Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro:Viongozi wa Dini na Serikali simamieni sheria

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amewaomba viongozi wa dini na wa serikali wasimamie sheria za nchi katika maeneo yao kwa lengo la kudhibiti mauaji dhidi ya wanawake.

Gama aliyasema hayo jana mjini hapa na kufafanua kuwa kama viongozi hao watasimamia sheria na kuhakikisha zinatekelezwa, matukio hayo yatupungua.

“Hayo yote yanasababishwa na watu kunywa pombe wakati wa kazi, vijana kuvuta bangi na kutofanya kazi, usipokuwa busy (shughuli) lazima ujikute unafanya matukio ya ajabu,” alisema Gama.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama
 Hata hivyo. Gama alisema wakati umefika kila mtu kujua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani ya nchi badala ya kuliacha jukumu hilo kwa watu wachache.

“Kama vijana hawatafanya kazi, watakuwa wanafanya matukio ya ajabu kama hayo ya kuua wake zao na wapenzi wao kwa sababu ya wivu. Utakuta mwanamke anajishughulisha na anachelewa kurudi nyumbani kwa kuwa anakuwa anatafuta fedha ya kulisha familia,” alisema na kuongeza:

“Baba alitakiwwa amsaidie, lakini anashindwa kufanya hivyo kutokana na kulewa muda wote na kumwachia mke wake mzigo.”

Alisema madhara yanayotokana na kulewa wakati wa kazi ni makubwa na kwamba matukio ya wanaume kuwaua wake zao yanasababisha  kupotea kwa  nguvu kazi ambayo ingesaidia kuinua uchumi wa nchi.

Nesi wa Hospitali ya Mabwepande ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema baadhi ya wanaume wanachukia wanawake kudai kuwapo usawa kati yao.

Matukio ya wanaume kuua wake zao kwa wivu wa mapenzi mkoani Kilimanjaro yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Iddi Juma, alisema wakati umefika kwa viongozi wa dini kuhubiri amani kwa nguvu zao zote.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment