‘Tumegoma kupokea misaada ya waabudu shetani’

Mmiliki na mwanzilishi wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na yatima cha Hananasif Orphanage Centre (HOC) Bw. Hezekia Mwalugaja, amesema kituo chake kimekataa baadhi ya misaada yenye masharti ya kishetani, inayolenga kuwaunganisha na madhabahu ya kisheni.

Akiongea na moja la Kikristo katika Mahojiano maalumu, mara baada ya kupokea msaada wa vyakula wenye thamani ya Shilingi 700,000 iliyotolewa na kanisa la EAGT City Centre, linaloongozwa na Mchungaji Flarian Katunzi, Bw. Mwalugaja, alisema kuwa  anamshukuru Mungu kuwainua watakatifu kujitolea kufanya kazi pamoja na kituo hicho katika mazingira safi na yenye kumpa Mungu utukufu.



Alisema kuwa kituo hicho kina zaidi ya watoto 100, 98 miongoni mwao wakiwa wanafunzi wa Sekondari ambao wanatunzwa na kusomeshwa na kituo, huku wanafunzi wanne wakiwa katika shule za msingi.

Awali akishukuru mbele ya maelfu ya waumini wa kanisa hilo waliochanga fedha kwa ajili ya kununulia chakula cha msaada kwa watoto hao, alisema kuwa kwake huo ni muujiza kwani Mungu alisema na Mtumishi wake, Mch. Katunzi na wauminini wake wakachanga chakula hicho kwa ajili ya watoto yatima kwa wakati huu ambao wamekataa misaada mingi ya wafadhili kutoka Magharibi.

Akifafanua alisema: “Wafadhili tuliowakatalia kupokea mamilioni ya misaada yao walitupa masharti magumu, ikiwa ni pamoja na kuacha kuendesha ibada na maombi, kituoni hapo na kufanya mambo mengine ambayo ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Ni mambo ya kishetani kabisa.”

Kisha aliendelea: “Miongoni mwa mambo ambayo wafadhili hawataki ufundishe kinyume chao ni pamoja na ndoa za jinsi moja, kuwa ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na ni dhambi. Wanataka ufundishe mafundisho ya mseto ya dini zote. Kwetu tulikataa kwa kuwa hiyo sio imani yetu.”

“Mkazo mkubwa kwenye kituo chetu ni kuwafunzisha watoto wale jinsi ya kumtegemea Mungu na kuishi maisha matakatifu, tunawaandaa kuwa vyombo vya kumtumainia Mungu, lakini wafadhili wa kimagharaibi hawataki kabisa mafundisho ya dini kituoni na hilo ndilo sharti kubwa la kupokea misaada yao.”

Alisema kuwa wamefikia mahali pa kuamua kumtumainia Mungu na kuwaambia misaada ya masharti ya kufundisha watoto ndoa za jinsia moja na dini za mseto baina ya madhehebu yote, ni  ibada ya Mungu mwingine na wao hawako tayari kuifanya.

Akikabidhi misaada hiyo muda mfupi kabla ya ibada kuanza, Mchungaji Katunzi alisema kuwa kanisa lake lina program ya kuigusa jamii kwa Neno na tendo, hivyo waliamua kujitoa, ili kuwasaidia watoto hao waliopoteza wazazi na walezi.

Kiongozi huyo alisema kuwa michango hiyo ilitolewa na waumini wa kanisa hilo kwa ajili ya kuwasaidia wenzao. Aliwashukuru wana EAGT City Centre, kwa moyo wao wa huruma walionyesha kuwa kujitoa kusaidia watoto hao.

Ambassadors of Christ ndani ya Tamasha la Pasaka 2013

Katika Kuelekea Tamasha la Pasaka mwaka 2013 watakaokuja kuhudumu kwenye tamasha hilo imezidi kuongezeka na sasa Ambassadors of Christ wamethibitisha kuwepokatika Tamasha hilo

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama amesema kuwa kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda inayotamba na albamu ya Mtegemee Yesu imethibitisha kushiriki tamasha hilo litakalofanyika Machi 31 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

 “Watakuja kung’arisha tamasha la mwaka huu na wamejipanga vya kutosha kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya nguvu, nia yetu ni kuwa na wasanii wakubwa Afrika na hilo ndilo tutakalolifanya mwaka huu.


 “Kabla ya Jumatano tutatangaza msanii mkubwa mwingine ambaye bado tunaendelea na mazungumzo naye kuhakikisha mambo yanakuwa safi, ili aje kutumbuiza kwenye tamasha letu,” alisema Msama.

 Alieleza kuwa katika albamu yao hiyo ina nyimbo nane ambazo ni JY’ Ushima Uwite, Mtegee Yesu, Ndifuza Kugerayo, Iyana Iby’ Isi, Yesu Niwe Mungeri, Parapanda, Abasaruzi na Nenda.


 Wasanii wengine wa nje ya Tanzania ambao tayari wamethibitisha kushiriki tamasha hili ni , Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya. Wasanii wa Tanzania ni Rose Muhando, Upendo Nkone na John Lissu.

 Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na  litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana avamiwa na majambazi.

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa, amevamiwa na majambazi nyumbani kwake, Mbezi kwa Yusufu, Kimara jijini Dar es Salaam usiku wa uamkia juzi.

Katika tukio hilo, mlinzi wa askofu, amejeruhiwa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni katika kumshinikiza aonyeshe alipo Askofu Mokiwa.

Kwa mujibu wa Askofu Mokiwa, tukio hilo lilitokea jana saa 8:45 usiku ambapo watu hao walikata uzio na kufanikiwa kuingia kwenye uwanja wa nyumba yake.

Alisema baada ya watu hao ambao idadi yake haifahamu kuingia ndani ya uzio, walikutana na mlinzi na kumshinikiza awaonyeshe alipo yeye (askofu). Aliongeza kuwa, mlinzi huyo baada ya kuwaeleza watu hao kuwa, askofu hayupo, walianza kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili.

