Mkesha wa Kuliombea Taifa la Tanzania wafana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira amesema kuwa amani iliyopo Tanzania inatakiwa itumike kupambana na ufisadi.

Pia amesema amani ambayo ni haki ya kila mtu na Taifa la Tanzania inatakiwa itumiwe kudumisha haki kwani amani ni tunda la haki.

Waziri Wasira alisema kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa kuhakikisha amani ambayo pacha wake ni maendeleo vinalindwa kama mboni ya jicho.

Mkesha huo uliozihusisha taasisi za dini ya Kikristo 50 ziliongozwa na Askofu Emmanuel Malasi ambaye katika maneno yake kubwa alilokuwa akisisitiza ni kudumisha, amani, upendo na uvumilivu.

Kwenye mkesha huo wa kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013 walihudhiria viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dodluck Ole Medeye na Mbunge wa Viti Maalumu Mbeya, Dk. mary Mwanjelwa.

Pia zilikuwepo nafasi za uwakilishi katika idara na mashirika mbalimbali ya kimataifa huku ubalozi wa Marekani nao ukiwakilishwa na Elizabeth Petro.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira (katikati), akipunga bendera pamoja na viongozi wengine wa Dini,Katika Mkesha huo uliofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam siku ya amkesha wa mwaka mpya Wasira alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkesha huo.

Baadhi ya viongozi wa Serikali walioudhlia mkesha huo uwanja wa Taifa ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Goodluck Ole Madeye (kulia), Balozi Mdogo wa Marekani nchini, Elizabeth Petro (kushoto), na Mbunge wa viti maalumu (CCM), Mbeya mjini Dk. Mary Mwanjelwa wakiwa kwenye ibada hiyo.

Waumini wa dini ya Kikristo walioudhulia mkesha huo wakishangilia na kumshukuru Mungu baada ya kuvuka mwaka mpya.

Idadi ya Watanzania kujulikana leo

Idadi  ya Watanzania itajulikana leo wakati Rais Jakaya Kikwete atakapolihutubia Taifa kwa ajli ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013 kupitia vyombo vya habari.

Pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete atatangaza idadi ya Watanzania ikiwa ni hatua ya kukamilisha zoezi la sensa ya watu na makazi iliyofanyika nchini Agosti hadi Septemba, mwaka huu.

Sensa hiyo ilianza Agosti 26 na ilitarajiwa kumamilika Septemba Mosi, lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza, ilisogezwa mbele kwa siku saba na hivyo, kukamilika Septemba 8.

Miongoni mwa changamoto zilizolikabili zoezi hilo ni baadhi ya vikundi vya dini kuwahamasisha wafuasi wao wasihesabiwe, makarani kugoma kutokana na kucheleweshewa au kukatwa posho, vifaa kuchelewa kufikishwa katika maeneo pamoja na maeneo mengine kupokea vifaa vichache.

Kwa mara ya mwisho, Tanzania ilifanya sensa ya watu na makazi mwaka 2002, ambayo ilibainisha kuwa nchi ilikuwa na watu milioni 35.

Hivi sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wapatao milioni 40.

Changamoto, ambazo serikali ilikumbana nazo, mafanikio yaliyopatikana na matarajio kwa mwaka ujao wa 2013.

Kanisa Katoliki Zanzibar latoa tamko

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Mhashamu Augustino Shao
Kufuatia kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya nchini, Kanisa Katoliki jimbo la Zanzibar, limesema wafanyabishara wakubwa wanaoingiza biashara hiyo na kuuza visiwani humo wanajulikana.

Kanisa hilo, limesema wakati umefika kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwakamata wafanyabiashara hao badala ya kuwashughulikia watumiaji wadogo.

Askofu wa kanisa hilo, jimbo la Zanzibar, Mhashamu Augustine Shao, alisema hayo siku chache zimepita katika misa ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa la Minara Miwili Shangani katikati ya mji Mkongwe.

Mhashamu Shao alisema wimbi la vijana kutumia dawa za kulevya Zanzibar litapungua kama SMZ itachukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wakubwa.

Alisema kuendelea kwa biashara hiyo kunasababisha madhara kwa vijana na watu wazima.

“Tuache kukimbizana na waathirika waliojikuta wakitumia dawa za kulevya kwa matatizo yao ya umasikini,” alisema.

Hata hivyo, alisema jamii inapaswa kuwasaidia waathirika wa dawa hizo badala ya kuwanyanyapaa kwa sababu kama watapata ushauri nasaha, wana nafasi ya kuacha kuzitumia.

