Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka Watanzania kukataa kugawanywa kwa misingi ya udini.Akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr mjini Tabora jana, Dk.
Bilal, alisema ni busara waumini wa dini na madhehebu kujenga utamaduni
wa kuvumiliana hasa zinapotokea hitilafu miongoni na kati yao.Pia, Dk. Bilal alikemea ubaguzi unaotokana na kabila, rangi, jinsia au mahala mtu alipo au anapotoka.
“Kaeni pamoja na kutafuta muafaka kwa njia ya majadiliano ya amani na
upendo, pasipo kutawaliwa na jazba wala chuki. Tukumbuke kauli na
angalizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba vita ya dini haina mshindi,”
alisema.Dk. Bilal, alisema Tanzania imekuwa kisiwa cha amani na utulivu, jambo
lisilompendeza kila mtu kutokana na kuwapo wanaotutazama (nchi) kwa
jicho la husda na kuiombea mabaya.
 |
| Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal |
“Wanatuombea tufike mahali tuharibikiwe ili wao wafurahi. Lakini
wakumbuke kuwa dua la kuku halimpati mwewe," alisema. Alisisitiza kuwa
amani katika taifa au jamii yoyote ni sharti la kwanza katika mchakato
wa kuleta maendeleo.
Alisema anaamini viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga
maadili mema katika taifa hili na kwamba watu wakishiba imani ndani ya
nafsi zao, wakaelewa na kuzingatia mafundisho ya dini zao, maovu
yataondoka kati yao.
Alisema, uwapo wa amani na utulivu unaifanya serikali kupata ahueni,
kwamba badala ya kutenga bajeti kubwa kupanua magereza, kugharamia
wafungwa na mahabusu na uendeshaji wa mahakama, rasilimali hizo
zitaelekezwa katika mipango mingine ya maendeleo.
Dk. Bilal alisema katika siku za hivi karibuni, yameibuka matukio kadhaa
yanaoashiria kutaka kuvuruga amani na utulivu wa taifa na kwamba hujuma
hizo zinafanywa na watu wachache wasiolitakia mema taifa kwa maslahi
yao binafsi.
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ipo madhubuti na itahakikisha
inapambana kwa nguvu zote kudhibiti hujuma zote zenye nia mbaya ya
kuchafua sifa njema ya amani na utulivu wa Tanzania.
“Watanzania tumeishi kama ndugu na taifa moja kwa muda mrefu na kamwe
hatutakubali tunu hii njema ivurugwe kwa kisingizio chochote kile,”
alisema.
Aliongeza kuwa kamwe serikali haitakuwa tayari kuona Mtanzania anaishi
kwa hofu na mashaka ndani ya nchi yake kutokana na vitendo vya wahuni
wachache.
“Kila itakapobidi, tutawasaka, tutawakamata na kuwakomesha kwa rungu la
mkono wa sheria. Nawahakikishieni kwamba Tanzania yetu itabaki nchi
salama ya amani na utulivu na ya kupigiwa mfano daima.“
Alisema uhuru wa kuabudu katika taifa hili umejengewa misingi ndani ya
katiba na kutokana na ukweli huo, kila mmoja anapaswa kuheshimu imani au
dini ya mwenzake pasi kujiona kwamba imani au dini yake ni bora zaidi.
“Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia mwamko mkubwa kwa taasisi hizi
kuanzisha shule za msingi, vyuo hadi vyuo vikuu jambo ambalo sisi katika
serikali tunaridhishwa nalo na kuhamasisha kasi zaidi ya kuimarisha
sekta ya elimu," alisema.
Alihimiza kuongeza kasi zaidi katika
kuboresha sekta ya elimu na kuongeza kuwa uhai wa taifa hili na lolote
lile duniani utategemea ubora wa elimu inayotolewa leo
Source: NIPASHE