Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), limemfukuza kazi mmoja wa wainjilisti wake katika mission ya Rukwa, kwa madai ya kupotosha waumini wake, huku mwenyewe akishikilia msimamo kuwa anakinywea kikombe alichonyweshewa Martin Luther, na atashikilia msimamo huo hadi pumzi yake ya mwisho hapa duniani.
Mwinjilisti huyo, Goodlove Kyenda, amesisitiza kuwa hatahama wala kuanzisha kanisa lake, bali atashikilia msimamo wake wa kupinga fundisho jipya lililopo katika kitabu kipya cha Mwongozo wa ibada kilichotolewa mapema mwaka huu, kiitwacho “Tumwabudu Bwana” kilichochukua nafasi ya kile cha zamani kiitwacho, “Mwimbieni Bwana.”
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na mchungaji wa KKKT, Usharika wa Rukwa, Zebedayo Mbilinyi, mwinjilisiti Kyenda aliamuriwa kuondoka mara moja na kikao cha Kamati Tendaji ya Misioni ya Rukwa iliyoketi kujadili shauri hilo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo iliiagiza Halmshauri ya usharika wa Luther kuwa Kyenda aondoke ndani ya siku tatu (saa 72) katika nyumba aliyokuwa akiishi ambayo ni mali ya kanisa.
Akielezea mkasa huo, mwinjilisti huyo alisema kuwa haogopi hali iliyomkuta kwa kuwa anatetea kweli na lengo lake ni kuponya kanisa kama alivyofanya Martin Luther alipopinga baadhi ya mafundisho ya kanisa katoliki akiibuka na hoja 95 zilizodhihirisha mapungufu makubwa.
Akifafanua alisema kuwa katika kitabu hicho kipya kilichotolewa mwaka huu, katika ukurasa wa 607, kuna mafundisho ya kuwaenzi watu waliokufa, yaani Mungu amhamishe kutoka alipo (pugatolio) jambo ambalo ni kinyume na Neno la Mungu.
Mwinjilisti huyo amekumbana na mkasa huo ikiwa ni mwaka mmoja tu, tangu apewe barua ya ajira, katika utumishi ndani ya kanisa lenye jumla ya waumini 400.
Alisema sakata lilikuwa hivi: “Oktoba 28, 2012 ilikuwa ni siku ya Matengenezo kama ratiba ya kitabu cha “Tumwabudu Bwana” Kilichohakikiwa na wasomi nchini Ujerumani kikiwa na nyongeza ya vipengele tata; kinavyoonesha, na mimi ndiye niliyeongoza ibada.”
Kisha aliongeza: “Nilifundisha, lakini ilipofika kipengele cha kuwaenzi wafu kama kitabu kinavyoonesha niliweka sawa fundisho hilo kama linavyoelezwa kwenye Biblia kitabu cha Mhubiri 9:4-6 kwamba hakuna namna yoyote unayoweza kumuombea mtu aliyekufa akapata rehema, niliwaambia hatma ya maisha ya kila mmoja inategemea maisha yake aliyoishi duniani.”
Mwinjilisti huyo alikiambia chanzo cha blog hii kuwa, baada ya hapo vilianza vikao vya uongozi wa misheni hiyo kimyakimya huku yeye akishiriki kikao kimoja, na kwamba ndani ya vikao hivyo kulikuwa na makundi mawili; ya wanaomuunga mkono elimu aliyowapa na wanaopinga.
Kiongozi wa kanisa alilofukuzwa mwinjilisti Kyenda, Mchungaji Mbilinyi, akiongea na chanzo cha habari hii alisema kuwa mwinjilisti huyo alikiuka mwongozo wa taratibu za ibada kwa kufundisha mafundisho yanayopingana na imani ya KKKT.
Alisema mwongozo wa ibada zote uko kwenye kitabu cha Tumwabudu Mungu ambacho kimeandikwa na wasomi na wanatheologia wabobevu wa kanisa hilo duniani, ambacho mhubiri anapaswa kukifuata na kwamba mwinjilisti alikwenda mbali zaidi ya kile kilichomo kwenye mwongozo huo.
“Ikiwa ataomba msamaha kwenye Halmashauri, kanisa linaweza kumsikiliza, la! Hajafanya hivyo, basi hatokuwa na sehemu ya uongozi wa kanisa,” alisema.
Hata hivyo, chanzo cha habari hii kilienda mbali zaidi na kutaka ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa KKKT, hususan kipengele hicho ambacho kimebainishwa kuwa kinaleta msuguano wa chini kwa chini hivyo kutengeneza makundi mawili.
Chanzo cha habari hii Kiliongea na Katibu wa kanisa hilo ambaye alisema: “Mimi niko safarini Bukoba, siwezi kusema chochote, subirini hadi nitakaporudi, nimekuelewa sana! Ila siwezi kujibu chochote.”
Hatukuishia hapo, tuliongea na Mkuu wa Dayosisi ya Arusha, mchungaji Godwin Lekashu, naye alikuwa na haya ya kusema: “Siko ofisini, nipo mahali pagumu, nitakupigia baada ya dakika ishirini.”
chanzo cha habari hii kilisubiri dakika hizo 20, lakini hakupiga kama alivyosema, na zilipokatika dakika 30 lilimpigia tena, lakini mtumishi huyo hakuweza kupokea simu baadala yake simu ya mkuu huyo ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
Sakata hilo limesababisha baadhi ya wazee wa kanisa usharikani hapo kupita nyumba kwa nyumba kwa baadhi ya wazee wa mitaa wa kanisa kulinusuru na mpasuko uliopelekea kutokea makundi mawili ya Mchungaji wa kanisa hilo na Mwinjilisti.
No comments:
Post a Comment