Mhashamu Shao, alisema vijana visiwani Zanzibar wanaishi katika mazingira magumu, kutokana na matatizo kama ukosefu wa ajira, dawa za kulevya na maambuziki ya virusi vya ukimwi.

Ushauri wa Mhashamu Shao, umekuja huku takwimu zikionyesha asilimia 20 ya wagonjwa wa akili katika hospitali ya Kidongochekundu ni waathirika wa dawa hizo.

Kuhusu vurugu za Mei na Oktoba mwaka huu zilizotokea Zanzibar, alisema zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini ambao wameamua kutumia vijana wasiokua na kazi kufanikisha malengo yao binafsi.

“Ghasia na uchomaji wa makanisa zilizofanyika chini ya mwamvuli wa Muungano ni dhana nyemelezi ya wenye madaraka nje na ndani katika kutumia umasikini wa vijana wetu kutimiza malengo yao binafsi,” alisisitiza.

Alisema watu hao wameamua kutumia migongo ya masikini kwa manufaa yao binafsi na kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa.

“Kataeni kutumiwa kwa misingi ya dini, itikadi za siasa na uchumi kwa manufaa ya watu binafsi au kuneemesha watu wachache,” alionya Mhashamu Shao.

AZUNGUMZIA KATIBA MPYA

Akizungumzia mabadiliko ya Katiba, Mhashamu Shao , aliwataka wananchi kutoa maoni ambayo yatasaidia kupata katiba yenye manufaa kwa maslahi ya Taifa na wananchi wa pande mbili za Muungano.

Hata hivyo alisema wakati huu wa mjadala wa Katiba mpya, ni muhimu wananchi wakazingatia umuhimu wa kulinda misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

Benjamin Dube- Bow Down and worship


Nabii Flora Peter ataka amani idumishwe nchini


Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Nabii Flora Peter
Watanzania wametakiwa kudumisha na kuithamini amani ya nchi iliyopo badala ya kuiharibu kwani kuirudisha kwake ikitoweka itachukua muda.

 Wito huo ulitolewa na Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Nabii Flora Peter alipokuwa akihubiri katika siku chache zimepita katika ibada ya Krismasi katika Kanisa hilo lililoko Mbezi SalaSala Dar es salaam juzi.

“Kuwa na amani ni jambo jema kwa wananchi wote na dini zote lakini kuharibu amani ni jambo ambalo halimpendezi mungu” alisema Nabii Flora

Alisema Tanzania inajivunia amani iliyopo ambayo imedumishwa na wanzania wenyewe hivyo kila mmoja mwananchi ana wajibu wa kuitunza.

Alisema mahali palipo kosekana amani hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika ikiwa pamoja na kuabudu kwani mifano halisi inaonekana katika nchi zenye machafuko kama vile somaria, Siria na nyinginezo.

“Katika nchi hizo watu wanahitaji kuabudu kama tulivyo sisi lakini wanashindwa kwa sababu hakuna amani hivyo tuidumishe amani tuliyo nayo” aliongeza Nabii Flora.

Alisema amani ya Tanzania idumishwe ili mataifa mengine yaje kujifunza kwetu kuliko kuiacha ikapotea kwa kugombana baina ya dini moja na nyingine.

Alisema Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano na gumzo kwa nchi nyingine kutokana na wananchi wake kuwa na upendo na utulivu wa kipee hata mtu akiwa nje ya nchi anakuwa kifua mbele kusema anatoka Tanzania hivyo ni jambo la kujivunia.

 Katika hatua nyingine  Nabii Flora amewataka waananchi wote bila kujali imani za dini zao kujitokeza kushiriki mchakato wa kujadili katiba mpya kwani ndiyo dira ya nchi yetu.

Alisema ni vizuri watu mbalimbali wakajadili kwa kina mchakatio wa katiba mpya badala ya kujadili chama kwani katiba ndiyo itakayaotuongoza kwani suala hilo ni letu sote na si la mtu au kundi fulani.

   Nabii Flora alitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukubali kupitisha mchakato wa katiba mpya pamoja na kuweka uhuru kwa kila mwananchi kufanya jambo lake kwa uhuru pasipo kuvunja sheria.

” Kila mtu anaona utawala wa Rais Kikwete jinsi unavyofanya kazi kwa uwazi na kasi kubwa na ndiyo maana kila idara na taasisi imepewa nafasi ya kuamua na mamuzi hayo yanaheshimiwa na kila mtu kwa maslahi ya Taifa” alisema Nabii huyo.

Christmas Production ndani ya VCCT ilivyo bamba...!!

Siku ya jana katika Kanisa la VCCT (Victory Christian Centre Terbenancle) Mbezi Beach kulifanyika Moja ya matamasha makubwa yanayochukua nafasi katika kufunga mwaka wa 2012 jijini Dar.

Limekuwa likijulikana kwa jina Christmas Production,  tukio hilo hufanyika kila tar 26 Disemba 2012, siku moja baada ya siku Mwokozi wetu Yesu Kristo alipozaliwa,Katika tukio hilo watu watu waliopata kufika walimsifu na kumwabudu Mungu kwa namna nisiyoweza elezeka,wakiongozwa na waimbaji mbalimbali waliokuwepo.

Katika  event hiyo Christmas Production kulikuwa na Rivers of Joy International, Glorious Celebration, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Amani Isayah, Bomby Johnson, Samuel Yonah, President Chavala, Mc Pilipili, CASFETA Dar P & W team. 

 Mch. Dkt Huruma Nkone, Mchungaji Kiongozi VCCT
 Upendo Kilahiro
Mch Joyce Nkone
 Upendo Nkone
Rivers of Joy  junior wa VCCT
Upendo Kilahiro & Mpelo Kapama, Kiongozi wa Muziki na Uimbaji, VCCT

Mc & President  Chavala
Ilikuwa  fullshangwe
  Timothy Kyara na mkewe


Rivers Of Joy International katika Kumsifu Mungu
The Blogger...Papaa kama kawaida yake uwanja wa nyumbani
Glorious Celebration walikuwepo
 Upendo Nkone akiwa amezama!!
Ukumbi haukutosha. Na watoto nao hawakubaki nyumbani; walikuwepo.


King Chavala Kufunga Mwaka na Laugh Again Concert ......Omega De One !!!!!


 

 


Padri apigwa risasi huko visiwani Zanzibar

Paroko  wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye, visiwani Zanzibar, Padri Ambrose Mkenda, amepigwa risasi na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya.

Padre Mkenda ambaye jana alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili (MNH) kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja visiwani humo, alikokuwa amelazwa baada ya tukio hilo, alipigwa risasi katika taya na mgongoni.

Tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda limekuja miezi mitatu tangu Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, amwagiwe tindikali na watu wasiojulikana na kupelekwa kwenye matibabu nchini India.

Matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa yametanguliwa na matukio ya kuchomwa moto baa 12 na makanisa 25 katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi wa Shule ya Francis Maria Libaman Tomondo iliyopo mjini Zanzibar ambayo inamilikiwa na kanisa hilo, Padri Arbogast Mushi, akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya  Muhimbili, alisema Padri Mkenda alipigwa risasi juzi majira ya saa 1:30 jioni nyumbani kwake.

Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye, Ambrose Mkenda, akitolewa Hospitali ya Mnazi Mmoja visiwani Zanzibar na kupelekwa uwanja wa ndege kisha kumsafirishwa
Alisema Padri Mkenda ambaye nyumba yake ipo ndani ya shule hiyo, alipigwa risasi na watu wawili wasiojukana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa.

Mushi alisema Padri Mkenda alipigwa risasi kupitia kioo cha mbele ya gari yake aina ya Toyota Rav4  lenye namba za usajili Z 586 AW wakati akirudi nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.

“Padri tumemleta leo (jana) kwa ndege, alipigwa risasi akiwa nje ya lango la nyumba yake wakati akisubiri kufunguliwa na mlinzi ili aweze kuingia ndani ,” alisema Padre Mushi ambaye alimsindikiza Padri Mkenda.

Alisema  tukio hilo limewashtua sana waumini wa kikristo kwa sababu ni mara ya kwanza kutokea na kwamba bado hawajafahamu kuna visa gani vilivyopelekea kupigwa risasi kwa Padri Mkenda.

Alisema baada ya tukio hilo ambalo lilimfanya Padri Mkenda kuvuja damu nyingi, alimchukua na kumpeleka Hospitali ya Alrahama na baadaye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alifanyiwa upasuaji mdogo katika eneo la taya.

MUHIMBILI WAELEZEA HALI YAKE

Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Muhimbili, Agnes Mtawa, alisema walimpokea Padri Mkenda majira ya saa 4:00 asubuhi na kuanza kumpatia vipimo mbalimbali ikiwamo X-Ray.

Mtawa alisema kuwa katika uchunguzi wao wa awali wamebaini kuwa alipigwa risasi eneo la kidevu na mgongoni na kwamba wanaendelea kumchunguza kubaini alipigwa risasi ngapi na kufanya utaratibu wa kuziondoa kama bado zipo mwilini.

