Waziri Mkuu Msaafu Sumaye akemea udini na ufisadi

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amekemea harakati zinazoendelea nchini za kutaka kupandikiza mapambano ya kidini, ufisadi na kuwataka wasomi kuacha kusononeka na badala yake wachape kazi huku wakieneza amani.

Akihutubia jana katika harambee ya kuchangia kanisa la Chuo Kikuu cha Iringa, kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Simaye aliwafunda wasomi wa chuo hicho akiwataka watumie nafasi waliyonayo kwa ajili ya kueneza amani na kuachana na masikitiko yasiyokwisha yanayotokana na  baadhi yao kutojituma katika kazi.

Alisema maandiko matakatifu ya Bibilia yanaeleza kwamba rushwa na ufisadi ni dhambi kubwa katika taifa na kuonya kwamba dhambi hiyo ikilelewa inasababishia matatizo makubwa.

Alisema kaburi pekee la mambo machafu ni ujenzi wa kanisa hilo na matumizi yake kutumika kwa malengo ya kuhubiri amani na kukemea ufisadi.

"Mfano ni nani kati yenu amepata kutozwa rushwa na mkulima? Rushwa inatozwa na wenye nafasi na hivyo lazima vijana wasomi mkimaliza hapa muende kubadilisha taifa .... ndiyo maana nilipoitwa na baba askofu kwa ajili ya harambee ya kanisa nikasema nitafika kwani ni jambo jema," alisema Sumaye.

Bila kutaja jina, Sumaye alisema kumshangilia mtu anayeendesha gari la kifahari kwa kulipata kwa njia ya wizi ni hatari.

Alisema hivi sasa watu wanajenga chuki kati ya wanyonge na matajiri na kuwa hivi sasa limezuka jambo baya zaidi kwa watu kuchukiana kwa misingi ya dini zao na kuwa  nchi yeyote itakayoingia katika machafuko ya imani ni hatari.

Sumaye alisema vita ya kiimani ni mbaya zaidi. “Na siku zote vita hiyo huwa haina mshindi hivyo ni vema kila dini kuanza utaratibu wa kuwafundisha vijana wake ili kuwa na uzalendo katika taifa hili.”

Aidha,  alisema mapambano ya dini yanayoendelea mbali ya kutokuwa na mshindi, hata vita nayo haitakuwa na mshindi na hivyo ni vyema kila mmoja kuachwa akiendelea kuamini kile ambacho ana amini hata kama ni chini ya mti na kuwataka Watanzania wasiruhusu vita hiyo kupandikizwa.

Sumaye alisema anafurahishwa kuona nyumba za ibada zinaendelea kujengwa na hivyo ni imani yake kuwa zitasaidia kuhubiri amani na utulivu pamoja na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Mbali ya Sumaye, harambee hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Christine Ishengoma pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

No comments:

Post a Comment