“Wamemjeruhi mshipa wa mguu wa kushoto, sehemu za kichwani na kukata kidole, wakati haya yakiendelea mlinzi wangu alipiga kelele ambazo ziliwezesha kumshtua mke wangu na mlinzi mwingine wa jirani yangu,” alisema Mokiwa alisema baada ya mke wake kusikia kelele hizo, alimuamsha na baada ya watu hao kubaini hilo, walikimbia kusikojulikana. Alisema walitoa taarifa kituo cha polisi Mbezi Luis ambapo polisi walitoa ushirikiano.

“Baada ya polisi kutupa PF3 tulimpeleka majeruhi hospitali ya Tumbi, Kibaha ambapo hapo alitibiwa na kuruhusiwa, hali yake sio mbaya ingawa analalamika anamaumivu makali maeneo yenye majeraha,” alisema.

Askofu Mokiwa akizungumzia kuhusiana na kauli za watuhumiwa hao kumtaka yeye baada ya kuingia kwenye nyumba yake, alisema anafiriki watu hao watakuwa wametumwa na mtu.

“Nadhani wametumwa lakini sijui ni nani amefanya hivyo, kiukweli sina chuki, uadui wala kinyongo na mtu yeyote, ninaishi na watu wangu vizuri, sijui haya yanayotokea yanalenga nini,” alisema.

Alisema katika maisha yake tukio la kuvamiwa ni la kwanza na kwake amesema ni la aina yake.

Aidha, wakati akizungumza na chanzo cha habari hii Jumapili kwa njia ya simu majira ya saa 8: 15 mchana, Askofu Mokiwa alisema polisi wamewasili nyumbani hapo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, analifuatilia.

Source:Nipashe

Historia ya Askofu Kulola yaandaliwa

Taasisi isiyo ya kiserikali, inayojihusisha na utafutaji na ukusanyaji wa taarifa na shuhuda, ijulikanayo kama; Moses Kulola Faundation, imeanza kuandaa historia ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dk. Moses kulola.

Histolia ya Askofu Kulola kwa ufupi, alizaliwa mwezi Juni 1928 katika familia ya watoto kumi. Alisomea shule ya msingi ya Ligsha Sukuma, halafu taasisi ya usanifu. Alibatizwa kikristo mwaka 1950 katika Kanisa la AIC Makongoro. Alimwoa Elizabeth wakawa na watoto kumi.

Alifanya kazi ya uchungaji wa kanisa la AIC miaka ya 1961-1962 akaendelea na masomo ya kitheolojia. Baada ya kujiunga na dhehebu la kipentekoste alifanya kazi ya uchungaji ndani ya kanisa la TAG miaka ya 1966-1991. Akajitenga na kanisa hilo na kuanzisha kanisa jipya mwaka wa 1991, kanisa la EAGT (kwa Kiingereza Evangelistic Assemblies of God) akawa askofu wao wa kwanza tangu mwaka uleule.
(Chanzo wikipedia)

Msemaji wa Shirika hilo Mwinjilisti Willy Kulola aliliambia gazeti la Kikristo la Jibu la Maisha siku chache zimepita kuwa lengo la kuandaa historia hiyo ni kutaka kuonyesha kazi kubwa ya Mungu aliyoifanya Askofu Kulola ya kuwaleta watu kwa Yesu.

Aliongeza kuwa mpakwa mafuta huyo wa Mungu ametimiza miaka 67 sasa tangu aanze huduma ya kumtumikia Mungu, huku akibainisha kuwa  kuna mafanikio makubwa yamepatikana ya kuvunja ngome za ibilisi katika maeneo mbalimbali ya taifa  ya Tanzania hata nchi za nje

“Katika hatua nyingine, ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na watanzania walio wengi  nchini na nje ya nchi ni kuwepo kwa maandishi ya kueleza huduma ya kiroho ya Mtumishi wa Mungu Dk. Moses Kulola,” alisema  Mwinjilisti huyo na kuongeza.

Hivi sasa mpakwa mafuta huyo wa Mungu metimiza miaka 67 tangu alipoitwa kumtumikia Bwana Yesu, kwa hiyo mchakato wa kuandaa historia ya baba yetu Dk. Kulola umeanza na utakamilika hivi karibuni.

Alisema lengo ni kumtukuza  Mungu kwa matendo makuu anayoyafanya kwa watu wake na kuangusha ngome za mwovu ibilisi, sambamba  na  kujipanga imara katika kuifanya kazi ya Bwana, ikiwa ni pamoja na kupata mbinu mpya  za kumkabiri shetani.
Askofu Dr Moses Kulo akiwa na kundi la wakristo wa Tanzania walipokuwa Israel

Askofu bandia ajipenyeza mkutano wa makadinali

Askofu bandia amefanikiwa kujipenyeza na kuingia kwenye mkutano wa makadinali unaoendelea mjini Vatican, kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya.

Askofu huyo bandia, Ralph Napierski ambaye ni mzawa wa Ujerumani alifanikiwa kujipenyeza na kusalimiana kisha kupiga picha za kumbukumbu na baadhi ya makadinali waliopo kwenye mkutano huo bila kugundulika.

Uzamiaji wake ambao ulileta mashaka kuhusu uimara wa usalama eneo hilo wanapokutana makadinali 103, ambao wamekusajika kwenye Makao Makuu ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya, huku wengine 12 wakiwa hawajawasili.

Katika mkutano huo, Kadinali wa juu kutoka Uingereza, Cormac Murphy O'Connor pia anahudhuria.

Mtu aliyejifanya Kardinali wa Kanisa Katoliki, Ralph Napierski (kushoto) akisalimiana na Kardinali Sergio Sebiastiana. Napierski alikamatwa akijaribu kuingia kwenye mkutano wa makardinali unaoendelea Vatican 
Napierski alionekana akisalimiana na Kadinali Sergio Sebiastiana nje ya ukumbi wa Papa Paul VI akiwa hajatambua kuwa siyo miongoni mwa wenzake, huku akiwa amezungukwa na makasisi wengine wa kanisa hilo ambao pia hawakuweza kutambua.

Walinzi wa kundi la Swiss Guars linaloshughulika na ulinzi wa Makao Makuu ya Kanisa Katoliki  Vatican, walimbaini kuwa siyo miongoni mwa wahusika kutokana na vazi lake alilofunga kiunoni, ambalo siyo sahihi bali ulikuwa ni mtandio uliokunjwa vizuri.