“Padri anaendelea vizuri, Madaktari watakapokuja watamfanyia uchunguzi wa kina kubaini amepigwa risasi ngapi na kufanya utarativu wa kuziondoa ili zilete madhara zaidi kwake,” alisema Mtawa.

Hata hivyo, uongozi wa Muhimbili haukuwaruhusu waandishi wa habari kuonana na Padri huyo aliyesafirishwa kwa ndege kutoka Zanzibar kwa maelezo kuwa hakuwa katika hali nzuri.

ASKOFU ZANZIBAR ATOA TAMKO

Askofu wa  Katoliki Jimbo la Zanzibar, Cosmas Shao, alisema tukio hilo limewashtua sana wananchi na kwamba hata hivyo, waumini wa dini ya kikristo wana imani kuwa vyombo vya usalama vitafanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwakamata waliohusika.

“Krismasi tumeendesha vizuri na kimsingi waumini wa dini ya kikristo walikuwa katika wasiwasi mkubwa sana kutokana na tukio la kupigwa risasi Padri Mkenda, tuna imani polisi na vyombo vya usalama kwa ujumla vitafanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika,” alisema Askofu Shao.

Askofu Shao alisema Padri Mkenda ambaye ni Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye kupigwa risasi kwake hakumaanishi  kuwa waliompiga risasi walitaka kupora fedha kwa sababu hatembei na fedha za kanisa hata siku moja.

Alisema  kabla ya tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya vitisho  na watu wasiojulika vikiwa na ujumbe: “Viongozi wa Uamsho waachiwe uhuru na serikali mara moja kabla ya kufanyika sikukuu ya Kirsimasi,  vinginevyo kutatokea tukio kubwa Zanzibar.”

Askofu Shao alisema kwamba kutokana na majeraha aliyopata Padri Mkenda, waliamua kumsafirisha kwenda kutibiwa zaidi  Muhimbili.

Baada ya kutokea tukio hilo, waumini mbali mbali walifika katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na wengine kushindwa kujizuia na kutokwa machozi.

RPC ATANGAZA MSAKO

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika waliofanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni kitendo cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki kwa hivyo bado ni mapema kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani kwa kuwa bado uchunguzi wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusikana na tukio hili,” alisema Kamanda Aziz.

Kamanda Aziz alisema walipata taarifa za kupigwa risasi Padri Mkenda wakati akitokea kanisani kuelekea nyumbani kwake akiwa ndani ya gari ndipo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana na kuanguka.

“Tumekuta mabaki ya risasi ndani ya gari yake na katika vioo vyake vya gari vimevunjika na tumekuta damu chini pale,” alisema Kamanda Aziz.

Kamanda Aziz alisema kwa kuwa Padri Mkenda ni mhasibu katikia kanisani hilo, inawezekana waliompiga risasi walidhani kuwa alikuwa na fedha hasa ikizingatia kuwa katika sikukuu za krismasi fedha nyingi za sadaka hukusanywa kutoka kwa waumini.

Aliongeza kuwa kwa kuwa Padri Mkenda ni mhasibu katika miradi ya kanisa, huenda waliofanya kitendo hicho wakawa ni majambazi.

Hata hivyo, alisema  uchunguzi wa awali ndiyo utakaoeleza ni suala gani lililopelekea kupigwa risasi, lakini wanaendelea na uchunguzi huo ambao ndiyo utakaobainisha ukweli wa tukio hilo.

Alisema kwamba watu waliompiga risasi walikuwa na bastola na Padri huyo alipigwa kwa risasi umbali wa mita mbili na kwamba baada ya mlinzi wa nyumba hiyo kutoka nje, alikuta Padri Mkenda  tayari amepigwa risasi na watu hao wakiwa wameshatoweka.

Kuhusu kusambazwa kwa vipeperushi, Kamanda Aziz alisema hana taarifa hizo.

ASKOFU ANGLIKANA ANENA

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael  Hafidhi, alisema  Jeshi la Polisi limeonyesha udhaifu wa kusimamia ulinzi dhidi ya raia na mali zao.

Askofu Hafidhi alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya kutishia amani, lakini hakuna hatua za tahadhari zilizochukuliwa kabla ya Padri Mkenda kupigwa risasi.

Askofu Hafidhi alisema   vitisho hivyo vilitolewa na wafuasi wa Uamsho kuwa watafanya tukio kubwa  iwapo viongozi wao hawataachiwa uhuru kabla kumalizika sikukuu ya  Kirismasi Zanzibar.

