Askofu KKKT atahadharisha uanzishwaji vikundi vya ulinzi

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu, amesema kitendo cha viongozi wa vyama vya siasa ya kuamua kujianzishia vikundi vya ulinzi wa kujilinda kwenye vyama vyao, ni ishara tosha ya kuhatarisha amani ya Taifa.

Askofu Kinyunyu amesema viongozi wa siasa wanaoanzisha vikundi vya namna hiyo ni kuashiria jinsi gani walivyokosa heshima kwa Mungu na kwa mamlaka ya serikali ambayo ina ulinzi na usalama unaolinda nchi kwa ujumla.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu.
Alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa miradi ya mifumo ya miundombinu ya watoto ikiwamo ya maji, madarasa na vyoo vya kisasa iliyodhaminiwa na shirika la Compassion International Tanzania kwa kushirikiana na washirika wenza kutoka kwenye Makanisa ya Huduma ya Mtoto iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Tag Miyuji mjini hapa.

Askofu Kinyunyu alisema kitendo cha vyama hivyo kuanzisha vikundi vya kujilinda, ni ishara ya kuleta machafuko ya amani ya nchi.

Pia alisema kitendo hicho kitawafanya vijana waliopo katika vyama hivyo kuendelea kuchukiana badala ya kupendana.

Alisema viongozi wa kisiasa hawana budi kutambua kuwa kwa kuanzisha vikundi hivyo ni kuzidi kujenga uhasama mkubwa utakaoiumiza jamii isiyohusika wakiwamo watoto, wanawake, wazee na walemavu.

“Hapa wanatakiwa kujua kuwa kitendo hicho ni ishara tosha inayoashiria kuanzisha vita ambayo washirika wakubwa ni vijana tunaowategemea kushika madaraka mbalimbali ya kiserikali na ya kisiasa,” alisema.

Askofu Kinyunyu amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuheshimu amani iliyopo iliyobarikiwa na Mungu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Compassion Intenrational Tanzania (CIT) hapa nchini, Mchungaji Joseph Mayala, alisema kitendo hicho ni sasa na uwekezaji kwa vijana wawe na roho ya ukatili badala ya upendo na amani.

Source:Nipashe

No comments:

Post a Comment