Maaskofu watema moto Katiba, Tokomeza ujangili

Siku ya Juzi Wakristo nchini waliungana na wenzao duniani kuadhimisha sikuu ya Krismasi kama kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo takribani miaka 2,000 iliyopita huku maaskofu wakitoa maubiri mbalimbali ukiwamo mchakato wa Katiba Mpya.

Katika mahubiri yake kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki  Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, aliwataka Watanzania kuiombea rasimu ya pili ya Katiba Mpya ili  ipatikane katiba  inayokidhi mahitaji ya watanzania kwa maslahi ya nchi na ustawi wa jamii.

Aidha, alisema viongozi wanapopewa madaraka wametakiwa kuacha kujineemesha na kujilimbikizia mali na kushindwa kuwasaidia wale ambao wanatakiwa kuwahudumia na kuwaacha katika hali duni.

Alisema kipindi hiki cha maandalizi ya kupata katiba mpya wananchi wanapaswa kuiombea nchi ibaki katika umoja, mshikamano na amani kwa kuwa mwaka 2013 amani ya nchi ilitikisika katika mambo mbalimbali.

Askofu Nzigilwa alisema ikipatikana katiba inayokidhi mahitaji ya watanzania italeta ustawi wa nchi na jamii kwa ujumla na nchi itabakia kuwa amani na utulivu.

Kuhusiana na viongozi wanapopata madaraka, alisema utakuta mtu akiwa duni kabisa, lakini anapopewa nafasi anajineemesha kwa kununua magari, kujenga majumba bila kuwasaidia watu wanaowatumikia.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Anglikan la Mtakatifu Alban, jijini Dar es Salaam, Aidano Mbulinyingi, aliwataka Watanzania kuondoa woga juu ya mchakato unaoendelea wa kupata katiba mpya, ambayo alisema imebeba mawazo mbalimbali,yakiwamo potofu.

Mchakato huo wa katiba utafanikiwa kwa kuwa Kristo aliyezaliwa miaka 2,000 iliyopita aliwaasa Wakiristo kuwa wasiogope kwa jambo lolote litakalotokea mbele ya jamii.

Alisema baadhi ya Watanzania wamekuwa na woga kuhusu mchakato wa katiba huku wengine wakitafuta mbinu mbalimbali ili zoezi hilo la kuandika katiba lishindikane.

“Tusiwe waoga kiasi hicho, bali tumtegemee Mungu na neno, usiogope katika Biblia limeandikwa mara 360, hii nikionyesha yote yaliyopo sasa tayari Mungu anayajua na kutuasa,” alisema.

Mchungaji Mbulinyingi alisema ni ajabu kuona wengine wakihofia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuanza kujitangaza kwa wananchi, na kusema kuwa hali  hiyo inapaswa kuombewa ili iwatoke  wenye roho hizo na kuwa raia wema.

MAPIGANO YA ARDHI
Selyvester Thadey wa kanisa la International Evangilism Sinai Ipagala mkoani Dodoma, alisema hivi sasa Watanzania wamechoshwa kusikia vurugu za mapigano zinazotokea za wakulima na wafugaji, hivyo kuwataka viongozi wa serikali waliokabidhiwa dhamana ya kiutendaji wanakomesha hali hiyo.

“Sisi kama kanisa tuna mashaka miongoni mwa viongozi wa serikali wananufaa pindi inapotokea vurugu kati ya wakulima na wafungaji kuwa, wanapata maslahi kwa ajili yao binafsi,” alisema.


ASKOFU PHAM APONGEZA MAWAZIRI KUJIUZULU
Askofu wa Kanisa la PHAM Kanda ya Kati Dodoma Julius Bundala, aliwapongeza mawaziri ambao wizara zao zimeshutumiwa kuhusika katika unyanyasaji wakati wa Operesheni ya Tokomeza Ujangili kwa kukubali kuachia madaraka yao.

Bundala akizungumza mara baada ya ibada iliyofanyika ya Krismas Kanisa la Makole mjini Dodoma.

Alisema hatua walizochukua mawaziri hao kujiuzulu ni ukomavu.
Hata hivyo, alisema watendaji wengine wanapaswa kufahamu kuwa hakuna kificho kutokana na mawaziri hao kuwekwa wazi na Kamati ya Ardhi, Maliasili, Ardhi na Mazingira kwenye kikao kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

Hata hivyo Askofu huyo amemtaka Rais Kikwete kutoishia kwa Mawaziri hao bali anatakiwa kuchunguza baraza lake hilo ili kuwabaini ambao wanaotumia madaraka yao kinyume na sheria na utaratibu zilizopo ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.