Hata hivyo, alisema jamii lazima ielewe kuwa jamii ya Wakiristo Zanzibar wana haki sawa na waumini wengine kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

CCM  ZANZIBAR  YALAANI

Chama  Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeeleza kushtushwa na tukio la kikatili alilofanyiwa Padre Mkenda.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, katika taarifa yake jana  kwa vyombo vya habari, alisema mfululizo wa vitendo hivyo vya kinyama na kiharamia ni ukiukaji wa misingi ya kiungwana, ustaarabu na upendo.

“Tukio hili na lile la kuchomwa moto kwa makanisa, kumwagiwa tindikali kiongozi wa kiislam Sheikh Fadhil Soraga, miezi mitatu iliopita na Padri Mkenda kupigwa risasi, kunaweza kuipunguzia Zanzibar fahari na sifa zake njema,” Alisema Warid.

Alisema kwa karne nyingi Waislamu, wakristo na wenye dini mbalimbali wamekuwa wakiishi kwa umoja, maelewano kinyume na hali inavyojitokeza sasa visiwani humo.

Alisema CCM kinaamini kuwa Zanzibar na Tanzania si nchi za kidini, kila mtu anafuata imani anayoitaka bila kuingiliwa au kubugudhiwa na mtu yeyote.

“Uhuru wa kuabudi ni haki ya kikatiba katika katiba zote mbili za Tanzania na Zanzibar, hivyo CCM kinawalaani wale wenye mtazamo wa kuona imani zao ndizo thabiti kuliko za wengine,” alisema.

Waride aliviomba vyombo vya dola kufanya kila linalowezekana na kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mikono ya sheria.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinamtakia nafuu kwa Mungu Padri Mkenda ili apone haraka na kuwataka wananchi

Source:Nipashe

Maaskofu nchini watoa tamko zito

Maaskofu nchini, jana walitumia ibada za Krismasi kukemea maovu, huku baadhi yao wakiwatuhumu matajiri nchini kuwa ndiyo kiini cha vurugu zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa yao hivi karibuni.Wakihubiri kwa nyakati na makanisa tofauti, viongozi hao walisema uhasama huo dhidi ya Wakristo ulioanza kujengeka katika siku za hivi karibuni, unafadhiliwa na baadhi ya matajiri kwa masilahi yao binafsi.

Katika tamko lao lililotolewa na Umoja na Makanisa Tanzania, maaskofu hao wameitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mbegu za chuki zinazopandikizwa ili kuwafarakanisha Watanzania kwa misingi ya imani za dini.Tamko hilo ambalo litarejewa Desemba 30, mwaka huu, ni makubaliano ya pamoja kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moravian, Anglikana, Pentekoste, Wasabato na Kanisa Katoliki.


Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo 

 
Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini akisoma tamko hilo wakati wa ibada ya pamoja, alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya kidini, vinawachochea watu ili wawaue maaskofu na wachungaji mbalimbali wa makanisa.

Pia, alihoji kauli zinazoenezwa kuwa nchi hivi sasa inaongozwa kwa mfumo wa Kikristo ilihali asilimia 90 ya viongozi wa juu nchini ni Waislamu.“Labda niwakumbushe, viongozi wote waandamizi wa ngazi za juu nchini, asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe kwa mfumo wa Kikristo?” alihoji Askofu Shao.

Aliwataja kuwa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).“Kule Zanzibar, asilimia 100 ya viongozi wote ni Waislamu na si kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa ya kuongoza,” alisema na kuongeza:

“Hata uwakilishi kwenye Tume kama ya kuandikwa kwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu… Nchi hii haina mfumo wa Kikristo, bali ni nchi yenye mfumo wa kidemokrasia.”Aliitaka Serikali ithibitishe ukweli kuwa haiendeshwi kwa mfumo wa Kikristo badala ya kukaa kimya wakati maneno hayo ya uchochezi yanaenezwa hadharani.

“Ni wakati wa kukubali kuwa misingi ya haki, amani na upendo katika taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Kumekuwapo na dalili za wazi za uchochezi na kashfa dhidi ya Ukristo,” alidai.Maaskofu hao wamewalaumu baadhi ya viongozi wa dini kutumia vyombo vya habari vya kidini, vipeperushi, mihadhara na kanda za video kukashfu dini nyingine.

“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa linakashfiwa unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga mkono.”“Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari kubwa ya kiuhusiano siku za usoni. Tunaitaka Serikali ichukue jukumu lake la msingi la kusimamia amani.”

Askofu Pengo
Katika mahubiri yake jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo aliwaponda matajiri wanaojivunia mali, akisema siyo kigezo cha mtu kuwa na furaha maishani.

