi watu,watu wakikimbia kutafuta msaada katika sherehe hiyo.


Mahali ambapo inasemekana bomu lililipuka
Kanisa ambalo mbele yake ndio ilikuwa inafanyika sherehe hiyo na bomu kulipuliwa
Makamu wa Rais Dk. Gharibu Bilal akimsikiliza Askofu mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania Askofu Dk Alex Malasusa akizungumza katika matukio hayo kusho wakati akizungumza na majeruhi na wafiwa waliopteza ndugu katika milipuko ya mabomu iliyotokea leo jijini Arusha

Waandishi wa habari Afrika Mashariki watakiwa kuepuka habari za uchochezi

Dk. Richard Sezibera
Waandishi wa Habari wa nchi za Afrika Mashariki wametakiwa kuzitangaza nchi zao kwa kuandika habari zenye kuleta tija kwa taifa husika na kuepuka habari za kuharibu amani.

Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Afrika wa siku mbili wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa habari duniani, unaofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa umuhimu wa vyombo vya habari duniani ni mkubwa na hasa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa zaidi ya watu milioni 33 Afrika Mashariki wanategemea vyombo vya habari kupata habari za nchi zao.

“Kutokana na hili naomba sana nyie waandishi wa habari nchi hizi muunganishe nguvu kwa kuzitangaza nchi zenu mambo mazuri kama vivutio vya asili na vingine, ili pia muweze kuwabadilisha viongozi pale wanapokwenda pabaya,” alisema.

Dk. Sezibera, alisema habari zinapatikana kupitia simu na kompyuta yenye mitandao ya jamii, hivyo kikubwa kuhakikisha wanahabari mnadumisha amani kwa kuandika mazuri ya nchi zenu. Akitoa mfano alisema uchaguzi wa Kenya kila mtu aliyekuwa nje ya nchi hiyo aliweza kufuatilia uchaguzi huo mwanzo hadi mwisho, kupitia vyombo vya habari, hivyo ni jambo la kupongezwa.

Aidha aliwasihi wanahabari, kujenga utamaduni wa kuandika kwa wingi matukio yanayofanyika nchi za Afrika Mashariki, badala ya kutegemea kupata habari za nchi zao kupitia CNN.

“Mimi nasikitika sana kuona habari za nchi zetu hizi za Afrika Mashariki zinaelezewa kwa kiasi kikubwa na nchi zingine, jamani tubadilike,” alisisitiza.

Aliwapa pole waandishi wa habari wote waliopatwa na majanga, vifo mbalimbali wakati wa ufanyaji wa kazi zao.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, ametoa ujumbe wake uliosomwa na Vibeke Jensen na Mkurugenzi wa UNESCO, kwenye maadhimisho hayo. Alisema uhuru wa kujieleza kama unavyoelezwa kwenye kifungu cha 19 cha tamko la ulimwengu la Haki za Binadamu ni muhimu kuwawezesha watu na kujenga jamii huru na za kidemokrasia.

Alisema Ikiwa ni haki ya msingi, haki hii ya kujieleza pia ndani yake ina maelekezo ya jinsi ya kulinda na kuendeleza haki nyingine zote za binadamu.

“Lakini utekelezaji wake hauji tu, unahitaji mazingira salama ya mjadala, ambapo kila mmoja anaweza kuongea kwa uhuru na uwazi, bila woga wala wasiwasi wa kulipiziwa kisasi,” alisema.

Alisema kwa sasa kuna changamoto nyingi tangu miaka 20 ipite ya maadhimisho hayo, sababu waandishi wengi wamekuwa walengwa wa mara kwa mara wa vitendo vya vurugu.

“Zaidi ya waandishi wa habari 600 duniani wameuawa katika miaka kumi iliyopita wengi wao wakiwa kazini kuripoti tena kwenye maeneo ambayo hayana vurugu,”alisema.