Namba 666 yazua hofu kubwa Jijini Nairobi

Baadhi ya viongozi wa Kikristo nchini Kenya, wameonya kuwa vijana wa taifa hilo wako hatarini kufuatia kuanzishwa rasmi kwa kanisa la Shetani mjini Nairobi, linalojitangaza kwa njia mbalimbali kuwaalika waumini wakamtumikie Ibilisi, huku likitoa nambari zake za simu ambazo zinashabihiana na namba ya mpinga Kristo iliyotajwa katika Biblia kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura ya 13.

Askofu wa Kanisa la Pentecoste mjini Nairobi, Joseph Wairuri, alionya kuwa  ikiwa kanisa la kweli la Kristo halitasimama imara kuwaelimisha waumini wake, kuwaombea  na kumlilia Mungu; vijana wataishia humo kutokana na ahadi nono za kupata utajiri na umaarufu.

Katika tangazo la kanisa hilo, ambalo chanzo cha habari hii kimeliona, Kuhani wa kanisa la shetani Hekalu la Nairobi,  Khan Mohamed Kahan, alisema  hekalu lao ni huru na watu wote wanaruhusiwa kuhudhuria ibada, lakini sharti moja kubwa ni kutotaja jina la Yesu, wala kumtukuza Mungu mmoja.

Akinukuliwa na Gazeti la Standard, kuhani huyo alisema kuwa ndani ya ibada zao jambo baya na lisiloruhusiwa ni kutaja jina la Yesu, na wanawajali na kuwapongeza wageni wanaohudhuria ibada hiyo.

“Kwenye kanisa letu dhambi siyo mambo binafsi kama vile; kufanya uzinzi au uasherati, kutembea na mke wa mwenzio na mengineyo.

Hekalu au kanisa halina shida na mtu kuwa na mahusiano ya kingono na mwenzake, bora tu wakubaliane. Hatufuatilii mambo ya kipuuzi ya kufuatiliana. Waumini wetu wanaamini katika uchawi na ushirikina na siyo ibada. Hatuamini katika kumuabudu mwingine. Ingawa kwa sababu maalum wanajichanganya na wale wanaodai kuwa waabudu Mungu,” alisema na kuongeza:
 “Tunawakaribisha wote wanaokabiliana na changamoto nyingi hapa Kenya, waje kwetu kwa kuwa sisi tuna fursa za aina yake na tumetumwa kuwaokoa. Wamedanganywa sana na mwisho wanapaswa kuona tulivyo na suluhisho.”

Baadhi ya wale walioitikia wito wa kujiunga na shetani wanaeleza kuwa wametakiwa kulipa kiasi cha shilingi 4000 za Kenya na bado wanatakiwa kulipa kiasi kingine cha fedha kama hicho ili kukamilisha uanachama halisi.

Kanisa au hekalu la shetani nchini Kenya, ni tawi la kanisa la kishetani lililoanzishwa Aprili 30, 1966 na Magus Anthony Szandor LaVey, na kuushangaza ulimwengu alipotokeza hadharani na kueleza imani yake dhidi ya shetani badala ya Mungu.

LaVey alikuwa mpinzani wa Ukristo na mwanamuziki aliyependa kujisifia mwenyewe, alijaribu kuunganisha waabudu shetani na hata kuandika Biblia yao iliyojulikana kama ‘Satanic Bible’, alijitangaza kuwa kuhani mkuu wa kanisa hilo hadi alipofariki dunia mwaka 1997 na nafasi yake kutwaliwa na mkewe Blanche Barton.

Alipofariki kanisa lake likazidi kuenea kila kona ya dunia na mapema mwaka huu likaingia rasmi nchini Kenya, katika mji wa Nairobi lakini wanaojua vyema ni wale waliokwisha timiza masharti na kupewa uanachama.

Tangazo la namba zao za simu ni 666, Nairobi, Kenya, 100100+254 716 ***666, na wanaalika watu kwa njia mbali mbali ili kuwavuta kujiunga na kundi hilo la kishetani. Namba 666 inayotumiwa na kanisa hilo inatajwa katika Biblia kitabu cha Ufunuo wa Yohana kama namba ya mpinga Kristo, ambayo wale watakaosalia baada ya unyakuo watateswa ili kuipokea.

Wakati huohuo, ile harusi baina ya mzee wa miaka 74 na mbuzi imefungwa wiki imepita katika kanisa la waabudu shetani nchini Brazil. Wiki zilizopita Bwana harusi alitangaza kuwa katika sherehe yake hakuta kuwa na nyama ya mbuzi ili kumuenzi mkewe.

Bwana Harusi huyo mtarajiwa, mzee Aparecido Castaldo,alitangaza kuwa maandalizi yote ya harusi hiyo ya kihistoria na wageni walimiminika nchini Brazili  kushiriki tukio hilo la kishetani.

Mwenyewe anajivunia mahusiano yake na mbuzi wake aitwaye Carmela, ndani ya kanisa pekee ambalo limeridhia kufanya kazi hiyo.

“Niliomba makanisa kadhaa yakiwepo ya kiinjili, lakini yaligoma nikaonana na Toninho do Diabo (Tom the Devil), nikazungumza naye na kukubaliana, nitaweka historia ya pekee si hapa Brazil pekee, bali ni pamoja na dunia yote,” alisema Bw. harusi huyo.

Sherehe ilifanyika katika kanisa la kishetani la Sao Paolo, usiku wa manane na wafuatiliaji wa mtandao waliweza kuliona moja kwa moja.

Kulingana na maandiko matakatifu, mambo hayo yote yanaashiria mwisho wa dunia uliotabiriwa na Bwana Yesu Kristo mwenyewe (soma Mathayo 24 na Ufunuo 13).

No comments:

Post a Comment