Baaadhi ya viongozi wa Serikali na Siasa wanaotafuta madaraka kupitia kwa waganga wa kienyeji (wachawi) wanachangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Tanzania kupoteza sifa ya utawala bora.
Kauli hiyo ilitolewa siku chache zilozopita na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG Kawe, Jijini Dar es Salaam, Rev. Elingarami Munisi wakati wa ibada.
Mchungaji huyo, alisema kuwa anashangazwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wapo tayari kwenda kwa mganga wa kienyeji kutafuta vyeo kama vile, ubunge, uwaziri na baadhi ya wanasiasa ambao hutumia muda mwingi kwenda kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kupata vyeo.
“Hapa lazima niseme wazi, mimi sitaki kuwaremba watu hao, nasema kuwa wanaoenda kwa watumishi wa shetani, yaani wanaoenda kwa wachawi kutafuta vyeo ni jambo la hatari, hatuwezi kuwa na viongozi waadilifu, haiwezekani kiongozi akatumia muda wake mwingi kutafuta uongozi kwa kutumia nguvu za giza,” alisema Mchungaji huyo.
Aidha Mchungaji Munisi alisema kuwa machafuko yanayoonekana karibu dunia nzima ni dalili za dunia kujikusanya pamoja kuunda serikali moja na dini moja ili kutoa nafasi kwa Mpinga Kristo kuchukua nafasi.
Kiongozi huyo alizidi kufafanua kuwa kwa sasa machafuko mbalimbali ya udini pamoja na vita kati ya nchi na nchi ni mpango mahususi ya kuwafanya viongozi wa dunia kuona kuwa njia pekee ya kuifanya dunia itawalike ni kuanzishwa kwa dunia moja na serikali moja yenye dini moja.
Mtumishi huyo alizidi kuweka wazi kuwa, kwa sasa viongozi wa nchi wanatakiwa kushikamana ili kuiombea Tanzania ili isipoteze amani yake ambayo ilijengwa na waasisi wake miaka 50 iliyopita.
Alisema kama viongozi pamoja na watanzania kwa ujumla wasipokuwa na hofu ya kimungu ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa nchi ikashindwa kutawalika kutokana na amani kupotea kutokana na machafuko ambayo yanafanywa na baadhi ya watu ambao ni wafuasi wa shetani.
Hata hivyo amekemea baadhi ya watanzania ambao wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuiga mambo ya nchi za Magharibi na kuusahau utamaduni wa kitanzania kwa kukiuka maadili bora ya kiafrika.
No comments:
Post a Comment