Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ), Askofu Dk.Alex Malasusa amesema nchi haitakuwa na amani kwa kuongeza idadi ya polisi bali amani itapatikana kutokana na Watanzania kuheshimiana.
Askofu Malasusa aliyasema hayo jana alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Faragha na maombi katika Kijiji cha Chasimba wilayani Bagamoyo kitakachojengwa kwa ushirikiano wa Usharika wa Dayosisi ya Kariakoo.
Askofu Dk.Alex Malasusa |
“Nchi haiwezi kuwa na amani kwa kuongeza idadi ya polisi njia pekee ni kuheshimiana na kuheshimu madhehebu mengine ili kuendeleza amani,” alisema Dk.Malasusa.
Aidha, alisema kituo hicho kitajengwa kumbi za kisasa za mikutano, zahanati, chuo cha ufundi, maktaba na nyumba ya faragha kwa ajili ya maombi na viwanja mbalimbali vya michezo.
Katika ibada hiyo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais Dk.Gharib Bilal, lakini aliwakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa rais Mazingira Dk.Theresia Huvisa.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais Dk.Huvisa alisema serikali itashirikiana na taasisi mbalimbali zikiwamo za kidini kusaidia kuendeleza maendeleo.
Ofisi yake ilichangia Shilingi milioni mbili katika harambee iliyofanyika kwa lengo la kupata milioni 200 kuendeleza ujenzi huo.
Katika harambee hiyo iliyoshirikisha viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi Mchungaji Daniel Thabita kutoka Botswana alichangia Sh.milioni 1.5.
Source:Nipashe
No comments:
Post a Comment