Kanisa la TAG, katika
kijiji cha Nihongola Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo, mkoani Kagera
limeteketezwa kwa moto na kusalia majivu, usiku wa manane wiki iliyopita na
watu wasiojulikana, huku wachomaji wakiacha ujumbe mkali uliojaa matusi.
Akiongea na chanzo cha habari hii,
Mchungaji wa kanisa hilo, Samwel Baguma, alisema tukio hilo, lilitokea wakiwa wamelala, lakini walishtushwa na mwanga uliosababishwa na moto
uliokuwa ukiteketeza viti na meza zilizokuwa ndani ya kanisa hilo.
Mchungaji Baguma alieleza
kuwa, walipoona moto umepamba moto huku ukiwa umekwisha kuharibu kila kitu,
walitoka nje na kuita watu ambao walitoka na kuzima licha ya kuwa ulishafanya
uharibifu wa kutosha.
“Ilikuwa majira ya saa nane
hivi, tulihisi kuna kitu kinachoungua kanisani, tulipokurupuka na kutoka nje
ndipo tukaona moto mkubwa ukimalizia kuunguza jengo la kanisa na vitu kadhaa vilivyokuwemo
ndani,” alisema na kuongeza:
“Tulipiga kelele na watu
walitoka kutusaidia kuuzima ingawa ulikwisha teketeza vitu karibu vyote, baada
ya kumaliza kuuzima huku kukiwa kumepambazuka niliona tofali moja likiwa
limeegesha karatasi nyeupe na nilipoichukua na kuiangalia nilishtushwa na
ujumbe wake.”Alisema alipoisoma ilikuwa imeandika maneno ya
kumtukana vikali yakiambatana na vitu vilivyoashiria ushirikina kwa kumtaka
aache eneo hilo alilojenga kanisa kwa madai lina wenyewe.
Alisema, barua hiyo amekwisha iwasilisha
Polisi, huku akieleza kuwa ana vielelezo vya kutosha juu ya upatikanaji wa eneo
hilo la kuabudia ambapo alibainisha kwamba aliuziwa kihalali na sheria zote
zilizingatiwa.
“Kwa sasa tunaabudia kwenye boma letu lingine,
hatuna mpango wowote wa kuogopa kile kilichotendeka, siwezi kushtushwa na mambo
ya kichawi kwa kuwa Yesu ni zaidi ya wachawi wote, tutaendelea kukaa hapa hadi
Yesu anarudi,” alisema.
Aidha alilaani kitendo hicho, kwa kuwa
kinarudisha nyuma maendeleo, huku akibainisha kwamba ni vema kama mtu ana jambo
akaliweka mezani, watu wakalijadili kuliko kufanya uharibifu ndani ya nyumba ya
Mungu.
Akiongea na chanzo cha habari hii Askofu wa Jimbo la Kagera, Julius Bibuhinda
alidhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani kitendo hicho, huku akieleza
kuwa wameiachia Polisi kuwasaka wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, ACP Philipo
Karange, akiongea na chanzo cha habari hii alidhibitisha kutokea kwa tukio hilo nyakati za usiku mnene na kuongeza kuwa, wameshawakamata watu watatu
na upelelezi bado unaendelea.
“Hii ni kesi ya jinai,
waliokamatwa hadi sasa ni watu watatu wakiwemo ndugu wawili, Bw. James
Bugarukanyi na Fabian Bugarukanyi, waliouza kiwanja hicho kwa Mchungaji muda
mrefu.Kamanda huyo alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Rinus Nikodemo, na watafikishwa
mahakamani.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na
matukio ya uchomwaji moto wa nyumba za kuabudia, kushambuliwa kwa watumishi na
hata kumwagiwa tindikali,Hayo yanatokea, wakati zipo juhudi kubwa
ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa dini kuleta suluhu baina yao.