Pamoja na vazi hilo la rangi ya zambarau kutokuwa sahihi, pia kofia aliyokuwa ameivaa haikuwa miongoni mwa zile zinazotambulika kuvaliwa na viongozi wa kanisa hilo.

Tofauti nyingine iliyobainika ni ufupi wa kanzu yake na rozari aliyovaa haikuwa halisi, kwa kuwa ilikuwa ni fupi kuliko wanazotumia viongozi wa kanisa hilo.

Kabla ya kubainika, Napierski alijitambulisha kwa waandishi wa habari kwamba jina lake ni Basilius ni miongoni mwa wawakilishi wa Kanisa la Orthodox kutoka Italia.

Awali, kulikuwa na taarifa kwamba aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kanisa Katoliki limefanya “Kosa kubwa” kwa kuwaruhusu makasisi wanaotuhumiwa kwa makosa ya ngono kubadilishwa kutoka maeneo yao ya awali na kupelekwa kwingine, kuficha kashfa zao badala ya kuzishughulikia.

Mtuhumiw ahuyo ambaye baada ya kubainika aliondolewa eneo hilo, anaongoza tovuti ambayo aliitumia kujitambulisha kwamba yeye ni kasisi kupitia Shirika la Kikatoliki la Corpus Dei, huku akiwa amevaa mavazi ya kikasisi na kujidhihirisha kama “Mtumwa na Nabii kama Mtakatifu Paul”.

Msemaji wa Kanisa Katoliki mjini Vatican, Federico Lombardi alisema hayupo tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu hajapata taarifa yoyote na muda wote alikuwa  akishughulika katika mkutano

Source:mwananchi.co.tz

Watumishi wa Mungu 30 kuikabili Kondoa

Watumishi wa Mungu wapatao 30 toka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, wanameanza kazi ya kuuvamia mji wa Kondoa kiinjili ikiwa ni katika mpango wa kupeleka Neno la Mungu katika vijiji vya Dodoma, kumnyang’anya shetani mateka na kutawala.

Akizungumza hayo Jijini Dar es salaam yaliyofanyika mwanzilishi wa huduma hiyo, Gospel For All People, (GFAP), Mchungaji Tumaini Chanjarika, alisema kuwa mpango huo umekamilika.

Mchungaji huyo alisema, timu hiyo imewasili wilayani Kondoa mwishoni mwa mwezi uliopita mwaka huu, ambapo mikutano itaanza rasmi katika vijiji vinne, watakuwa na ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba na jioni watafanya mkutano mkubwa wa injilii, katika vijiji hivyo.

“Safari ya Kondoa kwa sasa imekamilika, tuta chukua takriban mwezi mmoja, kuwaeleza watu wa vijiji vya wilaya hiyo habari za Yesu, kutakuwa na timu itakayotangulia wiki moja kabla, kisha timu ya pili itafuata, lengo ni kuwaleta watu kwa Yesu,” alisema Mchungaji Chanjarika. 

Alisema mara baada ya kufika wilayani humo zitagawanywa timu ambapo kila moja itakuwa na kijiji chake, na itafanya kazi hiyo ya kumkanyaga shetani wilayani humo pasi mzaha.

Mbali na hilo aliongeza kuwa, mikutano itachukua wiki tatu na semina kwa waongofu wapya wiki moja, huku akiamini kuwa kwa neema ya Mungu watayaona mafanikio makubwa katika kazi hiyo ya kuwaleta watu kwa Bwana ili kuachana na dunia iliyoharibika.

“Katika huduma ya Kondoa tutaingia nyumba kwa nyumba kushuhudia, lengo letu ni kuwaleta watu kwa Yesu, waache kuteswa na ibilisi baada ya mikutano ya vijijini timu zote zitaungana na kufanya mkutano mkubwa mjini Kondoa,” alisema Mchungaji Chanjarika.

Mbali na hilo Mchungaji huyo aliweka wazi kuwa bado wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha kama vile; upungufu wa fedha.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa vyombo vya injili ambapo zinahitajika seti nne, pamoja na usafiri wa vyombo, hivyo kuwataka watumishi wa Mungu kujitoa kusaidia ili kazi ya Bwana isonge mbele.

Huduma hiyo alieleza kwamba ni endelevu, ambapo mara baada ya Kondoa, wana mikakati ya kwenda maeneo mengine kumhubiri Kristo.

Mwenyekiti wa (GFAP) Paul Kashaga, akitokea wilayani Kondoa kwa ajili ya utafiti kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa Neno la Mungu hasa vijijini, kutokana na kuzungukwa na dini ya kiislamu.

Aliongeza kuwa bado kuna umuhimu wa wadau wa injili kuelekeza macho katika wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kujitoa kuwasaidia watumishi wa Mungu walioanzisha huduma katika maeneo ya vijiji vya Kondoa.   

Dhamira ya huduma hiyo, aliizungumzia ni kumtangaza Kristo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ili watu wamjue Mungu kwa lengo la   kukomesha migogoro isiyo na tija inayoibuka kila kukicha katika taifa la Tanzania.

Niko ambaye Niko Studio yatoa Ofa Kubwa kwa Wateja wake.

Studio ya kisasa ya NIKO AMBAYE NIKO, iliyojikita katika kuwawezesha waimbaji wa muziki wa Gospel, kufikisha ujumbe wao kwa jamii, imetangaza neema kwa wale wanaotaka ‘kutoka’ kimuziki, kwa kuwapunguzia karibu nusu  ya gharama za kuandaa na kurekodi muziki. Ungana na Mkurugenzi wa Studio hiyo, yanye sifa za kimataifa, Steven Wambura, katika makala haya yanayokupa mwanga wa kile kinachoendele.

Katika Mahojiano maalumu na chanzo kimoja kimoja cha habari ofisini kwake Mwananyamala, Jijini Dar es Salaam, Wambura ambaye pia ni mwimbaji wa muziki wa Injili, mpiga ala na muongozaji, lakini pia aliyejikita kikamilifu katika biashara mbalimbali, alisema kuwa, NIKO AMBAYE NIKO STUDIO,  imeamua kudhihirisha kwa vitendo kuwa, imedhamiria kuwainua watanzania wenye kiu ya kumwimbia Muumba wao.

