Kundi kubwa la Maaskofu waliokutana jijini Dar es Salaam, kujadili madhala yanayoikabili Tanzania, wamejikuta wakimwaga machozi hadharani baada ya kuguswa na wosia wa Rais wa kwanza na mwasisi wa Tanzania, hayati Julius Kambarage Nyerere.
Nyuso za maaskofu hao kutoka ndani na nje ya Tanzania, zilianza kubadilika baada ya watoto wa shule ya msingi Muhimbili ya jijini Dar es Salaam, kuimba wimbo wa kuililia ardhi ya Tanzania, uliokuwa na hisia kali.
Hata viongozi wa kitaifa waliohudhuria mkutano huo usio wa kawaida walishindwa kustahimili ambapo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Dk. Benjamini William Mkapa, alionekana kuinamisha kichwa chini na kufikicha macho yake kama ishara ya kilio cha mtu mzima.
Katika mkutano huo wa aina yake uliofanyika katikati ya Jiji la Dar es Salaam, mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kayanza Peter Pinda (mtoto wa mkulima).
Kabla ya Waziri Pinda kuzungumza chochote na kufungua Mkutano huo rasmi, kikundi mahili cha kwaya ya watoto kutoka Shule ya Msingi Muhimbili, kiliimba wimbo uliowafanya viongozi waliokuwepo kuinamisha vichwa vyao huku wengine wakitokwa na machozi.
Miongoni mwa viongozi wa Serikali waliohudhuria mkutano huo ni Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mh. Dk. Benjamin Wiliam Mkapa, ambaye aliinamisha kichwa chake kwa huzuni kutokana na kuguswa na ujumbe wa wimbo wa watoto hao.
Watoto hao waliimba wimbo wa kuuliza viongozi wa Serikali sababu za kuuza ardhi ya watanzania kwa wageni, pia katika wimbo wao walihoji kama Rais Nyerere angeuza ardhi, wao wangeishi wapi, walihoji pia au lengo lao ni kutaka kulirudisha taifa utumwani.
Kiukweli sitanii, wimbo huo wenye hisia uliwatoa machozi si Maaskofu tu bali hata viongozi wa Serikali ikiwa ni pamoja na viongozi wa mashirika mbalimbali waliohudhuria mkutano huo kutokana na ujumbe mzito uliowasilishwa mbele yao kupitia uimbaji wa kwaya hiyo ya watoto wadogo wa shule hiyo ya msingi.
Kisha Waziri Mkuu wa Tanzania Mh.Pinda akasimama kuzungumza na mamia ya Maaskofu na washiriki wa mkutano huo na hatimaye kufungua rasmi shughuli hiyo kuanza.Katika hotuba yake Waziri huyo ambaye tayari alikwisha pokea ujumbe mzito kupitia uimbaji wa watoto hao, akaanza kwa kuwashukuru watumishi hao wa Mungu kukutanika ili kujadili masuala ya ardhi ya nchi yetu.
Mhe.Pinda akakiri taifa la Tanzania kukabiliwa na changamoto mbalimbali za ardhi ambazo kwa namna moja au nyingine zimegharimu maisha ya watanzania wasio na hatia kwa kutetea haki yao, na kuongeza kuwa ni changamoto kubwa kwa nchi.
Pamoja na hilo, akasema, Serikali ya Tanzania inaithamini ardhi ya watanzania na kusema ndiyo chanzo cha uchumi wa taifa na muhimili wa wananchi walio wengi.Waziri Pinda akafunguka kuwa, Serikali itawashughulikia viongozi walio na tabia ya kujimilikisha ardhi na kuiuza kwa wageni kutoka mataifa ya nje huku wazawa wakibaki kama wakimbizi katika nchi yao wenyewe, akasema hilo halitakubalika.
Akizungumzia suala la uwekezaji nchini, alisema wananchi wanaruhusiwa kuwekeza katika ardhi yao, na kwamba hata wageni kutoka mataifa ya nje lakini kwa vibali maalum ili wazawa wanufaike na uwekezaji wao na siyo kuitumia nchi kwa manufaa ya mataifa yao pekee.
Pinda hakusita kuzungumzia mgogoro wa wakulima na wafugaji, wananchi na migodi akasema suala hilo bado linaipasua kichwa Serikali na kusema linatafutiwa ufumbuzi na kwamba litakomeshwa kabisa, ili watanzania wasizidi kupoteza maisha kwa ajili ya ardhi yao.
Kisha mtumishi huyo wa Serikali ya JK, akawataka viongozi na watumishi wa Umma wasiitumie ardhi kama sehemu yao ya kujipatia kipato kwa manufaa yao wenyewe, bali wawe mstari wa mbele kupinga unyang’anywaji wa ardhi kwa wananchi.Baada ya nasaha hizo, Waziri Pinda, maarufu kama mtoto wa mkulima, alifungua rasmi mkutano huo wa siku tatu na kusema ufanyike kwa amani na salama.
Chanzo cha habari kilizungumza na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, likitaka kujua juu ya uuzwaji wa ardhi ya wananchi kiholela kwa wageni kutoka mataifa ya nje.
Waziri Tibaijuka alikana kuuzwa kwa ardhi ambapo alisema hii nchi ni ya watanzania hivyo ardhi iliyopo ni kwa ajili yao na siyo ya wageni, lakini akakiri kuwepo kwa wawekezaji na kusema Serikali itaendelea kuilinda na kuithamini kwani ni kama zawadi kutoka kwa Mungu.
Naye Askofu Stiven Munga kutoka Dayosisi ya Kaskazini-Mashariki Tanga, akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa, kitu pekee cha kuyabadili maisha ya mtanzania na kuondokana na umaskini, hususan kwa mtu wa kipato cha chini, ni ardhi.
Hivyo akawataka watanzania na Serikali kwa ujumla kuitunza ardhi ya Tanzania kwa manufaa ya taifa na kwa ajili ya vizazi vijavyo, huku akitaka wawekezaji kuwekeza kwa wingi ili nchi iondokane na baa la umaskini.“Ardhi ndiyo kila kitu, kwa maisha ya mtanzania, maana inaweza kuyabadilisha maisha ya watanzania hata wenye kipato cha chini, lakini ni vyema tukawapa nafasi wawekezaji pia, ili nchi ijinusuru na umaskini,” alisema Askofu Munga.
Mtumishi huyo wa Mungu alimaliza kutoa nasaha zake kwa kusema “Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania” kama ishara ya kumuachia Bwana ashughulike na nchi hii na Afrika kwa ujumla.