Kadinali Pengo alisema hayo katika misa ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika juzi katika Parokia mpya ya Mongolandege, Ukonga, Dar es Salaam.
Alisema ni makosa mtu kuhesabu mali kama sehemu ya mafanikio katika maisha kwani kuna wenye mali nyingi ambao hawana furaha.

“Utajiri unaambatana na shaka, hofu na wasiwasi kwa kufikiri kuwa huenda mali hii isinitoshe au itachukuliwa na watu wengine,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza:
“Tusitafute mali kiasi cha kuwafanya watu wengine waumie, wahuzunike. Kila mmoja atimize wajibu wake pale alipo, matokeo yake ndiyo yatakayoleta furaha.”

Askofu Mhongolo
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo amewataka waumini kuendelea kuienzi Krismasi kwa kujali na kuwekeza katika elimu ambayo ni msingi wa mambo yote.

Kiongozi huyo alisema kwa Wakristo, kuwa na dhana ya kujenga elimu katika maisha yao itawasaidia kujiletea heshima na kwamba watakuwa juu.

Askofu huyo alisema dhana nzuri ya kuthamini elimu hadi sasa waumini wa Kikristo nchini wamekuwa ni mfano wa kuigwa na jamii na taifa kwani kati ya jumla ya vyuo vikuu 19 vilivyoko nchini vyuo saba vinamilikiwa na Wakristo, 11 na Serikali huku kimoja kikiwa cha Kiislamu.

Askofu Mkude
Askofu Thelesphory Mkude wa Jimbo la Morogoro amewataka waumini wa dini zote kushiriki vyema katika kuendeleza na kushika neno la Mungu na kuombea nchi hasa katika kipindi hiki cha kufunga mwaka na kukaribisha Mwaka Mpya.

Katika ibada ya mkesha wa Krismasi, Askofu Mkude alisema kuwa imefikia wakati sasa wa kumshirikisha Mungu kila jambo kwani kila siku matendo maovu yanaendelea kutokea na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Askofu Sehaba
Askofu wa Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka pale inapoona kuna tishio la uvunjivu wa amani nchini kuliko kukaa kimya na kusubiri likitokea ndipo ianze taratibu za kudhibiti.
Alisema kumekuwapo na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya waumini wa dini kama uchomaji wa makanisa na kusema Serikali inapaswa kutovifumbia macho.

Askofu Mwombeki
Askofu Edson Mwombeki wa Kanisa la Free Evangelism Tanzania amewataka Watanzania wote kulinda amani na utulivu.
Akihubiri kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Manispaa ya Shinyanga, aliwaomba Watanzania wote wabadilike na kuwa na tabia njema kwani kwa sasa watu wengi wamepoteza uadilifu, amani na uzalendo.


 Source NIPASHE

Aliyefugwa kwa kukojolea Kura’n atinga Mahakama Kuu

Rufaa ya msichana Eva Abdallah anayetumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kukojolea Kura’n imefikishwa Mahakama  Kuu jijini Dar es Salaam, ambapo wiki iliyopita ilitolewa amri ya kusafirishwa kutoka gereza la Bagamoyo mkoani Pwani na kuletwa jijini Dar es Salaam.

Katika rufaa hiyo namba 132, ya mwaka 2012, iliyopo mbele ya Jaji Dk. Fauz. mrufani Eva anawakilishwa na mawakili wawili chini ya usimamizi wa taasisi ya Bibilia ni Jibu.

Uchunguzi wa chanzo kimoja cha habari hii umebaini kuwa Wiki iliyopita Jaji Dk. Fauz, alitoa amri ya mrufani kusafirishwa kutoka katika gereza anakotumikia kifungo chake huko Bagamoyo  na kufikishwa Mahakama Kuu, Jumanne saa nne asubuhi tayari kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Hata hivyo, Jumanne iliyopita mawakili wa pande zote pamoja na wanaofuatilia shauri hilo walifika mahakamani  na shauri iliaanza kusikilizwa, lakini mrufani hakufikishwa mahakamani.

Karani wa Mahakama alimweleza Jaji kuwa amri yake ilitekelezwa na uongozi wa Magereza uliahidi kumfikisha mahakamani siku hiyo. Baada ya maelezo hayo mawakili wa pande zote mbili walijaribu kumshawishi Jaji kesi isikilizwe wakati bila mrufani kwa kuwa mawakili wake wangemuwakilisha, lakini aliwaeleza kuwa angependa rufaa iendelee wakati Eva akiwepo.

Baada ya msimamo huo walikubaliana kuahirisha shauri kwa muda ili kutoa nafasi kwa mrufani kufika, hata hivyo baada ya kusubiri kwa muda mawakili waliitwa tena kwenye chumba cha mahakama ambapo mjadala wa hoja zinazojadiliwa kwenye rufaa hiyo.

Jaji aliwaambia mawakili kuwa iwapo mrufani angefika mahakamani basi shauri hilo lingesikilizwa na hata kufikia mwisho siku hiyo.
Hata hivyo Karani wa Mahakama alimjulisha Jaji kuwa uongozi wa Magereza umeahidi kumhamishia Eva kwenye gereza la Segerea ili iwe rahisi kupelekwa mahakamani.

Baada ya majadiliano Jaji aliahirisha shauri hilo hadi Januari tisa saa nne asubuhi ambapo mrufani atafikishwa mahakamani akitokea Gereza la Segerea.

Eva anatetewa na Mawakili wawili ambao ni Mark Lebba na Barnaba Luguwa, wakati upande wa Jamhuri (Mjibu rufani) unawakilishwa na Wakili wa serikali, Mwakamale.
Eva alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, Agosti mwaka huu baada ya kutiwa hatiani na mahakama ya Wilaya ya  Bagamoyo.

Inadaiwa kuwa Eva ni mtoto wa imamu mmoja huko Luhangwa, lakini aliisikia Injili ya Bwana Yesu Kristo akaiamini na kuikimbia hukumu ya Mungu kwa kuokoka katika kanisa la Pentekoste Bagamoyo.
Wito umetolewa kwa Wakristo kuingia katika maombi ili kumuombea binti huyo anayeteseka gerezani.

Source Jibu la Maisha










Serikali: Uhamaji ‘Analojia’ kwenda ‘Dijitali’ ufanyike kwa awamu

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
Serikali  imeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kuwa zoezi la uhamaji wa mfumo wa matangazo ya analojia kwenda dijitali unafanyika kwa awamu   ili kuondoa hofu ya wananchi ya kukosa matangazo ifikapo Desemba 31, mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wakuu wa TCRA, ambao waliwasilisha taarifa ya mabadiliko ya mfumo huo ofisini kwake.

Aidha, waziri huyo aliusisitizia uongozi huo kuendelea kutoa elimu sahihi kwa umma   kwa kuzingatia ratiba ya uzimaji wa mitambo hiyo iliyotolewa.

Mkurugenzi wa Utangazaji TCRA, Habi Gunze, akiwasilisha taarifa hiyo kwa waziri mwenye dhamana alisema uzimaji wa matangazo hayo utafanywa kwa awamu tano.

Alisema kwa Kanda ya Dar es Salaam, mitambo ya analojia itazimwa Desemba 31, mwaka huu, saa sita usiku na maeneo husika ni jiji la Dar es Salaam, miji ya Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe na Mkuranga.

Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel Ten, Star tv, DTV na Capital TV.

Vituo vingine ni pamoja na Tumaini TV, ATN, Mlimani TV, C2C, CTN, Clouds TV na Efatha.

Kwa Kanda ya Dodoma na Tanga, mitambo hiyo itazimwa Januari 30, 2013, maeneo husika yakiwa ni Manispaa ya Dodoma Kibaigwa, Mvumi, Mtera, Miyuji na Hombolo. Maeneo mengine ni pamoja na Muheza, Mkanyageni, Nguvu-Mali, Mabokweni na Mkinga.


Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel ten, Star tv, TV ya Manispaa ya Tanga na ATN.

Kanda ya Mwanza, mitambo itazimwa Februari 28, mwaka 2013 na maeneo yatakayohusika ni jiji la Mwanza, Sengerema, visiwa vya Ukerewe na Kisesa. Vituo vitakavyohusika ni TBC1, ITV, EATV, Channel ten, Star tv na ATN.


Kanda ya Kaskazini Moshi na Arusha, mitambo hiyo itazimwa Machi 31, 2013 maeneo husika yakiwa ni jiji la Arusha, Usa River na Tengeru.

Maeneo mengine ni Manispaa ya Moshi, Mweka, TPC Gate, Mabungo, Himo, Mwika, Marangu Mtoni, Chekereni, Bombang’ombe na Machame.

Kanda ya Mbeya, mitambo hiyo itazimwa Aprili 30, 2013, maeneo husika yakiwa ni jiji la Mbeya, Mbarali, Igulusi, Igawa, Rujewa na Chimala, vituo vitakavyohusika ni TBC1, Star tv, TV ya jiji la Mbeya na ATN.