TAG yalaani TOKOMEZA UJANGILI
Mchungaji wa Kanisa la TAG Mlima wa Moto lililopo soko la Sabasaba mjini Dodoma, Silivanus Komba, alisema njia iliyowezesha kuweka wazi unyama waliofanyiwa wananchi na mawaziri ambao walioondolewa kwenye nyadhifa zao ni  baada ya kufanyika  kwa mahojiano mbalimbali na kamati.

Alisema hali hiyo inatokana na vilio vingi vya wananchi ambao walionyanyaswa wasiokuwa na hatia na kunyanganywa na mali na fedha zao kwa watendaji wasiokuwa na huruma.

Hata hivyo, alisema kuwa ni matumaini yake na kanisa kuwa serikali pia inasafisha safu yake kwa wale ambao bado wanaonyoshewa vidole kutokana na utendaji wao mbovu.

ASKOFU MKUDE APINGA UMEME KUPANDA
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphory Mkude, alieleza kushangazwa na serikali kwa kuruhusu bei ya umeme kupanda kwa asilimia 50 na kueleza kuwa hali hiyo itazidi kuongezea mwananchi mzigo na kuendelea na hali ya umasikini kwa kuwa watashindwa kumudu gharama hizo.

Badala yake Askofu Mkude alitaka serikali kutoruhusu kupanda kwa bei ya umeme kwani wananchi watashindwa kutumia huduma hiyo na kubaki kwa watu wachache ambao watakuwa na uwezo.

Katika mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Patrice, alisema inasikitisha kuona bei ya umeme inapandishwa kwa kiwango kikubwa na kuendelea kumuumiza mwananchi wa nchini ambaye kipato chake ni duni na kueleza hali hiyo itasababisha watanzania waendelee kudidimia na hali ya umaskini.

Alisema cha kusikitisha ni kwamba Tanzania ndiyo nchi inayotoza gharama kubwa za umeme ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

“Watanzania wanakipato duni sana, leo hii wanapandishiwa bei ya umeme, mimi nadhani sasa watashindwa kuitumia huduma hiyo na kurudi katika matumizi ya vibatari ,” alisema na kuongeza:

“Katika hili serikali inapaswa kulitafakari kwa kina suala hili la kupandisha bei ya umeme.”

Alisema anadhani kwa nchi kama ya Tanzania ambayo inanza kupiga hatua ya kutafuta maendeleo kwa kasi, huduma hiyo ilipaswa kutolewa kwa gharama nafuu ili kila mtu amudu, lakini hali imekuwa tofauti kutokana na kupandishwa mara kwa mara huku umeme ukiendelea kuwa tatizo.

ASKOFU MALASUSA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amesema viongozi na wanasiasa waliopo madarakari kwa njia zisizo za halali wamekuwa wakihangaika kufanya jambo lolote liwezekanalo ili kuzilinda  nafasi zao, pindi unapotokea mtetereko katika nafasi walizopo jambo alilosema linasababisha uvunjifu wa amani.

 Aidha aliwafananisha viongozi hao na Mfalme Herode ambaye alikuwa mfalme wa Wayahudi na baada ya kusikia kuwa Yesu Kristo amezaliwa ambaye atakuwa mfalme wao, alitetereka na kuanza kutafuta mbinu za kumuangamiza.

 Akihubiri katika Kanisa hilo Kuu la Azania Front, jijini Dar es Salaam, Dk. Malasusa, alisema ni vema jamii ikasherehekea Krismasi kwa kuyafanya yale mema ambayoYesu aliyatenda ili kudumisha amani na ushirikiano duniani kote.

Aliwataka watanzania na dunia nzima kusherehekea sikukuu hiyo kwa kuishi maisha ya amani ambayo yataendelea kutuunganisha dunia nzima ili kuepukana na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyotokea duniani.

“Rasilimali nyingi duniani  hutumika kutengeneza na kutafuta amani kwa mambo ambayo hayampendezi Mungu badala ya kuelimisha watu ili  kuzilinda imani zao, mfano mzuri ni kwa watu ambao wamekuwa wakirekebisha maovu ya watu au viongozi, huonekana hawafai kwa kupigwa vita badala ya kuungwa mkono,” alisema Dk. Malasusa.

