Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye, visiwani Zanzibar, Padri Ambrose Mkenda, amepigwa risasi na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya.
Padre Mkenda ambaye jana alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili (MNH) kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja visiwani humo, alikokuwa amelazwa baada ya tukio hilo, alipigwa risasi katika taya na mgongoni.
Tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda limekuja miezi mitatu tangu Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, amwagiwe tindikali na watu wasiojulikana na kupelekwa kwenye matibabu nchini India.
Matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa yametanguliwa na matukio ya kuchomwa moto baa 12 na makanisa 25 katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Shule ya Francis Maria Libaman Tomondo iliyopo mjini Zanzibar ambayo inamilikiwa na kanisa hilo, Padri Arbogast Mushi, akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Muhimbili, alisema Padri Mkenda alipigwa risasi juzi majira ya saa 1:30 jioni nyumbani kwake.
|
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Parokia ya Mtakatifu Michael
Mpendaye, Ambrose Mkenda, akitolewa Hospitali ya Mnazi Mmoja visiwani
Zanzibar na kupelekwa uwanja wa ndege kisha kumsafirishwa |
Alisema Padri Mkenda ambaye nyumba yake ipo ndani ya shule hiyo, alipigwa risasi na watu wawili wasiojukana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa.
Mushi alisema Padri Mkenda alipigwa risasi kupitia kioo cha mbele ya gari yake aina ya Toyota Rav4 lenye namba za usajili Z 586 AW wakati akirudi nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.
“Padri tumemleta leo (jana) kwa ndege, alipigwa risasi akiwa nje ya lango la nyumba yake wakati akisubiri kufunguliwa na mlinzi ili aweze kuingia ndani ,” alisema Padre Mushi ambaye alimsindikiza Padri Mkenda.
Alisema tukio hilo limewashtua sana waumini wa kikristo kwa sababu ni mara ya kwanza kutokea na kwamba bado hawajafahamu kuna visa gani vilivyopelekea kupigwa risasi kwa Padri Mkenda.
Alisema baada ya tukio hilo ambalo lilimfanya Padri Mkenda kuvuja damu nyingi, alimchukua na kumpeleka Hospitali ya Alrahama na baadaye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alifanyiwa upasuaji mdogo katika eneo la taya.
MUHIMBILI WAELEZEA HALI YAKE
Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Muhimbili, Agnes Mtawa, alisema walimpokea Padri Mkenda majira ya saa 4:00 asubuhi na kuanza kumpatia vipimo mbalimbali ikiwamo X-Ray.
Mtawa alisema kuwa katika uchunguzi wao wa awali wamebaini kuwa alipigwa risasi eneo la kidevu na mgongoni na kwamba wanaendelea kumchunguza kubaini alipigwa risasi ngapi na kufanya utaratibu wa kuziondoa kama bado zipo mwilini.
“Padri anaendelea vizuri, Madaktari watakapokuja watamfanyia uchunguzi wa kina kubaini amepigwa risasi ngapi na kufanya utarativu wa kuziondoa ili zilete madhara zaidi kwake,” alisema Mtawa.
Hata hivyo, uongozi wa Muhimbili haukuwaruhusu waandishi wa habari kuonana na Padri huyo aliyesafirishwa kwa ndege kutoka Zanzibar kwa maelezo kuwa hakuwa katika hali nzuri.
ASKOFU ZANZIBAR ATOA TAMKO
Askofu wa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Cosmas Shao, alisema tukio hilo limewashtua sana wananchi na kwamba hata hivyo, waumini wa dini ya kikristo wana imani kuwa vyombo vya usalama vitafanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwakamata waliohusika.
“Krismasi tumeendesha vizuri na kimsingi waumini wa dini ya kikristo walikuwa katika wasiwasi mkubwa sana kutokana na tukio la kupigwa risasi Padri Mkenda, tuna imani polisi na vyombo vya usalama kwa ujumla vitafanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika,” alisema Askofu Shao.
Askofu Shao alisema Padri Mkenda ambaye ni Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye kupigwa risasi kwake hakumaanishi kuwa waliompiga risasi walitaka kupora fedha kwa sababu hatembei na fedha za kanisa hata siku moja.
Alisema kabla ya tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya vitisho na watu wasiojulika vikiwa na ujumbe: “Viongozi wa Uamsho waachiwe uhuru na serikali mara moja kabla ya kufanyika sikukuu ya Kirsimasi, vinginevyo kutatokea tukio kubwa Zanzibar.”