Dk. Mukangara alisema wananchi wanaoishi katika maeneo, ambayo hayakutajwa katika ratiba hiyo wataendelea kupata matangazo kupitia mfumo wa matangazo ya televisheni kama ilivyo sasa hadi hapo mitambo ya kupokea mfumo wa matangazo ya dijitali itakapokamilika kwenye maeneo yao.

Alizitaka kampuni zinazoweka mitambo ya dijitali kuongeza kasi ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo inakamilika nchi kote kabla ya mwaka 2015.

Source:Nipashe

Viongozi wa Dini wataka mihadhara ikomeshwe

Viongozi wa Dini nchini wameiomba Serikali na taasisi zinazohusika kufuta mihadhara ya dini ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Wakizungumza wakati wa warsha ya kujadili nafasi ya dini katika kulinda na kudumisha amani, viongozi hao  walisema mihadhara ya dini ni moja ya sababu zinazoweza kuchangia kutokea kwa migogoro nchini.

“Ni lazima tuchukue tahadhari kabla migogoro haijatokea sababu kila jambo huanza taratibu...hata mauaji ya kimbari yalianza hivi," alisema Mkurugenzi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Peter Mitimingi.

Alisema suala la dini ni kama kidonda kilichofunikwa kwa kitambaa na kikifunuliwa kitaleta madhara makubwa kwa nchi.

Kwa upande wake,  Mhadhiri wa Chuo cha Kiislamu Morogoro, Abdallah Tego,  alisema matatizo yanayojitokeza katika nchi yanatakiwa kutatuliwa haraka ili kuepusha migogoro.

“Tunaomba serikali ichukulie suala hili kwa uzito na kulitatua kwa haraka kabla hakujatokea madhara," alisema.



Rose Muhando ndani ya Uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba

Rose Muhando Mwimbaji nyota wa muziki wa injili nchini  pamoja na waimbaji wenzake waliweza kulipendezesha tamasha kubwa la Shangwe Kagera zilizofanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na kukusanya mamia ya wakazi wa mji huo pamoja na viongozi wa dini na serikali.

Tamasha hilo liliandaliwa na kampuni ya Beula Communication kwa lengo la kukusanya fedha ili kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Kagera.

Kati ya viongozi waliohudhuria tamasha hilo ni pamoja na mkuu wa wilaya Bukoba bibi Zippora Pangani, bwana Melkzedek Mutayabarwa ambaye ndiye kiongozi wa kampuni ya Beula iliyoandaa tamasha hilo pamoja na wauguzi kutoka kituo cha watoto cha Tumaini cha mjini humo.


Rose Muhando  pamoja na waimba wake
Rose Muhando akiimba mbele ya viongozi wa Dini na viongozi wa serikali walioudhulia katika event hiyo.



   
SOURCE: gospelkitaa.blogspot.com

Tamasha la Praise in the City funga kazi 2012


 Praise in the City tamasha lililoandaliwa na Kanisa al Living Water Makuti Kawe jijini Dar es salaam limefanyika kama ilivyopangwa na kuwa barika wengi waliohudhuria katika ukumbi wa Diamond jubilee ambako limefanyika tamasha hilo.

Waimbaji kama John Lisu, Glorious Celebration,R.I.O.T Dancers walipata kuhudumu katika Tamasha hilo,Living Waters ndio waandaaji wa tamasha hilo pamoja na waimbaji wengine waliweza kuwabariki wengi kwa uimbaji wao wa viwango mbele za Mungu, pia katika tamasha hilo kulifanyika live recording ya kundi la Living Waters ambao waliimba nyimbo takribani kumi na saba.

Akizungumza katika Tamasha hilo Kiongozi wa Kanisa la Living Water Center Kawe Mtume Onesmo Ndegi amesema pamoja na changamoto walizopitia katika maandalizi ya Tamasha hilo wanamshukuru Mungu kwa kufanikisha tukio hilo la aina yake,aliongeza kwa kusema kulingana na Tamasha hilo kuwa la baraka kwa watu wengi litakuwa jambo la mwendelezo. 

 Mtume Onesmo Ndegi Kiongozi wa Kanisa la Living Water Center Kawe

Waandaaji wa Tamasha hilo Living Waters kutoka Kanisa la Living Water Center Kawe

Filipo Rupia akiwa na Living Waters


John Lisu
Glorious Celebration

R.I.O.T Dancers

Ma Mc wa Tamasha hilo Papaa ze Blogger na Rose Mushi

Joyous Celebration Live Recording ilivyo pagawisha mashabiki