ASKOFU AICT: VIONGOZI NI WABINAFSI
Askofu wa Africa Inland Church (AICT)  Jimbo la Geita, Mussa Magwesela, alisema amani barani Afrika haitapatikana iwapo viongozi waliopewa dhamana ya kuwaongoza wananchi hawataacha ubinafsi wa kung’ang’ania madaraka, kujilimbikizia mali, rushwa na matumizi mabaya ya raslimali za umma vinavyosababisha mataifa mengi duniani kumwaga damu.

Akizungumza katika Ibada ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika kitaifa katika kanisa hilo Kalangalala mjini Geita, alisema hali hiyo inatokana na viongozi kukosa hofu ya Mungu na kutaka kujinufaisha kwa maslahi binafsi.

Askofu Mwagwesa, alisema viongozi hao wameshindwa kufuata misingi iliyoachwa na watangulizi wao (waasisi wa mataifa hayo) Kwame Nkuruma, Mwalimu Julius Nyerere, Jomo Kenyatta na Nelson Mandela ambao walikuwa wanyenyekevu mfano wa Yesu Kristo alipojitoa na kukubali kufa msalabani ili kuwakomboa watu na dhambi za ulimwengu.

“Viongozi hawa waliimarisha misingi ya Utawala bora, lakini suala la uongozi katika Taifa letu na bara la Afrika kwa miaka 50 hadi 60 iliyopita tumejionea matukio mengi ya umwagaji wa damu kwa sababu ya baadhi yao kung’ang’ania madaraka,” alisema Askofu Magwesela.

Kadhalika, alisema sekta ya ardhi imekuwa kinara wa  rushwa, hali ambayo imekuwa ikisababisha uvunjwaji wa sheria na hatimaye mauaji baada ya viongozi hao kutumia madaraka yao vibaya kama ilivyojitokeza kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina.

Alisema kugoma kwa madakatari na walimu nchini  kwa kisingizio cha ukosefu wa vitendea kazi sehemu za kazi na mishahara  midogo inatokana na kukosa wito wa kazi zao licha ya kuwa elimu hiyo wameipata kutokana na kodi za wananchi.

“Serikali iboreshe miundombinu ya maji,barabara na hospitali badala ya kuendelea kuwahadaa wananchi.

ASKOFU DALLU: RASILIMALI ZISITUGOMBANISHE
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Damian Dallu, aliwataka Watanzania kuepuka mafarakano na uvunjifu wa amani  kunakosababishwa na rasilimimali za nchi.

Aidha, aliwata kushirikiana katika kuondokana na mambo yanoyoleta uadui kati ya wenye madaraka, vyeo na waliyonacho na wasiyo chacho  kwani vinaweza kuligawa taifa katika matabaka.

Rai hiyo aliitoa jana mjini Geita katika ibada ya Krismasi iliyoadhimishwa kitaifa katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani mkoani Geita.

Alisema ni vyema Watanzania kusherehekea Krisimas kwa amani na upendo wa kweli kwa kusaidiana bila kujali tofauti zetu  katika njia halali ya kujikomboa  na umasikini na kujenga mshikamano.

“Ni vema mambo yanayoonekana kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani vikaepukwa mapema kwa kushirikiana kwamba aliye nacho aumie kwa ajili ya yule asiye nacho ili kuishi kwa amani na furaha, kiongozi bora ni yule anayeumia kwa ajili ya watu wake na huo ndiyo upendo unaoleta amani,” alisema Askofu Dallu.

Alisema, ni vema Watanzania wakatafuta amani na furaha ya kweli kwa kuomba, kusameheana yale yote yaliyopita pamoja na kushiriki sala, kuinua elimu na kufanya kazi kwa bidii.

Pia aliwataka wakazi wa mkoa mpya wa Geita kuhakikisha wanauendeleza mkoa huo kwa kusoma na kufanya kazi kwa bidii ili kujiinua kiuchumi hasa katika sekta ya elimu na afya ambazo bado ziko chini.

ASKOKU MKUU ANGLIKANA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya, ameitaka serikali kuwa na mipango madhubuti ya kuwahudumia watu badala ya kupata dhiki katika nchi yao yenye utajiri mwingi.

Akitoa salamu zake za Krismasi katika Kanisa la Dayosisi ya Mpwapwa mkoani Dodoma, alisema ni lazima Watanzania wote wapate elimu.