Askofu Shao alisema kwamba kutokana na majeraha aliyopata Padri Mkenda, waliamua kumsafirisha kwenda kutibiwa zaidi Muhimbili.
Baada ya kutokea tukio hilo, waumini mbali mbali walifika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na wengine kushindwa kujizuia na kutokwa machozi.
RPC ATANGAZA MSAKO
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika waliofanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni kitendo cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki kwa hivyo bado ni mapema kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani kwa kuwa bado uchunguzi wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusikana na tukio hili,” alisema Kamanda Aziz.
Kamanda Aziz alisema walipata taarifa za kupigwa risasi Padri Mkenda wakati akitokea kanisani kuelekea nyumbani kwake akiwa ndani ya gari ndipo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana na kuanguka.
“Tumekuta mabaki ya risasi ndani ya gari yake na katika vioo vyake vya gari vimevunjika na tumekuta damu chini pale,” alisema Kamanda Aziz.
Kamanda Aziz alisema kwa kuwa Padri Mkenda ni mhasibu katikia kanisani hilo, inawezekana waliompiga risasi walidhani kuwa alikuwa na fedha hasa ikizingatia kuwa katika sikukuu za krismasi fedha nyingi za sadaka hukusanywa kutoka kwa waumini.
Aliongeza kuwa kwa kuwa Padri Mkenda ni mhasibu katika miradi ya kanisa, huenda waliofanya kitendo hicho wakawa ni majambazi.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa awali ndiyo utakaoeleza ni suala gani lililopelekea kupigwa risasi, lakini wanaendelea na uchunguzi huo ambao ndiyo utakaobainisha ukweli wa tukio hilo.
Alisema kwamba watu waliompiga risasi walikuwa na bastola na Padri huyo alipigwa kwa risasi umbali wa mita mbili na kwamba baada ya mlinzi wa nyumba hiyo kutoka nje, alikuta Padri Mkenda tayari amepigwa risasi na watu hao wakiwa wameshatoweka.
Kuhusu kusambazwa kwa vipeperushi, Kamanda Aziz alisema hana taarifa hizo.
ASKOFU ANGLIKANA ANENA
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidhi, alisema Jeshi la Polisi limeonyesha udhaifu wa kusimamia ulinzi dhidi ya raia na mali zao.
Askofu Hafidhi alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya kutishia amani, lakini hakuna hatua za tahadhari zilizochukuliwa kabla ya Padri Mkenda kupigwa risasi.
Askofu Hafidhi alisema vitisho hivyo vilitolewa na wafuasi wa Uamsho kuwa watafanya tukio kubwa iwapo viongozi wao hawataachiwa uhuru kabla kumalizika sikukuu ya Kirismasi Zanzibar.
Hata hivyo, alisema jamii lazima ielewe kuwa jamii ya Wakiristo Zanzibar wana haki sawa na waumini wengine kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
CCM ZANZIBAR YALAANI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeeleza kushtushwa na tukio la kikatili alilofanyiwa Padre Mkenda.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alisema mfululizo wa vitendo hivyo vya kinyama na kiharamia ni ukiukaji wa misingi ya kiungwana, ustaarabu na upendo.
“Tukio hili na lile la kuchomwa moto kwa makanisa, kumwagiwa tindikali kiongozi wa kiislam Sheikh Fadhil Soraga, miezi mitatu iliopita na Padri Mkenda kupigwa risasi, kunaweza kuipunguzia Zanzibar fahari na sifa zake njema,” Alisema Warid.
Alisema kwa karne nyingi Waislamu, wakristo na wenye dini mbalimbali wamekuwa wakiishi kwa umoja, maelewano kinyume na hali inavyojitokeza sasa visiwani humo.
Alisema CCM kinaamini kuwa Zanzibar na Tanzania si nchi za kidini, kila mtu anafuata imani anayoitaka bila kuingiliwa au kubugudhiwa na mtu yeyote.
“Uhuru wa kuabudi ni haki ya kikatiba katika katiba zote mbili za Tanzania na Zanzibar, hivyo CCM kinawalaani wale wenye mtazamo wa kuona imani zao ndizo thabiti kuliko za wengine,” alisema.
Waride aliviomba vyombo vya dola kufanya kila linalowezekana na kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mikono ya sheria.
Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinamtakia nafuu kwa Mungu Padri Mkenda ili apone haraka na kuwataka wananchi
Source:Nipashe