“Lengo langu tangu mwanzo nilipoanzisha Studio hii, lilikuwa na linabaki kuwa hilo hilo, kusaidiana na wenzangu wenye ujumbe kuufikisha kwa jamii, ndio maana kwangu kupata fedha nyingi sio jambo la kipaumbele, naitazama huduma kwanza. Nafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa, nafikia lengo, katika kuzingatia hilo, nimeamua kuwapunguzia nusu nzima ya gharama za kurekodi, kuandaa, kupigiwa ala, na ushauri wa kibiashara na kiufundi wateja wangu wote,”alisema Wambura.
Mkurugenzi wa Studio, Steven Wambura
Alisema kuwa, Studio hiyo imezidi kujiimarisha kwa kumpata mtaalamu aliyebobea katika uzalishaji muziki (Producer), kutoka Dodoma, ambaye amekuwa chachu ya ubora wa kazi za Studio hiyo, ya kisasa zaidi jijini Dar es Salaam.
Alimtaja Producer huyo kuwa ni; Zakayo Shushu, ambaye  ni mtaalamu wa kuchanganya muziki na pia mshauri wa muziki ambaye amekuwa akiwasaidia  wasanii wengi waliofanikiwa na kazi zao kuwa lulu katika jamii.

“Mwaka huu tuna Program nyingi zilizolenga kuigusa jamii, kwa mfano; tumejipanga kuwasaidia wasanii ambao Albam zao zimedumaa, wako wengi ambao wamejaribu kutoka wakashindwa kutokana na makosa katika  hatua mbalimbali za uandaaji wa muziki.
Unajua muziki una hatua nyingi na kosa katika hatua moja tu linaweza kuifanya kazi isipokelewe na jamii kwa uzito wake hata kama maeneo mengine ni bora kiasi gani,”alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza:

“Mtu anaweza kuwa na albam nzuri tu, lakini akakosea katika kuipa jina, au katika baadhi ya ala  na mpangilio wa mashairi na ikadumaa sokoni. Ninaposema kudumaa sokoni namaanisha, kutonunuliwa na wateja, haya mambo yanaendana sana, ili muziki wako ukubalike ni lazima kwanza upokelewe na jamii husika. Uguse hisia zao wainunue wasikilize ujumbe. Ni lazima muziki ukamilike kila eneo ndipo uiguse jamii  ivutwe kwa Yesu.


Aliziasa Kwaya, vikundi vya uimbaji, bendi na hata watu binafsi kutochezea ofa hiyo  kwa kuwa ni ya wakati tu, waende wakakutane na wenzao waliofanikiwa kimuziki.

Mbali na Studio, Wambura pia hujihusisha na Biashara ya kununua na kuuza magari  na tayari amefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Akizungumzia biashara hiyo alisema: “Namshukuru sana Mungu, kwa kuwa alinipa fursa ya kumtumikia kwa njia nyingi, nimekuwa nikifanya biashara ya magari na kwa kweli nimefanikiwa kuwasaidia hata watumishi wengi kupata magari ya kisasa na bora  kwa gharama sahihi,” alisema Wambura na kuongeza:   “Hapa mjini mambo ni mengi na wengine wanatumia kutojua kwa wengine kama mtaji wa kuwaibia, lakini mimi nimejikita katika kuwahudumia wengine kwa hofu ya Mungu aliye juu.”
 
Wambura akifafanua zaidi alisema: “Nilianza taratibu lakini sasa nimefanikiwa kwa kiwango  cha juu nanunua na kuuza magari mengi tu, na kwangu mimi ubora na uaminifu ni silaha kubwa, hivyo nimekuwa wateja wengi na wengine wananiambia ….Wambura nataka Gari pesa sina zote nitaleta  nawaamini nawapa na wanalipa, hii ni kwa kuwa nafanya haya yote kwa kumwamini Mungu, kwangu mimi Mungu ni wa kwanza na mengine yanafuata.”

Niko ambaye niko studio ipo Mwanyamala A. eneo la Mwijuma, katika majengo ya kanisa la Pentekoste, karibu na Ofsisi za kikundi cha TOT,  na unaweza kuwasiliana nao kwa Simu namba:
0657-334006 au 0714-678544

Kwa wale wanaohitaji magari wanaweza kuwasilina na Steven Wambura kwa simu namba 0784-252522 au 0655-252522.
KARIBU NIKO AMBAYE NIKO uhudumiwe kwa upendo wa Kristo aliyehai.

Viongozi wa Dini wakutana Arusha kwa ajili ya kuomba Amani kwa Nchi za EAC

Viongozi wa dini wakiwemo wachungaji zaidi ya 400 kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wamekutana Jijini Arusha katika Kongamano  kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya uongozi wao pamoja na kuombea nchi hizo amani hasa ya Nchi ya Kenya na Tanzania.

 Akiongea na chanzo kimoja cha habari jana mratibu wa kongamano hilo ambalo limeandaliwa na mtandao wa wachungaji mkoa wa Arusha,alisema kuwa kongamano hilo lina manufaa makubwa sana kwa Nchi hizo

 Ayo alisema kuwa amani ya nchi inatakiwa ipite hata kwa viongozi wa dini kwa kuwa wao wana nafasin kubwa sana ya kuweza kuhubiri amani tofauti na viongozi wengine wowote hivyo basi mtandao huo umechukua nafasi hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa nchi hizo zinakuwa na amani

 Alisema kuwa wachungaji hao zaidi ya 400 ambao wamekutana Jijini Arusha wameweza kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hata jinsi ya kulinda amani ambayo baadhi ya Nchi imepotea kwa sababu mbalimbali hivyo kupitia kwa waumini wao wataweza kuwafanya wananchi walinde amani

 “Tumekutana hapa kuhakikisha kuwa tunajadili mambo mbalimbali ya msingi lakini pia kuhakikisha kuwa kila Kiongozi anakuwa balozi wa kulinda amani na wala sio kwenye serikali kwani sisi Viongozi wa dini tuna nafasi kubwa sana ya kutekeleza suala hilo ambalo wakati mwingine tunaachia Serikali pekee’aliongeza Ayo

 Mbali na hayo aliwataka Viongozi wa dini kuhakikisha kuwa wanajiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa mbali na kuomba amani kwa nchi husika lakini watumie nafasi mbalimbali ambazo wanazo kwa kuwataka waumini wao waweze kufanya kazi kwa bidii na kisha kupambana na Umaskini

 Alifafanua kuwa kama Viongozi wa dini wataweza kufanya hivyo basi wataweza kuondoa Mataifa ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki hususan Tanzania kutoka katika  hali ya umaskini ambayo ipo na kufika katika viwango vya hali ya juu ambapo hata hali ya ugumu wa maisha wakati mwingine inachangia sana uharibifu wa amani, pamoja na umaskini.