”Kwa mfano ukizungumzia habari ya elimu mtanzania anahitaji kupata elimu ambayo itakuwa mkombozi katika maisha yake na serikali iwe na kipaumbele chetu kwa mfano kwenye elimu ya msingi na sekondari kuliko kwenye elimu ya chekechea,” alisema Askofu Chimeledya.

Alibainisha kuwa Watanzania wanahitaji kupata elimu ambayo itakuwa mkombozi katika maisha yao na kusema kuwa matarajio yake ni mtoto aingie elimu ya msingi anajua kusoma na kuandika hivyo aandaliwe chekechea akiwa na miaka mitatu hadi mitano.

“Pia Watanzania watapata matumaini kama serikali itashuka chini na kwenda kushughulikia watendaji mmoja mmoja na waziri anawajibika kama mimi ninavyowajibika kwa kanisa langu au dayosisi yangu kama kweli chini kuna watu wanafanya vibaya kwa hiyo kuwajibika kwangu hakutaleta faraja kama bado watendaji hao wapo,” alieleza.

Alisema kuwa inatia moyo mawaziri wanne wamewajibika kwa kujiuzulu na anawapongeza sana, lakini serikali irudi kufuatilia watendaji wote katika ngazi mbalimbali kamwe kuna mtu hataweza kutowatendea haki wananchi.

Askofu Shao: Tuwaombee Sudan Kusini
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Dk. Martin Shao, amesema ingawa Tanzania inatajwa kukomaa kisiasa katika ukanda wa Afrika, lakini iko haja kama taifa kuandaa funga maalumu kwa ajili ya kumwomba mwenyenzi Mungu aingilie kati na kukomesha mapigano yanayoendelea Sudan ya Kusini kati ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wanaomuunga mkono hasimu wake, Riek Machar.

 Alisema machafuko ya kisiasa yanayoendelea kuangamiza wanadamu katika mataifa yenye utajiri mkubwa wa mafuta ikiwemo Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Misri ni mwangwi ambao Tanzania haipaswi kukaa kimya kama kinara wa ukombozi katika nchi za Afrika.

Dk. Shao alikuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika katika Usharika wa Moshi mjini.

 “Asilimia 73 ya Wakristo duniani kote leo jana) wanaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo, lakini wakati tunashangilia na kufurahi kwa kula na kunywa, kila kona ya nchi,wenzetu wanaendelea kufa huko Sudan ya Kusini,Kongo na Misri kutokana na machafuko ya kisiasa na ulafi wa madaraka ambao tuna kila sababu ya kuomba yasiendelee kuua maelfu ya wanadamu wenzetu,” alisema Dk. Shao.

Kuhusu hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na mataifa kwa ajili ya kuepusha dhahama hiyo, askofu huyo alisema bila ya kujali ni dhehebu gani mtu anakoabudu, watanzania kwa ujumla wake wanapaswa kuweka pembeni itikadi zao na kuomba waafrika wenzetu waondoke katika mahangaiko na mateso yanayotokana na siasa hasi za kung’ang’ania madaraka.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Katoliki Sombetini, jijini Arusha, Padre Peter Shibale, alisema kuwa inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa  Kikiristo wanaacha kufuata nyayo za Kristo na wanaanza kurubuniwa na baadhi ya wahubiri wanaotoa mahubiri yanayokwenda kinyume na ya Yesu Kristo.

Akihubiri kwenye Kigango cha Utatu Mtakatifu Kwamurombo, alisema wahubiri wanaopotosha wanadai wanatoa wokovu.

“Wokovu mwenye kuutoa ni bwana Yesu Kristo pekee na siyo mwingine, hivyo tusiyumbe na tusimame imara katika makanisa yetu,” alisema Padre Shibale.

Padri Leonard Mariva wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Consolata Parokia ya Mshindo mjini Iringa, aliwataka waumini kuendelea kuiombea dunia ili yasitokee  machafuko ya vita, matetemeko,utoaji wa mimba ovyo na mauji ya kupigania mali.

Alisema siku hizi machafuko kama hayo yametokea na watu wengi kupoteza maisha yao, hivyo tuna kila sababu za kumuomba machafuko kama haya yasitokee tena.

Imeandikwa na Jimmy Mfuru, Leonce Zimbandu, Mary Geofrey, Dar; Augusta Njoji na Peter Mkwavila, Dodoma; Ashton Balaigwa, Morogoro; Godgrey Mushi, Moshi; Cynthia Mwilolezi, Arusha;  George Tarimo Iringa na Daniel Limbe, Geita.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment