Katika kuelekea Tamasha la Pasaka Sipho Makhabane, Mkongwe wa muziki wa Injili Afrika Kusini atahudumu katika tamasha hilo katika na ametunga wimbo maalum kwa Watanzania katika tamasha la Pasaka
Historia ya muziki Duniani, inaonesha kuwa muziki wa makanisani, ambao unajulikana kama muziki wa Injili ndio chimbuko la aina zote za muziki ulimwenguni,Hakuna ubishi kuwa kila mwanamuziki mwenye kuujua muziki, ukimuuliza chanzo cha yeye kujihusisha na muziki ni lazima atakueleza kuwa alianzia kwenye kwaya.
Hata hivyo pamoja na ukongwe wa muziki huo, bado unaonekana kutopewa nafasi sana kwenye vituo vya redio na Televisheni, labda kutokana na kuegemea dini fulani.
Pamoja na hilo, lakini pia haujaweza kuwanufaisha wanamuziki wa muziki huo hapa nchini tofauti na wanavyofaidika wanamuziki wa mataifa mengine kama ilivyo nchini Afrika Kusini.Sipho Makhabane ambaye anajihusisha na muziki huo nchini Afrika Kusini ni mmoja wa wanamuziki wa Injili wenye mafanikio makubwa.Makhabane ambaye pia ametajwa kuja nchini kushiriki tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Machi 31, mwaka huu, anamiliki kampuni kubwa ya Big Fish, ambapo kazi yake kubwa ni kukuza na kuibua vipaji vipya vya wanamuziki wa Injili.
Jina la mwanamuziki huyo ni kubwa barani Afrika, ambapo umaarufu wake umepatikana kutokana na uwezo wake wa kutunga nyimbo zenye ujumbe wa hali ya juu wa kumsifu na kumtukuza Mungu.Kutokana na uwezo wake huo mashabiki wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakimfananisha na wanamuziki mahiri kama Joyous Celebration ama Sfiso Ncwane.
Makhabane mwenye umri wa miaka 45 ni mmoja wa magwiji wa uimbaji nchini Afrika Kusini, ameshiriki katika shughuli mbalimbali za kiroho na kijamii.Kutokana na kutingwa na shughuli zake mwaka 2010 alitangaza kuachana na kazi ya kuimba, hata hivyo mwaka 2012 aliushangaza ulimwengu kwa kuachia albamu yake mpya iliyokubalika na watu wengi.
Historia ya maisha yake inaonesha kuwa ni mtu aliyekulia katika muziki huo.Kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa ukiikabili familia yake, Makhabane alilazimika kuacha shule akiwa darasa la tano na akiamua kufanya kazi katika shamba la miwa la Kaaruls huko Mpumalanga kama ilivyokuwa kwa mwimbaji mwingine nguli Rebecca Malope.
Makhabane alifanya hivyo walau aweze kupata fedha ya kuwasaidia wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walikuwa wakimtegemea yeye.
Alipotimiza miaka 17, alihamia kwenye kazi za ujenzi kwenye hifadhi ya Taifa ya Afrika Kusini ya Kruger.
akiwa huko alifanya kazi ya kuwasaidia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba kambini hapo na alipotimiza miaka 21 alikuwa tayari na ujuzi wa kutosha katika kazi ya ujenzi na akapata kazi katika eneo la Pienaar.
Mwaka 1986, Makhabane alipata ofa nzuri katika kampuni ya Telkom kama fundi, lakini katika kuhangaika kwake alijikuta akiishia kwenye muziki wa Injili.
Hata hivyo hakuwa akijua kuwa nyota ya mafanikio yake ilikuwa kwenye huduma hiyo ya uimbaji na badala yake alikuwa akifanya muziki wa kujifurahisha zaidi na si wa biashara.
Mwaka 1990, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Makhabane alifunga ndoa na binti aliyekuwa na umri wa miaka 18.
Baada ya hapo ndipo alianza kazi ya kununua na kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi ya Afrika Kusini.
Kutokana na kuona muziki umeanza kuingia kwa kasi kwenye maisha yake, Makhabane aliamua kuachana na kazi ya ufundi mitambo ya simu na kujikita kwenye muziki.
Katika kuhakikisha anaingiza kipato mwanamuziki huyo aliamua kusambaza kazi zake mwenyewe, lakini kikwazo kwake kikawa ni namna ya kuwavutia wasambazaji waliokuwa tayari kununua kazi kutoka kwake.
Kazi yake iliyomfanya kukubalika ilianza kusikika kwenye redio ya Swazi ambayo inajulikana zaidi kwa jina la Ligwalagwala FM, ambapo kibao kilichomtambulisha ni kile cha Ngitinikela Kuwe.Hatimaye mwaka 1996, Makhabane aliamua rasmi kuifanya kazi hiyo ya muziki wa Injili na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kampuni ya simu.
Mwaka huo huo aliachia album yake iitwayo “Yek’intokozo” wimbo ambao mpaka leo unakumbukwa na mashabiki wake kwani ndio ulimtambulisha vema, ingawa tayari alishatoa album nyingine mbili miaka ya 1993 hadi 1999 za ‘THUM’UMLOLO” na “JESU ULIQHAWE”.
Mwaka 1998, kupitia kampuni ya CCP Records aliachia album yake ya nne iitwayo “Uyigugu” iliyofanya vema kabla ya mwaka uliofuata kuachia nyingine iitwayo “Makadunyiswe,”.
Mwaka 2001, alifyatua album ya Calvary ambayo iliuza kufikia kiwango cha juu na mwaka uliofuata (2002), aliachia albamu nyingine ya ‘Akukhalwa’ ambayo ilitikisa kama album ya “Yek’intokozo,” akiuza zaidi ya nakala 70,000.
Mwaka 2003, Makhabane aliachia album ya ‘Moya wami’ ambayo pia iliuza zaidi ya nakala 70,000.
Kutokana na umahiri wake, Makhabane ameweza kushirikishwa katika album na waimbaji wakongwe wa nchini kwake kama Jabu Hlongwane, Marehemu Vuyo Mokoena, Lundi, Hlengiwe Mhlaba na wengine wengi.
Pia akiwa nyuma ya mafanikio ya waimbaji lukuki kama Hlengiwe Mhlaba, Ncandweni Christ Ambassadors, Shongwe na Khuphuka Saved Group.
Nje ya uimbaji, Makhabane ni mtayarishaji wa kazi za muziki wa injili akiwa daraja la waimbaji wengine kutokana na kuwika vilivyo kupitia kazi zao zilizoandaliwa na gwiji huyo.Makhabane ametunga wimbo maalum kwa ajili ya mashabiki wake wa Tanzania.Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam siku chache zimepita na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa amezungumza na msanii huyo na amemueleza kuwa amewaandalia zawadi Watanzania kwa ajili ya tamasha hilo.
“Sipho amefurahi sana kumualika kwenye tamasha letu, amenihakikishia licha ya nyimbo zake za kawaida, lakini pia atakuwa na wimbo maalum kwa Watanzania, amesema anawapenda Watanzania na ameandaa wimbo mzuri ambao ana uhakika mashabiki wataupenda.
“Mashabiki watakaokuja kwenye tamasha Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 31 watapata fursa ya kumsikiliza msanii huyo pamoja na wimbo wake mpya ambao jina hakunambia lakini amesema ni zawadi nzuri kwa Watanzania,” alisema Msama na kuzitaja baadhi ya nyimbo za msanii huyo kuwa ni Moya Wami, Indonga, Akukhalwa, Over&Over, Nguy’zolo, Yizwa Nkosiseju, Hlalanami Nkosi Jesu, Yek’intokozo, Injabulo, Hlalanami Jesu, Makadunyiswe, Vuka Mphemlo, Mphefumlo na Moya Wami.
Kuhusiana na maandalizi mengine ya tamasha hilo alisema yanaenda vizuri na kwamba mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwamba ni matumaini yake mashabiki watajitokeza kwa wingi.
Licha ya Sipho Makhabane, wasanii wengine wa nje ya Tanzania ambao tayari wamethibitisha kushiriki tamasha hilo ni , Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya na kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda inayotamba na albamu ya Mtegemee Yesu. Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone na John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.