 “Kwa sasa kuna changamoto kubwa sana za masuala ya kimaisha lakini viongozi wa dini wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kusisisitiza watu wahakikishe kuwa wanafanya kazi na waache kukaa kaaa ovyo mitaani na pindi wanapokaa mitaani ndipo wanapofanya na kuwaza hata mbinu za kuharibu amani’aliongeza Ayo

Source: fullshangweblog.com

Pata Kutiwa Moyo na Ushuhuda wa Neema alivyoponywa UKIMWI


Tunampa Mungu utukufu wote kwa Ushuhuda wa uponyaji wa UKIMWI jinsi alivyodhihirisha nguvu za uponyaji wake, pia kutuwezesha kushuhudia zaidi ya watu 50 wakiponywa UKIMWI katika huduma yetu. Nina imani kwamba shuhuda hizi zitaweza kusaidia kuinua imani, ya wale wanaomwamini Mungu kwa ajili ya uponyaji wa magonjwa yasiyo na tiba kama UKIMWI na kutoa changamoto kwa watumishi wa Mungu kuwasaidia wagonjwa kupokea uponyaji wao kwa kuhubiri Neno la imani na uponyaji.

Neema aliponywa na ugonjwa ambao kwa madaktari hauna dawa wala tiba yaani UKIMWI Agosti 2012 kwa msaada wa mafundisho ya uponyaji aliyoyapata kwa Mchungaji Prosper Ntepa mwaka 2006 hadi 2008 baada ya kuishi na virusi vya UKIMWI kwa takribani miaka sita. Wakati watu wengi wamekata tamaa kwa sababu ya taarifa ya madaktari inayosema UKIMWI hauna dawa wala tiba kuna dawa imegunduliwa katika maabara za kiroho na kitabu kinachoitwa Biblia ambayo inaanza kumponya mgonjwa kuanzia katika mizizi ya roho yake na kufisha vidudu vya UKIMWI. Mafundisho ya ugunduzi wa dawa hii kiboko yameonekana kuleta matokeo katika huduma ya mchungaji Prosper Ntepa, ambapo kuna taarifa zinazosema watu zaidi 50 wameponywa UKIMWI kwa uthibitisho wa madaktari. Dada Neema ni mojawapo wa watu waliopata neema ya kuponywa kwa njia ya imani katika dawa ya Neno la Mungu ambayo imethibitika kuleta matokeo ya ajabu kwa wale wanaoiamini na kuimeza kwa umakini na kufuata masharti yake. 

Mchungaji Prosper Ntepa wa The Oasis of Healing Ministries
Ni muhimu kukumbuka kwamba kuwa na UKIMWI siyo tatizo bali ni mtazamo unaokuwa nao juu ya UKIMWI ndio tatizo kubwa kuliko UKIMWI wenyewe. Kwa maneno mengine, kuwa na tatizo sio tatizo bali ni mtazamo unaokuwa nao juu ya tatizo ndio tatizo kubwa kuliko tatizo lenyewe. Mmoja ya watu waliokuwa wakimwamini Mungu kwa ajili ya uponyaj aliwahi kusema kwamba, “Watu wengi walioathirika na UKIMWI wameathirika katika ufahamu na mawazo yao.” Jambo hili nimeliona kuwa kweli katika uzoefu wa kufanya ushauri kwa mamia ya watu walioathirika na UKIMWI. Ufahamu au mawazo yanaathirika kwa sababu ya ripoti inayosema UKIMWI hauna dawa wala tiba. Kwa hiyo mtu akipata ugonjwa huu anaathirika katika ufahamu na mawazo yake kiasi kwamba mtazamo wake unakuwa ni hasi au mtazamo mbaya. Katika akili mtu huyu anajaa mawazo yanayoamini katika hali ya kutokuwezekana au hali ya kutokuamini.
Sauti ya mawazo ya kutokuamini inaanza kumpa taarifa mtu kwamba hana haja ya kumwamini Mungu kwa ajili ya uponyaji au muujiza wake. Hatimaye anatawaliwa na mawazo ya kufa zaidi kuliko kupona na kuishi.

Dada Neema alizaliwa Itigi akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto wawili. Baba na mama ni Waislamu. Alioana na mume wake wa sasa Novemba 2003. Wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kike anayeitwa Abighail katika ndoa yao ambaye alizaliwa tarehe 27 Mei 2009.  Abighail alizaliwa wakati mama yake akiwa ameathirika na UKIMWI. Wakati wanaoana hawakupima afya kwa habari ya UKIMWI.
  
 Je, uliambukizwaje virusi vya UKIMWI?
 Ninashindwa kuelewa jinsi nilivyopata maambukizo ya UKIMWI. Niliwahi kuolewa na kuachika kabla ya kukutana na mume wangu wa sasa. Mume wangu wa sasa alifiwa na mke wake kwanza. Tumeshindwa kujua kwamba tatizo la maambukizo lilitoka kwangu au kwa mume wangu. Taarifa nilizozipata ni kwamba mke wa kwanza wa mume wangu alifariki Machi 2003 kwa ugonjwa wa maralia na kuchanganyikiwa. Tatizo ni kwamba hatukupima afya zetu wakati tunaingia katika ndoa.

