Rais Jakaya Kikwete, ameelezea kuogopeshwa na kulegalega kwa amani,
utulivu na usalama wa nchi hasa katika kipindi cha mwaka jana.
“Nimeogopeshwa sana na hali ya kulegalega kwa hali ya amani, utulivu na
usalama wa nchi yetu, hususani kipindi cha mwaka jana na naomba hali
hiyo isitokee tena mwaka huu wa 2013,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
"Maana hata nilipolazimika kutumia vyombo vya dola vyenye dhamana ya
kutuliza ghasia, bado hali ilikuwa ngumu…lakini naamini kupitia misikiti
na makanisa mkiendelea kuwahubiria waumini wenu, hali itakuwa shwari,”
alisema wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Mteule wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)- Dayosisi Kati-Singida, Mchungaji
Dk. Alex Mkumbo, iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo, Usharika wa
Imanuel, mjini hapa jana.
|
Rais Jakaya Kikwete |
Kwa msingi huo, Rais Kikwete, ameyataka madhehebu ya dini kurejesha
utaratibu wa zamani wa kukutana pamoja mara kwa mara kujadili mahusiano
baina yao ili kuepukana na uhasama wa kidini unaoweza kusababisha
machafuko makubwa nchini.
Alisema masuala ya udini siku za nyuma hayakuwapo hapa nchini kutokana
na viongozi wa madhehebu ya dini kukutana na kumaliza tofauti zao
mapema.
Hata hivyo, alisema hivi sasa utamaduni huo umetoweka hali inayoweza kuchangia kutokea kwa machafuko ya udini nchini.
Aidha, Rais Kikwete aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwahubiria
waumini wao kujiepusha na vurugu za udini, matumizi mabaya ya dawa za
kulevya, uvivu, biashara ya ukahaba na kupiga vita vitendo vya kuomba na
kupokea rushwa ili washiriki vema kujiletea maendeleo yao.
“Dini na serikali wote tunafanya kazi ile ile ya maendeleo na wananchi
wanahimizwa kujiletea maendeleo na dini pia inahimiza waumini wake
kupata maendeleo. Kwa hiyo nawaomba tuendelee kushirikiana pamoja,
serikali yangu inaahidi kushirikiana na madhehebu ya dini,” alisema.
Alisema utaratibu wa zamani wa viongozi wa dini waliokuwa wanautumia
kukaa na kujadili masuala mbalimbali, ulisaidia kutuliza ghadhabu,
kuonya na kufundisha, hali aliyotaka ufufuliwe na kuhuishwa upya ili
kuimarisha amani na utulivu nchini.
|
Askofu Mteule wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)- Dayosisi Kati-Singida, Mchungaji
Dk. Alex Mkumbo mbele, na kwanyuma ni yake ni Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa |
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT, Alex Malasusa, alimshukuru Rais
Kikwete, kwa kutoa kauli hiyo inayowahakikishia waumini wa madhehebu
yote uhuru wa kuabudu kila mtu na dini yake pasipo kuingiliwa.
Dk. Malasusa alimweleza Rais Kikwete kuwa Kanisa litakuwa bega kwa bega
na serikali kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini,
licha ya wachache kutaka kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.
Mapema baada ya kuwekwa wakfu, katika risala yake, Dk. Alex Mkumbo,
alimwomba Rais kurejesha Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruruma iliyopo
wilaya Iramba, kutokana na eneo hilo kuwa kitovu cha madhehebu ya
Lutherani, kwenye dayosisi hiyo.
Dk. Mkumbo alimweleza Rais Kikwete kuwa shule hiyo ilichukuliwa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na yeye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,
Kanisa linaiomba shule hiyo ili kuweka mambo mengi muhimu ya ukumbusho
wa KKKT Dayosisi ya Kati.
Hata hivyo, katika majibu yake, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa
kanisa hilo kukutana na wenzao viongozi wa ngazi ya mkoa wa Singida ili
kumaliza kabisa tatizo hilo.
Katika sherehe hizo, wageni mbalimbali walihudhuria wakiwamo Maaskofu wa
kanisa hilo kutoka ndani na nje ya nchi kama Norway, Ujerumani, Afrika
Kusini na Marekani.
Source:Nipashe