Waandishi wa habari Afrika Mashariki watakiwa kuepuka habari za uchochezi

Dk. Richard Sezibera
Waandishi wa Habari wa nchi za Afrika Mashariki wametakiwa kuzitangaza nchi zao kwa kuandika habari zenye kuleta tija kwa taifa husika na kuepuka habari za kuharibu amani.

Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Afrika wa siku mbili wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa habari duniani, unaofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa umuhimu wa vyombo vya habari duniani ni mkubwa na hasa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa zaidi ya watu milioni 33 Afrika Mashariki wanategemea vyombo vya habari kupata habari za nchi zao.

“Kutokana na hili naomba sana nyie waandishi wa habari nchi hizi muunganishe nguvu kwa kuzitangaza nchi zenu mambo mazuri kama vivutio vya asili na vingine, ili pia muweze kuwabadilisha viongozi pale wanapokwenda pabaya,” alisema.

Dk. Sezibera, alisema habari zinapatikana kupitia simu na kompyuta yenye mitandao ya jamii, hivyo kikubwa kuhakikisha wanahabari mnadumisha amani kwa kuandika mazuri ya nchi zenu. Akitoa mfano alisema uchaguzi wa Kenya kila mtu aliyekuwa nje ya nchi hiyo aliweza kufuatilia uchaguzi huo mwanzo hadi mwisho, kupitia vyombo vya habari, hivyo ni jambo la kupongezwa.

Aidha aliwasihi wanahabari, kujenga utamaduni wa kuandika kwa wingi matukio yanayofanyika nchi za Afrika Mashariki, badala ya kutegemea kupata habari za nchi zao kupitia CNN.

“Mimi nasikitika sana kuona habari za nchi zetu hizi za Afrika Mashariki zinaelezewa kwa kiasi kikubwa na nchi zingine, jamani tubadilike,” alisisitiza.

Aliwapa pole waandishi wa habari wote waliopatwa na majanga, vifo mbalimbali wakati wa ufanyaji wa kazi zao.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, ametoa ujumbe wake uliosomwa na Vibeke Jensen na Mkurugenzi wa UNESCO, kwenye maadhimisho hayo. Alisema uhuru wa kujieleza kama unavyoelezwa kwenye kifungu cha 19 cha tamko la ulimwengu la Haki za Binadamu ni muhimu kuwawezesha watu na kujenga jamii huru na za kidemokrasia.

Alisema Ikiwa ni haki ya msingi, haki hii ya kujieleza pia ndani yake ina maelekezo ya jinsi ya kulinda na kuendeleza haki nyingine zote za binadamu.

“Lakini utekelezaji wake hauji tu, unahitaji mazingira salama ya mjadala, ambapo kila mmoja anaweza kuongea kwa uhuru na uwazi, bila woga wala wasiwasi wa kulipiziwa kisasi,” alisema.

Alisema kwa sasa kuna changamoto nyingi tangu miaka 20 ipite ya maadhimisho hayo, sababu waandishi wengi wamekuwa walengwa wa mara kwa mara wa vitendo vya vurugu.

“Zaidi ya waandishi wa habari 600 duniani wameuawa katika miaka kumi iliyopita wengi wao wakiwa kazini kuripoti tena kwenye maeneo ambayo hayana vurugu,”alisema.

No comments:

Post a Comment