Je ulijuaje kama umeathirika na virusi vya UKIMWI?
 Mwishoni mwa 2006 nilipima katika hospitali ya Amana na kukutwa na virusi vya UKIMWI. Baadaye nikapima tena sehemu nyingine mbili ambako walithibitisha pia kwamba nimeathirika na UKIMWI. Vile vile mume wangu alipimwa na kukutwa kwamba alikuwa naye ana virusi vya UKIMWI.   
Je, ulikuwa na dalili gani za magonjwa nyemelezi?
 Nilikuwa na dalili nyingi za magonjwa nyemelezi ya UKIMWI. Dalili hizi ni pamoja na homa za mara kwa mara, malaria, kuwashwa sehemu za siri na kuvimba mwili. Pamoja na mwili wangu kubadilika rangi ya weupe na kuwa mweusi kama mkaa nikajikuta nikawa na vidonda mdomoni kiasi cha kuanza kutoa harufu. Kuna wakati ambao niliumwa sana na kusababisha kupungukiwa na damu kiasi cha kufikia tatu nukta nne. Pia nikapata mkanda wa jeshi kwa muda wa miezi mitatu ambao ulinitesa sana.

Uliokoka lini?
Nilikuwa mwislamu kwa  sababu baba na mama ni waislamu. Nilikuwa nina tabia ya kupenda kusikiliza kanda za nyimbo za Kikristo. Niliokoka Julai 2003 kupitia vipindi vya Neno la Mungu kupitia redio za Kikristo za hapa Dar es Salaam. Baada ya kuokoka nilisali makanisa mbalimbali ya Kipentekoste. Kuna wakati nilianza kusali katika kanisa la Full Gospel Bible Fellowship la Mwenge, ambako sikukaa zaidi ya mwezi mmoja. Baada ya kuokoka nilibatizwa kwa maji mengi katika kanisa la Askofu Sylvester Gamanywa. Mume wangu aliponywa ugonjwa sugu wa fangasi iliyomsumbua kwa miaka takribani miaka kumi na nne. Baadaye mimi na mume wangu tulihamia katika kanisa la The Oasis of Healing Ministries, baada ya kusikia mafundisho kupitia Praise Power Radio. Tulijiunga na huduma hii kuanzia mwishoni mwa 2006. Tulipokuja katika ukumbi wa Mhasibu house tulisikia ushuhuda wa dada Hellen ambaye aliponywa UKIMWI katika wiki ya kwanza aliyokuja katika maombezi wakati ni mjamzito kabla ya kuolewa. Tulisikia shuhuda za watu wengine ambao pia walikuwa wameponywa UKIMWI katika huduma ya mchungaji Prosper Ntepa. Matokeo yake tulitiwa moyo sana.


Je, ulipima mara ngapi kuthibitisha kwamba una virusi vya UKIMWI? 
Nilipima mara tatu kuthibitisha kwamba nina maambukizo ya UKIMWI. Mara ya tatu nilipima katika kituo katika afya kilichoko Mbagala.

Je, uliponywaje ugonjwa wa UKIMWI? Ni vitu gani vilikusaidia kupokea uponyaji wa UKIMWI?
 Nilikuwa mshirika katika kanisa The Oasis of Healing Ministries kuanzia mwishoni mwaka 2006 mpaka mwishoni mwa 2008. Baada ya hapo tukawa tumehamia Sanya Juu, Kilimanjaro. Kuna mchungaji mmoja ambaye alikuja kufungua kanisa Sanya Juu tukaongozwa kushirikiana naye katika kazi ya Mungu. Kama shukrani kwa Mungu kwa yale ambayo Mungu alitufanyia mume wangu aliamua kutoa sehemu ya kiwanja chake cha urithi kwa ajili ya kujenga kanisa pale Sanya Juu. Nilipata uja uzito mwishoni 2008. Tulipata mtoto wa kike ambaye tulimpa jina la Abighail ambaye alizaliwa kabla ya muda wake tarehe 27 Mei 2009 akiwa na miezi saba. Mwaka 2008 nikiwa na mimba nilipimwa damu na kugundulika kuwa bado nilikuwa ninaishi na virusi vya UKIMWI. Lakini bado sikukata tamaa katika imani. Niliendelea kumwamini Mungu na Neno lake bila kutetereka. Hatimaye uponyaji wangu ulikuja kuthibitika Agosti 2012 baada ya kuvumilia na kusimama katika Neno la Mungu kwa takribani miaka mitano na nusu. Uponyaji wangu ulikuja kugundulika wakati nilipoumwa sana malaria nikalazimika kulazwa katika hospitali ya Kibongoto. Madaktari wakanishauri nilipokuwa ninatibiwa malaria nipime pia damu kuangalia kama bado nina UKIMWI. Baada ya madaktari kunipima damu wakashangaa kugundua kuwa nilikuwa sina maambikizo ya UKIMWI. Jambo hili liliwapa mshangao mkubwa kwa sababu walikuwa wamewahi kunipima na kunikuta na maambukizo ya UKIMWI. Huko nyuma wakati nilipokuwa na dalili nyemelezi za UKIMWI madaktari walikuwa wamenipima mara kadha na kunikuta nina virusi vya UKIMWI. Kwa maneno mengine, baadhi ya madaktari walikuwa wanajua kwamba nilikuwa nimeathirika na virusi vya UKIMWI. Madaktari hao walishangaa sana kunikuta nikiwa na majibu tofauti na matarajio yao ya awali. Wakaanza kunihoji maswali kwamba imekuwaje hali yangu imebadilika ghafla hivi na kutokuwa na virusi vya UKIMWI. Nikawajibu kwamba Bwana Yesu ameniponya na UKIMWI. Nikawapa ushuhuda jinsi nilivyoishi katika imani ya kulitegemea Neno la Mungu. Nikawasimulia jinsi nilivyokuwa ninakiri au kutamka  mistari ya uponyaji mara kwa mara. Nikawashauri kwamba kama wana mashaka na jambo hili basi wawasiliane na Mchungaji Prosper Ntepa kanisa la The Oasis of Healing Ministries, Ubungo ili wapate ushahidi zaidi wa uponyaji wa UKIMWI.

Matokeo yake madaktari wale wakarudi tena kunipima kipimo cha CD4 yaani kiwango cha kinga yangu. Baada ya kunipima walishtuka kugundua kuwa CD4 au kiwango cha kinga za mwili wangu zikiwa zimeongezeka sana yaani kiwango cha mtu ambaye hana virusi vya UKIMWI. Kiwango cha kinga zangu zilipanda sana tofauti na kiwango cha awali wakati nikiwa ninaishi na virusi vya UKIMWI. Pia waliporudia kunipima kipimo cha kubainisha kama nimeathirika na UKIMWI au sina maambukizo ya UKIMWI. Wakapima tena damu na kukuta sina maambukizo ya UKIMWI yaani HIV negative. Kwa hiyo madaktari walinipima mara tatu yaani vipimo viwili vilivyoonyesha sina UKIMWI au HIV Negative na kipimo kingine cha kupima CD4.
 
Magonjwa nyemelezi yalipungua baada ya kujifungua mtoto wangu Abighail kuanzia 2009. Niliacha kutumia dawa za kurefusha maisha kuanzia Juni 2009. Badala yake nilikuwa ninatumia dawa ya Neno la Mungu yaani kuzitamka ahadi na kweli za uponyaji. Nilisimama katika ahadi na kweli za uponyaji mbalimbali ambazo zilinisaidia kuniimarisha kiimani. Baadhi ya mistari niliyokuwa ninaisimamia kwa njia ya kuikiri na kuitamka ni hii ifuatayo: Niliamini kwamba Mungu analitumia Neno kama dawa ya kuniponya mimi. Zaburi 107:20, “Hulituma neno lake, huwaponya, huwatoa katika maangamizo yao.” 1 Petro 2:24, “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” Nilikuwa nanakiri kwamba kwa kupigwa Yesu nimepona na niko huru na UKIMWI.

Mathayo 8:17, “Ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.” Katika Mathayo 8:17 nilikuwa ninakiri kwamba Yesu alitwaa udhaifu wangu na kuyachukua magonjwa yangu. Kutoka 15:26, “Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.”
Yohana 10:10, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Nilimtambua Ibilisi kama mwizi wa afya yangu lakini Yesu alikuja ili niwe na uzima na niwe nao tele. Nilianza kuamini katika hali ya kutokufa kabla ya wakati wangu. Ayubu 5:26 ilinitia moyo, “Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.”

 Katika mchakato huu wa kulipanda Neno la Mungu kama dawa kwa ajili ya uponyaji nilifikia hatua ya kukariri mistari mingi. Mimi na mume wangu tuligundua kwamba Neno likiwa katika Biblia ni Andiko lakini linapokuwa ndani ya roho yako linakuwa Neno lililo hai. Biblia inasema katika 2 Wakorintho 3:6, “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.” (Kwa maneno mengine, walitofautisha logos yaani Neno la Mungu la jumla lisemwalo na rhema yaani Neno la Mungu maalum au la ufunuo linasema kitu sasa. Watu wengine wanashindwa kujenga imani ya uponyaji pamoja na ukweli kwamba wanalijua Neno kwa akili zao lakini hajafikia hatua ya kuwa na Neno lililofunuliwa katika roho zao)


Unamshauri nini mtu anayemwamini Mungu kwa ajili ya uponyaji wa UKIMWI na unaonekana kuchelewa?
Ningependa kushauri mambo matatu yafuatayo. Kwanza, ninashauri wazingatie kumkubali na kumwishia Mungu. Pili, ninawashauri walikubali na kulitafuta Neno kwa bidii. Tatu, ninashauri wasikate tamaa katika kumwamini Mungu. Waendelee kukiri mistari ya uponyaji hadi uponyaji wao utakapodhihirika. Nina imani wataweza kupona kama mimi nilivyopona.


  Je, ulikutana na hali zozote za kukatisha tamaa?

Ni kweli nilikutana na hali za kukatisha tamaa katika mchakato wa kufikia kupokea uponyaji wangu. Halikuwa jambo rahisi kuendelea kumwamini Mungu. Sikuwa na roho ya kuogopa kufa. Nilikuwa ninasikia sauti ndani yangu inayosema, “Unasimama katika Neno la Mungu lakini hakuna mabadiliko yoyote katika mwili wako. Unaomba kila siku hupati uponyaji wako. Wewe utaishia kufa tu. Huwezi kupona UKIMWI.” Nikawa ninakataa kukubaliana na maneno haya kutoka kwa adui shetani. Nilikuwa ninaipinga sauti hiyo kwa jina la Yesu.



Kwa upande mwingine nilikuwa ninasikia sauti inayosema “Umekwisha kupona UKIMWI. Wewe ni mzima.” Sauti ya adui ilikuwa inanihubiri kwamba nitakufa wakati sauti ya Mungu ilikuwa inanithibitishia kuhusu kupona. Nikaamua kuifuata sauti chanya iliyosema kwamba nimepona. Mwishowe nikaanza kujiona na kukubaliana juu ya uponyaji wangu. Nikaanza kumshukuru Mungu kwa ajili ya uponyaji wangu. Nikawa ninasema, “Asante Yesu Kristo kwa kuniponya UKIMWI. Asante Yesu Kristo kwa sababu wewe ni mponyaji wangu.” Kwa maneno mengine niliacha kukazana kuomba dua za Mungu kuniponya UKIMWI na kuanza kumshukuru Mungu kwa ajili ya uponyaji wangu kana kwamba tayari ulikuwa umefanyika halisi. 


Je, kuna mtu yeyote aliyeponywa UKIMWI ambaye alikutia moyo katika kumwamini Mungu?
Michael aliyeponywa na UKIMWI 2006 baada ya kuishi na UKIMWI kwa miaka mitano alitutia sana moyo mimi na mume wangu. Niliposikia ushuhuda wa kuponywa kwake virusi vya UKIMWI nilifarijika sana kwamba kwa Mungu hakuna ugonjwa usioweza kutibika. Kuna wakati Michael alikuja nyumbani kumwona mume wangu wakati anaumwa.

 Una washauri nini watu wanaotaka kupokea uponyaji wa UKIMWI?
 Ninataka kushauri mambo manne yafuatayo: Kwanza, ninawashauri wanaotaka kupokea uponyaji wa UKIMWI waishi maisha matakatifu. Kuishi katika dhambi kama za uzinzi kunaweza kumzuia mtu kupokea uponyaji wake. Pili, usiwe na shauku kwamba ukipona ugonjwa wa UKIMWI utajitoa kufanya maovu. Ninashauri mtu atengeneze shauku ya kumtumikia na kumwishia Mungu. Tatu, ninashauri mtu anayetaka kuponywa UKIMWI akatae kuathirika kwa ufahamu au mawazo yake. Unaweza kuathirika na UKIMWI lakini ukakataa kuathirika kimawazo kwa njia ya kuwa mtazamo chanya. Mungu anaweza kufanya njia pasipo na njia. Asikubali sauti ya milango mitano ya maarifa inayotumia kuona, kusikia, kuonja, kugusa na kushika. Ni jambo la muhimu kuipinga sauti ya shetani inayowasiliana katika mawazo yako. Nne, ni muhimu kujifunza kunukuu na kukiri Neno linavyosema katika hali ya ugonjwa wako kwa kulitamka. Nina ushahidi wa Neno la Mungu linavyosema. Yeremia 33:6, “Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.”

Je, kuna mtu yeyote ambaye ameponywa UKIMWI kwa msaada wako?
Tulipokuwa Sanya Juu, Kilimanjaro mume wangu alianza kufundisha Neno la Mungu katika kanisa moja na kufanya huduma ya kuombea wagonjwa. Watu walianza kuja kuombewa magonjwa mbalimbali na wakawa wanapona. Mimi na mume wangu tulimsaidia mama mmoja ambaye yeye na mume wake walikuwa wameathirika na UKIMWI. Huyu mama alianza kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu, ambayo mume wangu alikuwa anafundisha. Ilikuwa ni Oktoba 2012. Tulimfundisha kukiri mistari ya uponyaji ambayo tulijifunza kwa Mchungaji Prosper Ntepa. Huyu mama alikuwa amepima mara nne kwamba ana virusi vya UKIMWI. Wakampima na kukuta hana virusi vya UKIMWI. Mama huyu aliambiwa arudi tena Januari 2013 baada ya miezi mitatu.  

Aflewo Tanzania 2013 Bishop Breakfast yafana


Katika Kuelekea Event ya Aflewo Tanzania 2013,Siku ya jana ilikuwa Bishops Breakfast Forum katika Hotel ya Regency Park Mikocheni,ikiwa ni katika kuwashirikisha Maaskofu na Mtume wa huduma mbalimbali maono na maana ya kuwepo kwa Aflewo Tanzania mwaka 2013.

Mnamo terehe 5-5-2013 BCIC Mbezi Beach itakuwa ni usiku wa aina yake katika Kumsifu na Kumwabudu Mungu ambapo Aflewo Mass Choir yenye waimbaji zaidi ya 90 watapaza sauti zao wakiimba sifa kwa Mungu.

Katika Bishops Breakfast hiyo iliyoudhuliwa na baadhi ya Maaskofu kama Apostle Ntepa,Bishop Fredie Kyara, Bishop Elly Mwende,Bishop Simtovu,Bishop Mwasota, Bishop Shegga, Pastor Fredie (UpperRoom Minisry )Bishop Gamanywa alitoa hudhuru kwa Kuwalilishwa na Pastor Amoni Kalahilo na wengine wengi na kusifu Aflewo kuweza kuwa kutanisha na wao kama Maaskofu katika Jiji la Dar es salaam kuwashirikisha Maono ya Aflweo Tanzania na kusifu juhudi zinafanywa maana ni katika Kuujenga mwili wa Kristo na kulileta pamoja Kanisa la Tanzania na Afrika Kwa Ujumla.

Pastor Paul Safari na Abel Orgenes Kama walezi wa huduma ya Aflewo Tanzania,wakieleza umuhimu wa huduma hiyo kwa waimbaji ni pamoja na kukua kwa maisha ya kiroho kati ya waimbaji na Mungu maana tofauti na uimbaji pia kuna mafundisho kuhusu Maisha ya wokovu na Maana ya Kufisu na Kuabudu kwa ujumla

Pastor Fredie Kyara aliweza kutoa ushuhuda wa jinsi Mkesha huo ulivyo wa baraka sana kwa kusema jinsi ilivyoweza kukutana na uwepo wa Mungu kwa Mkesha uliopita mwaka 2012,na kusihi Maaskofu wengine kukubali na kuunga mkono huduma hii ya Aflewo kwa kuwa ruhusu waumini wao makanisani kuhusika kikamilifu.

Kwa kumalizia Maaskofu hao walipata nafasi ya kuchangia na kusema kuwa wanakubaliana kwa nia moja na kusema wako tayari kushiriki kwa namna moja au nyingine kuhakikisha mkesha wa Aflewo Tanzania 2013 unafanikiwa.
Pastor  Pastor Paul Safari mmoja wa mlezi wa huduma ya Aflewo akizunghumza mbele ya akizungumza na Maaskofu.
Mlezi wa huduma ya Aflewo Pastor  Abel Orgenes
Maaskofu wa huduma mbalimbali Jijini Dar es salaam Katika Bishop Breakfast,iliyoandaliwa na  Aflewo Tanzania 2013 siku ya jana, Maaskofu hao walipata kushirikishwa maono na maana ya huduma ya AFLEWO Tanzania,na jinsi Aflewo Tanzania mwaka 2013 itavyofanyika.Pia walipata kuzungumza kwa namna wao watakavyoweza kuhusika katika kufanikisha Aflewo Tanzania 2013
Bishop Elly Mwende kutoka makanisa ya PAG Dar es salam akitoa mchango wake katika Breakfast
wakwanza kulia ni Aflewo Music Director Samweli Mwangati,akifuatiwa na Bishop Mwasota,Aflewo Event Manager Mc Antony Luvanda na Mwenyekeiti wa Aflewo Tanzania Geofrey Obiro akizungumza na Maaskofu.
Ndani ya ukumbi kama unavyoonekana Mwenyekeiti wa Aflewo Tanzania kwa mbali Geofrey Obiro akizungumza na Maaskofu.
Maaskofu wakijadiliana mara baada ya kumalizika wa Breakfast kwa mbali Bishop Shegga akizungumza na Maaskofu wenzake kwa kubadilishana mawazo.